![]() Historia ya Wafransisko
|
![]() |
1.1.1. MWANZO WA MAPAMBANO
(1226-1318)
Mt. Fransisko alipokuwa hai alisongwa na kundi
la Watumishi na wasomi wa utawa wake, likisaidiwa na viongozi wa juu wa Kanisa,
ili alegeze masharti ya ufukara na kulinganisha zaidi shirika lake na yale ya
zamani. Kwa karama yake ya pekee aliweza kukabili upinzani huo wote. Juhudi yake
ya mwisho ya kuzuia shirika lisipotoke ni wasia aliouandika ili kusisitiza
msimamo wake, kudai kanuni yake isifafanuliwe, pamoja na kukataza wanashirika
wasimuombe Papa hati yoyote. Alipokufa utawa ukabaki mikononi mwa Watumishi hao,
wakiongozwa na nd. Elia Bombarone, Mkuu wa shirika miaka 1221-1227, halafu
1232-1239.
Katikati
ya hivyo vipindi vyake viwili vya uongozi, Mtumishi mkuu alikuwa nd. Yohane
Parenti. Chini yake yalizuka mabishano makali kati ya walioshikilia wasia huo na
wale waliotaka shirika lishindane na mashirika mengine. Yeye na Watumishi
wengine wakadhani utatuzi unaweza kutokea kwa viongozi wa Kanisa tu. Akipokea
ombi lao, Gregori IX (1227-1241) alitoa tamko rasmi la kwanza juu ya kanuni
(1230), akitumia mamlaka yake ya Kipapa na pia ujuzi wake wa nia ya Mt.
Fransisko (ndiye aliyemsaidia sana kutunga kanuni alipokuwa bado Kardinali, jina
lake Ugolino). Upande wa ufukara kwa jumla alitetea msimamo wa mwanzilishi (kwa
jinsi alivyomheshimu hata akamtangaza mtakatifu), ila aliulegeza kiasi, kwa
lengo la kufanikisha zaidi utume wa Ndugu Wadogo na hivyo kurekebisha Kanisa
lililokuwa na hali mbaya kiroho. Kwa ajili hiyo aliwapa hati na ruhusa nyingi za
pekee dhidi ya mamlaka ya Maaskofu na maparoko. Kuhusu wasia alitamka kuwa si
sheria inayowabana Wafransisko wasiweze kufafanua kanuni yao wala kufafanuliwa
na Kanisa, wala kuomba wala kupewa hati na fadhili za Papa. Sababu ya msingi ni
kuwa Kanisa liko juu kuliko kanuni.
Hivyo
njia ikawa wazi kuligeuza shirika la wadogo walio wote sawa, wanaohubiri toba
kwa unyenyekevu chini ya padri yeyote, liwe shirika imara la kikleri, lisilo
chini ya Maaskofu isipokuwa kwa machache. Mageuzi hayo yalisababisha kwa muda
mrefu upinzani mwingi wa Maaskofu na mapadri wanajimbo. Aliyesukuma sana shirika
kufuata njia hiyo ni nd. Elia, ambaye alimjengea Mt. Fransisko kanisa zuri sana,
halafu jirani nalo konventi kubwa mno, ili kushindana na abasia za Wabenedikto.
Alimgeuza mwanzilishi kuwa fahari ya shirika badala ya kielelezo cha kufuatwa.
Mwenye vipawa na elimu, ingawa bradha, aliathiri sana viongozi wa dini (Gregori
IX) na wa siasa (Federiko II), alistawisha misheni huko Mashariki na kukuza
nyumba za masomo, lakini pia alidhulumu vikali watetezi wa kanuni (hasa
alimuacha nd. Kaisari wa Speyer afe kwa njaa kisha kumfunga). Bila ya kutembelea
kanda za shirika, alishika uongozi wote mikononi mwake, akichagua Watumishi na
walinzi, akihamisha ndugu, akituma wawakilishi wake huko na huko kusimamia kazi
ya Watumishi, na akikataa kuitisha mkutano mkuu. Fahari zake binafsi, ushuru
aliowatoza mfululizo Watumishi (kwa ajili ya ujenzi n.k.) vilisababisha wafanye
njama dhidi yake, hadi Gregori IX akaitisha na kuendesha mkutano mkuu ambao
ulimuondoa madarakani na kutunga sheria ili kupunguza mamlaka ya Mtumishi mkuu.
Nd.
Aimoni wa Faversham, Mwingereza aliyeongoza upinzani, akaja kuwa Mtumishi mkuu
(1240-1244), na kulipatia shirika sura ya kudumu kufuatana na mfano wa
Wadominiko upande wa muundo, utume, masomo na liturujia. Taratibu za maisha
zikazidi kufuata mitindo ya kimonaki, pamoja na watawa kujitafutia visingizio
vya kisheria wasibanwe nazo. Makao ya kifukara ya upwekeni yalizidi kuachwa ili
wanashirika wahamie nyumba kubwa za mijini, zenye makanisa makubwa ambamo
wafanye utume, wakiwanyang’anya maparoko waamini na sadaka zao. Kama
alivyofanya mwenyewe huko Paris, Ndugu Wadogo wakazidi kushika nafasi kwenye
vyuo vikuu na vinginevyo, na kuwa na uzito mkubwa ndani ya Kanisa, jambo
lililowasogeza mbali na udogo uliowapasa. Mabradha wakanyimwa kabisa nafasi za
uongozi na kukubaliwa tu kutoa huduma ndogondogo za nyumbani (bustani n.k.),
wakiwaachia raia huduma duni zaidi. Kazi za mikono nje ya konventi zilikatazwa;
badala yake ile ya kuombaomba ikaja kusifiwa na kushika nafasi ya kwanza upande
wa uchumi. Zilipangwa pia njia za hakika za kupata mahitaji, hasa kwa nyumba za
masomo.
Alipokufa,
nd. Kreshensi wa Iesi alishika nafasi yake (1244-1247), akatambua hali halisi,
lakini hakuweza kuirekebisha (pia kwa sababu ya uzee wake). Akiona
kwamba Mt. Fransisko alikuwa bado kielelezo cha wadogo, aliagiza zikusanywe
habari zote juu yake, halafu akamuagiza nd. Thoma wa Celano aandike upya maisha
ya mwanzilishi. Juhudi zake kwa ajili ya kushika njia ya kati hazikuridhisha
wala upande mmoja (wenzi wa Mt. Fransisko na ndugu “wa Kiroho”, yaani wenye
nia ya kushika kanuni kadiri ya Roho Mtakatifu) wala upande wa pili (“jumuia”,
yaani waliopenda maisha katika konventi kubwa na hali ilivyo). Inosenti IV
(1243-1254) alikubali kutoa tamko la pili juu ya kanuni (1245) ili kuilegeza.
Hasa alifungua milango ili Ndugu Wadogo wajipatie vitu vingi, akitamka kuwa
vyote walivyonavyo, kama si vya wafadhili tena, basi ni vya Papa. Hivyo kwa
kutofautisha kutumia vitu na kuvimiliki kisheria, Ndugu Wadogo waliweza kujidai
fukara ingawa wanatumia vingi, eti si vya kwao! Lakini wengi hawakuridhika na
ujanja huo.
Akachaguliwa M.H. Yohane wa Parma (1247-1257), mtu wa kufaa sana kwa
elimu na utakatifu, aliyeongoza hasa kwa mfano wa maisha yake bora. Alikusudia
kurudisha shirika katika hali ya mwanzoni kufuatana na wasia, kwa kuheshimu
Maaskofu na mapadri na kukataa fadhili za Papa. Alitembelea kwa miguu kanda zote
akiamsha nia ya kushika kanuni na wasia. Hivyo mkutano mkuu (1254) ulisimamisha
utumiaji wa fadhili kadhaa; lakini, alivyosema M.H. Egidi
wa Asizi (+1262), juhudi hizo nzuri zilikuwa zimechelewa zisiweze kurekebisha
shirika lote. Wapinzani walimshtaki M.H. Yohane, akalazimika kujiuzulu. Mkutano mkuu ulitaka aendelee, lakini mwenyewe hakurudi nyuma. Hatimaye
walimuomba walau amchague mwandamizi wake, naye akamtaja Mt. Bonaventura
wa Bagnoregio akaenda kuishi upwekeni.
Mt. Bonaventura (1257-1274), kufuatana na tabia yake,
alikubali hali ilivyo na kujitahidi kuepusha shirika na hatari za nje na za
ndani alizoziona mapema. Upinzani wa Maaskofu na maparoko dhidi ya Ndugu Wadogo
ulikuwa umeungwa mkono na chuo kikuu cha Paris: hapo hazikupingwa tu ruhusa
kadhaa walizopewa, bali msingi wenyewe wa mtindo wao na wa Wadominiko. Baada ya
Mt. Bonaventura na Mt. Thoma wa Akwino kuutetea, Papa alilaani upinzani na
kusifu sana mtindo wa Kiinjili. Mwalimu huyo kuchaguliwa kuwa Mtumishi mkuu
kukawa ushindi mwingine mkubwa chuoni.
Mashambulizi ya kutisha zaidi yalitokea ndani, upande
wa ndugu “wa Kiroho”. Mt. Bonaventura alijipangia kulinganisha uaminifu kwa
kanuni na mabadiliko ya shirika, akionyesha hayo hayaendi kinyume cha nia ya
mwanzilishi. Ili athibitishe hayo ilimpasa kuziondolea lawama msingi wowote kwa
kupigania uaminifu kwa wito wa shirika. Mwenyewe alikubali bila ya wasiwasi
matamko ya Mapapa juu ya kanuni kama ufafanuzi rasmi wa wachungaji wakuu wa
Kanisa na wa shirika pia. Kielelezo cha Mt. Fransisko kilitakiwa kuzingatiwa na
wote kwa umoja, bila ya kupishana kuhusu namna ya kukitazama. Kwa ajili hiyo
alitunga kitabu rasmi cha maisha yake kilichopitishwa na mkutano mkuu hata
ukaagiza maandishi yote yaliyotangulia yatekelezwe. Ndivyo shirika lilivyopotewa
kwa muda mrefu na habari nyingi muhimu juu ya mwanzilishi. Kitabu alichokiandika,
bila ya kusema uongo, kinaleta baadhi tu ya matendo na mafundisho ya Mt.
Fransisko yaliyochaguliwa kwa makini ili kumchora kama mfano kamili wa Kristo
msulubiwa na kusisitiza mang’amuzi yake bora ya kiroho, lakini kwa kuficha
mambo fulanifulani kuhusu kipeo cha udogo. Aliheshimu ufukara kama sifa kuu na
utukufu wa shirika, ingawa alijali mabadiliko yaliyotokea, yaani konventi kubwa
mijini n.k. Kwake elimu pamoja na utume ni sehemu ya lazima ya utendaji wa
Kifransisko. Kwa ajili hiyo alikubali ruhusa lilizopewa shirika, ingawa kwa
udogo alipenda kupatana na Maaskofu na maparoko. Basi, chini ya uongozi wake
shirika likatulia, kwa jinsi alivyoweza kulinganisha upendo kwa Mt. Fransisko na
furaha kwa mabadiliko, hamu ya kuishi upwekeni muda mrefu pamoja na ndugu “wa
Kiroho” na utetezi wa konventi za mijini.
Hata kwa nje shirika likazidi kuheshimiwa na kushika
nafasi katika maisha ya Kanisa (utume mbalimbali, uchaguzi wa Papa, Mtaguso mkuu).
Mt. Bonaventura akafa akiwa Kardinali, wakati wa Mtaguso II wa Lyons, ambao
ulionyesha hatari kwa mashirika ya Ombaomba, kwa kuwa ulipitisha hati ya
kuyafuta yote isipokuwa Wadominiko na Wafransisko, pamoja na Waaugustino na
Wakarmeli. Lakini iliwabidi hao wapatane na wanajimbo kwa kujinyima baadhi ya
ruhusa walizopewa. Hata hivyo Mapapa waliofuata wakaendelea kuwarudishia au
kuwanyang’anya tena, mpaka Mtaguso wa Vienne (1311-1312) ulipofaulu kuwatungia
sheria ya kudumu baada ya miaka mia ya mashindano: kwamba kuhusu maisha yao ya
ndani na uongozi watawa wawe chini ya Papa moja kwa moja, ila kuhusu utume nje
ya makanisa yao wawe chini ya Maaskofu na maparoko.
Mambo
yakawa magumu zaidi ndani ya shirika, hata suala la ndugu “wa Kiroho” likawa
zito kwa Kanisa lote. Mwelekeo wao ulianza kutia wasiwasi ulipoingiwa na unabii
na mafundisho yaliyolaaniwa ya abati Yohakimu wa Fiore (+1202). Huyo aligawa
historia katika nyakati tatu: ule wa Baba tangu Adamu hadi Kristo (ulioongozwa
na watu wa ndoa), ule wa Mwana tangu Kristo hadi kipindi cha Yohakimu (ulioongozwa
na makleri); hatimaye ule wa Roho Mtakatifu utakaoongozwa na watawa na kupindua
Ukristo kwa kufuta uongozi wa Kanisa, sakramenti na sheria ili kuanzisha Kanisa
la Kiroho, la furaha, upendo na uhuru kama matunda ya maisha ya kujikatalia.
Shirika jipya la watu “wa Kiroho” litakuwa kielelezo cha maisha ya Kikristo.
Wakati mpya utatangazwa na malaika wa mhuri wa sita, mwenye alama ya Mungu aliye
hai na mleta Injili ya milele, yaani ya Kiroho. Wafransisko wengi wakachangamka
na kumuona Fransisko kuwa ndiye malaika mwenye alama ya madonda matakatifu na
mleta Injili ya milele, yaani kanuni yake! Ndugu Wadogo wakajiona kuwa shirika
hilo jipya ambalo lilete Kanisa la Kiroho lenye kufuata ufukara. Hapo jina
“ndugu wa Kiroho” likawa na maana mpya na kuwaelekeza kupinga uongozi wa
Kanisa, kuanzia Mtaguso II wa Lyons, walipojiandaa kukataa maagizo waliyoambiwa
watapewa kinyume cha haki.
Ufransisko uliathiri vilevile mwelekeo wote wa sanaa ya Magharibi. Ukiitikia vizuri matarajio yote ya kidini na ya kijamii ya kipindi cha mageuzi, ulieneza mtazamo mpya wa maisha unaojali mtu na viumbe vyote. Hivyo ulichangia sana upatikanaji wa mitindo mipya na njia mpya za kufurahia uzuri, ingawa bila ya kupotewa na imani. Fasihi ya Kifransisko inapenda kusimulia, tunavyoona katika maisha ya mwanzilishi yaliyoandikwa na wafuasi wake; uchorahi unaonyesha sura halisi ya kwake na ya wengineo; hata ujenzi unafuata njia mpya, hasa kufuatana na kielelezo cha kanisa la Mt. Fransisko huko Asizi. Hata katika ujenzi wa nyumba zao Ndugu Wadogo waliweza kuzingatia ufukara bila ya kupuuzia uzuri, kiasi kwamba upendevu wake unavutia wengi hadi leo.
1.2.
MAREKEBISHO KUENDELEA (1517-1762)
1.2.1.
MATAWI MAPYA KUCHIPUKA
Utengano
wa Waoservanti na Wakonventuali ulitatua tatizo moja, lakini haukufaulu
kuunganisha makundi yaliyorekebishwa, ingawa Papa alikuwa ameagiza itungwe mara
katiba moja kwa yote. Baadhi yalidumu kuwa na kanda zao, Waoservanti wa Italia
wakaikataa katiba hiyo wakaendelea kuirekebisha mfululizo ile maalumu ya kwao,
na kanda nyingine zilijitungia vilevile na kuzidisha tofauti shirikani.
Kilichohatarisha zaidi umoja ni utaifa uliochochewa na serikali mbalimbali kwa
faida ya siasa ya nchi zao dhidi ya nyingine. Wafalme waliingilia kwa njama na
vitisho masuala ya mikutano mikuu, sawa na walivyoingilia uchaguzi wa Papa,
lakini kila mara idadi iliwapa ushindi Wahispania, hata washindani wao (Wafaransa)
wakagoma kuhudhuria mara kadhaa.
Matatizo
mengine yalihusu maisha yenyewe, hasa ufukara. Waliolazimika kujiunga na
Waoservanti, na wale wasioacha kutumia fadhili walizokuwanazo wakiwa
Wakonventuali, walikataa kurekebishwa. Kinyume chake, wengine hawakuridhika tena
na namna OFM ilivyoshika kanuni, wakadai ruhusa ya kuishika kabisa. Ndivyo
walivyofanya watawa wa mashirika mbalimbali, kwa kuwa haja ya urekebisho
ilitambulikana na wote katika Kanisa la karne ya XV na ya XVI. Kwa namna ya
pekee Ndugu Wadogo walichochewa kufanya hivyo na sura ya X ya kanuni pamoja na
wasia. Ndiyo sababu Mt. Bonaventura aliona haja ya kuwepo makao ya upwekeni
katika kila kanda ili kuwaachia uhuru wa kuishi hivyo wale wapendao. Kumbe
Waoservanti wengi na baadhi ya viongozi wao hawakukubali kuwaachia wenye bidii
uhuru huo, kwa sababu ingekuwa sawa na kukiri kwamba wamelegea. Hivyo
wakawatenda ndugu hao kama Wakonventuali wa zamani walivyowatenda Waoservanti wa
kwanza. Walioamini urekebisho unaweza kutoka kwa viongozi wakaja kujionea
haiwezekani. Miundo iliyoanza kama urekebisho ikajikuta inajaribu kuzuia juhudi
za waliopenda urekebisho, na viongozi wa shirika lililoanza kwa kushindana na
viongozi wakawalaumu waliotaka kufanya vile wakisema eti, ni wakaidi tu! Kwa
kukosa busara na wema walisababisha waliotaka urekebisho wakafuate njia zao ili
kupata ruhusa walizozihitaji, kwa kumkimbilia Papa au viongozi wa serikali. Mara
nyingine Wakonventuali walipokea makundi hayo chini ya ulinzi wao ili kuwakomoa
Waoservanti waliokuwa wanawadharau wakijidai ndio wafuasi halisi wa Mt.
Fransisko. Ndiyo asili ya matawi mapya, hasa lile la kujitegemea la Wakapuchini.
Mwaka
1525 nd. Mateo wa Bascio alimkimbilia Klementi VII (1523-1534) ili kuruhusiwa
ashike kanuni, avae kanzu asili na kuhubiri huko na huko alivyotaka.
Alipokubaliwa, walijiunga naye ndugu wawili, Ludoviko na Rafaeli wa Fossombrone.
Mtumishi wa kanda aliwatafuta sana, lakini walilindwa vizuri na Katerina Cibo,
ndugu wa Papa. Ili kukwepa dhuluma, wakajiunga na Wakonventuali, halafu wakapewa
na Klementi VII haki ya kuwa na Mtumishi wao chini ya Mkuu wa Wakonventuali na
ya kupokea wanovisi (1528). Mapema walianza kuitwa Wakapuchini kutokana na kofia
yao kubwa. Upinzani wa Mkuu wa OFM dhidi yao haukufaulu; kinyume chake, kwa kuwa
alitaka kuzuia hata makao ya upwekeni ndani ya shirika, ndugu wengi wenye bidii
wakakata tamaa wakajiunga na Wakapuchini. Njama nyingine za kuwakomesha
zikashindikana, hivi kwamba mwaka 1535 walikuwa tayari 700. Ndipo aliposhika
uongozi wao nd. Bernardino wa Asti aliyelipa shirika jipya sura ya kiroho ya
kudumu, hasa kwa njia ya katiba iliyotungwa mwaka huo na kupitishwa mwaka
uliofuata.
Hatari
nyingine zilitokea ndani ya shirika, kwa ukaidi wa nd. Ludoviko, halafu kwa
uzushi wa mwandamizi wa nd. Bernardino. Hatimaye mambo yakatulia na tawi jipya
likazidi kustawi kiroho na kitume, ingawa Julius III (1550-1555) alikataza
Waoservanti wasihamie tena kwa Wakapuchini. Hivyo hawa wakazidi kujisikia
tofauti na Wafransisko wenzao. Mkutano mkuu wa mwaka 1552 ulionyesha kuwa juhudi
kali za awali zimeanza kutulia na kujilinganisha na maisha: shirika lilipanga
masomo na kuwa na watu maarufu upande wa elimu, utume na uongozi. Jambo muhimu
zaidi, lilimzaa mtakatifu wa kwanza, bradha Felix wa Cantalice (+1587),
kielelezo cha unyofu. Mtaguso wa Trento (1545-1563) ulisifu tawi hilo kama
urekebisho wa kufaa na wenye uaminifu kwa wito wake hata kustahili kutazamwa na
Kanisa kwa namna ya pekee. Shirika likazidi kukaza nidhamu ili kuzuia ulegevu,
likaanza kuenea ng’ambo ya milima ya Italia Kaskazini (1573). Ulipozuka
upinzani wa Wakonventuali, Kanisa lilikuwa limeshang’amua ubora wa Wakapuchini;
basi, Paulo V (1605-1621) alitamka kuwa ni Ndugu Wadogo halisi na wana wa Mt.
Fransisko sawa na matawi mengine (1608), halafu akawaondoa chini ya Mkuu wa
Wakonventuali na kuwapa Mtumishi wa kwao mwenye haki ya kuhesabiwa mwandamizi
halali wa mwanzilishi (1619). Kwa wakati huo shirika limeshazaa tena watakatifu
Serafino wa Montegranaro (+1604), bradha asiye na vipawa vingi kiutu bali mwenye
karama za ajabu, Yosefu wa Leonesa (+1612), padri Mkapuchini wa kwanza kutumwa
kwa Waturuki Waislamu halafu mhubiri bora Italia, na Mt. Laurenti wa Brindisi
(+1619), “mwalimu wa Kitume”, mtimilifu kuliko Wakapuchini wote kwa
utakatifu, elimu na utume. Wakafuata Mt. Fidelis wa Sigmaringen (+1622), wa
kwanza kutoka nje ya Italia, na wa kwanza kufia dini kati ya waliotumwa na Idara
ya Papa kwa Uenezaji wa Imani, halafu Mt. Bernardo wa Corleone (+1667), mwongofu
mwenye toba kali. Pia walipatikana wenye heri 6.
Kipindi
hicho ndicho cha ukomavu wa shirika, mitazamo ya Kiitalia ilipopanuka kwa kuenea
nje ya nchi na wanashirika waliposhika nafasi muhimu katika Kanisa. Baadaye
hakuna matukio ya maana zaidi, isipokuwa mengine ya kufaa na mengine yasiyofaa
ambayo yaliathiri shirika: idadi ya watawa na ya shughuli iliongezeka pamoja na
sifa kutoka kwa viongozi wa Kanisa na serikali, lakini zilizuka vurugu pia kama
ile ya utaifa (1636-1678). Benedikto XIV (1740-1758) aliamua mhubiri wa Papa awe
daima Mkapuchini, akasema, “Shirika la Wakapuchini linastahili yoyote yale,
kwa kuwa ndilo kielelezo pekee cha ukamilifu wa Kiinjili kilichobaki hadi
nyakati zetu”. Kweli urekebisho huo uliendelea kushika kikamilifu kanuni kwa
muda mrefu kuliko mengine yote. Nyumba ziliendelea kujengwa ilivyoagizwa toka
mwanzo, ndogo sana, nje ya miji na vijiji, zikielekeza ndugu kufuata ufukara na
unyofu hata ulimwengu ulipokazania fahari. Watakatifu wa kipindi hicho ni bradha
Krispino wa Viterbo (+1750), kielelezo cha furaha ya kiroho, Ignas wa Santhià
(+1770), padri mwenye bidii kwa wagonjwa na wakosefu, Ignas wa Lakoni (+1781),
bradha ombaomba aliyesaidia sana fukara, na Felix wa Nicosia (+1787), bradha
mtiifu ajabu, mbali ya mwenye heri 1.
