KATIBA
ya Utawa wa
Ndugu Wadogo wa Afrika
YALIYOMO
0. DIBAJI
1. KUISHI KIINJILI KAMA FAMILIA YA
MUNGU
2. KUITIKIA WITO
3. KUMUONEA KIU MUNGU
4. KUZAA KWA KUPENDANA NA MUNGU TU
5. KUTUMIKIA NA KUFANYA KAZI
6. KUSHIKAMANA NA YESU FUKARA
7. KUISHI KIDUGU KATIKA JUMUIA
8. KUTII KWA UPENDO
9. KUWA MASHAHIDI WA KRISTO
0. DIBAJI
0.1.1.
Yesu, Mwana pekee wa Mungu, alikuja duniani aokoe kila kabila la watu na kuongozana na kila mmoja
katika safari ya maisha.
0.1.2.
Alikuja kutuangazia utamaduni tulioachiwa na wazee, ili tuone unavyomuelekea
yeye Adamu Mpya.
0.1.3.
Alikuja kutukusanya tena kwa njia ya Roho wake wa upendo, anayetufanya familia
ya Mungu Baba, jamaa ya wadogo wake walioshinda hofu na chuki kati yao, mfano wa
Utatu mtakatifu, ushirika kamili katika tofauti za nafsi, ambapo lugha zote
ziungane kutangazia maajabu aliyotutendea Mwenyezi Mungu.
0.2.1.
Kwa upendo wake alitaka Afrika iwe bara lake la pili, ambapo asalimike utotoni
na azidi kuwa Mwafrika kwa njia ya viungo vyake.
0.2.2.
Kanisa la bara letu, baada ya kutendewa naye makuu na kustawishwa kwa juhudi na
damu za wazee wetu katika imani, sasa linatakiwa kueneza wokovu hata miisho ya
dunia, lisitosheke na kazi ya kukidhi mahitaji ya majimbo yake tu.
0.2.3.
Kutuatana na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano, Roho Mtakatifu katika Sinodi ya
Kwanza ya Afrika ameliambia Kanisa hilo anavyolitaka lijionyeshe familia ya
Mungu na kutangaza habari njema ya Yesu Kristo, aliye njia, ukweli na uzima kwa
Mwafrika na kwa yeyote duniani.
0.2.4.
Miaka ya elfu mbili, nafasi ya pekee ya kufikisha Injili kwa watu wote, ndiyo
saa yake tena.
0.2.5.
Ingawa Waafrika wengi wanazidi kuachwa nyuma kisiasa na kiuchumi, utamaduni wao
wa uzima na mshikamano unahitajiwa haraka na ulimwengu wote.
0.3.1.
Mtakatifu Fransisko wa Asizi alimshuhudia Kristo kwa upole na ushujaa mbele ya
Waislamu wa bara letu, akitamani kumwaga damu yake kwa wasiomjua bado.
0.3.2.
Mfano wake huo na karama aliyojaliwa, yenye sifa kuu mbili yaani udugu na udogo,
vinafaa sana kuchangia utekelezaji wa maazimio ya Sinodi hiyo.
0.4.1.
Tukizingatia hayo, sisi Ndugu Wadogo wa Afrika tunajisikia wito wa kutimiza
karama hiyo katika mazingira halisi ya Waafrika, kwa kudumisha, kustawisha na
kueneza tunu za utamaduni huo ambazo zinalingana na Injili.
0.4.2.
Hivyo tunatumaini kuwa nguvu ya Mungu, inayojionyesha wazi katika udhaifu wa
binadamu, itatutumia kwa ustawi wa Kanisa lote, ambao unategemea na kulenga
utakatifu, yaani kushiriki kikamilifu uzima wa Mungu.
0.5.1.
Utawa wetu wa Kifransisko wa kimisionari una makao makuu mjini Morogoro, ambapo
askofu wa jimbo, mhashamu Telesphore Mkude, katika juhudi zake za kueneza Injili,
ameuunda kama chama rasmi cha waamini kadiri ya kanuni 312 CIC.
0.5.2.
Ni juu ya askofu wa jimbo hilo kuzidi kufanya utambuzi wa karama hiyo ili aweze
kupendekeza utawa huo ukubaliwe kama aina mpya ya maisha yaliyowekwa wakfu,
kadiri ya kanuni 605 CIC, au aufute kwa sababu nzito.
0.6.1.
Mwenyewe amethibitisha katika hii itusaidie kumfuata kwa hakika Yesu na kutimiza
matakwa ya Baba kwetu.
0.6.2.
Tunaohusika nayo moja kwa moja ni sisi wanachama tuliojifunga kushika useja
mtakatifu, ufukara na utiifu kwa kuishi Injili kijumuia katika jamaa za kiume na
kike.
0.6.3.
Ni wanachama halisi pia makleri wanajimbo na walei wanaume na wanawake, waseja
na wenye ndoa, ambao kisha kupata malezi ya kufaa wanaishi ulimwenguni karibu na
jumuia mojawapo ya namna hiyo, wakishirikiana nayo katika maisha ya kiroho na ya
kitume: hao wanafuata kanuni na katiba za Utawa wa Kifransisko wa Ulimwenguni (S.F.O.)
kama washiriki wengine wa Utawa huo wa Kipapa.
0.7.1. Katiba hii ina mambo yale tu ya karama na taratibu zetu ambayo
hayatarajiwi kubadilika.
0.7.2. Hata hivyo tuzidi kuomba mwanga wa Mungu na kufaidi mang’amuzi yetu
ili tuelewe vizuri zaidi anataka nini kwetu, kwa kuzingatia ufuasi wa Kristo
kadiri ya Injili, hazina ya kiroho ya Kifransisko, malengo ya Kanisa na mahitaji
ya ulimwengu, tukiweka daima mbele ustawi wa roho zetu na wokovu wa watu.
0.8.1. Askofu wa Morogoro anaweza kuthibitisha marekebisho ya katiba
yaliyopitishwa na baraza pana kwa thuluthi mbili za kura, mradi yawe
yanahitajika kweli ili tuendelee kujenga juu ya misingi ileile.
0.8.2. Haja hiyo isipokuwepo, afadhali
yaachwe, kwa sababu mabadiliko
yanadhoofisha sheria, na yale madogo yanachochea mengine makubwa, mpaka mfumo wa
utawa unakuwa mwingine na kusababisha utasa wake.
0.9.1. Ili tuwe na heri kwa kutekeleza kikamilifu yale tuliyoonyeshwa,
tujitahidi sura halisi ya utawa wetu ilingane na picha iliyochorwa katika katiba
tuliyojaliwa na Mungu kwa njia ya Kanisa lake.
0.9.2. Mkutano mkuu unaweza kutoa kwa kiasi sheria ndogondogo zinazohusu
jamaa nzima, na ambazo ziweze kurekebishwa nao inapotakiwa, mradi zilingane
daima na kanuni na katiba.
0.9.3. Halmashauri kuu inaweza kutoa maagizo maalumu yanayohusu baadhi tu ya
ndugu au jumuia, kadiri ya mahitaji yao na ya mazingira wanapoishi.
0.9.4. Lakini tutegemee uaminifu mnyenyekevu wa kila mmoja wetu kuliko wingi
wa sheria na juhudi za watumishi na walinzi.
0.10.1. Ukitokea wasiwasi kuhusu utekelezaji wa sehemu ya katiba
hii,
halmashauri kuu iamue la kufanya, lakini baraza likikusanyika litoe maelezo
rasmi kwa kibali cha askofu wa Morogoro.
0.11.1. Ni juu ya askofu wa jimbo husika kusamehe ndugu wasitekeleze sehemu
fulani ya sheria zetu katika nafasi maalumu.
0.11.2. Ikiwepo sababu ya kutosha, watumishi na walinzi pia wanaweza
kuwasamehe ndugu walio chini yao, wale waliopo kwa muda na hata jumuia nzima,
isipokuwa katika yale yanayohusu miundo ya utawa wetu na kiini cha maisha yetu;
tena, ikihitajika ruhusa ya kudumu, itolewe na mtumishi tu.
0.11.3. Aliyesamehewa ajitahidi zaidi katika mengine
anayoyaweza, akijua
urahisi wa ruhusa hizo unavyozima upesi hamu ya ukamilifu.
0.12.1. Hasa tujihadhari na kishawishi cha kuona sharti fulani la katiba hii,
eti ni gumu mno, au kuacha kulitimiza kwa makusudi au kwa ulegevu.
0.12.2. Tuamini kuwa wokovu umetokana na upumbavu wa msalaba, halafu tung’amue
jinsi mzigo wowote ulivyo mwepesi ukibebwa kwa ajili ya Yesu mpenzi ili kuungana
naye.
1 . KUISHI KIINJILI KAMA FAMILIA YA MUNGU
1.1. YESU NA INJILI YAKE
1.1.1. Yesu wa Nazareti ndiye mfano kamili wa Mungu asiyeonekana, na ndiye
anayetufumbulia kikamilifu ubinadamu wetu.
1.1.2. Injili takatifu, iliyo moyo wa Maandiko Matakatifu yote, inatufunulia
matendo na maneno yake, na hivyo inatuelekeza njia pekee ya kumfikia Baba katika
Roho Mtakatifu na ya kuwa watu waliokomaa anavyotutaka yeye.
1.1.3. Mzee wetu Fransisko wa Asizi tangu aanze kuongoka hakuwa kiziwi kwa
ujumbe wa Injili, bali kwa kuushika sawasawa alikuja kufanana na Yesu kwa namna
ya pekee.
1.1.4. Upendo wa Kristo uliotupata sisi pia, ndio asili ya maisha yetu yote
ambayo tunalenga ukamilifu wa Injili yake, kwa kushika sio tu amri za Mungu,
bali pia mashauri yanayotokana na mafundisho na mifano aliyotuachia, ili
tumfuate kwa karibu iwezekanavyo huyo Mwanakondoo kokote aendako.
1.1.5. Tuzingatie hivyo Injili zaidi kuliko mapokeo ya kibinadamu, hata kama
ni ya kitawa.
1.1.6. Kwa njia hiyo Roho Matakatifu atamfanya Yesu kuwa kiini cha maisha
yetu na kuunda upya utamaduni wetu ndani mwake, kwa sifa na utukufu wa Mungu
Baba.
1.2.
VIUNGO VYA MWILI WA KRISTO
1.2.1.
Kristo ameunganika kabisa na bibiarusi wake na kuishi ndani yake, kiasi kwamba
kushikamana na Kanisa na kushikamana naye ni mamoja.
1.2.2.
Tumtolee huyo Mama yetu maisha na moyo, maneno na matendo, muda na nguvu ili
sikuzote tuishi na kufanya kazi ndani yake na kwa ajili yake, tukiamini tunaye
Roho Mtakatifu kadiri tunavyolipenda Kanisa.
1.2.3.
Tushirikiane na vyombo vyake mbalimbali katika kazi na hasa katika adhimisho la
ekaristi, ili kuonyesha na kuimarisha umoja tulionao.
1.2.4.
Tutegemeze pia miundo yake ya lazima kwa njia ya sadaka na michango mbalimbali,
hasa kwa ajili ya mfuko wa pamoja kama umeanzishwa jimboni.
1.2.5.
Sisi watawa ni zawadi ambayo Baba amelijalia Kanisa ili kuwakumbusha watoto wake
undani wa miito yao maalumu, ambao kwa wote ni mmoja tu, yaani kuwa watakatifu
katika mwenendo wao wote.
1.2.6.
Kama vile sisi tunavyohitaji msaada wa waamini wenzetu, nao wanahitaji kuvutwa
na sisi ambao tumekataa tamaa za ulimwengu, na kuweka pembeni hata tunu kadhaa
za kidunia, ili kulenga moja kwa moja heri ya milele kwa kufuata njia
aliyoielekeza Yesu katika hotuba ya mlimani.
1.2.7.
Kwa mfano wa Maria wa Bethania, tumwage maisha yetu kama manukato ya miguu yake,
ili Kanisa lote lijae harufu nzuri ambayo imchochee kila Mkristo kusikiliza upya
Neno la uzima na kuchangia juhudi motomoto za familia yote ya Mungu katika
kutangaza, kuadhimisha na kutekeleza Neno hilo.
1.2.8.
Hivyo katika Mwili wa Kristo tutashika nafasi yetu hasa, yaani kuwa moyo wa
maisha yake, wa utakatifu wake na wa utume wake.
1.3.
MAKANISA MAALUMU
1.3.1.
Kanisa Katoliki linaishi katika Makanisa maalumu ya Mashariki na ya Magharibi,
yenye sura mbalimbali kadiri ya mazingira, historia na utamaduni wa watu wake.
1.3.2.
Tuthamini utajiri huo wote na kuuzingatia hasa tunapohamia jimbo fulani ili
karama yetu istawi humo kama mahali pake, na kulijenga kweli.
1.3.3.
Popote pale tutekeleze kwa ushujaa karama yetu ya kinabii, tukitenda na kusema
kwa niaba ya Mungu, bila ya kufuata mkondo au kutaka kuwapendeza watu; lakini
kwa unyenyekevu pia, tukikubali waandamizi wa Mitume waifanyie utambuzi.
1.3.4.
Tukiongozwa na imani tuwapende na kujali kazi zao tatu za kutufundisha,
kututakasa na kutuchunga.
1.3.5.
Tuwe tayari kushirikiana nao katika ziara rasmi wanazotufanyia kwa maendeleo ya
utawa wetu ndani ya Kanisa.
1.3.6.
Tuwaone mapadri wao kuwa ni kaka zetu katika Kristo na tupokee kwa shukrani
huduma zao, hasa za maparoko wetu na za wale ambao askofu wa jimbo kwa
kushauriana na watumishi amewateua kuwa washauri na waungamishi wetu utawa
usipojitosheleza.
1.4
UMOJA WA KANISA
1.4.1.
Umoja wa Mungu katika nafsi tatu ni asili, kielelezo na lengo la familia yake
inayounganishwa na Roho wa upendo.
1.4.2.
Ubora wa Kanisa unategemea mafungamano yetu watoto wake, yaani jinsi
tunavyotunzana na kushikamana na kupendana, tunavyokaribishana na kujadiliana na
kuaminiana.
1.4.3.
Kwa ajili hiyo askofu wa Roma amekabidhiwa kundi lote la Kristo duniani, kusudi
alichunge kwa upendo, na kuliimarisha katika imani liwe nguzo na msingi wa
ukweli.
1.4.4.
Kwa ahadi yetu tunawajibika kuwapenda na kuwatii kwa namna ya pekee yeye na
Kanisa lake, tukijitahidi kujua na kutekeleza hati zote wanazozitoa.
1.4.5.
Sisi tunaoshuhudia uzuri wa kuishi kidugu, tujenge madaraja kati ya makleri,
walei, watawa na miundo yao pia, ili tufanye kwa nguvu ya umoja kazi ile kubwa
ajabu tuliyoagizwa na Yesu.
1.4.6.
Vilevile tujadiliane na kufahamiana, tushirikiane na hasa tusali na kutubu
pamoja na ndugu zetu wa madhehebu mbalimbali, kusudi ushuhuda wetu kwa Kristo,
amani yetu, uweze kuaminika hadi mafarakano yoyote yaishe kabisa.
1.5. TOBA YA KIFRANSISKO
1.5.1. Yesu Kristo akitangaza utawala wa Mungu aliwaita watu kuupokea kwa
kufanya mapinduzi ndani mwao, wakianza kuwaza, kupima mambo na kupanga maisha
kulingana na upendo wa Baba aliotufunulia.
1.5.2. Mwenyewe akamtuma mzee wetu Fransisko ili kwa mfumo wake alirekebishe
Kanisa ambalo ni takatifu, lakini pia linahitaji siku zote utakaso na
matengenezo, ili waamini wote watekeleze maishani sakramenti zilizowaweka wakfu.
1.5.3. Tuzingatie hazina ya kiroho ya mtakatifu huyo, kwa kuitimiza,
kuilinda, kuichimba na kuikuza moja kwa moja, halafu kwa kuwashirikisha watu
wowote ili wapate wokovu na utakatifu.
1.5.4. Ndani ya Kanisa jumuia zetu zijengeke kama mazingira ya toba juu ya
msingi wa ubatizo unaowezesha maisha yote yawe Pasaka, tukizidi kufia dhambi ili
kufufuka na Kristo kwenye uzima mpya.
1.5.5. Ingawa hatujui mwaliko wa Yesu wa kupoteza maisha yetu nyuma yake
utatufikisha wapi, tusifadhaikie mambo ya hesko, ila tumuachie Mungu wa faraja
zote na kusaidiana kidugu kubeba msalaba siku kwa siku.
1.5.6. Baada ya kufunga safari ya kuufikia upendo kamili, tushinde
kishawishi cha kujipongeza kwa urahisi na kusimama katikati, tukijua kwamba
tusiposonga mbele, tunarudi nyuma tu.
1.5.7. Kama alivyofanya mtakatifu Fransisko, kwa uongozi wa Roho na vipaji
vyake, tuvue utu wa zamani na vilema vyake, tukamvae Kristo na maadili yake,
hata kuchuma matunda ya Roho na kuonja heri za Yesu, malimbuko ya uzima wa
milele.