Vilevile
Italia, ndugu waliojikusanya katika makao ya upwekeni kuanzia mwaka 1535 (mkutano
mkuu ulipowaruhusu ili kuzuia wengine wengi wasiwakimbilie Wakapuchini), kisha
kuongezeka waliwekwa moja kwa moja chini ya Mtumishi mkuu tu (1579), wakapewa
katiba maalumu (1595), ruhusa za pekee sana (1596), hatimaye Kiongozi mkuu na
mkutano mkuu wa kwao. Hivyo mamlaka ya Mtumishi wa OFM kwao ikawa jina tu. Kati
ya hao Wariformati katika kipindi hicho tunawakuta watakatifu mabradha watatu:
Mt. Benedikto Mwafrika (+1589), mtoto wa watumwa huko Italia, Mnegro wa kwanza
kutangazwa mtakatifu, Mt. Umile wa Bisignano (+1637), mnyenyekevu ajabu, na Mt.
Karolo wa Sezze (+1670), aliyeandika vizuri sana kuhusu maisha ya kiroho; halafu
mapadri Mt. Pasifiko wa San Severino (+1721), aliyezingatia sana maisha ya sala,
na Leonardo wa Portomaurizio (+1751), tunda bora la Kirekebisho kilichoanzia
mjini Roma karne ya XVII. Pia walipatikana wenye heri 4.
Huko
Hispania, baadhi ya wafuasi wa urekebisho wa Pekupeku, baada ya kuunganishwa na
Waoservanti (1517) walimkimbilia Mkuu wa Wakonventuali ili kukwepa vizuio vya
OFM, na mmojawao, Mt. Petro wa Alcantara (+1562) akafanywa Mkurugenzi wao
(1557). Alipokufa, Pius IV (1560-1565) akawahamisha Waalkantara chini ya
Waoservanti lakini bila ya kufuta kanda zao, katiba yao na mavazi yao maalumu.
Gregori XIII (1572-1585) akamkataza Mkuu wa OFM asiingilie masuala yao ya ndani
(1578), na Urbani VIII (1623-1644) akawaruhusu wasifuate tena katiba ya shirika
lote (1642). Jinsi sisitizo la sala na toba linavyozaa matunda imethibitishwa na
umisionari wao (Amerika na Asia Mashariki) na hasa na watakatifu 9 wa urekebisho
huo, wakiwa ni pamoja na Mt. Paskali Baylon (+1592), mwenye ibada ya pekee kwa
Ekaristi, wat. Petro Batista, Martino wa Kupaa na Fransisko Blanco, mapadri,
halafu Fransisko wa Mt. Mikaeli, Gonzalo Garcia na Filipo wa Yesu, mabradha,
ambao wote walifia dini Japani (+1597), hatimaye Mt. Yohane Yosefu wa Msalaba
(+1734), mpenda ufukara mkuu. Pia walipatikana wenye heri 22.
Huko
Ufaransa makao ya upwekeni hayakustawi sana hadi mwisho wa karne ya XVI. Mwaka
1601 walioishi huko wakapewa na Kanisa Mkurugenzi mwenye mamlaka pana sana; hapo
wakaenea haraka kwa msaada wa mfalme, hata kanda zote za Ujerumani na Uholanzi
zikajirekebisha na kujiunga nao, wakaitwa Warekoleti. Mmojawao
ni Mt. John Wall (+1679), aliyefia dini huko Uingereza.
Katika karne ya XVI na ya XVII karibu kila mkutano mkuu wa OFM ulizungumzia
katiba na kupigania umoja, ambao haukuwa rahisi kutokana na mchanganyiko wa
ndugu waliopenda fadhili za Wakonventuali na wengine waliotaka urekebisho.
Katika hali hiyo Watumishi wakuu walijitahidi kuhuisha shirika lote, lakini
wengi wao walitumwa na Mapapa kama mabalozi kwa wafalme na Maaskofu wa Ulaya, au
walipewa uaskofu wa miji muhimu. Shirika halikupendezwa kwa sababu lilikuja
kukosa uongozi imara: ndiyo maana mara kadhaa liliwadai kiapo cha kutokubali
kazi hizo au walau cha kujiuzulu Utumishi. Watakatifu waliopatikana kipindi
hicho ni: Mt. Salvatore wa Horta (+1567), bradha aliyefanya miujiza mingi ajabu
(labda milioni moja), wat. Nikolaus Pieck, Jeromu wa Weert, Teodoriko van der
Eem, Nikasi wa Heeze, Wilehadi wa Denmaki, Godefrid wa Melveren, Antoni wa Weert,
Antoni wa Hoornaert, Fransisko wa Roye, mapadri, halafu Petro wa Assche na
Korneli wa Wijk-bij-Durstede (+1572), mabradha, ambao wote walifia dini Uholanzi,
Mt. John Jones (+1588), aliyefia dini Uingereza, hatimaye Fransisko Solano
(+1610), mmisionari bora Amerika Kusini aliyezunguka kotekote kwa miaka 14,
akihubiri na kuimba. Wenye heri wa kipindi hicho ni 17.
Karne ya XVII ikawa ya utulivu na utendaji, lakini ongezeko kubwa mno la
watawa lilisababisha matatizo makubwa na ulegevu hata katika marekebisho. Pamoja
na utaifa kuzidi, matawi ya Italia yalishindana kwa maandishi makali ya kukwaza.
Makwazo mengine yalitokana na desturi ya Watumishi kadhaa kutuma watawa wasiofaa
kwenye kanda nyingine au kuwaacha nyumbani mwa marafiki au ndugu. Badala ya
juhudi za watawa kwa ajili ya kanuni kama katika karne zilizopita, sanasana
tunakuta viongozi wakijitahidi kuwalazimisha washike kanuni, lakini bidii za
namna hiyo hazikuweza kufanikiwa kwa kuwa hazikutoka moyoni mwa watawa. Hatimaye
mwaka 1676 mkutano mkuu ulikubali na kuagiza kila kanda ianzishe makao 3-4 ya
upwekeni ambapo yafanyike malezi ya watakaji na wanovisi wote: baadaye katika
mazingira hayo walistawi wat. Thomas wa Cori (+1729), mhubiri maarufu na Teofilo
wa Corte (+1740), mwanafunzi wake. Lakini katika karne ya XVIII ilionekana wazi
jinsi matazamio ya wengi yalivyolenga kupata kwa visingizio vyovyote fadhili na
nafasi za kwanzakwanza. Kupitia
mikutano mikuu upuuzi wa namna hiyo uliathiri sheria za shirika. Pia mabadiliko
mengi mno ya katiba, badala ya kusaidia nidhamu, yalizidi kuipunguza kwa
kusababisha ndugu wasiijali katiba isiyodumu.
Upande
wa Wakonventuali, utengano na Waoservanti haukuwaondolea baadhi yao wasiwasi
kuhusu utekelezaji wa kanuni, ingawa Mtaguso wa Trento ulitamka (1563) kwamba
OFM na Wakapuchini tu hawaruhusiwi kuwa na mali hata kishirika, tofauti na
Wakonventuali na mashirika mengine yote. Uhusiano na matawi yaliyokimbilia chini
ya Mkuu wao ili kufuata urekebisho ulichochea hamu ya kuwaiga. Ndivyo
walivyoanza Wakonventuali wa Urekebisho Hispania: uenezi wao ulichangia uamuzi
wa Mt. Pio V (1566-1572) wa kuunganisha na OFM Wakonventuali wote wa Hispania na
Ureno (1566-1567). Juhudi za mikutano, za Watumishi wakuu na za watawa wenyewe
zilileta nidhamu na ustawi, hasa mmojawao alipochaguliwa kuwa Papa Sisto V
(1585-1590) akaanza kuwasaidia kwa kila njia, kama vile kuunganisha chini ya
Wakonventuali marekebisho madogo yaliyokuwa yameanza Italia (1562). Ila mwaka
1669 yakaja kutawanywa, baada ya kusumbuliwa sana na Wakonventuali wa kawaida na
Wakapuchini (kuhusu sare zao zilizofanana). Kabla ya hapo mkutano mkuu ulitunga
katiba mpya kabisa (1625) ili kuondoa misimamo tofauti kuhusu kanuni: katiba
hiyo haikufuata matamko ya zamani ya Mapapa juu ya kanuni, bali ilipitisha moja
kwa moja desturi za shirika zilivyokuwa. Baada ya kuthibitishwa na Urbani VIII,
Wakonventuali wakaanza kuweka nadhiri zao kwa kutamka wazi kuwa watashika kanuni
“kadiri ya katiba ya Urbani” tu.
Baada
ya kujipatia hivyo msimamo wa kudumu, Wakonventuali wakazaa mwenye heri 1 na
watakatifu 2 waliong’aa mmoja hasa upande wa sala, mwingine upande wa utume:
Mt. Yosefu wa Copertino (+1663) na Mt. Fransisko Antonio Fasani (+1742), wote
mapadri. Pia shirika liliendelea kusifiwa upande wa elimudini likaona mtawa wake
mwingine kuwa Papa (Klementi XIV, 1769-1774) ambaye naye alilipendelea sana,
k.mf. kwa kuwahamisha Waoservanti wote wa Ufaransa chini ya Wakonventuali. Kwa
mara nyingine upendeleo huo ukazaa chuki ya wengine ilivyojitokeza kisha kufa
kwake.
Takwimu
ya jumla ya Utawa I ni kama ifuatavyo:
Matawi |
Mwaka
1575 hivi |
Mwaka
1700 hivi |
Mwaka
1762 hivi |
(Waoservanti) |
32,750 |
36,400 |
39,900 |
(Pekupeku) |
1,700 |
6,600 |
7,000 |
(Wariformati) |
500 |
13,900 |
19,000 |
(Warekoleti) |
50 |
9,200 |
11,000 |
OFM
jumla |
35,000 |
66,100 |
76,900 |
Wakonventuali |
12,000 |
15,200 |
21,000 |
Wakapuchini |
3,600 |
27,300 |
34,000 |
Jumla kuu |
50,600 |
108,600 |
131,900 |
Bila
ya kujali tofauti kati ya tawi na tawi, karibu 60% walikuwa mapadri, ambao nusu
ya idadi yao walikuwa wahubiri, nusu “mapadri wa Misa na sufuria” tu.
Ongezeko lilipungua kwanza kutokana na Uprotestanti kuenea na kufuta kanda
kadhaa Ulaya Kaskazini, na utawala wa Kiislamu kuenea Ulaya Mashariki Kusini,
ingawa pande nyingine zilifidia. Karne yenye ongezeko la kasi zaidi ni ile ya
XVII: ndio mwanzo wa wasiwasi na hofu kwa viongozi wa Kanisa na serikali, kwa
kuwa mashirika mengine pia yalikua. Kuanzia mwaka 1634 Mapapa walichukua hatua
kuzuia upokeaji wa wanovisi na kupunguza konventi (Italia zilifungwa 24.2%),
hata kufikiria uwezekano wa kuwapeleka watawa vijana kupigana na Waturuki ili
kuwapunguza! Lakini hatua hizo hazikufanikiwa. Kuhusu uenezi, wakati wa kufikia
kilele cha idadi ya wanashirika mgawanyo ulikuwa ifuatavyo:
Nchi |
OFM |
OFMConv |
OFMCap |
Jumla |
Italia na visiwa |
26,000 |
10,700 |
15,700 |
52,400 |
Hispania na makoloni |
23,000 |
0 |
3,100 |
26,100 |
Ufaransa |
9,500 |
5,400 |
6,100 |
21,000 |
Ujerumani n.k. |
9,600 |
2,600 |
8,100 |
20,300 |
Ureno na makoloni |
4,000 |
0 |
0 |
4,000 |
Dola la Waturuki |
1,700 |
800 |
300 |
2,800 |
Polandi na Urusi |
1,500 |
1,500 |
0 |
3,000 |
Uingereza na Irelandi |
1,600 |
0 |
150 |
1,750 |
1.2.2. MAISHA NDANI YA SHIRIKA
Kadiri ya hati ya utengano (1517) Mkuu wa Waoservanti tu alikubaliwa
kuitwa Mtumishi mkuu, wakati yule wa Wakonventuali alipewa jina la Mwalimu Mkuu;
vilevile viongozi wa kanda. Lakini jina hilo jipya halikuja kutumika. Mkuu wa
Wakapuchini aliitwa Makamu (wa Mkuu wa Wakonventuali aliyetakiwa kumthibitisha
baada ya kuchaguliwa). Jina la “Mtumishi mkuu wa Shirika lote” lililotumiwa
na Mkuu wa OFM lilichukiwa na kulalamikiwa na Wakonventuali na Wakapuchini, hadi
Paulo V alipotamka kuwa hao wote ni wana halisi wa Mt. Fransisko, na Wakuu wao
ni waandamizi wake halali (1619). Hata hivyo mabishano ya wazi yakaendelea
kuhusu mlolongo wa uandamizi huo, mtindo asili wa kanzu na hasa kofia yake,
mpaka Aleksanda VIII (1689-1691) alipokataza maandishi yote juu ya hayo.
Kwanza Kardinali mlinzi
alikuwa mmoja kwa wote, halafu Wakapuchini wakakubaliwa kuwa na mmoja wa kwao
(1564), na vilevile Wakonventuali (1580). Mara kadhaa waliingilia mno masuala ya
shirika hadi kulivuruga na kusababisha Mapapa walazimike kuwazuia. Mamlaka yao
ilipungua ilipoanzishwa Idara ya Papa kwa Watawa (1586). Tofauti
kati ya matawi kuhusu miundo ya ndani ziliendelea, hasa upande wa mikutano,
lakini hazikupata kamwe kuwa kubwa mno, kwa sababu ya kanuni na mapokeo yao kuwa
mamoja.
Haikuwa
rahisi kwa viongozi kuhuisha kiroho umati mkubwa vile wa watawa, hasa
tukizingatia jinsi Wafransisko wasivyopangika. Ili kuleta nidhamu zilitumika
mbinu za kisheria: ziara za Mkuu zilizofanyika kwa ukali na adhabu hata ya
kufungwa na kufukuzwa. Mbinu mpya (hasa kuanzia katikati ya karne ya XVII) ni
mazoezi ya kiroho; pengine zilisambazwa pia barua za Mkuu.
Maisha ya kiroho yalistawi hasa Hispania katika karne ya XVI, Ufaransa
katika ile ya XVII, na Italia katika karne za XVI-XVIII. Katika hiyo karne ya
dhahabu ya Hispania, Ndugu Wadogo walichanga na wananchi wenzao walioandika juu
ya maisha ya kiroho: ufafanuzi kamili wa mang’amuzi ya ndani na teolojia ya
kiroho pamoja na ugumu wa maisha, ingawa walifuata mapokeo ya shirika kwa
kusisitiza zaidi uhuru wa roho, ubora wa upendo na usahili katika kumuelekea
Mungu. Ndugu wa Italia walielekea zaidi utendaji hasa katika huruma, hivyo
hawakulenga mirukoruko katika ibada. Hasa Wakapuchini walijitahidi toka mwanzo
kuandika vitabu vyenye lengo la kujenga kiroho wasomaji na kuwaelekeza wote
katika sala kama njia bora ya kurekebisha maisha. Ndugu wa Ufaransa walizingatia
hasa matakwa ya Mungu kama muhtasari wa hatua tatu za maisha ya kiroho.
Katika
karne hizo mtindo wa Baroko ulitawala sanaa na maisha ya jamii pia, ukijali sura
kuliko undani, vitendo kuliko moyo: hivyo mapambo na madoido yakazidishwa sana.
Hiyo ni sababu mojawapo ya marekebisho kusifiwa kadiri yalivyojitokeza katika
miguu mitupu, nguo duni, majengo fukara na mwenendo adili. Mambo hayo
yalipotokana na msimamo wa moyo yalijenga kweli, tofauti na yalipofanyika kwa
nje tu.
Maisha
katika marekebisho yalikuwa magumu, si ya kuvutia, ingawa riziki hazikukosekana
kwa ukarimu wa walei. Kila mmojawapo mwanzoni ulilenga kuwa na ndugu wachache
katika nyumba ili kurahisisha usahili, ufukara na udugu, lakini polepole idadi
ikaongezeka kwa faida ya taratibu za kitawa na hasa fahari ya ibada. Mwaka 1680
kwa wastani kulikuwa na ndugu 17 kwa nyumba; mwaka 1762 walifikia 20. Pamoja na
mapadri, mafrateri (kwa maana ya wenye kusomea upadri au walau walionyolewa
tonsura) na mabradha kulikuwa na Watersyari wa kudumu katika jumuia. Mwanzoni
mwa kila urekebisho mabradha walikuwa wengi, halafu wakazidi kupungua kutokana
na kuchujwa sana; lakini pia kwa sababu wakazidi kukosa nafasi, wakipangwa hata
baada ya wanovisi watakaosomea upadri! Mtaguso wa Trento uliwanyima haki ya
kupiga na kupigwa kura, ila Mt. Pio V aliwarudishia Wakapuchini. Hivyo mabradha
wengi walijitafutia ruhusa ya kuhamia kati ya mafrateri, kinyume cha sheria.
Wasio mapadri walizidi kupokea Komunyo kuliko zamani. Shida kubwa ilikuwa bado
namna ya kuwapa kazi mapadri wasio wahubiri, kwa kuwa hawakufanya utume wala
kazi za mikono. Shughuli kuu ilikuwa Misa na Sala ya Kanisa iliyoadhimishwa
usiku (lakini kwa Wakonventuali si mahali pote) na mchana kwa nyimbo (isipokuwa
Wakapuchini na Wariformati walipendelea kuacha nafasi zaidi kwa sala ya moyo).
Haja
ya kutafuta miito haikuwepo; kazi ilikuwa kuichuja tu kwa majaribu mengi. Hata
desturi ya Wakonventuali ya kupokea watoto ikaja kwisha karne ya XVI. Ili mtu
apokewe kama frateri alipaswa kuwa na elimu ya msingi na kujua Kilatini.
Hayakufikiriwa makao ya malezi kwa watakaji. Kwa wanovisi Klementi VIII
(1592-1605) aliagiza (1596) zichaguliwe tu nyumba ambapo maisha ya kitawa
yanashikwa kikamilifu; tena watengewe sehemu maalumu na kuwasiliana na mlezi wao
na msaidizi wake tu, pamoja na kushiriki ratiba ya jumuia (sala, milo n.k.).
Katika karne ya XVIII zikaanza kutokea nyumba za unovisi kwa mabradha tu,
zilizozidisha utengano wa kitabaka ndani ya shirika. Kazi ya mwaka wa jaribio
ilikuwa hasa kueleza kanuni na amri zake kadiri ya matamko ya Mapapa; mapokeo ya
shirika; nidhamu; juhudi za kiroho; taratibu za ibada (pamoja na kuimba, kwa
Wakonventuali na Waoservanti); Sala ya Kanisa; hasa utekelezaji wa sala na
maadili. Walezi bora waliandika vizuri juu ya mang’amuzi yao. Baada ya nadhiri
(ambazo zilikuwa za daima tu) watawa chipukizi walitakiwa kuendelea na malezi
miaka mitatu katika nyumba ya kuaminika. Kulikuwa na maagizo kuhusu malezi ya
kudumu pia (vipindi vya mara kwa mara kwa wote).
1.2.3. UTUME
Mikutano mikuu ilishughulikia utume wa kuhubiri ikisisitiza ndugu
waandaliwe na kuchujwa kwa makini, halafu wasiofaa wanyang’anywe ruhusa. Pia
zilipangwa ngazi mbalimbali: kuanzia wahubiri wa konventi na wa kanisa lake hadi
wahubiri wakuu wa mahali muhimu zaidi alipojiwekea Mtumishi mkuu (Italia
palikuwa 30). Lakini mvuto wa elimu ulisababisha huduma za kiroho zisizingatiwe
sana na ndugu wenye vipawa vingi zaidi. Basi, ili kuwavuta wakahubiri na
kuungamisha Mkuu wa OFM alipewa haki ya kuwapa fadhili na vyeo, kama kawaida ya
wakati huo.
Urekebisho
wa Wakapuchini ulipinga mitindo ya kuhubiri kwa kurudia unyofu wa Injili,
kuhimiza ushuhuda wa maisha na kulenga wongofu wa wasikilizaji. Kwa karne moja
na zaidi hao waliendelea kuwa wahubiri bora, kwa jinsi wanavyoelewa watu na
kugusa sio akili tu, bali mioyo pia, ya wadogo na hata ya wasomi. Hayo yalikuwa
matokeo ya maisha bora ya kiroho, lakini pia ya maandalizi ya mpango chini ya
walimu wa hakika. Walipoanza (1650 hivi) kufuata mitindo ya Baroko, matunda
yakapungua. Wahubiri waliongoza pia roho binafsi. Wafransiskani waliungamisha
sana, kumbe Wakapuchini walisita kupokea kazi hiyo, isije ikavuruga maisha yao
ya sala hasa. Walianza kuifanya nje ya Italia (katika mkoa wa Alsasya kati ya
mwaka 1740 na 1747 waliungamisha mara 24 milioni!), lakini walitakiwa kuwa na
sifa maalumu.
Kati
ya mahubiri zilishika nafasi ya pekee wiki za uamsho, hasa kuanzia mwaka 1650
hivi. Waliokusudiwa kuziendesha walidaiwa maandalizi kamili. Baadhi zilifanywa
na ndugu 30 hadi 60 kwa pamoja. Kulikuwa na mafundisho maalumu kwa makundi (watoto,
vijana, akina baba, akina mama) na pengine mfungo wa siku nne kwa makundi ya
pekee. Mbinu zilikuwa mbalimbali, lakini licha ya kufundisha imani na maadili
Wakapuchini hawakukosa kuelekeza watu wote namna ya kufanya sala ya moyo.
Wahispania walitumia sana maandamano ya toba, rozari za hadhara n.k. Waitalia
walikuwa wakipanda msalaba karibu na mji au kijiji uwe kumbukumbu. Maarufu
kuliko wote waliofanya kazi hiyo ni Mt. Leonardo wa Portomaurizio, aliyeendesha
wiki hizo mara 343, akiongozana kwa kawaida na mapadri 4 na bradha 1. Baada ya wiki mbili za mahubiri kulikuwa na wiki moja ya maungamo. Katika
miaka 44 aliokoa watu wengi ajabu, na kuinua hali ya roho ya mapadri wanajimbo
na watawa katika Italia karibu nzima. Ndiye mwenezaji mkuu wa Njia ya Msalaba,
ibada iliyoanza kustawi katika karne ya XV ikiwa na vituo 7 hadi 37, mpaka ile
ya 14 ilipopewa rehema ya pekee (1686) na hivyo kuenea popote. Kumbe kiini cha
wiki za uamsho za Wakapuchini kilikuwa ni kuabudu ekaristi kwa saa 40 mfululizo,
ibada iliyoanza mwaka 1535 na kutoa nafasi ya kuhubiri kwa nguvu zaidi.
Ndugu
Wadogo walieneza ibada nyingine pia, hata kabla Kanisa halijazikubali rasmi,
kama vile kwa Moyo wa Yesu, kwa Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili (aliyetangazwa na
mkutano mkuu wa mwaka 1645 kuwa msimamizi wa shirika) na ile ya kujifanya
watumwa wake. Kuanzia karne ya XV Wakonventuali walieneza rozari ya furaha saba
za Bikira Maria, na chama cha kamba ya Kifransisko (ambayo hata watakatifu 4
wasio wanashirika walipenda kuivaa kiunoni).
Ndugu
Wadogo waliendelea kushika nafasi muhimu katika Kanisa: 739 walikuwa Maaskofu (kati
ya mwaka 1503 na 1710), 16 Makardinali (karne ya XVI hadi ya XVIII), na 2
wakafikia Upapa. Wengine
pia waliathiri sana siasa, k.mf. katika vita vya madhehebu, katika kutetea haki
za Kanisa dhidi ya serikali, na hasa kama mabalozi wa Mapapa na wa wafalme
Wakatoliki.