1.6. MFUASI MKAMILIFU WA YESU
1.6.1. Vizazi vyote vinamshangilia Maria mwenye heri kwa jinsi alivyosadiki
Neno la Mungu na alivyokubali kujiliwa na Roho Mtakatifu: hivyo amekuwa
kielelezo cha namna ya kupokea neema na kujiweka wakfu kwa Mungu.
1.6.2. Vilevile, akishiriki toka mwanzo maisha yaliyofichika ya Mwanae,
halafu akihudhuria matukio makuu ya utume wake, ametuonyesha namna ya kuungana
naye, hasa kwa kuyaweka na kuyatafakari katika moyo safi yale yote yanayomhusu
Yesu.
1.6.3.
Maisha yetu ya kiroho, ya kijumuia na ya kitume yawe na tabia hiyo ya Maria hasa,
ili tuweze kukua katika imani, tumaini na upendo tunavyofundishwa na Injili.
2. KUITIKIA WITO
2.1 NJIA YETU
2.1.1. Roho Mtakatifu anawaongoza watoto wa Mungu kumfuata Yesu kwa namna
maalumu na kuunda ndani ya Kanisa familia za kiroho zenye karama za aina nyingi.
2.1.2. Kwa neema yake sisi tunawajibika katika familia ile iliyoanzishwa na
mzee wetu Fransisko katika matawi mbalimbali, ili mataifa yote yazidi kushuhudia
utakatifu wa Kiinjili unaopatikana kwa kufuata nyayo za Yesu fukara tena
msulubiwa.
2.1.3. Ndiye kitabu kikuu ambamo Roho Mtakatifu anatufundisha maana na namna
ya kuishi, kupenda na kuteseka, hata kupokea kwa amani matakwa ya Baba katika
nafasi ngumu zaidi za maisha.
2.1.4. Kwa upendo wa pekee Mungu Baba anawavuta mfululizo wale anaowataka
waache vyote wakaungane kabisa na Mwanae kiroho na kimaisha, hasa kwa njia ya
utiifu, ufukara na useja mtakatifu, ambayo ni yake kabisa na ambayo yalimfaa
sana ayashike duniani.
2.1.5. Kama vile upendo huo, mambo hayo pia yanahusu maumbile yetu mpaka
ndani kabisa, tunapojisikia misukumo ya kujifanyia mipango, kumiliki vitu na
kupendana kijinsia.
2.1.6. Sisi tuliojaliwa karama hiyo hatuwezi kuithamini vya kutosha, lakini
tuipokee kwa shukrani na kumrudishia Mungu utu wetu wote ili uwezo wake
uuzidishe kwa manufaa ya umati.
2.1.7. Hivyo tutawaelekeza watu kushinda tamaa za utawala, mali na anasa,
ambazo zimo mioyoni mwa wote kutokana na dhambi ya asili, na ambazo zinawapeleka
kwenye maangamizi.
2.2. MIITO
2.2.1. Maisha ya Bwana na agizo lake vinaonyesha kwamba toka mwanzo swala la
miito mitakatifu ni la msingi kwa Kanisa, na kwamba sala ndiyo njia ya
kulikabili kwa hakika kabisa.
2.2.2. Tushiriki katika kazi za Kanisa kwa ajili hiyo, tukiwafundisha hasa
vijana waiombee miito, tukikaribisha na kuchambua wanaojisikia wito ili
tuwatagemeze waitikie vizuri, tukionyesha kwa matendo ubora wa kuishi na Yesu na
tukitambulisha karama yetu.
2.2.3. Kila wito ni mwaliko maalumu wa Mungu kwa mtu fulani ambao unaleta
furaha na tumaini kwake na kwa jamaa, na kudai zifanyike juhudi mpya uweze
kustawi kwa uaminifu wa wote.
2.2.4. Padri au shemasi asipokewe kabla mtumishi hajashauriana na askofu
wake; aliyewahi kuwa mtawa au mseminari asipokewe pasipo taarifa ya mkuu wa
shirika au gombera wa seminari husika.
2.2.5. Wafuatao hawawezi kabisa kupokewa: wenye umri chini ya miaka 18;
wasiopata ubatizo, kipaimara na ekaristi; wasio ndani ya ushirika kamili wa
Kanisa; wanaoingia utawani kwa kulazimishwa au kwa hofu kubwa au kwa udanganyifu;
wanaopokewa na mtumishi kwa misingi hiyo; wenye madeni yanayowashinda; wenye
mwenzi wa ndoa; wenye nadhiri za kitawa na wanashirika wa aina nyingine;
waliowahi kuwa na ahadi ya daima katika jamaa yoyote ya utawa watu.
2.2.6. Ni lazima hatua za kuingizwa katika maisha yetu, ambazo ni utakaji,
zoezi na uchipukizi, zifanyike chini ya walezi, ambao wawasaidie ndugu wapya
kupata kwa taratibu ujuzi na mang’amuzi vinavyohitajika ili waendelee na
safari ya kiroho kwa uhuru wa ndani ulio mkubwa zaidi na zaidi.
2.2.7. Kumrudisha nyumbani mtakaji na mwanazoezi asiyefaa ni juu ya mtumishi
tu, ila kwa sababu nzito za haraka ni pia juu ya mlezi akiwa na kibali cha
halmashauri ya jumuia husika.
2.3. MALEZI KWA JUMLA
2.3.1. Tangu mtu aingie utawani hadi kufa kwake anahitaji malezi ya
Kifransisko kamili iwezekanavyo kuhusu utu, Ukristo, utawa na umisionari, ili
asaidiwe kushiriki upendo wa Yesu hata msalabani kwa tumaini la kutimilika
kabisa katika ufufuko.
2.3.2. Papo hapo malezi yanalenga kumfikisha kwenye ukomavu wa kibinadamu
kama msingi ambao umwezeshe kujenga utawa, Kanisa na jamii.
2.3.3. Wakimtegemea Roho
Mtakatifu, aliyetumwa kuwa
mtendaji mkuu wa malezi, wahusika wote, yaani ndugu wenyewe waliopokea wito,
baraza na halmashauri ya jamaa, walezi na viongozi wa kiroho, tena jumuia nzima,
wawe na nia moja na moyo mmoja, wakishiriki vizuri kwa kuwajibika.
2.3.4. Wenyewe wajitahidi mfululizo kuitikia wito na kutumia vema misaada
wanayopewa ili kulingana na Yesu, katika nafasi muhimu za maisha na katika zile
za kawaida, katika utamu na ugumu wa kuishi pamoja na katika juhudi za kitume.
2.3.5. Ingawa maisha na malezi yetu yanategemea na kulenga moja kwa moja
tuambatane naye kuliko kufuata mwongozo wenye vipengele vingi, hata hivyo baraza
liandae mpango mzuri kwa kazi hiyo yote ambao utimilizwe na maandishi mengine
maalumu kwa kila hatua na nyumba ya malezi.
2.3.6. Utekelezaji wake uhesabiwe na baraza kuwa ndio wajibu wake wa kwanza,
hasa kwa kuwaandaa katika kila jamaa ndugu wa kutosha kwa kazi hiyo muhimu kama
nini ya kuwalea na kuwafundisha wenzao.
2.3.7. Halmashauri ya jamaa inapowatuma ndugu kuanzisha jumuia katika nchi
nyingine ihakikishe baadhi yao wafae kuwa walezi.
2.3.8. Wajue vizuri hasa njia ya Mungu ili kuweza kuwaongoza wale
waliokabidhiwa na jamaa; halafu wasilemewe na kazi mbalimbali wasije wakashindwa
kuwashughulikia ipasavyo.
2.3.9. Wawaonyeshe vizuizi vya wazi na vilivyofichika, haja ya kujikaza
mfululizo, lakini hasa uzuri wa lengo na thamani ya karama inayofikisha huko.
2.3.10. Walau katika nyumba za utakaji, zoezi na uchipukizi, halmashauri ya
jamaa iwateue pia wale wanaofaa zaidi kuwa vyombo vya Mungu kwa uongozi wa
kiroho, kutokana na uzoefu wao wa kusikiliza Neno lake, kutumia vipaji vya Roho
Mtakatifu na kufanya utambuzi.
2.3.11. Wanajumuia wengine wanapaswa kuwasaidia ndugu wapya kwa kuwapokea
kwa upendo, kuwaombea na kuwatolea mifano bora.
2.4. UTAKAJI
2.4.1. Utakaji lengo lake ni kuziba mapengo ya malezi ya awali ya mtu ili
wito wake uweze kueleweka, naye akiendelea nasi aifaidi hatua ya zoezi.
2.4.2. Mbali ya muda unaotumika pengine kufuata masomo kwenye shule na vyuo
mbalimbali, mtakaji aishi katika jumuia zetu kati ya mwaka mmoja hadi mitatu.
2.4.3. Wakati huo ajichunguze na kuchunguzwa kuhusu ukomavu wa kibinadamu na
wa Kikristo, yaani ushirikiano wa kidugu, bidii ya kufanya kazi, msimamo wa
kijinsia na wa kimapenzi, imani halisi ya Kikatoliki, juhudi za kiroho na hamu
ya kuokoa watu.
2.4.4. Baada ya kuvumbua maana ya utawa na aina zake, mtakaji aiombe kwa
maandishi halmashauri ya jamaa husika aanze zoezi la kujipatia mpaka ndani sura
hiyo.
2.5.
ZOEZI
2.5.1.
Katika mazingira ya imani, sala na kuhudumiana kidugu, wanazoezi wajifunze elimu
ya upendo ili kuwa na msimamo uleule wa Yesu: kujikana kwa furaha na kuwa
wanyenyekevu na wapole kwa wote na katika hali yoyote.
2.5.2.
Wasaidiwe kufanya hivyo kwa mafundisho ya Kikristo na ya Kifransisko, na hasa
kwa maongezi ya binafsi na mlezi, kusudi watambue wanavyopendwa jinsi walivyo,
pamoja na wanavyoweza kukomaa.
2.5.3.
Zoezi hilo linachukua miaka mitatu, ila kama pengine utahitajika mwaka wa nne
uongezwe.
2.5.4.
Mwaka wa pili mtumishi, kwa ombi la mlezi, anaweza kuwapeleka wanazoezi wakaishi
kijumuia sehemu nyingine, au anaweza kuwaruhusu wauruke wakikusudia kuweka ahadi
ya muda.
2.5.5.
Kwa vyovyote katika hatua hiyo utiliwe mkazo juu ya kusali na kutafakari kama
Yesu alivyofanya Nazareti alipojiandaa kujitoa kabisa kwa Baba ili kuondoa
dhambi ya ulimwengu.
2.5.6.
Miezi mitatu hivi kabla muda wa zoezi haujaisha, kila mmoja aiombe kwa maandishi
halmashauri ya jamaa aweke ahadi kwa siku zote za maisha yake au kwa muda
usiopungua mwaka.
2.5.7.
Kisha kupata taarifa ya mlezi ikiwa ni pamoja na maoni ya jumuia, halmashauri
hiyo ijadili ombi hilo na kulipigia kura za siri, ikizingatia kama kuweka ahadi
kutamsaidia mwanazoezi kupenda zaidi au kutamuelemea.
2.5.8. Mwanazoezi
akikubaliwa,
kabla hajaweka ahadi ya muda amuachie mtu yeyote kusimamia na kufaidi mali zake
binafsi, pia aandike wasia wake; baada ya hapo atahitaji sababu zinazoeleweka na
ruhusa ya mlinzi ili kubadili alivyoviamua.
2.6. KUWEKA AHADI
2.6.1. Siku ya kuweka
ahadi,
mhusika awe ametimiza miaka 23 na kushauriana na ukoo wake walau kwa njia ya
barua; kwa ahadi ya daima awe amepata kibali cha ndugu zake wanaohusika zaidi.
2.6.2. Wakati wa Misa
atimilize ahadi za ubatizo kwa kujifunga hadharani kushika Injili kijumuia
kadiri ya Kanuni na Maisha ya Ndugu wa Kiume na wa Kike wa Utawa Hasa wa Tatu wa
Mtakatifu Fransisko, iliyokubaliwa na papa Yohane Paulo II, na kadiri ya katiba
hii.
2.6.3. Ahadi hiyo kwa Mungu
haimwajibishi aliyeiweka tu, bali pia jamaa iliyoipokea kwa niaba ya Kanisa,
kuhusu kuyafikia malengo ya wito wake, hasa kwa kumpatia mazingira na malezi ya
kufaa.
2.6.4. Kwa kuweka ahadi ya
muda tunataka kufuata njia ya upendo kamili bila ya vipingamizi kusudi tuungane
zaidi na Yesu ili azae matunda mengi ya utakatifu ndani mwetu; vilevile tuungane
zaidi na Kanisa na umisionari wake kadiri ya wito wetu.
2.6.5. Ahadi ya muda inaweza
kurudiwarudiwa bila ya mwisho: pia inaweza kuwa nafasi ya kukomaa ili baadaye
tujitoe mpaka kufa.
2.6.6. Atakayeweka ahadi ya
daima baada ya kuweka ile ya muda ili ajiaminishe kwa Mungu kama sadaka ya
kuteketezwa kwa wokovu wa watu wote, ajiandae kwa miezi miwili ya kukusanya
mawazo na kusali kama Mitume walivyojiandaa kumpokea Roho Mtakatifu awafanye
mashahidi wa Kristo mpaka mwisho wa dunia.
2.6.7. Kwa ahadi ya daima
tunaitikia kwa moyo usiogawanyika upendo wa Mungu Baba, kwa mfano wa Mwanae
aliyependa upeo na kwa karama maalumu ya Roho Mtakatifu; tunawekwa wakfu kwa
namna mpya na ya pekee kwa njia ya Kanisa; pia tunapokewa na utawa moja kwa moja
kama familia yetu mpya, na kujitoa kikamilifu kwake, tayari kutumwa kokote
duniani.
2.6.8. Kabla ya kuweka ahadi
ya daima ndugu aandike hati ya kujinyima moja kwa moja mali yoyote, kwa kupanga
namna ya kuwagawia maskini vyote alivyo navyo na vile vitakavyopatikana baadaye
kwa kurithi; hati hiyo iwe na nguvu kuanzia siku ya kuweka ahadi hiyo.
2.6.9. Mtu ambaye alimaliza
zoezi au kuweka ahadi ya muda, halafu akaacha vilivyo utawa, akiomba kwa
maandishi kupokewa tena, halmashauri ya jamaa ikimkubalia impangie muda na
masharti ya jaribio, ambalo likienda vizuri imkubalie kuweka ahadi ya muda,
baadaye akipenda ile ya daima.
2.7. UCHIPUKIZI
2.7.1. Miaka mitatu inayofuata
zoezi itumike kuendelezea malezi kuhusu Neno la Mungu na maisha ya kiroho,
pamoja na ndugu kuzoea polepole kazi mbalimbali ndani na nje ya jumuia.
2.7.2. Hizo zipangwe na
kutekelezwa hasa kwa manufaa yao, si kulingana na mahitaji ya sasa hivi ya jamaa
au ya watu wa nje, wasije wakalemewa.
2.7.3. Mwelekeo wa sala na
toba utawale hatua hiyo pia, ili wazidi kujitoa kwa upendo kadiri ya ahadi yao,
na kujiandaa kukabili yale yote yatakayoweza kutokea maishani, hasa katika
mazingira magumu.
2.7.4. Ihakikishwe kuwepo kwa
nyakati maalumu za watawa chipukizi kukaa faraghani ili kusali, kutafakari na
kuchimba mafundisho waliyoyapata.
2.8. MALEZI MAALUMU
2.8.1. Mungu ameunda utawa
watu naye anaufanya upya siku kwa siku kwa kutuangazia tuyashike maisha ya
Kiinjili ya Kifransisko, ambayo ni lengo kamili tena ni lazima liwe la kwanza
kwa yeyote anayejiunga nasi.
2.8.2. Pamoja na
hayo, ikiwa
ndugu ameitwa kweli awe pia padri au shemasi au kutoa kuduma nyingine ya
Kikanisa, mtumishi ampatie malezi yanayotakiwa awe mhudumu kadiri ya moyo wa
Mungu, aliye tayari kumwakilisha Kristo kwa uaminifu na ukarimu; uamuzi wa
mwisho ni juu ya askofu, lakini daraja inakusudiwa kutolewa kwa maisha na
umisionari wa utawa wetu, sio kwa ajili ya jimbo lake tu.
2.8.3. Vilevile ikihitajika
mmoja wetu akasome fani fulani, halmashauri ya jamaa imteue ndugu ambaye kwa
ukomavu wake anatumainisha kwamba ataendelea kuwa kielelezo cha wito wetu.
2.8.4. Chini ya mlezi hao wote
wakabili matatizo ya kipindi cha masomo, wakiangalia hasa yasidhuru roho ya
ibada na sala, wala yasiwavimbishe, bali yawaongoze kumshiriki zaidi Mungu
anayejifunua kwa wadogo, na yawaandae kuwahudumia watu vizuri zaidi.
2.9. MALEZI YA KUDUMU
2.9.1. Utawa unapaswa
kuwasaidia ndugu wote kwa mwendo wake wa kila siku na pia kwa njia ya kozi,
semina, mikutano na mang’amuzi mbalimbali ili wito wao wa Kifransisko ustawi
mfululizo na utume wao ufae daima katika mabadiliko ya mazingira.