Hasa
Wakapuchini walijihusisha na aina mbalimbali za utume wa kijamii, wakidaiwa na
katiba kujitosa hadi ushujaa. Kwa namna ya pekee walifanya hivyo yalipoenea
maradhi ya kuambukiza, hasa tauni. Katika karne ya XVI na XVII kila mara
walijihatarisha na kufa ili wahudumie kiroho na kimwili walioambukizwa. Ilivutia
sana kuona wanajumuia wote kujitolea. Tunafahamu zaidi ya ndugu 2,000 waliokufa
hivyo, lakini walikuwa walau mara mbili zaidi, bila ya kuhesabu ndugu wengi wa
matawi mengine. Katika miji mingi walikabidhiwa uongozi wa hospitali nzima, hata
nje ya nyakati za tauni. Zaidi ya hayo Wakapuchini hasa walihudumia kiroho
wagonjwa na walio mahututi, walianzisha vyama vya kutolea huduma hizo,
walichapisha vitabu juu yake, walipenya magereza ili kuhudumia wafungwa na
waliohukumiwa kufa. Ufaransa walikuwa wazimamoto pia. Hata vita viliwapa nafasi
za kujitoa kwa upendo kama mapadri wa wanajeshi, hasa katika kuzuia Waturuki
Waislamu wasiteke Ulaya nzima kati ya mwaka 1571 na 1686. Wafalme pia
waliwatafuta sana Wakapuchini kama wahudumu wa roho na wa mwili wa askari wao.
Ndugu Wadogo walipambana na mifumo mbalimbali iliyofuatana kuzuka karne
hizo na kupotosha imani na maadili, hasa Uprotestanti. Dhidi ya Rinascimento
iliyotaka kurudisha Ulaya kwenye mitazamo ya kipagani, marekebisho ya karne ya
XVI yalihubiri toba na kushuhudia dharau ya anasa. Dhidi ya Ujanseni shirika
lilitetea kwa mahubiri na maandishi kipeo cha Kiinjili na mapokeo ya ibada.
Dhidi ya waasi wa dini walioshambulia misingi ya Ukristo, huko Ufaransa
walianzisha hata gazeti la kutetea dini.
Ingawa
uenezi wa Uprotestanti ulifunga konventi nyingi, hakuna hata moja iliyoasi jumla.
Idadi ya Wafransisko waliouingia ni ndogo kulingana na ile ya walioupinga tangu
ulipoanza, kabla wengi hawajatambua hatari. Kardinali wa Brandeburg aliwakataza
(1519) wasiendelee kuhubiri dhidi ya Martin Luther, kumbe Mtumishi mkuu
alipofika Ujerumani aliagiza maandishi yake yachomwe, wahubiri waandaliwe
kumshambulia tena na wanashirika wote wasali na kujiandaa kufia imani (kama
walivyofanya walau 500 katika miaka 1520-1620). Walutheri walitokeza chuki yao
kwa kueneza kitabu cha dhihaka “Kurani ya Pekupeku”. Baadaye Ndugu Wadogo
wakawa kati ya mashirika muhimu zaidi katika kurudisha Ukatoliki kwenye miji na
vijiji. Wakapuchini walianza kupambana na Uprotestanti kwa mahubiri na katekesi
huko Italia usije ukaipenya, wakawa wa kwanza kujitolea kutumwa na Idara ya Papa
kwa Uenezaji wa Imani mara ilipoanzishwa (1622). Chini yake juhudi ziliongezeka
na kupangwa vizuri zaidi. Chuo chake mjini Roma kilianzishwa (1627) hasa kwa
juhudi na ukarimu wa Kardinali Mkapuchini. Idara ilikuwa ikituma wale wote
waliopendekezwa na wakubwa wao wakiwa na sifa upande wa maadili na elimu. Katika
karne ya XVII idadi kubwa ya waliotumwa ni Wakapuchini. Agizo la shirika
lilikuwa kuwasiliana na Waprotestanti kwa kufuata mbinu za Mt. Fransisko wa
Sales (+1622), yaani kwa upole, usikivu na ushuhuda wa maisha safi yenye
kujitosa. Pia Wakapuchini walishirikisha waamini katika kazi hiyo ngumu, na
kuandika vitabu vya mabishano. Huko Uingereza na Irelandi baada ya kufukuzwa
wote, kwa karne tatu Wafransiskani wakaendelea kuingia ili kufanya utume kwa
siri kutoka Ulaya Bara walipopokea na kulea miito ya visiwa hivyo.
Wakonventuali
walifanya kazi hasa kati ya Waortodoksi, wakivuta baadhi yao upande wa Roma na
kutunza makundi madogomadogo ya Wakatoliki waliosambaa Mashariki. Pia walizuia
Uprotestanti usienee kati ya Waortodoksi, hasa kwa kufaulu kumuondosha Patriarki
wa Kostantinopoli aliyetaka kuhalalisha ungamo la imani la Wakalvini. Idara ya
Papa ilistawisha pia misheni za Waoservanti chini ya utawala wa Waturuki, ambapo
wengi walifia dini. Vilevile Wakapuchini walienea sehemu hizo na Urusi. Katika
karne ya XVI Wafransiskani walichuma tunda bora India Kusini walipoungana na
Roma Askofu Msiro-Malabari na familia 30,000. Wariformati walifanya kazi miaka
160 Ethiopia wakamwaga damu yao kwa wingi wasikate tamaa.
Kuhusu
uenezaji Injili kwa wasio Wakristo, karne ya XVI na XVII zilikuwa na miito mingi
ya kimisionari, hata likatokea swali, “Je, Watumishi wanaweza kuzuia watawa
wasiende kwenye nchi za misheni?”. Kumbe karne ya XVIII wito huo haukuvutia
tena umati wa ndugu wasio na kazi, hata swali likawa tofauti kabisa, “Je,
Watumishi wanaweza kuagiza watawa wao waende Amerika?”. Mkuu wa OFM alifikia
hatua ya kutangaza atawatenga na Kanisa watakaozuia watawa wasifuate wito huo.
Kwa kuwachagua na kuandaa vilikuwa muhimu vyuo vya kimisionari, hasa miito hiyo
ilipopungua: pamoja na kuwakusanya, kazi yake ilikuwa kuwafundisha lugha na
kuwalea kiroho na kichungaji. Mara kwa mara Wakapuchini walisita kukubali
misheni za mbali kwa kuhofia mazingira yatafanya watawa washindwe kufuata maisha
ya shirika yaliyopangwa mtindo mmoja; pia umbali utamzuia Mkuu asiwatembelee
kama desturi: ndiyo sababu hawakuanzisha miundo ya kudumu huko.
Upande
wa Asia, Waturuki Waosmani walipoteka Yerusalemu (1517) walifunga
wamisionari wote kwa miaka mingi, wakaendeleza dhuluma za kila aina pamoja na
kuchochea ushindani na Waortodoksi kuhusu kumiliki mahali patakatifu hata
kusababisha wauane nao. Utaifa uliwavuruga vilevile. Wafransiskani walianzisha kanda huko India
(1583) wakazidi kuenea Mashariki hadi Indonesia walipoanzisha kanda nyingine
(1622). Misheni za Filipino ni sifa kubwa ya Pekupeku walioanzisha kanda huko
(1586) na kulipatia Kanisa (kwa msaada hasa wa Wajesuiti) nchi kubwa pekee ya
Kikatoliki katika Asia nzima. Toka huko wakaenea katika nchi zote za kandokando
kuanzia China, walipoongoa mtu aliyekuja kuwa Askofu Mchina wa kwanza. Ila
mabishano yao na Wajesuiti kuhusu mbinu za umisionari yalikwaza sana hata kudai
Papa aingilie kati. Dhuluma zilipoanza (1723), thuluthi moja ya Wakatoliki
300,000 wa China walikuwa chini ya Ndugu Wadogo, ambao wakafichama na kuendelea
na kazi yao, bila ya kujali jela na kifo, kama walivyofanya pia Vietinamu na
Kampuchia. Hata Japani ulizuka ushindani na Wajesuiti, halafu dhuluma kali za
serikali, lakini umisionari ukaendelea na kuongoa wengi zaidi. Baada ya
Wafransisko 354 wa Utawa I na III kufia dini, waamini wakaendelea kwa siri bila
ya mapadri: wamisionari wapya walipofika (1865) wakakuta Wakristo wenye majina
ya Kifransisko! Upande wa Wakapuchini walianzisha misheni India (1632) ambapo
walishindana na Wajesuiti kuhusu madhehebu ya Kimalabari hadi mwaka 1744. Sifa
kubwa zaidi ilipata misheni ya Tibet (1707-1745) iliyoeneza Injili hadi Nepali,
Butani na Bengala.
Tofauti na India, Afrika na Brazili (zilizokabidhiwa
na Papa kwa Wareno), sehemu nyingi za Amerika zilikabidhiwa kwa Wahispania.
Kanda OFM ya visiwani ilizidi kustawi hata watawa wake kufanya kazi ngumu
Venezuela na Guyana (1540); baada ya majaribio kadhaa wakafaulu kupenya kati ya
wazalendo wa Panama halafu kuenea Kolombia, ambapo hadi mwisho wa karne ya XVI
walibatiza Wahindi Wekundu 200,000. Wakati huo barani kulikuwa na kanda yenye
ndugu 145; miaka 100 baadaye walikuwa 338. Wafransiskani 2 walifika Mexico
pamoja na wavamizi (1519), lakini kazi rasmi ilianza miaka 5 baadaye,
walipotumwa Waguadalupe 12 walioandaliwa vizuri; hao wakatunga sarufi, kamusi na
katekisimu kwa lugha ya Kiazteka na kuanzisha shule. Watu waliongoka kwa wingi
mkubwa ajabu: 200,000 hadi mwaka 1529, 1,000,000 hadi 1531, 5,000,000 hadi 1536,
9,000,000 hadi 1540 (Wamersedari, halafu Wadominiko na Waagustino walisaidia
pia). Ndugu Wadogo walienea Kusini (1525) hadi Gwatemala, Honduras na Nikaragua,
na Kaskazini (1527) katika maeneo ambayo sasa ni Marekani Kusini. Kanda ya
Mexico iliyoanzishwa mwaka 1535 ikazaa nyingine 7 hadi Marekani Kusini (1612).
Pekupeku pia walianzisha kanda (1599). Mwisho wa karne ya XVII kulikuwa na
Wafransiskani 2,400, wengi wao wakiwa wananchi. Wavamizi wa Peruu pia
waliongozana na Wafransisko katika safari ya kwanza (1527), halafu wakaletwa
“mitume 12” waliofanya kazi bora Meksiko (1531), wakifuatwa na wengine wengi
kutoka Hispania hata ikaundwa kanda (1553) ambayo nyumba yake mojawapo ilifikia
kuhudumia parokia 29 kati ya Wahindi Wekundu: Wafransisko 129 waliuawa nao.
Mjini Lima ilianzishwa konventi kubwa ya malezi kwa wamisionari wa Amerika
Kusini karibu nzima. Mapema waliingia Ekwador (1533) wakaunda kanda (1565),
sawasawa na walivyofanya Chile, ingawa huko hawakuongezeka sana kwa sababu wengi
waliuawa katika mapigano ya muda mrefu ya wenyeji dhidi ya wakoloni. Toka Peruu
Ndugu Wadogo walifanya umisionari kati ya Wahindi Wekundu wa Bolivia pia hadi
mwaka 1793. Walikuwa pia wa kwanza kufika Amerika Kusini Mashariki (Paragwai,
Ajentina na Urugwai) ilipoanzishwa kanda (1612). Huko Brazili, kwa miaka 100
Pekupeku walianzisha kanda mbili (1657, 1675). Katika karne ya XVII waliingia
pia Wakapuchini na Waoservanti kufanya kazi hasa kwa Wahindi Wekundu, halafu kwa
Wanegro na Wazungu. Wafransiskani wengine walifanya kazi katika makoloni ya
Waingereza Marekani Magharibi, ingawa mmojammoja tu, halafu Wakapuchini
waliingia katika makoloni ya Wafaransa visiwani, Guyana na Marekani ya Kati
(1722), wakafanya kazi miaka mingi Panama, Haiti, Trinidad n.k. Hata Kanada
wamisionari wa kwanza walikuwa Ndugu Wadogo (Warekoleti kuanzia mwaka 1615,
halafu Wakapuchini): misheni zao zilifungwa kila mara maeneo ya Wafaransa
yalipotekwa na Waingereza.
Upande wa Afrika, misheni ya Moroko iliendelea hadi alipouawa Mfransiskani
wa Italia (1532) ikafunguliwa tena na Wakapuchini (1624-1700), wakifuatwa na
Pekupeku (kuanzia 1630). Huko Tunisia Wakapuchini walipojaribu mara ya pili
walifaulu kufungua nyumba (1674). Huko Libya Wariformati (1630), halafu
Wakapuchini waliendelea muda mrefu kwa matunda mengi. Huko Misri Wafransiskani
waliendelea hadi karne ya XIX. Afrika Magharibi (Gine, Kepuvede, Siera Leoni)
walifanya kazi zaidi Wakapuchini (kuanzia 1634), ingawa walifukuzwa mara kadhaa.
Wafransiskani walianzisha misheni ya kudumu Kabo Verde (1656), iliyoeneza kazi
yake hadi Siera Leoni. Misheni bora ni ile ya Wakapuchini Kongo-Angola
(1645-1835), ingawa kulikuwa na matatizo mengi (kwa miaka 100 walifia huko
wamisionari 144). Aliyeianzisha alikubaliwa kufungua nyingine Nijeria
(1651-1693). Wakapuchini walianzisha misheni nyingine ya kudumu katika kisiwa
cha Saotome (1686) wakihudumia hata Wakristo wa pwani.
Mtaguso wa Trento ulikuwa fursa kwa kila shirika
kutambulisha wasomi wake. Ndugu Wadogo waliuchangia sana kupitia Maaskofu na
wanateolojia waliohudhuria: Wakonventuali 67, Waoservanti 57 na Wakapuchini 8.
Idadi inaonyesha kuwa upande wa masomo, waliofanya juhudi zaidi ni Wakonventuali,
kwa kuwa hawakupatwa kamwe na wasiwasi wa marekebisho yote kuhusu hatari zake.
Labda ndiyo kazi kubwa zaidi waliyolifanyia Kanisa, hasa kama washauri wa Idara
za Mapapa na kama waandishi wa vitabu. Hata Waoservanti, walipoondoa wasiwasi
huo, wakaona masomo kuwa kazi ya lazima kwa shirika, wakaendelea sana katika
elimu (karne ya XVI na XVII). Kati ya Wakapuchini elimu ilishirikishwa kibinafsi
tu, wasianzishe nyumba za masomo mpaka Mtaguso huo ulipolazimisha kuyapanga.
Hapo wakasisitiza ndugu wasisome kwa ajili ya elimu, bali kwa kujirekebisha na
kurekebisha wengine. Kwa jumla Ndugu Wadogo, hasa Italia, walikwepa vyuo vikuu
na digrii mpaka Sisto V, katika jitihada zake kwa ajili ya Wakonventuali wenzake,
alipoanzisha (1587) Chuo cha Mt. Bonaventura kama kiini cha shirika lao upande
wa elimu. Mwalimu huyo na M.H. Yohane Duns Scoto ndio waliofuatwa zaidi na Ndugu
Wadogo wa karne hizo, ingawa hakuna aliyetangazwa rasmi kuwa afuatwe na shirika
katika falsafa na teolojia. Katika nusu ya kwanza ya karne ya XVII walimtetea
sana Scoto dhidi ya mashambulizi ya Wadominiko (washabiki wa Mt. Thoma wa Akwino),
hata baadhi wakajaribu kumfanya atangazwe hivyo ili shirika lijitukuze kwa
wataalamu wake kama mengine yalivyofanya. Mabishano hayakusaidia kujua ukweli,
bali yalijenga ukuta kati ya mashirika hayo mawili yenye udugu wa asili.
Hatimaye mkutano mkuu ukahimiza (1651) uhusiano mzuri na Wadominiko katika
elimudini, shetani asiachiwe nafasi ya kufitini. Wakonventuali na Waoservanti
waliujali sana muziki pia, kinyume cha Wakapuchini na Wariformati.
1.3.
NDUGU WADOGO KATIKA ULIMWENGU WA KISASA (1762–2005)
1.3.1. MATATIZO YA NDANI NA YA NJE (1762–1869)
Ongezeko
la watawa lilifikia kilele chake kati ya mwaka 1760 na 1770, likishinda vizuio
vilivyowekwa na viongozi wa Kanisa. Kama kawaida, shaka zilizosababishwa na mageuzi ya
harakaharaka katika jamii na uchumi zilichangia pia ongezeko la miito ya
wasiwasi yenye kutafuta usalama konventini. Kadiri hiyohiyo ilionekana wazi kuwa
wingi si hoja na kuwa umati wa watawa haukuhuishwa na vipeo halisi. Uvivu
haukuepukika ukazaa ulegevu na maovu mengi. Ingawa watu wadogo waliendelea
kuwaheshimu watawa, wasomi walizidi kuwaona vielelezo wa tunu zisizo na maana
tena. Jamii ilipokuwa inaelekea kasi matazamio mapya hata upande wa dini, watawa
walizidi kujitenga konventini wakijali desturi zao na elimu yao ya kidini bila
ya mawasiliano na elimudunia. Kati yao wachache tu walijitahidi kulinganisha
imani na sayansi.
Kwa
muda mfupi mashirika, hasa ya Ombaomba, yalikuja kudharauliwa na wengi.
Kufuatana na mawazo mapya kuhusu uchumi, serikali zilizidi kuyatazama kama mzigo
au donda kwa jamii. Bahati mbaya, hali ya mashirika ilistahili lawama nyingi
zilizotolewa. Sababu nyingine zilizoleta dhoruba juu ya watawa ni kwamba
serikali zilitamani mali za mashirika yao, na maadui wa Kanisa waliwafanya
shabaha ya kwanza, kwa kuwa kila mara ndio wanaohakikisha zaidi uimara wa
ukatoliki chini ya Papa na dhidi ya utaifa (ambao wakati huo ulichochewa na
serikali na kupendeza Maaskofu wengi). Ukweli wa dhati ni kwamba Mungu alitaka
kutakasa watu aliowakusudia wawe moyo wa Kanisa.
Katika
barua rasmi za miaka hiyo, Watumishi wakuu waliweka wazi matatizo yaliyokuwepo (utaifa,
ugomvi, uchu wa vyeo, wivu, malezi ya kulipua, kujiingiza katika masuala ya
siasa, utovu wa unyofu na unyenyekevu, utovu wa usafi na nidhamu) pamoja na
utabiri wa dhoruba ijayo. Ugumu wa hali unaonekana pia katika miundo mikuu ya
utawa kwenda kinyume cha kawaida: OFM toka 1791 karibu mfululizo iliongozwa na
Watumishi wakuu Pekupeku na Mriformati badala ya Waoservanti (waliokuwa na
msimamo laini); vilevile Wakapuchini toka 1754 hadi 1789 waliongozwa karibu
mfululizo na wasio Waitalia (tofauti na wanashirika wenzao, watawa wa nchi hiyo
walikuwa wakiridhika zaidi na hali ya shirika na kupinga urekebisho). Pia
mikutano mikuu haikufanyika muda mrefu: katika OFM tangu 1768 hadi 1856; kwa
Wakonventuali tangu 1789 hadi 1847. Iliwabidi Mapapa wateue Watumishi wakuu.
Utatuzi
ulijaribu kuelekea pande mbili: urekebisho wa hiari (kwa watawa wenyewe kujituma,
hasa kwa kuanzisha makao ya upwekeni) na wa lazima (kwa viongozi kuimarisha
nidhamu). Upande wa urekebisho wa hiari, kwa Waoservanti makao ya upwekeni
yalikuwepo rasmi na kuhitaji kuhuishwa tu; kumbe matawi mengine hayakuwanayo.
Watumishi wakuu wa Wakapuchini walijitahidi kuyaanzisha Italia na Hispania (huko
kwa jina la “vyuo vya kimisionari”, yaani vituo vya sala na malezi ambapo
watawa wajiandae kuhubiri) lakini walipingwa sana hata na washauri wao waliodai
eti, shirika linafuata kwa umoja katiba yake, hivyo kukubali urekebisho ni
kukiri limelegea; tena eti, anayetaka ukamilifu anaweza kuupata popote pale
shirikani, hakuna haja ya kujitafutia mazingira ya pekee. Zilipokosekana juhudi
za kutoka rohoni ililibidi shirika, hasa katika ngazi ya kanda, lidai vitendo
vya nje vilivyopangwa kikamilifu katika vitabu vya taratibu na desturi
vilivyoandikwa hasa wakati huo. Hivyo uaminifu ulidhaniwa kuishia katika
utekelezaji wa vipengele vingi hivyo, ambavyo tena viliachwa iwezekanavyo
vishikwe na vijana na mabradha, huku wengine wakijitafutia fadhili ili kuviepa.
Serikali
zilianza kuchukua hatua kali, zikidai haki ya kujihusisha na maisha yote ya
Kanisa. Kisha kuwafukuza Wajesuiti kutoka nchi mbalimbali (1759-1768)
zilimlazimisha Klementi XIV (1769-1774) kulifuta kabisa shirika lao (1773)
lililokuwa kizuio kikubwa kwa serikali kutawala Kanisa mahalia (Maaskofu
walikuwa wakiridhika au kunyamaza badala ya kutetea mamlaka ya Papa juu ya
majimbo yote duniani). Kuhusu mashirika mengine serikali (kuanzia Ufaransa,
1765) zilitumia mbinu ya kuanzisha “kamati ya urekebisho” chini ya Maaskofu,
zikificha hivyo malengo halisi. Hizo kamati zilitunga sheria za kunyongea
mashirika: kupunguza au kufunga konventi zote za sehemu fulani au za aina fulani,
kukataza kuombaomba, kupandisha umri wa kuingia unovisi, kupanga idadi yao, na
hasa kuzuia mahudhurio katika mikutano mikuu kwa kudai mikutano ya kitaifa tu,
vilevile katiba ya kitaifa badala ya ile ya shirika lote, uongozi wa kitaifa
usio chini ya ule wa shirika lote, kukataza kukata rufaa kwa Papa n.k. Tukiondoa
Dola la Kipapa, nchi zote za Ulaya zilipanga kunyonga mashirika. Kwa miaka 13
Ndugu Wadogo wa Ufaransa walipungua 3,756; kwa miaka 9 Hispania walipungua
5,582; kwa miaka 28 Polandi watawa walipungua asilimia 67! Chini ya siasa hiyo
mashirika yalielekea kwisha bila ya sifa.
Kumbe
mapinduzi ya Kifaransa yalipoanza kutumia nguvu zaidi na kuamua
kufuta mashirika yote (1790) watawa wengi walipata taji la kifodini. Kisha
kutupwa nje ya konventi, walipaswa kuchagua kati ya kula kiapo haramu cha kutii
serikali badala ya Papa, au kuhama nchi au kukatwa kichwa. Wengi walikubali kwa
furaha mwaliko wa kuacha utawa na kupewa pensheni; lakini wengiwengi pia
walikwenda kuishi kitawa hasa Amerika, au walitoa uhai wao ili kutetea haki za
Kanisa: kati ya wafiadini hao Wafransisko ni zaidi ya 250. Jeshi la Ufaransa
llilipovamia karibu Ulaya nzima, sheria za namna hiyo zilienezwa Ubelgiji
(1796), Italia Kaskazini-Magharibi (1802), Ujerumani Magharibi (1803), Italia
Kusini (1809), Hispania (1810). Hata nchi nyingine za Ulaya ya kati zilifuta
mashirika au kuyabana zaidi. Katika kipindi hicho waliishi watakatifu Egidi
Maria wa Mt.Yosefu (+1812), Pekupeku ombaomba, na Yohane wa Triora, Mwoservanti
aliyefia dini China (+1816). Akaja kufuata Mkapuchini Mt. Fransisko Maria wa
Camporosso (+1866), bradha ombaomba mwenye upendo mkuu. Pia kuna wenye heri 25.
Wafaransa
waliposhindwa, mkutano wa amani wa Vienna (1815) uliamua kurudisha iwezekanavyo
hali iliyokuwepo Ulaya kabla ya mapinduzi. Hata mashirika wakajaribu kufanya
hivyo, lakini haikuwa rahisi. Mawazo ya mapinduzi yalikuwa yameenea, yakidai
uhuru na maendeleo. Watawa waliozoea kwa miaka kadhaa kuishi mmojammoja
ulimwenguni, walipolazimishwa na Kanisa kurudi konventini hawakukubali tena
nidhamu ya nadhiri. Pia ilikuwa vigumu kwao kuishi pamoja kutokana na misimamo
yao tofauti kuhusu mapinduzi. Wasiwasi kuhusu kesho ukaendelea pia kwa sababu
serikali mpya zilikuwa na siasa ileile ya kabla ya mapinduzi, hivyo mashirika
yakaanza tena kufutwa: Urusi, ukiwa na Polandi chini yake (1831 hadi 1864),
Ureno (1832-1890), Hispania (1836-1880), Italia Kaskazini Magharibi (kuanzia
1855), Italia nzima (kuanzia 1866), Ujerumani (1871-1875), Ufaransa (1880 kwa
muda mfupi, tena kuanzia 1903). Wakati huo makoloni ya Amerika ya Kilatini
yalijipatia uhuru (1820-1824): watawa wananchi walisimama wote upande wa
mapinduzi, kumbe wamisionari (hasa Wahispania) waliyapinga wakateswa hadi kuuawa.
Baada ya ushindi jamhuri mpya pia zilianza kudhulumu mashirika hata karibu
kuyakomesha (k.mf. Brazili konventi zote ziliagizwa kufungwa mwaka 1822, Mexico
mashirika yote yalifutwa mwaka 1855). Hivyo kila yalipotaka kuinuka, mashirika
yalikumbwa na matatizo mapya. Hatimaye yalijikuta mali zake zimepungua sana, na
wanashirika vilevile, lakini waliobaki wametakaswa kiasi kikubwa.
Kwa
jumla, si wengi sana waliofurahia hatua za serikali kuwaondoa utawani, ingawa
katika nchi nyingi walipewa pensheni. Kati yao mapadri walifanya kazi ya
kichungaji jimboni, na baadhi wakawa Maaskofu; mabradha walitoa huduma katika
sakristia au hospitali, ila wengine walirudi kwa ndugu zao. Idara ya Papa kwa
Watawa ilitoa miongozo kuhusu hali yao na uhusiano na shirika, ikiwahimiza daima
waishi kijumuia kadiri iwezekanavyo. Ndizo juhudi za Watumishi wakuu pia, ingawa
waliona ugumu wa kuzitekeleza. Mang’amuzi ya maisha ya nje, yasiyo na hakika
kiuchumi, yaliwasaidia watawa kuelewa watu wa kawaida, ambao si wakulima hasa
kama zamani, bali umati wa wafanyakazi wenye kudhulumiwa na ubepari katika nchi
za viwanda. Wakiishi ulimwenguni hasa Ndugu Wadogo waliacha usomi wao na tabia
nyingine za tabaka la juu walizokuwanazo, wakajenga uhusiano mpya na watu na
kuwajibika kuwasaidia hata kijamii. Miaka ya kukaa nje ya konventi ndiyo miaka
ambapo mashirika mengi ya huduma yalianzishwa na watawa hao.
1.3.2.
UKARABATI (1869-1962)
Maisha
ya kitawa yalipoanza kuruhusiwa tena, waliojitahidi kufufua mashirika yao
hawakufikiria kutekeleza karama asili katika mazingira mapya, bali kukarabati tu
kilichobaki cha karne iliyopita. Waliridhika kujiona wanashangiliwa bado na watu
wema wengi, bila ya kujali jamii inavyozidi kusogea mbali na tunu zao. Hivyo
katika malezi wakasisitiza mambo yaleyale ya zamani hasa katika nchi (k.mf.
Italia) ambapo miaka ya utawa kuzuiwa haikuwa mingi. Ndugu Wadogo waliweza
kupata kwa urahisi miito ya kibradha, ila si ya kipadri, kwa kuwa wengi hawakuwa
na elimu au ilikuwa tofauti na ile iliyodaiwa na Kanisa. Tena, waliokuwa
wamesoma waliona wazi mbele yao njia za kufanikiwa ulimwenguni, na hawakuweza
kufuata mitindo ya malezi ya kitawa iliyokuwa ileile ya zamani, yenye
kusawazisha mno watu wenye vipawa tofauti. Basi, miito ikatafutwa kati ya watoto
wa familia bora za wakulima wasioweza kuwasomesha: kwao ilikuwa heshima kuwa na
mtoto padri mtawa. Ndivyo zilivyoanza (1869) seminari za kiserafi ambazo, baada
ya kupingwa na watawa wazee, zikaja kuenea haraka na kuhimizwa rasmi katika
matawi yote. Hapo muundo mzima wa malezi ukaja kubadilika, kwa kupatikana
madarasa ya vijana wa kuongozana kuanzia umri wa miaka 11-12 hadi upadri,
wakipata malezi yote utawani na hivyo kufyonza desturi, misimamo, mitazamo na
matarajio ya shirika. Hawakukosekana watawa maarufu waliopinga malezi ambayo
pengine haikuwa na maana tena wala ukweli na unyofu wa Kifransisko, ikitaka
kusawazisha wote katika mitindo ya nje, na kugeuza vijana kuwa wanasesere
wanaotenda lolote kwa kuongozwa. Hata hivyo seminari hizo ndogo zikawa mbinu kuu
kwa karibu miaka mia.
Jubilei
ya miaka 700 tangu azaliwe Mt. Fransisko (1882) iliadhimishwa kwa unyonge, lakini
Leo XIII (1878-1903) alitoa hati iliyohimiza kufufua miundo ya Kifransisko, hasa
Utawa III, dhidi ya ubinafsi unaotawala dunia. Miaka
miwili baadaye Wakapuchini wakaadhimisha mkutano mkuu muhimu sana, uliochukua
hatua mbalimbali na kumchagua Mtumishi mkuu bora aliyeongoza miaka 24 kwa
mafanikio makubwa katika yote, k.mf. wanashirika wakiongezeka kutoka 7,896 hadi
10,083. Mwaka 1889 Wafransiskani pia, baada ya kuongozwa miaka 20 na Mriformati
bora, wakafaulu kufanya mkutano mkuu uliotunga katiba kwa shirika lote, jambo
lililokusudiwa bure tangu mwaka 1517; hata hivyo Wariformati walidai ruhusa ya
kufuata pia sheria zao maalumu. Mwaka 1895 Leo XIII aliupendekezea mkutano mkuu
muungano wa matawi OFM uwe agenda kuu, na Kardinali akaeleza namna ya
kuyaunganisha. Waoservanti wote wakakubali, Warekoleti vilevile kwa sharti la
kutunza ufukara kwa uangalifu, kumbe Wariformati na Pekupeku walio wengi
wakakataa; jumla ya kura ikawa 77 ndiyo na 31 hapana. Basi kamati ikaandaa
katiba mpya iliyothibitishwa mwaka 1897, halafu Leo XIII akatangaza rasmi
muungano kamili wa matawi yote chini ya Mtumishi mkuu tu, ambao uonekane wazi
hata kwa nje (kanzu ya mtindo mmoja badala ya ainaaina na rangi ya kahawia
badala ya zile tofauti za awali: nyeusi, ya kijivu, ya zambarau na ya baharia).
Akaagiza kanda zisizokubali wasiweze kupokea wanovisi tena, na watawa binafsi
wasiokubali wapangiwe nyumba maalumu ambapo wakae wao tu, bila ya
kuchanganyikana na walioungana. Hata hivyo muungano haukufanikiwa vizuri;
Wahispania walikubali katiba lakini wakaendelea kujiongoza kitaifa hadi 1932;
hasa majaribio ya kuunganisha katika kanda moja Wafransiskani wa matawi
mbalimbali yalisababisha ushindani mwingi hadi juzijuzi. Hatimaye Wakonventuali
pia walianza tena kufanya mikutano mikuu (1891); mwaka 1904 wakamchagua Mtumishi
mkuu kutoka kanda ya Marekani, iliyoanzishwa 1872: hatua hiyo ilionyesha wazi
mwelekeo mpya wa kimataifa.
Jubilei
ya miaka 700 tangu shirika lianze (1909), iliadhimishwa kwa fahari zaidi,
kutokana na hali ya kutumainisha ya matawi yote. Ila lilizuka suala la uhalisi
wa shina na uongozi kuhusiana na Mt. Fransisko. Hapo Mt. Pius X (1903-1914) akatamka
kwamba, “Watumishi wakuu wa familia tatu za Kifransisko wako sawa kwa heshima
na mamlaka walizonazo, nao watazamwe sawia kama makamu na waandamizi halisi wa
Mt. Fransisko, kila mmoja katika familia yake... Mashirika matatu ya familia ya
Ndugu Wadogo ni kama matawi matatu ya mti uleule, ambao mzizi na shina lake ni
Mt. Fransisko, na viungo vyake ni Ndugu Wadogo kwa haki kamili na sawia”.
Vita
vikuu vya kwanza (1914-1918) na Mkusanyo wa Sheria za Kanisa (1917) havikuleta
mabadiliko makubwa utawani. Jubilei ya kifo cha mwanzilishi (1926) ilichochea
Wafransisko wote; hali ilikuwa tofauti na karne iliyopita, kwa sababu ya
kujitolea sana hata kijamii, jambo lililowafanya waheshimiwe upya na
Waprotestanti na waasi wa dini pia. Hata hivyo katika nchi chache dhuluma
zikawajia tena: kwanza Mexico (1926-1932), halafu Hispania (1936-1939),
walipouawa Ndugu Wadogo 320 na Wafransisko wengine 88. Baadaye vikazuka vita
vikuu vya pili (1939-1945) vilivyoharibu sana hasa Ulaya ya Kati na kanda zake.
Lakini
mabaya zaidi yakafuata Ulaya Mashariki ukiwa chini ya Ukomunisti ambao, pamoja
na kueneza mafundisho ya wakanadini na kupotosha maadili, pengine ulifuta
mashirika yote, pengine uliyawekea vizuio vingi. Kumbe Magharibi tunu nyingi
zikaja kufifia kadiri uchumi ulivyostawi na kuleta anasa. Watawa wote na Kanisa
zima wakajiuliza upya kuhusu maana ya uwepo wao katika ulimwengu wa kisasa.
Majibu yakawa tofauti, na vizazi vikabishana: katika hali hiyo M.H. Yohane XXIII
(1958-1963) aliitisha Mtaguso II wa Vatikani (1962-1965).
Ingawa
kesi za kutangazia watakatifu zinachukua kwa kawaida miaka mingi, baadhi ya
ndugu wa kipindi hicho wameshafikia hatua hiyo. Kuna Wafransiskani wanane waliofia dini China
(1900): Maaskofu Gregori Grassi, Francesco Fogolla na Antonino Fantosati, halafu
mapadri Elia Facchini, Teodoriko Balat, Giuseppe Maria Gambero na Cesidio
Giacomantonio, hatimaye bradha Andrea Bauer. Wakapuchini wako watatu: bradha
Konrado wa Parzham (+1894), bawabu; halafu mapadri Leopoldo Mandich (+1942) na
Pio wa Pietrelcina (+1968), mashujaa wa kitubio. Mkonventuali ni mmoja,
Maksimiliani Maria Kolbe (+1941), shahidi wa upendo katika makambi ya maangamizi
ya Wanazi. Wenye heri wako 50, wengi wao wakiwa wafiadini.
1.3.3.
CHANGAMOTO YA MTAGUSO II WA VATIKANI (1962-2005)
Mtaguso
huo ulisisitiza kweli za kudumu na kuelekeza namna ya kukabili kichungaji
ulimwengu wa kisasa. Kwa ajili hiyo watawa pia walidaiwa kujirekebisha upya,
hasa kiroho. Ndugu Wadogo, sawa na watawa wote, walipaswa kurekebisha katiba zao
pia kwa kutoa wote maoni yao, kufanya mikutano mikuu na majaribio mbalimbali.
Kazi hiyo ilichukua miaka mingi kuliko ilivyotarajiwa, kwa kufikiria upya
vipengele vyote vya maisha ya Kifransisko. Kwa mara ya kwanza mabadiliko ya
katiba yaliwekwa mikononi mwa wanashirika, kwa kujali wingi si ubora wao, basi,
iliwezekana kufuta harakaharaka mambo yaliyowashinda wengi, bila ya kujali kama
yanafaa bado au la. Halafu wasiwasi uliokuwepo kabla ya Mtaguso ulilipuka na
kusababisha wengi wapotewe na dira hata katika imani na maadili. Matokeo yake
wengi waliacha utawa na upadri. Wengine walibaki pasipo msimamo, kwa kuona mengi
ya zamani yamebadilishwa na mapya ni ya muda (yamekubaliwa kwa majaribio).
Ratiba ya sala ilipunguzwa sana, kama si kuachwa kabisa. Utafiti uliofanywa na
uongozi wa Wakapuchini ulionyesha kwamba wanashirika walio wengi wasingeshauri
kijana kujiunga nao. Ndiyo sababu, pamoja na miito kujitokeza kwa nadra Ulaya,
idadi ya Ndugu Wadogo ikapungua haraka tangu mwaka 1963 (OFM) na 1964 (OFMCap);
kumbe Wakonventuali walipungua haraka kati ya 1968 na 1975, halafu wakaanza
kuongezeka polepole sana.
Wengine
wasioridhika na mabadiliko hayo, baada ya kunyimwa na Watumishi wao uhuru
waliotaka kwa kufuata maisha ya kijumuia ya Kifransisko zaidi, wakaamua
kuanzisha matawi mapya. Wakapuchini kadhaa (wakifuatwa na Wafransiskani pia)
wakaanzisha Ndugu Wadogo Wapya huko Italia (1972) na Ndugu Wadogo Wamisionari
huko Brazili (1973). Akielewa nia yao njema katika hali ya fujo iliyotanda,
Paulo VI (1963-1978) aliwakubalia wabaki na nadhiri zao kuu baada ya kuacha
shirika walipoziweka. Wakapuchini wengine wa Italia walianzisha Ndugu wa Mt.
Fransisko (1983), na wa Marekani Wafransisko wa Upyaisho (1987). Hatimaye
Wakonventuali kadhaa wa Italia na Filipino wakaanzisha Wafransisko wa Imakulata
(1990) kwa ruhusa ya pekee ya Yohane Paulo II (1978-2005) iliyowafanya mara moja
kuwa shirika la Kipapa. Huko na huko kuna makundi mengine madogo, na akina dada wanaoyafuata kwa
kushika vilevile kanuni ya Utawa I. Juhudi za kuyaunganisha zimeshindikana kwa
kuwa yana sura tofauti. Kwa jumla mashirika hayo hayakuongezeka sana. Hata hivyo
uwepo wake umekuwa changamoto kwa matawi makubwa ambayo yakaanza kujirudi
kidogo, baada ya kupungukiwa na wengi wasiokuwa na msimamo pamoja na kutambua
matokeo ya majaribio yaliyofanywa; shida ni kwamba kujirekebisha baada ya
kulegea sana si rahisi, hasa kama kazi hiyo inahusu idadi kubwa ya watu.
Polepole
karama ya mwanzilishi na ya kila tawi ikaja kuzingatiwa tena kwa furaha, badala
ya kujali masuala ya miundo tu. Mambo mengi yaliyosahauliwa kwa karne kadhaa
yakaja kuonekana muhimu hasa leo, kama vile roho ya kanuni (udugu na udogo)
kuliko mtazamo wa kisheria uliotawala matamko ya Mapapa wa zamani; au usawa wa
watawa wote bila ya tabaka; au uwajibikaji wa kila mmoja katika uendeshaji wa
jumuia, kanda na shirika; au umuhimu wa mikutano, kuanzia ngazi ya nyumba
(ambapo ulikuwa umebaki kwa Wakonventuali tu). Wakati huohuo mabishano kati ya
matawi yakapungua sana kwa njia ya ushirikiano wa kidugu mkubwa zaidi na zaidi
katika ngazi zote. Hatimaye katiba zikaja kuthibitishwa na Kanisa kulingana na
toleo la pili la Mkusanyo wa Sheria zake kwa Walatini (1983). Utulivu upande huo
umeleta msimamo mkubwa zaidi kwa viongozi na kwa wanashirika jumla: kinadharia
njia imeeleweka; sasa kazi ni kuifuata hadi mwisho.
Baada
ya Ukomunisti kuanguka (1989) matawi yote yamejitahidi kujiimarisha Ulaya
Mashariki walipopata tena nafasi ya kuhubiri na kupokea miito, ambayo huko ni
mingi. Mungu anazidi kuongoza historia yetu.
Kati ya 1762 na 1889 dhuluma zilifyeka idadi ya Wafransisko kwa asilimia 82.1 na kufuta kabisa kanda nyingi (Ufaransa zote 32!) na kuziacha nyingine hoi. Hata hivyo, kanda chache zilistawi, kwa kuwa mawazo ya uhuru kwa wananchi yalikomesha dhuluma za kidini pale zilipokuwepo toka muda mrefu sana, hasa Irelandi na Uingereza. Kwa namna ya pekee mashirika yakaja kustawi Amerika Kaskazini walipohamia watawa wengi.
Baada ya dhuluma hizo kwisha, kadiri Ndugu Wadogo walivyorudi kupenya
maisha halisi ya Kanisa na ya jamii, walielewa ni tofauti sana na yalivyokuwa
kabla ya dhoruba. Iliwabidi kutumia ubunifu wa Kifransisko kuitikia mahitaji
mapya ya watu kwa utendaji usiozimika, ingawa ukatokea mgongano kati ya taratibu
za maisha ya kijumuia na madai ya utume huo.
Mahubiri yaliendelea kuwa njia kuu ya utume, sio tu katika wiki za
uamsho, maandalizi ya sherehe na mafungo, bali pia kwa njia ya vyombo vya
upashanaji habari: baada ya magazeti (la kwanza
lilianzishwa na Wakapuchini wa Ufaransa mwaka 1861; kufikia mwaka 1919 yalikuwa
164 tayari, halafu yakazidi tena), Ndugu Wadogo walifanya kazi katika redio na televisheni au kuzimiliki wenyewe. Katika nusu ya kwanza ya
karne ya XX utume wa maungamo ulishika nafasi kubwa hata kwa Wakapuchini, ambao
toka mwanzo hadi mwaka 1847 walikuwa wakizuiwa na katiba wasifanye kazi hiyo.
Nusu ya pili ya karne ya XIX na nusu ya kwanza ya karne ya XX juhudi za
Ndugu Wadogo zilizaa vyama vingi vya kitume. Kati ya vile vilivyoenea zaidi
tukumbuke kile cha Mashujaa wa Imakulata (1917) cha Mt. Maximiliani Maria Kolbe, na kile cha Makundi
ya Sala cha Mt. Pio wa Pietrelcina. Baadaye Ndugu Wadogo wengi wakaja kupendelea
matapo mapya ya kiroho, yaliyoanzishwa na walei, wakajihusisha nayo kuliko
walivyojihusisha na shirika lao, hata kusababisha swali: je, kwao ni muhimu
zaidi kuwa wanashirika au kufuata tapo fulani?
Utume wa kijamii ulipata sura nyingi kulingana
na mahitaji ya watu wadogo: huduma za huruma, mshikamano wa kutumia kiasi
(katika kunywa), upatikanaji wa kazi na vitendeakazi, vyuo kwa mabubu-viziwi,
benki, utume kwa wazururaji, kwa watu wa kuhamahama, na kwa wahamiaji wa nchi
zilizoendelea, huduma hospitalini n.k.
Baada ya vita vikuu vya pili, na hasa mara
baada ya Mtaguso, karama maalumu iliposahauliwa ili kujali zaidi upadri wa
mtawa, mashirika yalikimbilia utume wa mapadri wanajimbo kwa kupokea parokia
nyingi. Kumbe yalipokumbuka tena karama ya kitawa
yakaona ugumu wa kupunguza utume wa aina hiyo (kurudisha parokia kwa jimbo
lililopungukiwa mapadri). Hivyo, pamoja na uhaba wa miito yakajikuta yanalemewa
yasiweze kutua mzigo waliojitwisha.
Upande wa umisionari, katika karne ya XIX ukoloni wa Wazungu, waliokuja
kutawala maeneo makubwa duniani kote, ulifungua njia na milango kwa uenezaji wa
imani. Kanisa lilichangamkia tena kazi hiyo kuanzia Ufaransa, na kufanya mipango
mingi ya ushirikiano na wamisionari, hata kuanzisha miundo ya kimataifa ambayo
yakaja kuwekwa moja kwa moja chini ya Papa, na vilevile mashirika mbalimbali ya
kimisionari tu. Ndugu Wadogo walipoanza kuinuka baada ya dhoruba wakakuta juhudi
hizo zimeshaenea hata zikaja kufikia kilele chake kati ya vita vikuu. Basi
matawi yote matatu yakajitosa katika kazi hiyo, tena kwa upana na mpango kuliko
zamani. Kufikia mwaka 1934 Wafransiskani walishika
nafasi ya kwanza kati ya mashirika yote kwa wingi wa wamisionari (3,600). Pigo
kubwa lililowapata ni kufukuzwa wageni wote 550 waliokuwepo China katika majimbo
29 ya kwao (1949). Wakapuchini wamisionari waliokuwa 377 mwaka 1890,
wakaongezeka hadi kuwa 1,562 mwaka 1975, wengi wao Afrika, India na Indonesia.
Hivyo
kanda za Amerika ya Kilatini zikastawi (ndugu 1,600 wa mwaka 1905 wakawa 4,700
mwaka 1975); zikaanzishwa nyinginyingi Asia, na chache Afrika na Australia. Basi, kama inavyotokea kwa Kanisa lote, asilimia ya Wazungu shirikani
inazidi kupungua, kumbe ndugu wa kontinenti nyingine wanaongezeka. Kwa mfano,
kati ya Wakapuchini mwaka 1997 asilimia 15 walikuwa Amerika ya Kilatini, 14
Asia-Australia na 10 Afrika.
Takwimu ni kama ifuatavyo:
Matawi |
Mwaka
1762 hivi |
Mwaka
1889 hivi |
Mwaka
1964 hivi |
Mwaka
2005 |
(Waoservanti) |
39,900 |
6,200 |
|
|
(Pekupeku) |
7,000 |
900 |
|
|
(Wariformati) |
19,000 |
5,700 |
|
|
(Warekoleti) |
11,000 |
1,600 |
|
|
OFM
jumla |
76,900 |
14,400 |
27,100 |
15,794 |
Wakonventuali |
21,000 |
1,500 |
4,800 |
4,595 |
Wakapuchini |
34,000 |
7,600 |
15,800 |
11,229 |
Waimakulata |
|
|
|
282 |
Jumla
kuu |
131,900 |
23,500 |
47,700 |
31,902 |
Upande wa elimu, kulingana na sheria za Kanisa, mipango ya masomo
imebadilika, miaka
ya falsafa na teolojia kwa ajili ya upadri imeongezeka, mbali ya seminari ndogo
kuna vituo vingi wanaposoma pamoja watawa wa mashirika mbalimbali na pengine
waseminari wa majimbo, kila tawi limeunda kituo kikuu cha malezi ya juu huko
Roma, ambapo kuna vyuo vikuu vya Wakonventuali (Seraphicum) na OFM (Antonianum),
na digrii kati ya wanashirika zimeenea.
2.
UTAWA
WA PILI
Mt. Klara, aliyejiita “mche mdogo wa Mt.
Fransisko”, ndiye jiwe la msingi la Utawa II ulioleta karama ileile ya Ndugu
Wadogo kwa wanawake na kwa kujifungia faraghani. Ndizo nguzo mbili za utawa huo.