2.9.2. Kila mmoja
wetu, kadiri
ya uwezo na majukumu aliyonayo, awajibike kujiendeleza katika yale yanayomhusu,
kwanzia maisha ya kiroho ambayo ni ufunguo wa malezi yote kwake na kwa wengine.
2.9.3. Tuamini kuwa Mungu Baba
anailisha familia yake kwanza kwa Maandiko Matakatifu, ambamo anaongea nasi
mfululizo ili kutuingiza katika ushirika naye na kutujulisha matakwa yake kwa
maisha yetu.
2.9.4. Kila siku tushike
mikononi Biblia takatifu, tukilenga kwa unyenyekevu kuielewa kulingana na imani
ya Kanisa na mazingira yetu, ili tumfahamu Kristo ambaye ndiye Neno.
2.9.5. Halafu tupendelee
kusoma maandishi ya Ualimu wa Kanisa, ya mababu wake, ya walimu wakuu wa maisha
ya kiroho na habari za watakatifu, hasa Wafransisko, tukijitahidi kutekeleza.
2.9.6. Tushibe hayo kwa pamoja
walau mchana au jioni tunapolisha miili yetu, isipokuwa kwenye Jumapili, sherehe
na nafasi nyingine za kufaa.
2.9.7. Kwa mwanga huo wa
Kiinjili Roho wa hekima atatuwezesha kutambua hali ya ulimwengu na dalili za
nyakati zetu, kuchambua yanayotokana naye na yanayopingana naye, na kufurahia
jinsi Baba anavyoongoza yote ili mabaya pia yaweze kuleta mema.
2.9.8. Tutatambua pia tukabili
vipi matukio yoyote, kwa kumtumainia kama kwamba yote yanamtegemea yeye tu, na
kwa kuwa kuwajibika kama kwamba yote yanatutegemea sisi.
2.9.9. Kwa ajili
hiyo, vitabu
na magazeti machache vyenye msimamo wa Kikatoliki kweli viwepo tayari kwa faida
ya wote.
2.10. UAMINIFU
2.10.1. Kila mtawa wetu ana
wajibu na haki ya kutimiza wito wake, na kushiriki katika maisha na utendaji wa
jamaa na ngazi zake, kadiri ya katiba hii.
2.10.2. Adili la ibada na amri
ya kwanza ya Mungu vinatudai tutekeleze yale tuliyomuahidia ili kumuonyesha
heshima na upendo inavyotupasa.
2.10.3. Ili tutamani zaidi
kufanya hivyo na kuwajibika kulingana na sheria ya moyoni, ambayo ni Roho
Mtakatifu mwenyewe, kila siku tusome kwa pamoja sehemu ya katiba; halafu mara
moja kwa mwezi turudie ahadi yetu baada ya kusoma kanuni nzima, onyo na laana
vya mtakatifu Fransisko.
2.10.4. Tujiombee neema za
kuzishika, tuzitafakari mara nyingi na kuziongelea katika mikutano yetu, ili
zipenye zaidi na zaidi maisha ya kila mmoja na ya jumuia nzima na kutusaidia
kulenga utakatifu na kufanya utume anavyotutaka Mungu.
2.10.5.
Kwa uaminifu wake yeye hawezi kughairi kuhusu wito bora aliotujalia; vilevile
sisi tuwe waaminifu kwake tukitegemea neema tusiyoweza kupungukiwa, mradi
tukeshe na kusali pasipo kuchoka.
2.10.6.
Kwa hakika kizo tupige mbio kwenye njia nyembamba ya uzima, ili kujinyakulia
taji lisiloharibika, tukijua wengi wanaingia uwanjani bila ya kufanikiwa.
2.10.7.
Tujihadhari na uvuguvugu ambao ni mwanzo wa uasi, tena tusifuate mitindo ya
ulimwengu, bali tuzidi kujitoa kama sadaka hai, takatifu na ya kumpendeza Mungu.
2.10.8.
Kanzu tunayoivaa usiku na mchana, na mtindo wetu wa kifukara kwa jumla,
vimekusudiwa kutusaidia tudumu katika wito wetu, halafu kushtua na kufikirisha
watu.
2.10.9.
Hivyo tusivionee aibu ila tuangalie moyo wetu ulingane na sura ya nje kadiri
inavyoonyesha unyenyekevu na usafi.
2.11.
KUTENGANA NA UTAWA
2.11.1.
Ndugu mwenye ahadi akiwa na shida anaweza kuomba kwa maandishi muda wa kujitenga
na jamaa; baada ya mtumishi kuongea naye na kumpa nafasi ya kufikiri,
halmashauri ya jamaa ikate shauri kwa upendo na busara, ambalo liandikwe katika
rejesta na kuarifiwa kwa ndugu mhusika; hapo haki na wajibu vilivyotokana na
ahadi yake vinasimamishwa, isipokuwa haruhusiwi kufunga ndoa; muda aliopangiwa
ukiisha anaweza kuomba apokewe tena; asipoomba au asipokubaliwa, atoke moja kwa
moja utawani inapoelezwa hapa chini.
2.11.2.
Muda wa ahadi ukiisha, ndugu ana hiari ya kuacha utawa, na vilevile halmashauri
inaweza kumkatalia asiirudie au asiweke ahadi ya daima zikiwepo sababu zenye
msingi.
2.11.3.
Mwenye ahadi ya daima ambaye kwa sababu nzito anataka kuacha utawa, kisha
kushauriana na mtumishi wake, amuombe askofu wa jimbo anamoishi kitawa, ambaye
anaweza kumruhusu kwa kuwasiliana na halmashauri ya jamaa.
2.11.4.
Ndugu ambaye ameasi kabisa imani au amejitenga au ametengwa rasmi na ushirika
kamili wa Kanisa au ametoroka utawani, amepoteza papohapo kazi alizokuwanazo
utawani na haki zake kama mwanajumuia; mtumishi ajitahidi kumrudisha kwa kuwa
anapaswa bado kutimiza ahadi yake; ikishindikana amtumie barua ya tahadhari
kwamba ataondoshwa, ambayo isipoleta mafanikio baada ya mwezi mmoja halmashauri
ya jamaa imuondoe rasmi; aliyeachishwa anaweza kumkimbilia askofu wa jimbo
alimokuwa anaishi kitawa, na hivyo kusimamisha utekelezaji wa uamuzi huo, mradi
asichelewe zaidi ya siku kumi baada ya kuarifiwa.
2.11.5.
Kwa sababu nyingine nzito, wazi, zenye dhambi na thibitisho, zilizoorodheshwa
katika sheria zetu ndogondogo, mtumishi afungue kesi mbele ya halmashauri yake,
akimpa mhusika nafasi ya kujitetea, halafu awasilishe hati zote kwa askofu wa
jimbo anamoishi kitawa ili aondoshwe.
2.11.6.
Aliyetengana moja kwa moja na utawa kwa namna yoyote ile, hana tena wajibu na
haki vilivyotokana na ahadi yake, wala hawezi kudai chochote kwa kazi
alizozifanya utawani.
2.11.7.
Upande wake jamaa iwajibike kutumia upendo na usawa kwa ndugu yeyote aliyeiacha,
hasa kwa aliyekaa muda mrefu, ikimsaidia kukabili maisha na kuendelea katika
safari ya kiroho.
2.12. BIKIRA
MWAMINIFU
2.12.1.
Kisha kumfuata Yesu mpaka Kalivari, Maria alituzaa kwa uchungu na kufanywa na
Mwanae kuwa mama wa kila mmoja wetu, hasa wa wale aliowapenda zaidi.
2.12.2.
Toka mwanzo wa kukaa utawani tumpokee upya kama mama tukimpenda na kumuiga,
tukimfunulia siri za maisha yetu na kumuomba atulee kama alivyomlea Yesu.
2.12.3.
Kwa hisani yake atatushirikisha upendo ule unaowezesha kumtolea Mwanae maisha
yote bila ya kujitwalia tena hata chembe; kujiaminisha kwa Baba na kwa matakwa
yake hata msalabani; halafu kufurahia maajabu anayotutendea kwa Roho Mtakatifu.
2.12.4.
Furaha hiyo kudumu katika majaribu kutahakikisha ubora wa kuishi kwa ajili ya
Mungu tu, kutavuta miito mingine, na kuuelekeza ulimwengu njia za kugeuka sura
uwe ufalme wake.
3.KUMUONEA
KIU MUNGU
3.1.MUUNGANO
NA MUNGU
3.1.1. Kwa kuwa Yesu alidumu
moja kwa moja katika muungano wake na Baba, aliingiza duniani ile ibada kamili
katika Roho na ukweli inayompendeza.