Binti huyo wa ukoo bora alizaliwa Asizi
(1193). Kisha kuvutiwa na mifano ya Mt. Fransisko, na kusikiliza mahubiri na
mashauri yake, akaamua kujiweka wakfu kwa Kristo katika ufukara mkuu. Basi,
akatoroka nyumbani usiku (1212) akamuendea Mt. Fransisko huko Porsyunkula ambapo
alinyolewa naye na kuvikwa kanzu, kamba na shela nyeusi. Kesho yake asubuhi
akapelekwa kwa masista Wabenedikto, na baada ya wiki mbili kwenye monasteri yao
nyingine, alipofikiwa na mdogo wake (Mt. Anyesi) ambaye pia alipaswa kukabili
upinzani mkali wa ukoo wao. Mt. Fransisko alipomaliza kuandaa jengo la Mt.
Damiano, wakahamia huko kushika maisha ya ndani, wakaongezeka haraka. Miaka 40
baadaye Mt. Klara akaja kuandika kwamba mwanzo ulikuwa mgumu na walidharauliwa
sana. Mwaka huohuo (au ule uliofuata) mwanzilishi, alipoona walivyovumilia yote,
aliwaandikia kwa ufupi “mtindo wa maisha”. Wakati huo aliwaomba wamsaidie
kutambua kama Mungu anataka yeye na Ndugu Wadogo waishi upwekeni tu au wafanye
utume pia. Jibu likawa kwamba wakahubiri; lakini Mt. Klara na wenzake
watawafuata kiroho tu kwa sala na sadaka, wakichangia urekebisho wa Kanisa bila
ya kutoka nje ya kiota chao.
Baada
ya Mtaguso IV wa Laterano (1215) kukataza kanuni mpya iliwabidi wapokee mojawapo
ya zamani ili wakubaliwe na Kanisa kama watawa. Basi wakaichagua ile ya Mt.
Benedikto, wakiifuata katika mambo kadhaa kadiri yalivyopatana na mtindo wao
mpya, bila ya nia ya kuwa Wabenedikto. Hapo ilimpasa Mt. Klara kuitwa abesi,
jina alilolikubali tu kwa kumtii mwanzilishi, ingawa akaendelea kujiita
“mtumishi wa Kristo na wa akina dada fukara”. Hasa Mt. Klara hakutosheka na
uhalali wa monasteri yake mbele ya Kanisa, bali kwa njia ya Mt.Fransisko aliomba
akapewa na Inosenti III “fadhili ya ufukara” (1216), yaani ruhusa ya kuishi
bila ya mali hata kijumuia, kama jambo la msingi katika wito wake wa “kuishi
kadiri ya ukamilifu wa Injili takatifu”, kwa kuungana na Kristo fukara kama
bibiarusi fukara.
Kardinali
Ugolino, akiona monasteri za namna hiyo zinavyoongezeka huko na huko,
alizitungia katiba (1219) iliyopitishwa na Honori III (1216-1227) ambayo ikawa
msingi wa kanuni zote zilizoandikwa baadaye kwa Utawa II. Lengo lake lilikuwa
kukinga monasteri hizo dhidi ya upinzani na kuzipa mtindo wa kimonaki zaidi bila
ya kuondoa usahili wake maalumu, ziwe muundo mpya wa aina moja chini ya Kanisa
la Roma moja kwa moja. Katika juhudi zake za kurekebisha umonaki alielekeza hata
monasteri kadhaa za zamani zifuate mtindo wa Mt. Damiano. Desturi kali
alizoziagiza humo hazikumtisha Mt. Klara, ambaye alijishinda tayari na kujitesa
kwa ushujaa mkubwa (katika kula, kuvaa, kulala n.k.) mpaka akakatazwa
asizidishe. Wala hakuogopa ukali wa ugo ulioagiwa na katiba hiyo, ili kutunza
mazingira ya sala. Wasiwasi wake ulihusu ufukara mkuu akiona hautajwi na katiba
hiyo. Mwanzoni Ugolino alitaka msimamo huo udumu katika monasteri kadhaa, ila
alipochaguliwa kuwa Papa akaanza kuzipatia mali nyinginyingi, labda kisha
kung’amua matatizo yaliyojitokeza. Lakini Mt. Klara hakukubali kabisa
akamuomba amtibitishie “fadhili ya ufukara” akakubaliwa (1228), lakini si
kwa monasteri zote.
Suala
lingine lililojitokeza mapema, halafu likaendelea kusababisha migogoro, ni nani
awajibike kuwasaidia Waklara upande wa roho na upande wa riziki. Mt.
Fransisko alipokuwa Mashariki, nd. Filipo Longo aliteuliwa msimamizi wao, lakini
mwanzilishi aliporudi uteuzi huo ukafutwa, masista wakasimamiwa tena na wasio
Wafransisko, mpaka Gregori IX alipowalazimisha Ndugu Wadogo kuwajibika (1221).
Mt.
Klara alipoona wito wake wa Kiinjili upo hatarini upande wa sheria, kwa kuwa
kanuni na katiba hazikuwa za Kifransisko, akaanza kuomba aweze kuahidi kushika
kanuni ya Ndugu Wadogo badala ya ile ya Mt. Benedikto. Mwaka 1234 akaja kumuunga
mkono Mt. Agnesi wa Praha, binti mfalme ambaye alikataa kuolewa na mfalme mkuu
Federiko II wa Ujerumani akaanzisha monasteri yake iliyokubaliwa “fadhili ya
ufukara”. Alitunga kanuni mpya kwa kuchanganya “mtindo wa maisha”
alioandika Mt. Fransisko na katiba ya Ugolino, akamuomba Gregori IX, halafu
Inosenti IV waithibitishe, lakini akakataliwa. Kumbe Inosenti IV akathibitisha
katiba ya Ugolino (1245) na kusisitiza ifuatwe kanuni ya Mt. Benedikto
kwa sababu ina sifa nyingi. Wakati huohuo alijaribu kusuluhisha mgogoro wa
uhusiano kati ya Ndugu Wadogo na Waklara. Mt. Klara alikuwa akiendelea kudai kwa
nguvu msaada wa kiroho wa ndugu hao kulingana na ahadi ya mwanzilishi. Kumbe
Mtumishi mkuu Kreshensi wa Iesi aliomba shirika liondolewe mzigo liliobebeshwa
na Gregori IX, yaani himizo la kuanzisha konventi ndogo karibu na kila monasteri
ya Waklara. Basi, Inosenti IV aliamua Waklara wawe chini ya uongozi na mamlaka
ya Ndugu Wadogo, akapendekeza masista waunganishwe na Utawa I. Lakini shirika
likazidi kuona litalemewa na wingi wa monasteri.
Mwaka 1247
Inosenti IV akatunga katiba mpya badala ya ile ya Ugolino iliyokwishaenea katika
monasteri zote za Kifransisko, ikitumika pengine pamoja na desturi maalumu za
mahali. Katiba hiyo ilifanya kanuni ya Ndugu Wadogo kuwa msingi wa sheria za
Waklara bila ya kuwadai waishike katika yote, ila katika utiifu, utovu wa mali
na useja mtakatifu. Katiba hiyo ilimuondolea Kardinali mlinzi mamlaka juu ya
Waklara, ambao wakawekwa moja kwa moja chini ya viongozi wa Utawa I. Kwa katiba
hiyo Waklara wakaja kutambulikana Wafransisko kisheria, lakini ndani mlikuwa na
pigo kubwa kwa Mt. Klara, yaani iliandikwa wazi kuwa monasteri zao zinaruhusiwa
kuwa na mali za kujitegemea. Ndiyo sababu monasteri chache tu zikaipokea katiba
hiyo. Vilevile Ndugu Wadogo wakazidi kulalamika hadi Kardinali mlinzi
akajitwalia polepole mamlaka yao na hatimaye (1250) aliwaandikia wasithubutu
kujiingiza katika uongozi wa Waklara. Hivyo kwa muda mfupi katiba hiyo
ikashindikana pande zote.
Mt.
Klara, mgonjwa toka siku nyingi, alipoona kifo kinamkaribia, aliandika wasia
wake ambamo alimuiga Mt. Fransisko katika kukumbusha asili ya wito wake na wa
jamaa yake, na kutamka kwa msisitizo mkubwa nia imara ya kufuata ufukara mkuu
“aliouahidi kwa Mungu na kwa Mt. Fransisko” pamoja na kuhimiza sana umoja wa
dada zake. Lakini pia, upande wa sheria, aliona haja ya kutunga upya “mtindo
wa maisha” kwa kulinganisha kanuni ya Ndugu Wadogo na masharti ya maisha ya
ndani tu. Humo aliingiza pia maandishi mawili mafupi ya Mt. Fransisko kwao,
kuhusu ufukara mkuu na kuhusu ahadi ya kwamba yeye na Ndugu Wadogo watawahudumia
Waklara sawa na wenzao wa kiume. Upande wake Mt. Klara aliahidi kuwatii
waandamizi wa mwanzilishi. Kiini cha huo “mtindo wa maisha” kinasisitiza kwa
nguvu nia ya kuishi bila ya mali yoyote, isipokuwa monasteri na bustani. Jambo
lingine linalokazwa ni udugu: humo neno “dada” linapatikana mara 66! Udugu
huo unatimizwa siku kwa siku chini ya “abesi na mama” kwa umoja wa mioyo
pasipo ubaguzi wowote (tofauti pekee ni kati ya wanaojua na wasiojua kusoma
kuhusu Sala ya Kanisa). Hata dada “wa nje” (yaani “wanaohudumia nje ya
monasteri” bila ya kubanwa na ugo) washiriki maisha ya jumuia sawa na wenzao.
Hao ni kundi maalumu la mtindo wa Kiklara, linalohitajika kadiri wenzao
wanavyojifungia ndani: ni “akina Marta” kwa “akina Maria” kadiri Mt.
Fransisko alivyowapangia Ndugu Wadogo wanaoishi upwekeni. Udugu huo unajitokeza
hata katika mikutano, ambayo inatakiwa kufanyika kila wiki kwa mchango wa wote,
kupanga shughuli za maana na kuteua watakaoshika nyadhifa mbalimbali. Abesi
mwenyewe, ingawa anachaguliwa kwa maisha yake yote, kadiri ya mapokeo ya
kimonaki, anaweza kubadilishwa dada zake wakiona hawezi kutimiza vizuri kazi
zake. Uhusiano na Utawa I unasisitizwa tena kwa kudai msimamizi wa monasteri awe
daima Ndugu Mdogo, pamoja na kuomba Utawa huo uipatie monasteri mapadri 2 na
mabradha 2 kwa huduma za kiroho na za kimwili.
Huo
“mtindo wa maisha” ukakubaliwa na Kardinali mlinzi (1252) halafu na Inosenti
IV (1253). Mt. Klara akapewa hati yake kitandani akaibusu; siku mbili baadaye
akafa akiishika mikononi, wakihudhuria nd. Leo, nd. Angelo na nd. Ginepro wenzi
wa Mt. Fransisko; pia alijaliwa faraja za Bikira Maria na wanawake watakatifu
kadhaa. Mazishi yalihudhuriwa na Papa, Makardinali, Maaskofu na wengineo.
Inosenti IV alitaka ziimbwe sala za watakatifu mabikira badala ya zile za wafu,
ila akakubali shauri la Kardinali mlinzi la kufuata taratibu zilizopangwa kabla
mtu hajatangazwa mtakatifu. Miaka miwili baadaye, Kardinali huyo akiwa amepewa
Upapa kwa jina la Aleksanda IV (1245-1261), akamtangaza rasmi kuwa mtakatifu
(1255). Mwaka 1260 masalia yake yakahamishiwa mjini Asizi katika kanisa
lililojengwa kwa heshima yake.
Pamoja
na kanuni na wasia, Mt. Klara ametuachia walau barua nne (kwa Mt. Agnes wa
Praha). Maandishi hayo ndiyo chemchemi ya kwanza ambamo tuchote utajiri wa roho
yake na wa utu wake. Hasa ya mwisho inatuonyesha alivyogeuka ndani ya Yesu kwa
kuzidi kumkazia macho kama kioo chake na kujifunza toka kwake hasa ufukara,
unyenyekevu na upendo wa ajabu, vilivyong’aa katika hatua mbalimbali za maisha
yake kuanzia Bethlehemu hadi Kalivari. Mt. Klara alimfikia Mungu kwa kumfuata
Yesu kama bibiarusi mwaminifu katika hatua hizo za maisha yake halisi, kama
alivyoelekezwa na Mt. Fransisko, kadiri ya karama yake mpya katika kumtazama
Yesu na kuelewa Injili.
Katika
karne ya XIII monasteri chache ziliipokea kanuni ya Mt. Klara iliyothibitishwa
kwa ajili ya nyumba asili tu. Kumbe monasteri kadhaa zikaja kupokea kanuni
maalumu ambayo M.H. Izabela (+1270), dada wa Mt. Ludoviko IX mfalme wa Ufaransa,
aliiandika akakubaliwa na Aleksanda IV kwa monasteri yake ya Longchamp (1259).
Kanuni hiyo iliweka Waklara chini ya Ndugu Wadogo na kukubali mali na mapato ya
mara kwa mara.
Mwaka
1263 mkutano mkuu wa Ndugu Wadogo ulizidi kukataa wajibu wa kuwahudumia Waklara.
Akiwa Mtumishi mkuu, Mt. Bonaventura alijaribu kusuluhisha kwa kusema huduma za
kiroho kwa dada hao zinatokana na upendo, lakini si wajibu ambao waudai kwa
haki; pia zitegemee uamuzi wa Kardinali mlinzi. Kumbe mwaka huohuo Urbani IV
(1261-1264) alipitisha kanuni mpya ili kustawisha nidhamu na. umoja ikidai
monasteri hizo zote ziitwe Utawa wa Mtakatifu Klara (O.S.C.), kama ilivyoelekea
kufanyika baada ya kutangazwa mtakatifu. Kanuni mpya ilifuata kidogo ile ya
Klara, na zaidi katiba ya Inosenti IV, ikibana sana masista katika vipengele
vingi. Zaidi ya hayo ilipanga mali (mashamba na kodi zake) kuwa tegemeo la
kawaida la uchumi wa monasteri. Hatimaye iliwaondolea Watumishi wajibu wa
kuwahudumia Waklara. Kanuni hiyo ikakataliwa na monasteri bora na baadhi ya
Ndugu Wadogo. Hivyo ukatokea mgawanyiko unaodumu hadi leo kati ya Waklara
wanaofuata kanuni ya Mt. Klara (inayoitwa ya I) na wale wanaofuata kanuni ya
Urbani IV (Waurbani au wa kanuni ya II), na kufanana na Wakonventuali (ambao pia
wamekubali kuwa na mali kishirika). Kanuni nyingine zikaachwa kabla ya karne
kwisha. Kwanza ilienezwa sana ile ya Urbani, lakini ile ya mt Klara ikabaki huko
na huko ikiendelea kuathiri sana historia yote ya Waklara kwa kukumbusha tunu
asili na kuchochea marekebisho mengi kuliko yale ya Ndugu Wadogo, kutokana na
urahisi wa kubadili hali ya monasteri moja kuliko ya shirika kubwa
iliyotawanyika sehemu mbalimbali.
Tofauti
hizo hazikuzuia uenezi wa monasteri usiende kasi ajabu, kulingana na uenezi wa
Utawa I Ulaya na hata ng’ambo ya Bahari ya Kati. Kila monasteri ilijitegemea
kikamilifu; kilichowaunganisha ni hakika ya kutokana na moto ule uliowashwa na
Mt. Klara, uhusiano wa kiroho na Ndugu Wadogo na mamlaka ya Kardinali mlinzi. Kwa
kawaida monasteri zilikuwa na masista wengi sana. Miito mingi ilitokea kati ya
koo maarufu na za kifalme pia, hasa Urbani IV alipodai kila mtakaji alete
“mahari” monasterini, sheria ambayo ilienea kote. Karne ya kwanza ilizaa
watakatifu 4 (Klara na Agnes wa Asizi, Agnes wa Praha na Kinga wa Hungaria) na
wenye heri 6 katika nchi mbalimbali, hasa kutoka koo za kifalme. Halikukosekana
taji la ushahidi wa imani na wa ubikira (Waklara wote wa Tripoli mwaka 1289, na
wote 70 wa Tolemais mwaka 1291).
Takwimu
ni kama ifuatavyo:
|
Mwaka
1253 |
Mwaka
1300 |
Waklara |
|
Zaidi
ya 15,000 |
Monasteri |
111 |
413 |
Italia
+ visiwa |
68 |
196 |
Hispania
+ Ureno |
21 |
57 |
Ufaransa |
14 |
68 |
Ujerumani
+ Ulaya Mashariki |
8 |
46 |
Mashariki
+ Korasia |
|
23 |
Uingereza
+ Irelandii |
|
23 |
Karne
ya XIV ilileta ulegevu katika Utawa II, kama tulivyoona kwa ule wa kwanza, hasa
kutokana na wingi wa masista na wa mali. Walipokewa kwa urahisi wanawake
wasiofaa lakini wenye kuleta mahari kubwa, ambao waliingiza monasteri watumishi
wao binafsi, hata kuleta anasa, pengine kwa idhini ya Papa. Uovu ulizidi wakati
wa farakano la Magharibi na fujo iliyofuata. Hata hivyo si monasteri zote
zilipatwa kwa pamoja, kutokana na kila moja kujitegemea. Hazikukosekana pia
juhudi za kurudisha nidhamu zilizofanywa na wasimamizi wa Utawa I – ambao
Bonifas VIII (1295-1303) aliurudishia wajibu wa kuwahudumia Waklara (1296) –
na Makardinali walinzi na Mapapa wenyewe. Kati yao ni muhimu hasa Benedikto XII
(1334-1342), aliyekuwa mmonaki wa Citeaux, ambaye aliwapa Ndugu Wadogo katiba
(1336) ambayo sura yake mojawapo inahusu Waklara tu. Katiba yake ilibadili sura
ya monasteri. Kwanza ilipanga idadi ya juu ya masista katika kila monasteri;
pili ilisisitiza ugo wa Kipapa, taratibu za pamoja kwa wote, usimamizi mzuri wa
mali, katazo la pesa za binafsi na la dhuluma dhidi ya monasteri; tatu
alilazimisha hata dada waliohudumia nje ya ugo wabaki ndani na hivyo wakaja kuwa
tabaka la chini masista, wakiwatumikia wenzao bila ya kuwa na sauti mikutanoni
(ilikuwa hivyo kwa Wabenedikto, lakini ni kinyume cha udugu alioutaka Mt.
Klara); nne kwa huduma hizo za nje waliruhusiwa wanawake wasekulari wa kufaa;
tano vilikatazwa vyumba vya binafsi.
Jambo
lingine lililokuja kubadilishwa ni muda wa uongozi wa abesi, kwa kuzingatia
kwamba urefu wake unaweza ukafaa wakati wa juhudi, lakini unaweza ukasababisha
uharibifu wa kudumu ulegevu ukiingia. Mtindo wa maisha wa Mt. Klara hausemi
abesi adumu muda gani, ila unafuata kanuni ya Mt. Fransisko ukisema asipofaa
tena aondolewe, halafu achaguliwe mwingine. Lakini utekelezaji wake haukuwa
rahisi. Hivyo Inosenti VII (1404-1406) aliagiza (1405) abesi achaguliwe kila
baada ya miaka 10; baadaye muda ukapunguzwa tena hadi miaka 3. Lakini sheria
hizo hazikufuatwa popote, hivyo baadhi ya monasteri zikaendelea kumchagua abesi
hadi atakapokufa.
Pamoja
na juhudi hizo na nyingine za kurekebisha hali, historia ya watawa inaonyesha
kwamba nidhamu ya kuzalimishwa inaweza ikasidia kiasi, lakini haiwezi kuleta
hali mpya, kwa kuwa uhai unatoka ndani ya watawa wenyewe kwa kazi ya Roho
Mtakatifu. Si suala la miundo, bali la roho. Hata katika ulegevu wa karne ya XIV
mtindo wa maisha wa Mt. Klara ulivutia: kwa mfano malkia Sancha wa Napoli
(+1345), alipojifanya Mklara hakukubali kuingia monasteri ya fahari ya Mt. Klara
mjini, bali alianzisha nyingine ndogo fukara kwa kuita wamonaki toka Asizi na
kushika kanuni ya I. Huko na huko Ufaransa ilitokea vilevile. Katika
karne hiyo walipatikana wenye heri 3.
Takwimu
ni kama ifuatavyo:
|
Mwaka
1300 |
Mwaka
1385 |
Waklara |
Zaidi
ya 15,000 |
Zaidi
ya 15,000 |
Monasteri |
413 |
404 |
Italia
+ visiwa |
196 |
245 |
Hispania
+ Ureno |
57 |
51 |
Ufaransa |
68 |
39 |
Ujerumani
+ Ulaya Mashariki |
46 |
50 |
Mashariki
+ Korasia |
23 |
11 |
Uingereza
+ Irelandii |
23 |
8 |
Karne
ya XV hadi ya XVIII ziliona monasteri za Waklara kuhuishwa tena, kufuatana na
marekebisho ya Ndugu Wadogo (kama ilivyotokea kwa wanawake wa mashirika
mengine), halafu na Mtaguso wa Trento na maagizo ya Mapapa, lakini pia kutokana
na karama yenyewe ya Mt. Klara iliyojitokeza wazi katika kanuni yake. Toka
mwanzo utawa wake haukuwa tu muundo mpya wa kimonaki, bali mfumo mpya wa maisha
ya Kiinjili, ambao unadai kufuatwa, la sivyo monasteri hazitatulia, kama vile
Ndugu Wadogo.
Mwanzoni
mwa karne ya XV ulitokea urekebisho mkubwa kwa njia ya Mt. Koleta Boylet (+1447)
wa Corbie (Ufaransa). Baada ya kujifungia ndani amevaa mavazi ya Wafransisko
Wasekulari, alitokewa mara kadhaa na Mt. Fransisko na kuhimizwa arekebishe utawa
wake. Basi, akatoka (1406) akaenda kwa Papa wa Avignon (bila ya kutambua kwamba
ni wa bandia) akaweka mikononi mwake nadhiri ya kushika mtindo wa maisha wa Mt.
Klara, akafanywa naye abesi na mrekebishaji wa utawa wote wa Mt.Fransisko
(I-II-III), kutokana na karama yake wazi ya kurekebisha Kanisa kuanzia monasteri
na miundo mingine ya Kifransisko. Kwa neema ya Mungu na kwa msaada wa wakuu wa
dunia akaanza kutembelea Ufaransa na Benelux ili kueneza chachu ya Kiinjili,
hasa ufukara. Upande wa Waklara alirekebisha au kuanzisha monasteri 22 kufuatana
na kanuni ya I aliyoomba nakala yake halisi kwa monasteri mama ya Asizi.
Mwenyewe aliiongezea katiba iliyopitishwa na Mtumishi mkuu (1432) halafu
ikathibitishwa na Pius II (1458-1464). Humo alikataza mahari za masista, mali
yoyote na mapato ya hakika kwa monasteri, kodi na ghala za kutosha muda mrefu,
kila kitu cha thamani au kisicho cha lazima, majengo yasiyo duni. Aliagiza wote
wafanye kazi ili kupata riziki, bila ya kuagiza watu wa nje kwa kazi wanazoweza
kuzifanya wenyewe. Kwa udogo, alikataza baraka kuu kwa abesi na ibada ya kuweka
wakfu mabikira. Hata hivyo alisisitiza usafi na masomo na kupunguza masharti ya
ugo. Kwa ajili ya upendo wa kidugu alifuta matabaka, aliagiza vipindi vya
burudani (maongezi), alisisitiza mikutano ya kila wiki, alionyesha tena kuwa
wadhifa wowote ni utumishi tu. Ingawa alikubali vipengele kadhaa vya kanuni ya
Urbani IV vilivyopata kuwa vya kawaida, kwa jumla alirudia vizuri karama ya Mt.
Klara. Kama yeye alitaka mafungamano imara na Utawa I, monasteri zote zikiwa
chini ya Ndugu Wadogo, na wanne kati yao wakiwa tayari kuihudumia kila mojawapo.