3.1.2. Mwenyewe anaendelea
kufanya hivyo kwa njia ya Kanisa lake, akitupelekea Roho Mtakatifu atusaidie
sisi viungo vyake katika udhaifu wetu, na kutuongoza hata hali ya juu ya
muungano na Mungu, kama alivyomjalia Fransisko, mtu aliyefanyika sala, ambaye
alikuwa akimuona Mungu ndani ya vyote na vyote ndani ya Mungu.
3.1.3. Kwa kuwa tumeitwa
kufuata nyayo zake, tuchague kile ambacho peke yake ni cha lazima: kumjua kweli
Yesu anayetuvutia kumpenda na kumtangaza ulimwenguni kote, kwa kuwa ni mzuri
kuliko wanadamu wote na hakuna mwingine aliyewahi kusema vema kama yeye.
3.1.4. Katika sala tuzingatie
hasa alivyojishusha kwa ajili yetu, akikabili magumu yoyote hadi kilele cha
maisha yake msalabani, ambapo upendo wa moyo wake safi ulifikia upeo, ufukara
wake ulikuja kukosa yote kabisa, na utiifu wake ulijitoa mhanga.
3.1.5. Sala zetu zote
zilingane na liturujia, zitokeze karama ya udugu na udogo, na kuzilisha roho
zetu kwa mapokeo bora ya Kifransisko.
3.1.6. Tunasali kweli kama
ndugu tukiwa roho moja na mojo mmoja: na kama wadogo tukishiriki hali ya
wanaodhulumiwa na kumlilia Mungu usiku na mchana awapatie upesi haki zao.
3.1.7. Tuwaombee wenzetu
wote,
wazima na wafu, pasipo kubagua maadui, kwa kuwa nguvu ya sala ni upendo.
3.1.8. Tuwavute waamini kwenye
maji hai ya sala ili maisha yao ya kiroho yastawi kweli, kwa kuwa anayesali
ataokoka, lakini asiyesali atapotea kwa sababu anabaki pweke na unyonge wake.
3.2 LITURUJIA
3.2.1. Sala, ambayo ni pumzi
ya roho zetu na ya jumuia pia, kiini chake kiwe liturujia, na hasa ekaristi, kwa
kuwa ndimo kazi ya wokovu inamozidi kutendeka.
3.2.2. Upande wetu liturujia
ni jibu la kijumuia kwa Mungu, kilele cha utendaji wa Kanisa na chemchemi ya
uwezo wake wote.
3.2.3. Ukweli wa maneno hayo
unategemea jinsi imani inavyozingatia mafumbo yanayoadhimishwa; pia unachangiwa
na ubora wa ibada.
3.2.4. Mtindo mwepesi wa
Kifransisko unaosisitiza upendo kuliko fahari za ibada, uendane daima na heshima
inayodaiwa na kazi hiyo ya Kimungu.
3.2.5. Kwa kuwa liturujia
ndiyo uwanja wa kwanza wa urekebisho na utamadunisho wa Kanisa, tutie maanani
uzuri wa ishara zake mbalimbali, tukihusisha mwili na hisi zake; tufanye
mabadiliko yale yanayokubalika na kutumia nafasi za kimya; tuimbe kwa moyo na
sauti, tukipiga ala zetu za muziki za kuadhimishia ushindi wa uzima dhidi ya
mauti.
3.2.6. Kila siku tushiriki
kijumuia sadaka ya Misa au walau meza ya ekaristi, ambapo tujitoe kabisa kwa
Yesu anayejitoa kwetu kwa upendo mnyenyekevu, ili tupate nguvu mpya za
kumtumikia maishani.
3.2.7. Kwa ajili hiyo
tujiandae kwa makini, halafu tukae tukimshukuru kwa muda usiopungua dakika
ishirini, ili tuimarishe muungano wetu naye.
3.2.8. Zaidi
tena, matunda
tunayoweza kuchuma humo yanategemea usafi wa upendo wetu; basi, tuadhimishe kwa
imani na unyofu sakramenti ya upatanisho kila baada ya wiki moja au mbili, ili
kutengeneza upya roho na jumuia zetu.
3.2.9. Ili maisha yetu yote
yawe wimbo wa kushangilia uzima mpya tuliojaliwa, mwendo wa kila siku wa jumuia
zetu zote uongozwe na maadhimisho ya pamoja ya vipindi vyote vya Sala ya Kanisa
vinavyompasa padri.
3.2.10. Tusali kila kipindi
kwa wakati wake na kuamka usiku wa manane kwa Kipindi cha Masomo.
3.2.11. Tunatakiwa kusali kila
mtu peke yake vipindi vile ambavyo tumeshindwa kuviadhimisha pamoja na ndugu
zetu.
3.2.12. Hivyo tutakuwa mfano
wa Kanisa ambalo linamsikiliza Mungu na kufanya ukumbusho wa fumbo la wokovu,
likimsifu na kumuomba kwa umoja kwa ajili ya wote.
3.3. SALA YA MOYO
3.3.1. Katika kushiriki kabisa
liturujia tujifunze kustawisha zaidi na zaidi uongofu wetu na sala ya moyo.
3.3.2. Tusali hivyo kwa pamoja
kila siku, tukiwa na Yesu ekaristi ili tulingane na mawazo ya moyo wake.
3.3.3. Katika kuongea na Baba
kama watoto tutamani kuwaka kwa upendo wake kuliko kuangaziwa tu maneno na
matendo aliyojifunua kwetu.
3.3.4. Tumtegemee kama maskini
Roho Mtakatifu na kujitahidi ili nafasi hizo zifanikiwe kabisa, lakini tukipatwa
na majaribu yoyote tusikate tamaa, kwa sababu tunaamini kuwa tukidumu kwa
uaminifu tunaupokea vilevile upendo wa milele unaotufinyanga kimyakimya.
3.3.5.
Pengine, badala ya kunyamaza, tutamke kwa sauti yale yanayotutoka moyoni kumuelekea mpenzi wetu
ambaye amekuwa kwetu hekima, uadilifu, utakatifu na ukombozi.
3.4. MATENDO YA TOBA
3.4.1. Ili tuwe watu
wapya,
wenye uhuru wa ndani na amani ya kweli katika kuungana na Mungu, ni lazima
tujifahamu na kujitawala, kutambua jinsi dhambi zinavyomchukiza, kutubu kwa moyo
na kuzaa matunda ya toba katika maisha ya kila siku.
3.4.2. Katika kupanga juhudi
zetu, badala ya kujitafutia msalaba unaotupendeza, tuweke mbele kutekeleza amri
ya upendo kwa wote, kuwajibika kadiri ya ahadi yetu, kufanya kazi kwa uaminifu,
kupokea kwa furaha kamili matatizo ya maisha: usumbufu wa mazingira, ugonjwa na
uzee, misiba na vishawishi, masikitiko yanayosababishwa na wenzetu, na hasa
dhuluma kwa ajili ya Kristo.
3.4.3. Kwa kuwa ni lazima sisi
watawa tujikaze kuliko waamini wengine, tena kwa pamoja, mbali ya kushika siku
za toba walivyoagizwa hao pia, tufunge chakula mchana Kwaresima nzima; halafu
kila Ijumaa ya mwaka tufunge chakula na kujinyima nyama na vingine vya gharama;
isipokuwa siku za sherehe na Jumapili hatulazimiki.
3.4.4. Kwa njia hiyo
aliyoifuata Kristo mwenyewe kisha kutumwa rasmi na Baba, akisukumwa na Roho
Mtakatifu kushindana na Ibilisi, roho zetu zinakuwa wazi zaidi kwa Mungu na kwa
jirani, na kupata nguvu za kushinda mwili, ulimwengu na shetani.
3.4.5. Ili tuwe daima na
kiasi,
tule vya kutosheleza mahitaji ya mwili tu, sio vya anasa na kunoga mno; nje ya
vipindi vitatu vilivyopangwa kwenda mezani tusile wala tusinywe kinywaji
isipokuwa maji.
3.4.6. Tukimkumbuka aliyekosa
pa kupumzikia, tutumie kilalio kigumu hafifu, isipokuwa katika ugonjwa.
3.4.7. Ili kudumisha juhudi
zetu tufanye kila siku malipizi ya hiari pia, kufuatana na shauri la kiongozi wa
kiroho na pengine kwa ruhusa ya mlinzi.
3.4.8. Tuitunze afya
tuliyojaliwa na Mungu ili tufanye kazi katika shamba lake; ila tusiihangaikie
mno, kwa sababu tunapaswa kuzingatia kwanza mengine yaliyo muhimu zaidi na ya
milele; na kwa sababu tunaamini mateso yakipokewa kwa upendo yanatuunganisha
kabisa na Yesu katika kazi ya ukombozi na kuleta uzima tele.