Kwa sababu hiyo, kama tulivyokwishaona, watawa kadhaa wa kiume waliingia katika
juhudi zake za urekebisho (Ndugu Wadogo Wakoleta).
Waoservanti
mwanzoni walikataa kuwahudumia Waklara, lakini polepole wakalazimishwa na Kanisa
kwa ombi la monasteri zilizorekebishwa. Hapo urekebisho wa kina ukapamba kwa
juhudi za wamonaki bora, kama Mt. Katerina wa Bologna (+1463), M.H. Antonia wa
Firenze (+1472), Mt. Eustokia Calafato (+1485) na M.H. Batista Varano (+1524)
huko Italia, na wengineo Ufaransa na Hispania. Wote walishikilia kanuni ya I sio
tu kwa Waurbani, bali pia kwa monasteri nyingi za Utawa III na hata nyingine
zisizokuwa za Kifransisko! Si zote zilikubali kwa ridhaa yao urekebisho. Kumbe
Waoservanti walijaribu kuueneza kote, hata kwa mabavu, mpaka walifikia hatua ya
kutumia nguvu za kijeshi kupitia serikali! Kati ya wote aliyejitahidi zaidi ni
Mt.Yohane wa Capestrano, ambaye alitaka pia kuunganisha monasteri zote chini ya
Waoservanti, lakini akashindana na msimamo wa mt Koleta aliyetaka kubaki chini
ya Mtumishi mkuu na kudumisha uhusiano na Wakonventuali. Mt.Yohane akaandika
(1445) ufafanuzi wa kanuni ya Mt. Klara akiorodhesha amri mia na zaidi, jambo
lililowashangaza sana Waklara, hata mwaka uliofuata ulitolewa ufafanuzi mwingine
juu ya maana ya amri hizo, halafu Eugeni IV (1431-1447) akatamka kwamba chache
tu zinawabana masista kiasi cha kutenda dhambi wakizivunja (1447). Mwenyewe
aliweka chini ya Waoservanti monasteri zote zilizorekebishwa, hata zikifuata
kanuni ya II, akiziacha nyingine chini ya Mtumishi mkuu. Kwa maana sera ya
Kanisa haikuwa kulazimisha monasteri kufuata kanuni ya I, ila kuzirekebisha kwa
kufuata sawasawa sheria za kila mojawapo; pengine waliokataa urekebisho
iliwabidi wahame. Mwishoni mwa karne ya XV Waklara wa urekebisho wakawa wengi
kuliko wasiorekebishwa. Sehemu nyingine monasteri za hawa wa mwisho zilikuwa na
hali mbaya kweli. Hatimaye baadhi ya zile zilizokataa urekebisho zilibadili
kanuni na kufuata ile ya Mt.Benedikto. Jambo lingine lisilopendeza lilikuwa
kuona Waoservanti na Wakonventuali wakishindania monasteri za dada zao.
Kati
ya marekebisho hayo, Wakoleta wamedumisha hadi leo umoja fulani kati ya baadhi
ya monasteri zao. Vilevile Waklara Pekupeku walioanzishwa na Marina wa Villaseca
(Hispania) aliyeruhusiwa (1490) kurekebisha monasteri yake ya Utawa III kwa
kufuata kikamilifu kanuni ya I, na kupokea Waurbani wasirudie unovisi. Makundi
mengine yamepoteza umaalumu wao: kwa mfano Dada Fukara Waklareno ambao Sisto IV
aliwaweka (1473) chini ya Mtumishi mkuu kumpitia makamu wake Mklareno.
Inosenti
VIII (1484-1492) alimruhusu (1489) mt Beatriche wa Silva Meneses (+1490) aunde
monasteri ya Kibenedikto aina ya Citeaux kwa heshima ya Bikira Maria Mkingiwa
Dhambi Asili (Imaculata Concepcion). Baada ya mwanzilishi kufariki, Aleksanda VI
akawaruhusu hao masista Wakonsesioni wafuate kanuni ya Mt.Klara na kuunda
monasteri nyingine, halafu Julius II (1503-1513) akawapatia kanuni mpya (1511)
ambayo inafanana nayo, lakini inaruhusu mali ya monasteri na kulegeza mfungo.
Hata hivyo wakaachwa chini ya Ndugu Wadogo wakapewa fadhili zote za Waklara
(1520). Ndiyo sababu wanaorodheshwa pamoja na Utawa II. Hao wakastawi sana Ulaya
na Amerika hadi leo.
Tofauti
zaidi ni Utawa wa Bikira Maria (Waanunsyata) ulioanzishwa na malkia Mt. Yoana wa
Valois (+1505) kwa heshima ya Maria Mpashwa Habari. Tawi hilo halifuati kanuni
ya Kifransisko, lakini toka mwanzo liko chini ya Waoservanti na linashiriki
fadhili za Waklara: ndiyo sababu linaorodheshwa pamoja nao.
Katika
kipindi hicho ni vigumu sana kutoa takwimu za idadi ya masista. Kati yao, mbali
ya watakatifu 5 waliotajwa, walipatikana wenye heri 7.
2.2.
MAREKEBISHO KUENDELEA (1517-1762)
Baada
ya utengano wa Ndugu Wadogo (1517) monasteri zilizo nyingi ziliwekwa chini ya
Waoservanti, hata zile za Wakoleta (nyingine tena zikaongezwa baadaye, k.mf.
zile zote za Hispania na Ureno mwaka 1566). Kama kawaida mzigo huo ulilalamikiwa
na mkutano mkuu (1532); hivyo ikakatazwa monasteri nyingine zisipokewe chini ya
OFM pasipo ruhusa ya mkutano, na hasa wahusika washughulikie mahitaji ya kiroho
tu ya Waklara. Baada ya Mtaguso wa Trento kutoa maagizo kuhusu watawa wanawake
(1563) yaliyochangia marekebisho ya sheria na hasa juhudi kwa maisha magumu,
mkutano mkuu wa OFM ulitunga sheria muhimu kwa utekelezaji wake ukifuta wadhifa
wa ndugu msimamizi wa Waklara na kuwaweka moja kwa moja chini ya Watumishi wa
kanda (1565). Lakini Waoservanti walipojaribu kusawazisha mno, kwa kudai
monasteri zote ziwe na mali (ilivyoruhusiwa na Mtaguso) wakapatwa na matatizo
makubwa, hasa kwa sababu Wakoleta hawakukubali kuacha ufukara mkuu, na kuja
kulingana na Waurbani wenye kutegemea mali zao.
Urekebisho
wa Ndugu Wadogo Wakapuchini ulisababisha mapema tawi jipya la Waklara linalodumu
hadi leo. Mwanzilishi ni Maria Lorenza Llonc (+1542) mjane Mhispania aliyeishi
Napoli (Italia) na kuhudumia wagonjwa pamoja na jumuia ya wanawake Wafransisko
wasekulari aliyoianzisha. Wakapuchini walipohamia hospitali yake (1529),
akawakabidhi uongozi wa jumuia hiyo. Kati ya 1533 na 1538 wakaongozwa na Mt.
Gaetano wa Thiene aliyewaelekeza kwenye maisha ya sala tu na kuwatafutia idhini
ya kuishi kimonaki kwa kufuata kanuni ya Mt. Klara (1535). Baadaye akawakabidhi
tena Wakapuchini, kwa kuwa karama yao iliathiri sana monasteri hiyo na roho
yake, na ndivyo alivyotaka mwanzilishi. Paulo III (1534-1549) akathibitisha hayo
na nia yao ya kushika kikamilifu kanuni (1538). Kwa ajili hiyo mwanzilishi
aliikamilisha katiba ya Mt. Koleta kwa kutumia ile ya Wakapuchini. Sifa ya
monasteri ikaenea haraka na kusababisha kabla ya 1600 zianzishwe 17 nyingine
Italia (Mt. Karolo Boromeo aliunda tatu katika jimbo lake). Ila Wakapuchini
wanaume wakakataa katakata kuzisimamia, isipokuwa mbili. Hata hivyo dada zao
wakaendelea kuomba msaada huo kwa kuwapitia Maaskofu na wafalme, mpaka Mapapa
wakalazimisha hao wanaume kuhudumia walau kiroho monasteri fulanifulani. Hata
nje ya Italia wakaenea haraka: Hispania (1588), Ufaransa (1603), Ureno(1625),
Mexico(1665) ambayo ikawa nchi walipoongezeka zaidi hadi leo, Peruu (1713),
Gwatemala (1725), Chile (1727) n.k.
Hata
marekebisho mengine ya Utawa I yalijaribu bure kukataa huduma kwa Waklara, hasa
Wariformati waliojitahidi sana ili Mapapa wawaweke wote chini ya Maaskofu.
Hatimaye wakalazimika kuwahudumia Waklara. Masista wa Utawa II na III waliokuwa
chini ya Warekoleti wakaja kutumia jina hilo pia.
Marekebisho
mengine ya Waklara yalifanyika katika karne ya XVII, hasa Italia. Kati yake ule
wa Wakaapweke wa Mt. Petro wa Alkantara, ulioanzishwa na Kardinali Mkapuchini na
kuthibitishwa na Klementi X (1670-1676), ndio tawi gumu kuliko yote yaliyowahi
kuwepo. Masista hao waliishi kila mmoja peke yake kama Wakartusi na kujitahidi
kumuiga Mt. Petro wa Alkantara katika yote, lakini hawakuenea sana.
Katika
karne ya XVII na XVIII hata Waurbani wakapata marekebisho yao hasa upande wa
ufukara, Ufaransa na Italia.
Waklara
waliorekebishwa walitoa mifano bora ya kutetea imani na ubikira wakati wa uenezi
wa Kiprotestanti na vita vya dini vilivyofuata. Upungufu uliosababishwa na mambo
hayo Ulaya Kaskazini ulifidiwa kabisa sio tu katika nchi zilizobaki kuwa za
Kikatoliki, bali hata Amerika na Asia. Wakonsesioni walifika Mexico mwaka 1540.
Waklara wakafungua monasteri yao ya kwanza ya Amerika huko Hispaniola mwaka
1551. Monasteri nyingine zikaanzishwa karne hiyohiyo Peruu, Ekwado, Kolombia,
Chile, Gwatemala na Brazili. Katika karne ya XVII Waklara wakaenea Filipino
(1621) na China (1633). Katika karne ya XVIII ongezeko liliendelea ingawa kasi
yake ilipungua. Takwimu ni kama ifuatavyo:
|
Mwaka
1587 |
Mwaka
1680 |
Waklara tu |
28,000 |
38,000 |
Monasteri zao |
618 |
973 |
Hispania
+ Ureno |
277 |
394 |
Italia
+ visiwa |
199 |
248 |
Ufaransa |
91 |
182 |
Ulaya ya Kati |
46 |
128 |
Amerika |
5 |
21 |
Monasteri za Wakonsesioni |
76 |
90 |
Monasteri za
Waanunsyata |
9 |
40 |
Kati
yao wote anang’aa hasa Mt. Veronika Giuliani (+1727) aliyejaa karama na njozi
tangu utotoni, alivyosimulia kwa utiifu na unyofu katika shajara yenye kurasa
22,000. Wako pia wenye heri 4.
2.3. KARNE ZA MWISHO (1762-2005)
Kama
ilivyowatokea Ndugu Wadogo, Waklara pia walishambuliwa na siasa mpya za
serikali, kuanzia Austria na nchi zote zilizokuwa chini yake (1782-1783),
monasteri zote zilipofutwa. Uamuzi huohuo ulichukuliwa Ufaransa (1792); miaka 2
baadaye M.H. Yosefina Leroux akauawa kwa kosa la kuanza tena kuishi kijumuia),
halafu Ubelgiji, Italia, Ujerumani na Hispania. Katika nchi hiyo ya mwisho
monasteri nyingi zikaendelea hata baada ya sheria nyingine kudai zifutwe;
pengine ilitumika mbinu ya kukubali kutoa huduma fulani (k.mf. shule) Lakini
katika nchi nyingine monasteri nyingi zikaisha, hasa Ureno ambapo zilikwisha
zote kufuatana na sheria ya mwaka 1834.
Tangu
miaka ya kwanza ya karne ya XIX monasteri zikaundwa tena Ufaransa na Ubelgiji,
pamoja na kuanzishwa mashirika mengi ya Kifransisko. Mojawapo ni tunda la Maria
Klara Bouillevaux (+1871) aliyelianzisha Paris (1854), likifuata kanuni ya Utawa
Hasa III na katiba maalumu, yenye jambo la pekee la kuabudu ekaristi saa zote.
Mwaka 1912 monasteri zake zote zikapokea kanuni ya Urbani IV na kujiita Waklara
Fukara wa Kuabudu Mfululizo, halafu Wafransisko wa Sakramenti Kuu. Walienea sana
na kudumisha uhusiano na Wakapuchini. Hata katika nchi nyingine monasteri mpya
ziliundwa na nyingine zilifunguliwa tena. Baadhi ziligeuka kuwa mashirika ya
kitume, bila ya kuacha kanuni ya Kiklara.
Katika
karne ya XX uenezi ukaendelea hasa katika nchi za Amerika na za misheni. Baada
ya Mkusanyo wa Sheria za Kanisa idara ya Papa kwa Watawa iliagiza itungwe katiba
moja kwa Waklara wote, isipokuwa Wakapuchini. Kazi hiyo ilifanywa polepole na
OFM kwa kupokea mapendekezo ya maabesi pia, ikapitishwa (1930), lakini si kwa
Wakoleta. Kwa Waklara Wakapuchini katiba ilitungwa na wenzao wa kiume na
kupitishwa mapema zaidi (1927). Waurbani pia wakaja kukubaliwa katiba maalumu
(1973). Juhudi hizo za kuimarisha umoja zilichangiwa sana na Pius XII
(1939-1958) alipohimiza mashirikisho ya monasteri pamoja na kulegeza masharti ya
ugo (1950) kwa lengo la kuziondoa katika hali ya ukiwa, kuzisaidia upande wa
malezi na kuruhusu pengine uhamisho. Kazi hiyo ilianza Ufaransa (1953) na
kuendelezwa na Mtaguso II wa Vatikani hivi kwamba mwaka 1975 kulikuwa na
mashirikisho 43 (1 chini ya Wakonventuali, 7 ya Wakapuchini na 35 ya OFM). Ni
mafanikio makubwa tukizingatia ugumu wa kushinda desturi za siku nyingi na
tofauti za kila aina. Uhusiano kati ya monasteri na kati ya hizo na Wafransisko
wengine umeongezeka na kuinua ujuzi wa kidini na wa hali na mahitaji ya Kanisa
na ya ulimwengu. Mtaguso uliagiza pia matabaka kati ya masista yafutwe; hivyo
Waklara wakarudia mpango wa mwanzilishi kuhusu udugu, pamoja na kuzidi kuchimba
karama yake kwa jumla. Katika uchangamfu huo mpya monasteri nyingi zikapokea
kanuni ya I badala ya ile ya II. Hivyo mnamo mwaka 1975 kati ya monasteri za
Waklara, 660 hivi zilikuwa zinafuata kanuni ya I na 150 hivi ile ya II. Hata
sinodi ya Maaskofu kuhusu watawa (1994) ikajadili sana masuala ya wamonaki na
kuhimiza tena mashirikisho yaimarishwe na ugo urekebishwe hasa kwa faida ya
malezi.
Baada
ya ongezeko la nusu ya kwanza ya karne ya XX, uhaba wa miito Ulaya umerudisha
nyuma ustawi wa monasteri nyingi. Takwimu ya uenezi ni kama ifuatavyo:
|
Mwaka
1907 |
Mwaka
1980 |
Mwaka
2005 |
Waklara tu |
11,000 |
17,000 |
12,593 |
Monasteri zao |
561 |
824 |
930 |
Hispania
+ Ureno |
185 |
289 |
|
Italia |
157 |
144 |
|
Amerika |
40 |
172 |
|
Ulaya ya Kati |
53 |
78 |
|
Asia
+ Afrika + Australia |
|
60 |
|
Ufaransa |
43 |
52 |
|
Monasteri za Wakonsesioni |
88 |
153 |
157 |
Monasteri za
Waanunsyata |
6 |
4 |
8 |
Kuhusu
matawi, mwaka 2005 takwimu zilikuwa hivi:
|
Watawa |
Monasteri |
Waklara wa kawaida |
7,662 |
569 |
Waklara Wakoleta |
681 |
57 |
Waklara Waurbani |
1,122 |
86 |
Waklara Wakapuchini |
2,246 |
162 |
Wakapuchini wa
Sakramenti Kuu |
295 |
22 |
Waklara wa Kuabudu
Mfululizo |
587 |
34 |
Jumla
ya Waklara |
12,593 |
930 |
Wakonsesioni |
2,019 |
157 |
Waanunsyata |
96 |
8 |
Waklara
wafiadini wengine 6 wa karne ya XX, hasa Wahispania, wameshatangazwa wenye heri.
Mklara maarufu zaidi wa milenia mpya ni sr. Maria Anjelika wa Kupashwa Habari
ambaye, karibu na monasteri yake ya kuabudu ekaristi mfululizo, ameanzisha
(1981) mtandao wa Kikatoliki mkubwa kuliko yote ya Amerika (EWTN)!
3.1.
ASILI NA USTAWI WA UTAWA WA TOBA (1209-1517)
Tangu
mwanzo Kanisa liliona kufanya dhambi na toba si jambo la binafsi tu, bali
linaathiri wengine pia. Ndiyo sababu liliwadai waamini malipizi ili kuwapa
msamaha wa Mungu, na waliopaswa kuyafanya waliandikishwa katika orodha rasmi ya
Watubu (Ordo Poenitentium). Kitubio cha siri kiliposhika nafasi ya utaratibu
huo, wengi walijiamulia kufanya malipizi ya hadhara hata kwa dhambi za wengine
wakajulikana kama Watubu. Toba ni neno la msingi katika historia ya Kanisa.
Maana yake asili ni kujitoa kabisa kwa Mungu na kuishi kadiri ya Injili, lakini
Wakristo wa karne za kati waliona inadai sana huzuni na fidia kwa dhambi za
binafsi na za ulimwengu. Mtubu, akiwa peke yake au pamoja na wengine,
alitarajiwa kuacha kazi zilizotazamwa ni kinyume cha Injili (k.mf. biashara na
uaskari), kujitenga na jamii ili kufungamana zaidi na Mungu kwa maisha ya sala
na tafakuri, kuhiji, kufunga, kujinyima, kutoa sadaka na kujitesa kwa wokovu
wake na wa wote. Wengi kati yao walikuwa wanawake, hasa wa koo bora, kama mama
wa Mt. Klara.
Tapo
la toba liliwahusu walei, ambao baadhi yao wakawa baadaye watawa na hata
makleri, tunavyoona kati ya Wahumiliati waliostawi kidogo tu kabla ya Mt.
Fransisko. Wakati huo walei walihesabiwa kama ngazi ya chini (ya tatu) baada ya
makleri na watawa. Uenezi wa Watubu ukasababisha wapewe na sheria hadhi ya
pekee, kwa kuwahesabu kama kundi maalumu kati ya walei na watawa, na kuwapa haki
na fadhili kadhaa za watawa. Watubu walikuwa walei, lakini wa pekee kutokana na
azimio lao (propositum) lililowadai zaidi katika mengi. Kwanza walikuwa
wanashika usafi kamili, lakini kuanzia karne ya XII baadhi yao wenye ndoa
waliahidi tu kujinyima ndoa ya pili (wakifiwa) na hata tendo la ndoa siku za
kufunga chakula na za kupokea sakramenti.
Mambo ya namna hiyo yanasomwa katika maisha ya Mt. Fransisko, kwa jinsi alivyoathiriwa na roho hiyo. Ndiyo sababu alipozungumzia maisha yake mapya alitumia neno “toba”, na jina asili la kundi lake lilikuwa “Watubu wa Asizi”. Baadaye ukubwa wa karama yake ulimfanya ajitokeze kama kiongozi wa tapo hilo, kwa kuwa namna yake ya kuelewa Injili iliathiri Watubu wengi walioanza kumfuata. Nd. Thoma wa Celano aliandika (1229) kwamba, “kwa uvuvio wa Mungu, watu wengi, maarufu kwa wadogo, makleri kwa walei, walimkaribia mtakatifu Fransisko wakijitolea kuishi chini ya uongozi wake na ualimu wake. Hao wote aliwashirikisha maji tele ya neema za mbinguni ambayo yalibubujika toka rohoni mwake na kustawisha maua ya maadili katika shamba la mioyo yao. Wanaume kwa wanawake walifuata mifano yake, kanuni yake na mafundisho yake; hivyo tunapaswa kumtangaza kwa haki mtendaji asiye na kifani wa hali mpya ya Kanisa na wa ushindi wa majeshi matatu ya wateule. Aliwapa wote mwongozo wa maisha na kadiri ya hali ya kila mmoja alielekeza kwa unyofu njia ya wokovu”. Hayo yalianza kutokea muda mfupi baada ya kukubaliwa na Inosenti III, alipohubiri huko na huko (1211).
Kesi ya pekee ni ile ya kijiji cha Greccio, aliposhangaa kuona kilivyojaa
Watubu wengi kuliko wale wa miji mikubwa. “Mara nyingi, ndugu walipoimba
Masifu ya Jioni, kama walivyofanya sehemu nyingine nyingi, watu wa kijiji hicho,
wakubwa kwa wadogo, walitoka nje ya nyumba zao na kusimama barabarani na
kuwaitikia ndugu kwa sauti kubwa, Asifiwe Bwana Mungu wetu!” (Simulizi
la Perugia).
Tangu
zamani baadhi ya walei walikusanyika kuishi kando ya monasteri ili kufaidika
nazo kiroho na kiuchumi. Baadhi yao waliweza kujifunga kwa namna mbalimbali
waishi kwa useja, au kwa uadilifu, au kwa utiifu au kwa kufuata kanuni maalumu.
Ikawa vilevile kwa Wakanoni, aina mpya za watawa. Mageuzi ya jamii yalipozidi
kuvuta watu mijini ili wafanye kazi tofauti na kilimo, walei wengi waliona
mashirika ya Ombaomba yanalingana zaidi na mahitaji yao ya kiroho, wakayafuata
kama Watubu. Bila ya kuacha kazi zao mpya wala ndoa wakaanza kuvaa nguo ya
kitawa ya shirika husika (walau joho), nyeusi kwa Wadominiko, ya kijivu kwa
Wafransisko. Hata kabla Mt. Fransisko hajafa, walikuwepo Watubu, hasa wanawake,
walioamua kuishi pamoja ili kushika vizuri zaidi azimio lao; k.mf. mwaka 1213
kulikuwa na jumuia ya kike huko Padua.
Mt.
Fransisko, akiwajibika kwa watu hao, aliwaandikia aina ya kanuni katika Barua
kwa Waamini (1215), alimojumlisha mahubiri yake kwa waliotamani kushika toba
nyumbani kwao. Katika toleo la pili la barua hiyo (1221) akaongeza mawaidha na
miongozo akitanguliza dibaji iliyo nzito kiteolojia na kiroho.
Chini
ya Inosenti III, na zaidi chini ya Honori III, hasa kwa juhudi za Kardinali
Ugolino, Kanisa lilikusudia kulipa tapo la toba umoja na muundo fulani, pamoja
na kulikinga dhidi ya uzushi. Hivyo lilitunga kanuni maalumu (1221) kwa kuchota
mengi katika Azimio la Wahumiliati lililokubaliwa mwaka 1201. Kanuni hiyo mpya
iliitwa Kumbukumbu ya Azimio (Memoriale Propositi) ikarekebishwa 1228. Hiyo ni sheria hasa yenye namba 39. Ya kwanza inahusu uduni wa mavazi;
halafu kuna katazo la kuhudhuria karamu, tamasha na michezo; agizo la kufunga
chakula mara moja au mbili kwa wiki; la kusali Masifu kama makleri au Baba Yetu
kadhaa; la kupokea ekaristi Noeli, Pasaka na Pentekoste; la kulipa zaka; la
kutotumia silaha na kutokula kiapo kwa kawaida; la kufanya familia nzima iishi
Kikristo; la kukutana mara moja kwa mwezi kwa Misa, mafundisho na mchango kwa
ndugu na wengineo wenye shida; la mtumishi kutembelea ndugu wagonjwa kila wiki;
la kushiriki mazishi ya ndugu na kuwaombea; la kuandika wasia mapema ili kuzuia
ugomvi; la kupatana kidugu; la kuungama kila mwezi. Kati ya masharti ya kumpokea
ndugu mpya, lipo la kutokuwa na madeni, uadui na uzushi; pia mwanamke awe na
ruhusa ya mume. Baada ya mwaka wa jaribio, anayefaa aweke ahadi kwa maisha yote
asiweze kuacha jamaa tena isipokuwa kwa kuingia shirikani. Pia kuna taratibu za
kusamehe na za kufukuza ndugu. Hatimaye kuna maelezo ya kuwa kuvunja kanuni si
dhambi, ingawa kunastahili adhabu. Kwa jumla hakuna mambo ya pekee ya
Kifransisko.