3.4.9. Tujiandae kufa katika
Bwana saa na namna atakazopenda, kama tendo la mwisho la toba yetu hapa duniani.
3.5 UTULIVU
3.5.1. Ili tumsikilize kwa
makini Mungu kila anapopenda kusema nasi, na kuungana zaidi naye anayeishi ndani
mwetu, tunahitaji tusivurugwe na lolote lile moyoni.
3.5.2. Kusudi makazi yetu
yatusaidie kufikia hali hiyo ya ndani, tujitafutie mazingira ya utulivu halisi
na kuyalinda kwa ushirikiano wa wote.
3.5.3. Kwetu tuseme kwa shida
maalumu tu na kwa sauti ya chini, halafu tunyamaze kabisa katika vipindi na
mahali mbalimbali kadiri ya sheria zetu ndogondogo, kwa kuwa hata upendo
unatudai tusiwasumbue wanaohitaji kimya ili kusali, kusoma na kupumzika vizuri.
3.5.4. Tumkaribishe mgeni kwa
ukarimu wote, tukimtumikia Yesu katika kila anayepiga hodi, lakini mapokezi hayo
yasituhangaishe hadi kuzuia muungano wetu naye, taratibu za jumuia na
utekelezaji wa wajibu.
3.5.5. Kwa kawaida mgeni
asiingizwe ndani kabisa ya makazi yetu, isipokuwa aliyekubaliwa kufanya mafungo
kwetu.
3.5.6. Tukwepe urafiki wenye
maneno mengi mno; tusikae muda mrefu sebuleni, hasa jumuia inaposali; tusitoke
nyumbani bila ya lazima na ya ruhusa ya mlinzi.
3.5.7.
Mikutano ya jumuia itathmini na kulenga maendeleo ya maisha ya sala ili
tusaidiane na kukomaa pamoja.
3.6.
NAFASI ZA PEKEE
3.6.1.
Kulingana na watu, wakati, mahali na kazi maalumu, kila jumuia ipange ratiba ya
kila siku ambayo iidhinishwe na mtumishi, zikiwemo walau dakika 250 za sala za
pamoja, halafu nafasi fulani huru kwa ndugu binafsi.
3.6.2.
Mbali ya ratiba hiyo, zipangwe nyakati maalumu za kukaa na Bwana tu, ambazo
kadiri tunavyoishi kati ya watu zinahitajika ili zisafishe na kuimarisha upendo
wetu.
3.6.3.
Walau tufanye mafungo ya siku moja kila mwezi, na mazoezi ya kiroho ya wiki moja
kila mwaka; kwa kawaida tufanye hivyo kijumuia.
3.6.4.
Miaka kumi hivi baada ya kuweka ahadi ya kwanza, kila ndugu aruhusiwe kutumia
mwaka mzima katika mazoezi ya sala na toba tu, akiacha kazi maalumu na madaraka
yoyote ndani na nje ya jumuia.
3.6.5.
Katika safari ya kumuendea Mungu tuweze kupewa mida mingine mirefumirefu ya
kukaa naye jangwani, kwa mfano baada ya miaka kadhaa ya kuishi sehemu fulani au
kushika kazi fulani.
3.6.6.
Katika bara la Afrika ulipoanza umonaki, tuheshimu sana maisha ya kuzama katika
sala, ambayo yanadokeza kwa namna ya pekee uzima wa milele, Utatu mtakatifu
utakapokuwa heri yetu kamili kabisa.
3.6.7.
Kwa kuwa hata majimbo machanga yanahitaji mtindo huo wa maisha unaokamilisha
Kanisa, tupokee kwa furaha miito ya namna hiyo ikijitokeza kati yetu kulingana
hasa na kanuni iliyoandikwa na mtakatifu Fransisko kwa makazi ya upwekeni, au
ile ya mtakatifu Klara.
3.6.8.
Hasa bibiarusi kujifungia moja kwa moja mahali fulani ni njia maalumu ya kufia
ulimwengu ili kukumbatiana na Bwana mpenzi kwa niaba ya watu wote na kuwavuta
wamtafute kwa moyo wao wote.
3.7.BIKIRA
WA KIMYA
3.7.1.
Kwa nia ya kufanana na Bikira Maria, kielelezo cha wanasala, tutamani kutakaswa
na kimya ili tuwe tayari kupokea Neno la Mungu na paji la Roho Mtakatifu kwa
moyo usio na umimi.
3.7.2.
Tufuate kwa bidii himizo la Kanisa la kustawisha ibada, hasa za liturujia, kwa
Mama Maria.
3.7.3.
Kila siku tusali kijumuia Malaika wa Bwana mara tatu na thuluthi ya rosari, au
kufanya ibada nyingine ya Kimashariki.
3.7.4.
Kutoka kwa Maria tutajifunza kuzingatia kwa imani na kutimiza maishani mafumbo
ya Mwanae, hasa fumbo kuu la Pasaka, upendo wa Mungu ulipofurika ulimwenguni.
3.7.5.
Tukiungana na Mama wa Yesu katika sala, kama walivyofanya Mitume kabla ya
Pentekoste, tumuombe Roho Mtakatifu aufanye uso wa dunia uwe mpya, kuanzia mioyo
yetu.
4. KUZAA KWA KUPENDANA NA MUNGU TU
4.1.
KARAMA YA USEJA
4.1.1.
Wakati ule maalumu ulipotimia, Yesu mwenyewe alikuja kufunua jinsi Baba
anavyoupenda ubikira au useja uliotunzwa kwa ajili ya utawala wake, akampamba
bibiarusi wake kwa karama hiyo ya Roho Mtakatifu ambayo inafanya upendo wake
uonekane wazi na kustawi na kuzaa sana.
4.1.2.
Usafi katika useja unatusaidia kuungana na Bwanaarusi pekee kwa kushiriki zaidi
sala yake ya kudumu, maisha yake na Mitume na kazi yake ya wokovu,
aliposhughulikia matakwa ya Baba bila ya kizuio chochote, akitangaza ukweli na
haki pasipo hofu kwa familia yake, akiwapenda wote upeo, badala ya kujipendea na
kuwapenda baadhi ya watu tu.
4.1.3.
Kwa hiyo sio mzigo unaotulemea, bali ni fumbo la upendo na shauri la Kiinjili
tulilojaliwa kulielewa na kulipokea kwa furaha na moyo mkuu kusudi litupenye
mpaka moyoni tuje kufanana na Yesu kama ilivyomtokea mtakatifu Fransisko.
4.1.4.
Katika kutoa ushuhuda huo wa pekee wa uzima wa milele na wa kuwa Mungu
anatutosha kuanzia hapa duniani, tusijiamini kipumbavu bali tutegemee msaada
wake pamoja na kufuata masharti na kukwepa hatari.
4.2.
UPENDO WA MOJA KWA MOJA
4.2.1.
Useja uliowekwa wakfu kwa Mungu ni hali bora kuliko ule usafi wa moyo unaowapasa
wote; tena kwa uzuri unapita ndoa ya Kikristo, kama vile tumaini la ufufuko
lilivyo kuu kuliko matazamio yoyote ya binadamu katika maisha haya.
4.2.2.
Ukweli wake ni kuzidi kuchanganyikiwa na upendo wa Mungu na kung’amua kwa
imani jinsi anavyotaka tumrudishie, tukishiriki kabisa maisha ya Yesu mpaka
mwisho alipojitoa sadaka, yeye aliye mpenzi mkuu asiyependwa na watu.
4.2.3.
Kwa vile unatokana na upendo wa pekee na kuelekea matendo ya upendo mkarimu usio
na ubaguzi, useja mtakatifu unalishwa na upendo, hasa kwa kupokea sakramenti
ipasavyo, kujenga jumuia kama familia bora, na kujiwekea malengo makubwa ya
kitume.
4.2.4.
Kwa kuwa unadai usafi kamili wa mwili na wa roho, pamoja na kujinyima upendo wa
ndoa na uzazi wa kibinadamu, unamtaka mtu ajitahidi moja kwa moja kutekeleza
tunu za jinsia yake kwa namna bora isiyotegemea mwili, ila kule kujitoa kwa
upendo ambako ndiko ukuu wa binadamu.
4.2.5.
Usipohuishwa na kukomazwa mfululizo, unaweza ukaharibika upesi kutokana na
matatizo mapya ambayo yanazuka maishani katika hatua za mbele hata kufanya
uaminifu kwa ahadi uwe mgumu, kama vile inavyotokea kwa watu wa ndoa ingawa wana
sakramenti iliyowaunganisha.
4.2.6.
Hapo mtu anabaki hana kitu: wala upendo, wala ukomavu, wala uzazi wa kiroho au
wa kimwili.