Ugolino, kisha kuchaguliwa awe Papa Gregori IX, aliwaandikia Maaskofu wa
Italia (1227) juu ya aina mbili za Watubu: wale wa kawaida walioishi nyumbani
kwao, na wale walioishi upwekeni kwa mfano wa watawa halisi: ndio msingi wa
tofauti kati ya OFS na TOR iliyoratibiwa baadaye. Mwenyewe aliandika pia (1238)
kwamba Mt. Fransisko alianzisha aina tatu za utawa: “ule wa Ndugu Wadogo, ule
wa Akina Dada wa Ugo na ule wa Watubu”.
Jambo linalodhihirisha umuhimu wa Ufransisko ni uenezi wa aina hiyo ya
tatu katika Ulaya ya karne ya XIII, unaothibitishwa na hati nyingi zilizotolewa
na Mapapa ili kuitetea. Ingawa hatuwezi kujua idadi yao, walienea haraka nje ya
Italia, hasa Ujerumani, Ufaransa, Uswisi, Ubelgiji, Uholanzi na Hispania. Kwa
njia hiyo ujumbe wa Injili wa upendo na amani ulipenya maisha ya familia, kazi
na mazingira yote ya kila siku, ukiunganisha watawala na raia, wakubwa na
wadogo, wasomi na mafundi wa kila aina. Hao Ndugu wa Toba walijisikia viungo si
vya chama cha kitume kama vingine vingi, bali vya utawa wa kimataifa, wenye sura
na haki za pekee. Kilichowapa nguvu ni fadhili walizopewa na Mapapa: zile
zilizotolewa zamani kwa Watubu wote ziliongezewa kwa Wafransisko wa sehemu
mbalimbali. Muhimu hasa ni ile ya kutopaswa kuapa uaminifu kwa mtawala, uliodai
mtu awe tayari kwenda vitani; halafu ile ya kutopaswa kushika serikalini wadhifa
usiolingana na hali ya kitawa; tena ile ya kutumia mali yao bila ya kuingiliwa
(hasa kwa lengo la kumudu hospitali na huduma nyingine); hatimaye ile ya
kutoweza kuhukumiwa na mahakama ya serikali, ila na ile ya Kanisa tu. Mt.
Selestini V alifikia hatua ya kuwapa Watubu wa L’Aquila fadhili ya kutolipa
kodi! Bila ya shaka viongozi wa nchi walipinga vikali fadhili hizo
zilizodhoofisha mamlaka yao, wakasumbua sana jamaa za toba. Kwa Kanisa ilikuwa
njia ya kupunguza nguvu za mfalme mkuu wa Ujerumani dhidi ya Papa, lakini
ilisaidia pia kupunguza vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Italia.
Ndugu wa Toba walikuwa chini ya mamlaka ya Askofu wa jimbo, aliyetakiwa
kusimamia maendeleo yao na kuwatetea mbele ya serikali. Lakini Maaskofu pia
walipinga vikali fadhili nyingine muhimu, yaani ile ya kutobanwa na katazo la
kushiriki ibada likitolewa na Askofu dhidi ya Wakristo wa eneo fulani.
Upinzani huo wote, ukijumlishwa na ule uliowapata Ndugu Wadogo, unaeleza
kwa nini hao walisimamisha mara kadhaa huduma kwa Watubu (k.mf. 1232-1247,
halafu 1257-1284). Sababu nyingine ilikuwa kutotaka kulemewa nazo. Hasa
nd. Elia na Mt. Bonaventura walizikataa katakata. Hivyo kwa kiasi kikubwa Watubu
walijiongoza na kujieneza. Mkutano wa jamaa, chini ya mkaguzi toka nje, ulikuwa
na mamlaka ya juu katika kuamua, kuchagua, kufukuza. Polepole
jamaa zikafungamana. Zamani za Mt. Bonaventura zilikuwa zimeshaunda kanda
zikiongozwa na Mtumishi wa kanda; zilikuwa na mikutano mikuu pia zilizokusanya
wajumbe wa kanda nyingi, kabla ya mwisho wa karne ya XIII.
Pamoja
na hayo, jumuia za Watubu walioishi nyumba moja ziliongezeka haraka. Tuna hakika
ya kuwepo kwa jumuia hizo nje ya Italia pia: Ujerumani (1228), Korasia (1250),
Ureno (1285) na Ufaransa (1287). Kulingana na maelekeo mawili ya Mt. Fransisko
(moja la toba, sala na upweke, lingine la ushuhuda wa Kiinjili kati ya watu),
jumuia hizo zilikazania ama muungano na Mungu ama huduma kwa wenye shida. Toka
mwanzo wakaapweke wengi walijiunga na Utawa wa Toba, baadhi yao wakiwa na
wafuasi. Jumuia kubwa zaidi zilikuwa zile za kutolea huduma fulani, hasa kutunza
wagonjwa.
Katika
hali hiyo Nikola IV, Papa Mfransisko, alitoa (1289) kanuni mpya kwa Watubu wote,
wa kiume na wa kike, wa wakati huo na wa wakati ujao, akiwaweka chini ya Ndugu
Wadogo kama “wakaguzi na washauri” wao, kwa kumuona Mt. Fransisko kama
“mwanzilishi wa Utawa wa Toba” (tamko ambalo si sahihi kihistoria). Kanuni
hiyo haikubadili sana sheria za Memoriale, ila ilizipanga vizuri zaidi kulingana
na zile za kitawa. Ina sura 20 zenye jumla ya namba 60, ambamo 1-13 zinahusu
mapokezi na ustawi; 14-42 namna ya kuishi; 42-60 maisha ya kidugu na uongozi.
Kanuni hiyo iliweza kuchangia ustawi wa Watubu, lakini ilipingwa mapema na
mashirika mengine yenye watu wa namna hiyo (k.mf. mwaka 1285 Wadominiko walikuwa
wameamua kushughulikia Watubu waliofuata karama yao, hivyo wakaendelea mpaka
walipokubaliwa kanuni maalumu mwaka 1405, baada ya mfumo wao kumzaa Mt. Katerina
wa Siena). Shida nyingine iliyojitokeza ni kwamba kanuni ya Nikola IV
haikuzungumzia walioishi kijumuia: hiyo ilizidi kuwaletea matatizo mpaka
walipopewa kanuni tofauti (1521).
Kwa
kuwa kanuni hiyo ilikuwa ya tatu kwa Wafransisko (baada ya ile ya Ndugu Wadogo
na ile ya Waklara), Utawa wa Toba ulianza kuitwa Utawa III (Tertius Ordo) na
washiriki wake wakaitwa Watersyari (wa tatu). Kumbe kabla ya hapo Tertius Ordo
ilimaanisha kundi la tatu la waamini, yaani walei, waliopangwa baada ya makleri
na watawa. Wazo la toba pia lilibadilika, na tapo lake likamezwa na Utawa III wa
mashirika mbalimbali. Watersyari waliweza wakaishi ama nyumbani kwao, ama
kijumuia, ama upwekeni (pengine kwa kutunza patakatifu fulani au kwa kujifungia
mahali, k.mf. ndani ya mnara wa ngome ya mji); waliweza wakaishi katika ndoa au
kuahidi useja n.k.
Kati yao,
waliotangazwa watakatifu wanaweza wakafikia 4, mbali na wenyeheri 8. Idadi
kamili haieleweki kwa sababu mwanzoni taratibu za kujiunga na Utawa huo hazikuwa
wazi bado. Wa hakika zaidi ni mtakatifu Margerita wa Cortona (+1297) ambaye,
baada ya kuacha maisha ya dhambi, alishika toba kali na kukusanya jumuia ya
wafuasi. Somo wa Utawa III ni Mt. Elizabeti wa Hungaria (+1231), kwanza malkia
aliyemtambua na kumtumikia Yesu katika wenye shida, halafu mwanzilishi wa
jumuia, pamoja na Mt. Ludoviko IX (+1270), mfalme bora kabisa.
Wakarmeli walipoanza kuelekeza Watersyari wao kuweka nadhiri ya useja
(kuna ushahidi wa mwaka 1283), desturi hiyo ikaenea haraka: mwaka 1307 mwanamume
Mfransisko aliweka nadhiri tatu kufuatana na kanuni ya Nikola IV ingawa hiyo
haitaji kabisa nadhiri. Kadiri Watersyari walivyozidi kujilinganisha na
wanadhiri, yalizuka maswali juu yao: mbona kanuni haisemi juu ya kuishi pamoja?
Mbona wanaweka nadhiri kama si watawa? Mbona
wanawake wanaoishi kijumuia hawashiki ugo? Mbona wengine wanaweka nadhiri halafu
wanaendelea kuishi kwao? Je, ni watawa? Majibu yakapatikana polepole, mpaka
wakabainishwa Wasekulari (yaani ndugu wa ulimwenguni) na Waregulari (watawa
hasa).
Zaidi
ya hayo, tangu zamani tapo lolote la walei lililokazia Injili lilishukiwa kuwa
na uzushi. Basi, mwanzoni mwa karne ya XIV Utawa III wa Kifransisko (TOF)
ulijaribiwa sana, kutokana na matatizo ya Ndugu Wadogo, waliotaka kushindana na
Papa, na yale ya makundi ambayo yalifanana na TOF yakaja kukatazwa na Mtaguso wa
Vienne (1312). Ingawa laana hiyo haikuipata TOF, kwa kuwa Klementi V aliwahi
kuagiza utafiti halafu akathibitisha tena kanuni yake (1308), Maaskofu
wakaendelea kuwa na shaka na kusababisha dhuluma dhidi ya Watersyari. Isitoshe,
makundi mengi yaliyokatazwa yaliamua kujiunga na TOF ili kuendelea kihalali.
Jumuia ziliweza kuwa na ndugu 3 hadi 40. Maisha ya pamoja hayakuwa na lazima ya
ndugu kushirikishana mali. Baadhi yao waliendelea kuwa na mali binafsi kama
Wasekulari, ingawa baadhi walichanga kila kitu kama watawa hasa. Kazi zao
zilikuwa za ufundi (kushona, kuhariri, kutengeneza hostie na mishumaa n.k.), za
malezi (kufundisha watoto), za uuguzi (nyumbani kwa wagonjwa au hospitalini)
pamoja na kuwakeshea mahututi na maiti. Riziki zilipatikana kwa kazi hizo,
lakini pia (hasa kwa wanawake) kwa kuombaomba mlango kwa mlango.
Muundo
wa jumuia ulikuwa sawa na ule wa Wasekulari, yaani kila moja ilikuwa chini ya
Askofu, pamoja na mkaguzi au mshauri toka Utawa I, halafu ilikuwa na uongozi wa
ndani (Mtumishi na halmashauri yake). Muundo huo ukaja kubadilishwa na baadhi ya
jumuia mwishoni mwa karne ya XIV, kutokana na ongezeko kubwa la jumuia hizo za
kiume na za kike. Pengine moja ilizaa nyingine ambayo ikabaki chini ya ile mama.
Pia ulihitajika ulinganifu mkubwa zaidi wa taratibu (kanzu, ugo n.k.) kati ya
jumuia za jimbo au kanda moja. Kwa kibali cha Askofu na cha Mtumishi wa Ndugu
Wadogo, shirika jipya la namna hiyo liliweza kuwa na mkutano mkuu na kumchagua
Mkuu wake. Kila shirika lilikuwa na mkaguzi toka shirika lingine. Jaribio la
kwanza lilifanywa na Alfonsi Pecha aliyetaka kuunganisha wakaapweke wote wa
Italia ya Kati na Kusini (1373) asifaulu. Kumbe walifanikiwa Watersyari wa
Utrecht (Uholanzi, 1401), Ubelgiji wa Kiholanzi (1413), Koln (Ujerumani, 1427),
Hispania (1442), Ubelgiji wa Kifaransa (1443), Italia (1447), Irelandi (1456),
Marburg (Ujerumani, 1467), Ureno (1470), Korasia (1473) n.k. Wengine
waliruhusiwa kuweka nadhiri kuu ya useja (1401) au zote tatu (1413). Yalijipatia
kibali ingawa upinzani uliendelea kwa kuwa masuala yao hayakuwa bayana
kinadharia. Hata hivyo hayakuwa mashirika ya kimataifa, yanayotarajia kuenea
popote, bali ya kijimbo au ya kikanda. Kwa kuwa hayakuwa ya kitawa rasmi,
yaliweza kuunganisha jumuia za kiume na za kike chini ya Mkuu mmoja; hapo
kulikuwa na Mtumishi wa kike pia kwa jumuia za kike. Mashirika hayo yalitoa
huduma zilizopangwa vizuri kadiri ya katiba yake. Mwaka 1439 lile la Ubelgiji wa
Kiholanzi lilikuwa na konventi 70 na ndugu 3,000 hivi, wa kiume na wa kike, wote
wakivaa kanzu ya kijivu.
Elekeo
la kitawa la mashirika hayo lilikuwa wazi, hivyo si ajabu kwamba yalizidi
kujilinganisha na wanadhiri. Hata Waoservanti walichangia sana, hasa Italia: kuanzia mwaka 1380 nd.
Paolucho Trinci alijipatia ruhusa kadhaa, mojawapo ile ya kupokea Wasekulari
(1384), halafu ile ya kuanzisha monasteri kwa ajili ya wale wa kike huko Foligno
(1388). Tangu mwaka 1397 hadi 1435 monasteri hiyo ikaja kuongozwa na M.H.
Anjelina wa Marsciano aliyefaulu kuzianzisha 16 nyingine: ndio mwanzo wa shirika
la kike (1428) lililofanana sana na yale ya kisasa. Lilikuwa na Mtumishi mkuu
ambaye alichaguliwa na Watumishi wa kila monasteri na kuwa na mamlaka ya
kuzitembelea zote. Halikuwa na ugo wala nadhiri, isipokuwa ya utiifu. Kazi kuu
ya wanashirika ilikuwa kulea wasichana. Anjelina alipofariki, Eugeni IV alikuza
mamlaka ya Mtumishi mkuu, lakini uamuzi huo ulipingwa na Watumishi wa monasteri
na Waoservanti. Halafu ongezeko la nyumba hata nje ya Italia lilidai safari
nyingi za Mtumishi mkuu na za wengine, nazo zikasababisha vurugu. Basi, Pius II
alifuta wadhifa wa Mtumishi mkuu (1461), hivyo shirika likapotewa na sura yake
na umoja wake. Waoservanti walipozidi kudai Watersyari hao wote washike ugo wa
Kipapa, wengine wakakubali (Watersyari wa ugo, ambao baadhi yao wakaja kuwa
Waklara), ila wengine wakajitenga na Waoservanti ili kuendelea na utume. Ingawa
Sisto IV alitaka Watersyari wote wa kike wakae chini ya Ndugu Wadogo (1471),
wengine walijiweka chini ya Maaskofu, wengine chini ya TOR au chini ya Waamadei
wasibanwe na ugo.
Kwa
kweli Waoservanti walishughulikia sana Utawa III na kuustawisha upya. Katikati
ya karne ya XV Mt. Antonino wa Firenze, Mdominiko, alishuhudia kwamba,
“Watersyari Wadominiko ni wachache sehemu hizi, tena wa kiume ni mmojammoja
tu; kumbe chini ya kanuni na kanzu ya Utawa III wa Mt. Fransisko wako wengi wa
kiume na wa kike. Wengine kama wakaapweke, wengi kama wauguzi wa hospitali,
wengine wameunda shirika”. Ili kupunguza upinzani, Martino V (1417-1431)
alikuwa ameweka Wasekulari wote chini ya Watumishi wa Ndugu Wadogo (1428), ambao
tu waliruhusiwa kupokea watakaji, kufundisha, kukagua na kukosoa. Pengine
waandamizi wake wakawa na msimamo tofauti na kuwarudishia mamlaka Wasekulari
wenyewe. Mt. Yohane wa Capestrano aliwashughulikia na kuwatetea kwa namna ya
pekee, akikusudia kuratibu na kuunganisha jumuia zote za Watersyari zisizo na
sura maalumu kisheria ili azihusishe na urekebisho wa watawa na wa Kanisa lote. Alipokubaliwa na Eugeni IV kwa sauti tu (1436) ifutwe hati ya Yohane XXII
iliyokataza jumuia zote za Watersyari, akawatangazia haraka, ikaanza mikutano ya
kanda na mikutano mikuu. Kwa miaka 10 Watersyari wakaapweke wa Italia
waliunganika wote. Lakini wengine walipendelea kujitegemea zaidi, na wengine
walikataa kujilinganisha kabisa na watawa na kuweka nadhiri (walivyodai hasa
Waklareno, waliojitenga na OFM na kukimbilia Utawa III). Basi, Nikola V baada ya
miaka miwili alifuta kabisa ruhusa aliyoitoa mwaka 1447, akisema, “Wanaopenda
maisha magumu zaidi wanao tayari Utawa ulioanzishwa na Mt. Fransisko
mwenyewe”.
Lakini
mwaka 1457 Watersyari wa Lombardia walikubaliwa tena kuwa na Mkuu wa kwao,
halafu wakaenea katika mikoa mingine ya Italia, wakakubaliwa (1467) fadhili zote
walizopewa wenzao wa shirika la Hispania, zikiwa ni pamoja na ile ya kuweka
nadhiri kuu tatu. Mwaka 1472 mkutano mkuu ulitunga kanuni mpya. Mwaka 1476
walikuwa na kanda kadhaa tayari. Hatimaye Sisto IV alitamka rasmi (1480) kuwa
nadhiri za Watersyari wa kiume na wa kike zilizowekwa kwa fahari zihesabiwe kuwa
kuu kisheria. Tamko hilo likathibitishwa (1517) na Leo X aliyekanusha kuwa hivyo
pia kwa nadhiri ya useja ya wanaoishi nyumbani kwao, ingawa aliwakubalia fadhili
kadhaa. Hata kuhusu ugo kwa wanawake, uliobaki kuwatofautisha na wamonaki,
ilitamkwa (1487) kuwa ni wa hiari.
Pia
baadhi ya Watersyari waliishi utawani kwa Ndugu Wadogo ili wawatumikie kwa hiari
pasipo malipo wala nia ya kuwa watawa hasa, ingawa waliweza wakashiriki maisha
ya jumuia chini ya mlinzi, wakiweka nadhiri ya utiifu na useja. Ni kwamba katika
karne ya XIII Utawa I ulipojali mno ukleri na kuzuia ongezeko la mabradha pamoja
na kudharau kazi za mikono, ulikuja kuhitaji maboi (wanazungumziwa na hati za
Kanisa kuanzia mwaka 1248). Katiba ya OFM (1260) ilikataza wasiongozane na Ndugu
Wadogo ili kuwashikia pesa na kuzitumia kwa niaba yao; ila iliruhusu watoe
baadhi ya huduma konventini, mradi wasilale huko. Baadaye ndugu maarufu
waliruhusiwa kuwa na boi binafsi (katiba ya 1316 n.k.). Mwishoni mwa karne ya XV
maboi walianza kufikiriwa washirikishwe kwa kiasi fulani maisha ya kitawa:
kwanza wafuate vizuri dini, halafu wajiunge na Utawa III na kuvikwa kanzu
fulani, mradi ionekane wazi ni tofauti na ile ya Ndugu Wadogo.
Hasa
katika karne ya XIV, matunda ya Utawa III ni mengi na ya kila aina: malkia na
mapadri, watu wa ndoa na waseja, wakulima na mafundi, waanzilishi wa mashirika
na mashujaa wa huruma, wakaapweke, wafiadini n.k. Mbali na watakatifu ambao
hatuna hakika kama walijiunga na Utawa III, kuna Elzeario wa Sabran (+1323),
aliyeishi na mke wake (M.H. Delfina) kwa usafi kamili, malkia Elizabeti wa Ureno
(+1336), aliyemaliza maisha yake katika jumuia ya Utawa III, Konrado
Confalonieri (+1351) aliyeishi miaka mingi upwekeni, na malkia Birgita wa Sweden
(+1373), somo wa Ulaya. Kati ya wenye heri 23 wakumbukwe hasa Anjela wa Foligno
(+1309), anayeitwa “mwalimu wa wanateolojia” kwa ubora wa maandishi yake juu
ya mang’amuzi ya kiroho, na Raimundo Lull, mwandishi, mwanzilishi wa seminari
ya kimisionari na hatimaye mfiadini kwa mikono ya Waislamu (+1316). Umisionari
wa Utawa III ulijitokeza kwa namna ya pekee kati ya Waregulari wa Ureno,
waliosindikiza wapelelezi wa nchi yao katika safari za hatari pia, kama vile
Kongo na Angola. Mmojawao akasoma Misa mbele ya mfalme wa Kongo (1491)
akambatiza (1495). Lakini utume wa Watersyari ulijitokeza zaidi katika mazingira
ya kawaida ya walei wa Ulaya, na katika huduma mbalimbali walizozianzisha:
hospitali, wokovu wa makahaba, uombaji wa msaada kwa ajili ya maskini, ghala za
kugawia chakula bure, mafunzo kwa watoto fukara na kwa wanaosomea upadri n.k.
3.2. KANUNI TOFAUTI KWA WASEKULARI NA WAREGULARI (1517-1762)
3.2.1. WAREGULARI KUKOMAA KAMA
WATAWA HASA (1517-1762)
Mtaguso
wa V wa Laterano ulitofautisha (1516) aina nne za Watersyari: wanaoishi pamoja,
wanaume wanaoishi katika konventi za Utawa I, wanawake wanaoishi nyumbani kwa
nadhiri ya useja, na Wasekulari. Kwa msingi huo M.H. Gabrieli Maria alitunga (1517)
kanuni sahili kwa Waregulari ambayo ikaja kukubaliwa na Leo X, halafu na Julius
III, ikaendelea kufuatwa na konventi nyingi za Ufaransa. Lakini nyingi zaidi
zilikubali ile ya Leo X iliyokusudiwa (1521) kuleta umoja na usawa kati ya
Waregulari, ikiwafanya watawa hasa na kuwatenganisha na Wasekulari, walioendelea
kufuata kanuni ya Nikola IV hadi mwaka 1884. Katika sura zake 10, kanuni hiyo
mpya ilidai nadhiri za Waregulari wote ziwe tatu tena kuu, ingawa iliiachia kila
konventi ya kike kuamua kuhusu ugo kama haijaushika, kusudi utume kwa wagonjwa
na wasichana usizuiwe. Hata hivyo haikupokewa na Waregulari wote, na ilipingwa
vikali hasa Ulaya Kaskazini. Sababu mojawapo ni kwamba ilitaka konventi zote za
kiume na za kike ziwe chini ya Ndugu Wadogo, zikibaki na Mkubwa wa nyumba tu,
bila ya Watumishi wakuu wa mashirika. Uamuzi huo ulitokana na juhudi za
Waoservanti za kuzuia uwepo wa shirika lingine la Kifransisko lenye uongozi
unaolingana na ule wa Utawa I. Basi, mashirika yaliyokwishakubaliwa yakaendelea
kufuata kanuni ya Nikola IV pamoja na katiba zao. Lakini mapambano hayo yalidumu
muda mfupi tu, kwa kuwa uenezi wa Uprotestanti ulifuta mapema karibu jumuia zote
za Ujerumani na Uholanzi.
Hapo
katikati shirika la Waregulari wa Hispania, kisha kushindana sana na Ndugu
Wadogo waliodai kulikagua, lilikubaliwa na Paulo III kanuni mpya (1547) kwa
Watersyari wote wa Hispania, Ureno na makoloni yake. Kanuni hiyo, tofauti sana
na ile ya Leo X, ilikuwa na sehemu kuu tatu: ya kwanza kwa Watersyari wa kiume
walioishi pamoja kwa nadhiri; ya pili kwa wale wa kike wenye nadhiri walioishi
pamoja bila ya ugo; ya tatu kwa Wasekulari, pamoja na wakaapweke na mabikira
walioishi makwao. Jambo la pekee zaidi, lilikuwa kuwaweka wote chini ya Mtumishi
mkuu wa Waregulari wa kiume (aliyetakiwa kuwa padri): hivyo hao walifikia
kulingana na Utawa I. Nje ya Ufransisko jambo kama hilo halijatokea hata leo:
kuwepo Utawa III wenye masista na Wasekulari chini yake! Halafu Waregulari wa
Italia pia wakakubaliwa katiba na uhuru kamili kwa kanda zao.
Baada
ya hapo juhudi za urekebisho zilizofuatana na Mtaguso wa Trento zilidai masista
wote washike ugo ili kukwepa makwazo. Mt. Pius V kwanza alidai (1566) masista
wote wa shirika lolote wabanwe daima na ugo wa Kipapa, hata kama hawajawahi kuwa
nao; wenye nadhiri ndogo (ambazo wakati huo hazikuwa na nguvu za kisheria)
wahimizwe kuweka zile kuu na hivyo kukubali ugo, la sivyo wakatazwe wasipokee
tena miito waje kwisha. Haikuwa rahisi kutekeleza agizo hilo, pia kwa sababu ya
umuhimu wa huduma ambazo walikuwa wanazitoa na ambazo hazikupatana na ugo.
Matokeo, baadhi ya jumuia zikawa monasteri za Waklara, lakini nyingine
zikaendelea huru katika nchi zote na katika mashirika karibu yote. Halafu,
akiona maisha yao hayana toba na nidhamu za kutosha, ingawa Kardinali mlinzi
alijitahidi, aliwaweka wote, wanaume kwa wanawake, chini ya Waoservanti
(1567-1568). Hatimaye alifuta jumuia zote zenye nadhiri ndogo akakataza
zisianzishwe tena (1568): hata agizo hilo likashindikana, lakini yote yalikuwa
changamoto zifanyike juhudi za urekebisho. Hapo kwa wanaume wa Ufaransa kanda 7
zilikuja kushika maisha yaliyofanana sana na yale ya marekebisho ya Utawa I:
kuishi mbali na watu, kuamka usiku wa manane kwa sala, kufanya malipizi makali
na kutembea peku. Kwa wanawake pia mkazo ulikuwa kufuata mfano wa Wakapuchini au
marekebisho mengine, pamoja na kushika ugo na nadhiri kuu, hasa Uswisi,
Ujerumani, Ubelgiji, Ufaransa. Hata hivyo wakaendelea kushika kanuni ya TOR na
pengine kufundisha.
TOR ya Italia
ilijipatia tena uhuru (1586) kwa kanda zake 11 chini ya Mtumishi mkuu; polepole
Waregulari wa nchi nyingine ama walijiunga nayo katika karne ya XVII, ama
wakakoma kwa kumezwa na OFM au kwa kudhulumiwa na serikali. Mwaka 1700 wanaume
wa TOR jumla walikuwa 3,991 katika konventi 217 na kanda 20, takwimu ambayo
haikubadilika sana katika nusu ya kwanza ya karne ya XVIII. Upande wa wanawake
haiwezekani kukadiria idadi yao. Pamoja na hayo, yalianzishwa mashirika mapya ya
kiume Hispania, Ufaransa na hata Gwatemala kwa ajili ya huduma mbalimbali.
Watakatifu waliopatikana wakati huo ni Yasinta Mariscotti (+1640), aliyeongoka
baada ya kuishi miaka 15 utawani kwa ulegevu, Petro wa Betancur (+1667),
aliyeweka msingi wa shirika la Ndugu Wabethlehemu, na Maria Kreshensya Hoess
(+1744), aliyeabudu sana Roho Mtakatifu, mbali ya mwenye heri Mjapani aliyefia
dini kwao.
3.2.2. WASEKULARI KUZIDI KUENEA
(1517-1762)
Upande
wa Wasekulari, karne ya XVI iliwarudisha nyuma Italia (watu waliporudia sanaa za
kipagani) na Ulaya Kaskazini (ulipoenea Uprotestanti), kumbe iliwastawisha
katika nchi zilizoongoza kisiasa na kidini (Hispania na Ureno) pamoja na
makoloni yake huko Ulaya na ng’ambo (hasa Amerika na Filipino: mwaka 1586 nchi
hizo zilikuwa na Wasekulari zaidi ya 100,000!). Wahispania (hata wafalme,
majemadari, Maaskofu) walikuja kumheshimu sana Mt. Fransisko na kutamani waitwe
wanae na kuzikwa wamevaa kanzu yake. Uenezi ulileta pia ulegevu katika maisha
yote ya toba, hata uduni wa kanzu uliachwa, halafu badala yake vitambaa viwili
kifuani na mgongoni hadi kwenye kamba kiunoni vikaruhusiwa kuvaliwa chini ya
nguo yoyote, hata ya fahari.
Katika
umati huo kuna watakatifu pia, kuanzia Mt. Ajela Merichi (+1540) aliyeanzisha
kikosi cha Mt. Ursula kwa roho ya Kifransisko na chini ya kanuni ya Utawa III,
ambacho muda mrefu baadaye kikageuka kuwa shirika la kitawa. Wengine ni Gaetano
wa Thiene (+1547), Ignas wa Loyola (+1556), Filipo Neri (+1595) na Kamilo wa
Lellis (+1614), waanzilishi wa mashirika yasiyo ya Kifransisko, ambao ni vigumu
kusema walichota nini katika Utawa III. Walio wengi ni wafiadini 17 wa Japani
waliochanganya damu yao na ile ya wamisionari wa Utawa I waliowashirikisha
Injili kwa roho ya Kifransisko (+1597): Paulo Suzuki, Gabrieli wa Ize, Yohane
Kinuya, Thomas Danki, Fransisko wa Meako, Thomas Kozaki, Yohakim Sakakibara,
Bonaventura wa Meako, Leo Karasuma, Mathias wa Miyako, Antoni wa Nagasaki,
Ludoviko Ibaraki, Paulo Ibaraki, Mikaeli Kozaki, Petro Sukejiro, Kosma Takeya na
Fransisko Adauctus.
Katika
karne ya XVII uenezi uliendelea katika nchi hizo na pia Austria, halafu
Ufaransa, hasa Ndugu Wadogo wa matawi mbalimbali walipoamua kuwajibika zaidi
upande huo wakaanza kushindana kati yao tena na TOR. Mapapa, wakijua umuhimu wa
Utawa III katika kuzuia uzushi, walichangia uenezi huo kwa kuupatia rehema na
fadhili za pekee. Kwa ajili ya Wasekulari vilitungwa pia vitabu vingi vya sala
na maelezo ya kanuni, pamoja na kukaza maisha ya kiroho (tafakuri, mafungo ya
kiroho, sakramenti) na huduma kwa wenye shida. Hata hivyo hali ya jumla ilizidi
kudidimia, na OFS ilionekana kulingana na chama chochote cha kumheshimu
mtakatifu fulani, kuadhimisha sherehe yake n.k. Lakini mambo kama hayo hayapiti
bure yasiathiri roho za watu na jamii nzima, hasa yanapogusa umati (mwaka 1689
Madrid ilikuwa na Wasekulari 25,000!). Vilevile miundo ya huduma iliyoanzishwa
na Wafransisko hao iliendelea hata katika matatizo mengi, hivi kwamba mingine
ipo hadi leo.
Tunda
bora ni Maria Ana wa Yesu wa Paredes (+1645), Mfransisko wa kwanza wa Amerika
kutangazwa na Kanisa kuwa ni mtakatifu. Wengine waliojiunga na OFS au kuvaa
kamba yake ni wat. Fransisko wa Sales (+1622), Yoana Fransiska wa Chantal
(+1641) na Yosefu Kalasanzi (+1648). Kundi kubwa zaidi ni lile la wenye heri 30, hasa
wafiadini wa Japani tena.
Kwa
Watersyari walioishi utawani kwa Ndugu Wadogo katikati ya karne ya XVII
ulipangwa umri wa chini (miaka 20) na malezi ya miaka 3 chini ya padri. Baadaye
tena hali yao ikafafanuliwa kikamilifu na katiba, hasa ya OFM (iliyokuwa na
Watersyari wengi zaidi konventini).
3.3. WASEKULARI NA WAREGULARI NYAKATI ZETU (1762-2005)
Kwa Utawa III pia miaka ya mwisho ya karne ya XVIII na sehemu kubwa ya
ile iliyofuata ilikuwa kipindi kigumu cha majaribu, kutokana na dhuluma za
serikali nyingi. Falsafa ya waasi wa dini na utaifa wa wafalme na
Maaskofu wa nchi kadhaa vilielekeza hata kumwaga damu za wengi, hasa baada ya
mapinduzi ya Kifaransa kuenea Ulaya karibu nzima.
Ilianza
Jamhuri ya Venezia (1767) kwa kufuta kanda moja ya TOR. Akafuata malkia wa
Austria na Hungaria, aliyekataza (1776) OFS isipokee tena watakaji. Mtoto wake
akafuta Utawa III kwa namna zake zote (1782). Ufaransa ukafuta miundo yote ya
kidini (1790), ikiwa ni pamoja na Utawa III, na kutaifisha mali yake. Baadhi ya
Watersyari kwa uaminifu wao walifungwa hata kuuawa. Hispania (1812) na Ureno
(1834) pamoja na Brazili mashirika yote yakafutwa, ingawa jamaa za OFS
zikaendelea. Hata Italia jamaa hizo ziliondolewa hadhi yao mbele ya sheria
(1861-1866), lakini zikaendelea kama vyama vya hiari.
TOR
ni kati ya mashirika yaliyopigwa zaidi, hata karibu kutoweka: kwa miaka 30 hivi
kanda nyingi zilikwisha; katika mikutano mikuu iliyofanyika tena kuanzia mwaka
1824 waliweza kuhudhuria tu ndugu toka mikoa 3 ya Italia na pengine toka
Korasia.
Dhuluma
hizo zilipiga sio tu miundo na mali, bali pia mfumo wa maisha, kwa kudai watawa
wawe na faida kwa jamii, si mzigo kwake. Katika mazingira hayo yakaja kuanzishwa mashirika
mengi ajabu, hasa ya wanawake: karne ya XIX ndiyo iliyozaa mashirika mengi
kuliko nyingine zote. Kati yake, asilimia kubwa ni ya Kifransisko (siku hizi
yapo 22 ya wanaume na zaidi ya 400 ya wanawake, yanayojumlisha watawa 120,000
hivi, mbali ya monasteri 61 zenye masista 900!). Si rahisi kuandika historia ya
mashirika hayo yote. Kwa kifupi, mengine yalitokana na monasteri za Waklara
waliolazimika kushika utume fulani ili waruhusiwe kuendelea kuishi kijumuia
(baadhi yake wanafuata bado kanuni ya Utawa II kwa namna yao). Mengine
yalitokana na Wasekulari walioanza kuishi pamoja. Mengine yalianzishwa tu
kutokana na elekeo la kila jimbo kutaka liwe na shirika lake, hivi kwamba Askofu
(au hata paroko) alijitahidi kujianzishia jipya au kutenga tawi na nyumba asili;
katika hilo pengine hali ya siasa na ya jamii ilichangia, pamoja na hamu ya
kujitegemea. Ustawi huo ulitokea wakati uleule wa mashirika ya zamani kufifia:
tena watawa hao, waliofukuzwa na serikali kutoka konventi zao, ndio walioanzisha
mashirika mengi kulingana na mahitaji ya watu katika ulimwengu mpya wa kibepari.
K.mf. M.H. Honorati Kazminski
(+1916), padri Mkapuchini aliyeanzisha mashirika 27 tofauti (kati yake 17 bado
yapo), na Askofu Mkapuchini Luis Amigò (+1934), aliyeanzisha mashirika mawili
makubwa (la kiume na la kike) yaliyokwishapata wenye heri 22 wafiadini.
Kwa
kawaida ni mashirika ya nadhiri ndogo, au yasiyo na nadhiri, yanayotoa huduma
maalumu upande wa umisionari, huruma kwa maskini, ustawi wa jamii, malezi, tiba
n.k. Kwa sababu ya kutoweka nadhiri kuu, wanashirika hawakuhesabiwa kama watawa,
wala wale wa kike hawakubanwa na ugo. Walifuata katiba zao maalumu chini ya viongozi
wao. Waliotaka kuwa Wafransisko walijiunga binafsi na OFS. Kanisa, baada ya
kutamka (1887-1893) kwamba mtawa hawezi kuwa Mtersyari pia, na baada ya kutambua
(1900) mashirika hayo kuwa ya kitawa liliamua (1901) shirika la mchepuo fulani
wa kiroho lisianzishwe pasipo fungamano na Utawa I wa mchepuo huo. Hapo watawa
wote wa mashirika hayo wakahesabiwa kuwa Watersyari jumla, bila ya kujiunga
binafsi na Utawa III. Mashirika mengi ya Kifransisko yalifungamana kiroho na OFM
(1905 n.k.) na OFMCap (1906 n.k.).
TOR
ilipoomba ruhusa ya kuwa na mashirika ya Watersyari chini yake, ilikubaliwa
baada ya miaka 5, halafu ikaondolewa. Ugumu wa suala hilo ni kwamba TOR yenyewe
ni Utawa III: inawezaje kujilinganisha na Utawa I? Lakini Benedikto XV
(1914-1922), baada ya kuona TOR inameza mashirika madogo ya Watersyari,
aliiruhusu tena (1921) akipendekeza mashirika yote ya kiume na ya kike ya Utawa
III wa Kifransisko yaungane nayo. Kwa ajili hiyo aliilinganisha TOR na matawi
matatu ya Utawa I: tangu hapo familia ya Kifransisko ikahesabiwa kuwa na Wakuu
4.
Kufuatana
na Mkusanyo wa Sheria za Kanisa, Pius XI (1922-1939) alitoa kanuni mpya (1927)
iliyotungwa kwa ushirikiano wa Wakuu 4 wa familia ya Kifransisko iwe kanuni
pekee kwa mashirika ya Utawa III, yakiwa ni pamoja na TOR yenyewe iliyokuwa
imeikataa ile ya mwaka 1521. Ingawa juhudi ya kuyaunganisha yote chini ya TOR
ikashindikana kwa sababu karibu yote yalipendelea kujitegemea, kuanzia mwaka
1950 ilifanyika mikutano mingi ya pamoja na kuzidisha ushirikiano hasa kwa ajili
ya kutunga kanuni nyingine kufuatana na maelekezo ya Mtaguso II wa Vatikani.
Kanuni hiyo iliyothibitishwa (1982) na Yohane Paulo II ni ya Kifransisko kuliko
zile zote zilizotangulia. Hatimaye likaanzishwa (1985) Baraza la Kimataifa la
Kifransisko (IFC-TOR) linaloshirikisha mpaka sasa ¾ za mashirika yote ya Utawa
III.
Ushirikiano
mpya wa Utawa III na ule I uliimarishwa kwa kuunda (1995) Baraza la Familia ya
Kifransisko, linalojumlisha Wakuu wa OFM, OFMConv, OFMCap, TOR, IFC-TOR na OFS.
Utawa II hauna mwakilishi, kutokana na muundo wake wa monasteri zenye ugo.
Baraza la Familia ya Kifransisko linawakilishwa katika Umoja wa Mataifa kwa njia
ya asasi isiyo ya kiserikali inayoitwa Franciscans International.
Watersyari
Waregulari 40 wa kipindi hicho wameshatangazwa wenyeheri, k.mf. Maria wa Mateso
(+1904) aliyeanzisha shirika kubwa la Wafransisko Wamisionari wa Maria (wako
7,712 katika nchi 76), ambao 7 kati yao ni watakatifu waliofia dini China
(+1900): Maria Ermelina wa Yesu, Maria wa Amani, Maria Klara Nanetti, Maria wa
Mt. Natalia, Maria wa Mt. Yusto, Maria Amandina wa Moyo Mtakatifu na Maria
Adolfina Dierk. Muda mrefu kabla yao alistawi Maria Fransiska wa Madonda Matano
(+1791), aliyestahimili mateso mengi, na baada yao Mt. Alberto Chmieliwski
(+1916), aliyeanzisha mashirika mawili (la kiume na la kike) huko Polandi.
Kuna mambo mbalimbali yaliyochangia ustawi mpya wa Utawa III katika
matawi yake kuanzia mwisho wa karne ya XIX: kikomo cha dhuluma za serikali
katika nchi nyingi, hali mpya ya Utawa I, mvuto mkubwa wa mtakatifu Fransisko
kwa wenye elimu na uenezi wa roho ya Kifransisko kupitia magazeti. Ndiyo
sababu Utawa III ulianzishwa hata kati ya Waanglikana na Waprotestanti! Kwa
miaka 115 mfululizo (1848-1963) Mapapa wote walikuwa wa OFS (kuanzia M.H. Pius
IX hadi M.H. Yohane XXIII) wakahamasisha Maaskofu na wengineo kueneza Utawa huo,
hasa Leo XIII aliyetoa kanuni mpya (1884) yenye sura tatu na namba 24 jumla.
Pamoja na kufupisha ile ya zamani ilirahisisha mengi iweze kuwafaa Wakristo
wote, ikiwadai tu wavae skapulari ndogo na kamba, kupata malezi ya mwaka mmoja
kabla ya kutoa ahadi, kuvaa na kuishi pasipo makuu, kukwepa tamasha za
kilimwengu, kuwa na kiasi mezani, kuungama na kupokea kila mwezi, kusali Zaburi
au walau Baba Yetu, Salamu Maria na Atukuzwe mara 12 kwa siku, kuandika mapema
wasia, kujitafiti dhamiri kila siku, kushiriki Misa kila siku ikiwezekana,
kuhudhuria mkutano kila mwezi, kuchangia gharama za Utawa na misaada kwa
maskini, kukaguliwa na Ndugu Wadogo kila mwaka.
Kwa
juhudi hizo, na hasa kwa makongamano mengi makubwa, OFS ilionekana mshikamano wa
kidugu wa kimataifa mbadala wa Ukomunisti uliotangaza chuki kwa mabepari. Lakini
wengine waliogopa elekeo hilo la kijamii. Basi, Mt. Pius X aliweka Wasekulari
chini zaidi ya Ndugu Wadogo na kudai wawajibike katika siasa binafsi, si kwa
pamoja. Hivyo OFS ikarudi kutazamwa kama shule ya kiroho tu, ikachapishiwa
vitabu vingi, hasa juu ya masharti yake, namna za kusali na kujinyima, kujipatia
fadhili na rehema n.k. Mkusanyo wa Sheria za Kanisa ulipanga aina zote za Utawa
III katika nafasi ya kwanza kati ya vyama vya waamini, na kueleza kuwa lengo
lake ni ukamilifu wa Kikristo kadiri ya maisha ya ulimwenguni kwa kufuata kanuni
maalumu iliyokubaliwa na Papa na chini ya uongozi na roho ya Utawa I unaohusika.
Kwa hamasa za
Mapapa, wengi walijiunga na OFS (mwaka 1934 walikaribia kuwa 4,000,000!) lakini
muda mfupi kabla ya vita vikuu vya pili walianza kupungua kutokana na matapo
mengine ya kiroho kuanzishwa na kuhamasishwa na Mapapa, hasa Aksyo Katoliki; pia
kwa sababu wingi si hoja, yaani ongezeko lao lilisababisha ulegevu fulani hata
kusawazisha OFS na chama chochote. Kabla na hasa baada ya Mtaguso II wa Vatikani
ilitokea misukosuko na maswali mengi. Ili kuyakabili, ilifanyika mikutano mingi
ya matawi yake mbalimbali (1950 n.k.) na kuzidisha ushirikiano kati yake (pia na
Utawa III wa michepuo mingine) hata ikatolewa (1957) katiba moja kwa Wasekulari
wa matawi yote ya Kifransisko. Miaka hiyohiyo lilianzishwa kundi la Vijana
Wafransisko. Halafu ikaanzishwa halmashauri ya kimataifa ya OFS yote (1973) na
Paulo VI akathibitisha (1978) kanuni mpya ya OFS kulingana na maelekezo ya
Mtaguso huo. Ina sura tatu na namba 26 jumla kuhusu asili ya OFS na kanuni yake
(1-3), mtindo wa maisha (4-19) na taratibu zake (19-26). Ni kama mwongozo wa
maisha ya Kiinjili unaomkazia Yesu Kristo kwa kuwa Injili si nadharia, bali ni
mwenyewe (namba 12 kati ya 26 zinamzungumzia wazi). Haina tena maagizo ya
kinaganaga kuhusu toba, ambayo yaliachwa kwa katiba mpya (1990) iliyounganisha
moja kwa moja matawi yote yaliyokuwa chini ya Wakuu 4 wa familia ya Kifransisko.
Mwaka huo Wasekulari walikuwa 508,619, wengi wao wakiwa Meksiko na Italia. Hapo
katikati toleo la pili la Mkusanyo wa Sheria za Kanisa lilitaja Utawa III peke
yake kati ya vyama vya waamini, kutokana na heshima uliyopewa na mapokeo. Jambo
jipya ni kwamba sasa mashirika yoyote yanaweza kuanzisha aina ya Utawa III, hata
yale ya kike.
Kuhusu
Wasekulari kuishi katika nyumba za Ndugu Wadogo, mtazamo baada ya Mtaguso II wa
Vatikani ukawa tofauti: Ndugu Wadogo wanapaswa kutumikia, si kutumikiwa na
Wasekulari; watu wakiishi konventini kwa kufanya kazi fulani, basi walipwe
kadiri ya sheria za nchi. Hivyo idadi yao ikazidi kupungua haraka: kwa OFM mwaka
1968 walikuwa 536, mwaka 1994 wakabaki 155 tu.
Kati
ya Wasekulari wa hakika wa karne hizi za mwisho tunakuta wenye heri 11 na
watakatifu Yosefu Benedikto Cottolengo (+1842), Vinchensya Gerosa (+1847),
Vinchensyo Pallotti (+1850), Emilia wa Vialar (+1856), Yohane Maria Vianney
(+1859), Maria Yosefa Rossello (+1880), Yohane Bosco (+1888), Pius X (+1914) na
Fransiska Saverio Cabrini (+1917), wengi wao wakiwa waanzilishi wa mashirika
yasiyo ya Kifransisko. Pia kuna watakatifu 11 wa China waliofia dini (+1900):
Yohane Zhang Huan, Patrick Dong Bodi, Yohane Wang Rui, Filipo Zhang Zhihe,
Yohane Zhang Jinggwang, Thomas Shen Jihe, Simoni Chen Ximan, Petro Zhang Banniu,
Fransisko Zhang Rong, Mathias Feng De na Petro Wu Anpeng.
Jedwali la
matunda bora ya familia ya Kifransisko ni kama ifuatavyo:
|
Wenyeheri |
Watakatifu |
Jumla |
Utawa I |
181 |
85 |
266 |
Utawa II |
27 |
10 |
37 |
Utawa III - Waregulari |
45 |
15 |
60 |
Utawa III - Wasekulari |
69 |
55 |
124 |
Waliovaa kamba |
0 |
4 |
4 |
Jumla |
322 |
169 |
491 |
Kati
yao, 280 ni wafiadini, 3 mapapa, 14 maaskofu, 4 walimu wa Kanisa.