4.3.
TAHADHARI
4.3.1.
Maisha yanaonekana ni vita vya kiroho visivyo na mwisho vya kudumishia uhuru
tuliojaliwa, kwa kuwa ushindi wa Kristo hauzimi kabisa tabia yetu mbovu
inayotokana na dhambi asili, wala hautuepushi na vishawishi vya ulimwengu na
utamaduni unaotawaliwa na yule mwovu.
4.3.2.
Hasa adili la useja, ambalo si la kawaida hapa duniani, ni lazima lilindwe na
nidhamu ya hisi na ya moyo, na maisha magumu ya kujinyima hata vitu halali,
pamoja na kuepukana na uvivu, utengano wowote na vilevile urafiki usiofaa.
4.3.3.
Toka mwanzo tuuzuie moyo wetu usimuelekee mtu yeyote kwa namna ya pekee, wala
usijidanganye kuhusu hiyo sumu tamu kwa visingizio vya kutaka kumpa au kupata
toka kwake msaada wa kiroho, kwa sababu shetani akijipatia unywele wetu mmoja
anaufanya upesi kuwa boriti.
4.3.4.
Tusisahau onyo la Mungu kwamba kushirikiana na watu wa jinsia ya pili bila ya
kuvutiwa visivyo na maumbile yao ni jambo gumu sawa na kutembea juu ya moto bila
ya kuungua nyayo.
4.3.5.
Katika utawa wetu, mafungamano kati ya waseja wa kiume na wale wa kike yawe
madogo iwezekanavyo, yakifanyika tu kwa njia ya ndugu wenye maadili imara
walioteuliwa na baraza.
4.3.6.
Kwa kufuata mfano wa Yesu na uongozi wa Roho Mtakatifu, katika mafungamano
yoyote tuoanishe adabu na uangalifu, wema na busara, upole na msimamo, uhuru na
usafi, tusije tukachafua kwa kitambo cha udhaifu uzuri wa moyo ulioambatana
kabisa na Bwana.
4.3.7.
Katika nyumba zetu watu wowote wa jinsia ya pili waruhusiwe kuingia tu kwenye
kikanisa, vyumba vya wageni, na sebule, ambayo iwe imetengenezwa kwa busara
sana.
4.3.8.
Pamoja na kuuheshimu mwili kama zawadi ya Baba, kiungo cha Kristo na hekalu la
Roho Mtakatifu, tutunze safi macho na mawazo vilevile.
4.3.9. Tusikubali hata kidogo aibu za ulimwengu ziingie ndani au kati yetu
kwa vyombo mbalimbali vya upashanaji habari, kama vile magazeti.
4.3.10. Tuepuke maneno yasiyowafaa watu waliojiweka wakfu kwa Mungu, na
matendo yanayoweza kuwatilia wengine shaka juu ya usafi wa maisha yetu,
tukizingatia pia mwongozo ambao pengine umetolewa na askofu kwa makleri na
watawa wa jimbo lake.
4.3.11. Tuwaonyeshe wote jinsi usafi wa moyo unavyowezekana na unavyochangia
ukomavu wa binadamu, kwa sababu jinsia haitakiwi kuchezewa wala kuabudiwa, bali
inakusudiwa kuwa njia ya upendo yaani kujitoa kwa jirani na kumpokea kwa heshima.
4.4
BIKIRA, MKE NA MAMA
4.4.1
Roho Mtakatifu aliweza kumfanyia kazi Bikira safi bila ya kuzuiwa naye hata
kidogo, akamjalia kujaa upendo na kumzaa Bwana wa uzima.
4.4.2.
Tutamani sana usafi huo ili Roho amtunge Neno ndani mwetu pia, tukamlete kwa
wenzetu kama Maria alivyowaletea akina Elisabeti.
4.4.3.
Mwishoni, tutoe ushuhuda kuwa wale wote waliompitia Maria kwa unyenyekevu na
tegemeo katika kuomba neema ya usafi, wameona maombezi yake yalivyo na uwezo.
5. KUTUMIKIA NA KUFANYA KAZI
5.1.
NEEMA YA KAZI
5.1.1.
Yesu kwanza alifanya kazi kwa mikono yake, halafu akahubiri Injili na kusaidia
wenye shida.
5.1.2.
Hivyo alishiriki utendaji wa milele wa Baba yake katika kuumba, kudumisha na
kukomboa ulimwengu, tena alizitia heshima mpya kazi zote za binadamu.
5.1.3.
Sisi tunaotamani kukaa naye milele, tujiandae kukutana naye kwa kuwa sasa
watumishi wema na waaminifu kwake, kwa Kanisa, kwa utawa wetu na kwa wenzetu
wote.
5.1.4.
Tukizitumia kwa faida talanta tulizokabidhiwa na Bwana, kwa mfano wa mtakatifu
Fransisko, tusali pasipo kikomo, tutangaze Injili, tusaidie wenye tabu na
kufanya shughuli nyingine pasipo uvivu wowote.
5.1.5.
Tukiamini kuwa kazi ni wajibu na haki ya kila mtu ili apate maisha anayostahili,
tutoe mchango wetu ili wote wapate nafasi hiyo, halafu utekelezaji wake uheshimu
na kukamilisha utu wao.
5.1.6.
Hivyo kwa maisha ya kila siku tutaonyesha shukrani kwa Muumba wetu na kumfuata
Mwanae aliyekuja si kutumikiwa, bali kutumikia hata kutoa uhai wake.
5.2.
KUOKOA MUDA
5.2.1
Kisha kupata hakika ya kuwa Mungu ametuchagua tupende, tusifu na kutumikia tu,
tumejitolea muda anaotujalia usiwe mali yetu tena, bali wa kwake na wa wenzetu.
5.2.2.
Tujitahidi kutumia kila dakika ya maisha yetu kwa utukufu wake na kwa maendeleo
kamili ya binadamu, kwa kuwa ni nafasi ya kutenda mema ambayo haitarudi.
5.2.3.
Tukijua wokovu unatujia kwa nyakati maalumu kadiri ya mpango wa Mungu,
tujitahidi kutambua kila wakati unatutaka tufanye nini.
5.2.4.
Tuangalie tusizame katika kazi fulani, bali kuwe na uwiano mzuri kati ya mambo
yote ya maisha yetu: sala na kazi za mikono, utume na malezi ya kudumu, halafu
pumziko pia.
5.2.5.
Tuchangie burudani fupi za kila siku wakati wa chakula au baada yake, na sherehe
za kifukara zinazotupa nafasi ya kupumzika kirefu zaidi na kukaa na ndugu zetu.
5.3.
UDUGU KATIKA KAZI
5.3.1.
Tukizingatia jinsi Bwana Yesu alivyokuwa akiwatuma wanafunzi wake wawiliwawili,
tuthamini faida ya kiroho na ya kitume inayotokana na utendaji wa kijumuia, na
tupendelee kufanya kazi kwa vikundi.
5.3.2.
Watumishi, walinzi na walezi ndio wenye madaraka ya karibu kuhusu kazi za ndugu
zao.
5.3.3.
Katika kuzichagua na kuzigawa washauriane na baadhi ya wenzao, wakizingatia wito
wetu wa kitume, mahitaji ya Kanisa na ya watu, udogo wetu unaotuelekeza kufanya
kazi duni, halafu ustadi na vipaji vya kila mmoja.
5.3.4.
Mlinzi kabla hajawatuma ndugu wakafanye kazi nje ya utawa, ahakikishe kuwa
wataweza kutimiza masharti yote ya maisha yetu, kama vile kuhudhuria kwa kawaida
sala za jumuia.
5.3.5.
Katika mikutano ya jumuia zetu tuarifiane kuhusu kazi tunazozifanya, ili wote
tushiriki katika kazi za kila mmoja, naye aone kuwa anazifanya kwa niaba ya
ndugu zake.
5.3.6.
Tusishike shughuli yoyote nje ya jumuia bila ya ruhusa ya mlinzi, na hata
tukiimudu sawasawa kazi fulani tangu siku nyingi, tuwe daima tayari kuiacha ili
kuzifanya nyingine ambazo huenda tukaagizwa.
5.4.
RIZIKI
5.4.1.
Yesu ametuhimiza tumtegemee Baba wa mbinguni, ambaye hatatuacha tukose mahitaji
yetu tukitafuta kwanza utawala wake na kushughulikia tabu za jirani.
5.4.2.
Basi, tusijitafutie riziki kwa mafadhaiko na mahangaiko, yasije yakasonga
kilichopandwa ndani mwetu yakatuzuia tusifanye utume na kazi nyingine ambazo
hazituletei faida ya uchumi, lakini zinadaiwa na upendo.
5.4.3.
Kadiri iwezekanavyo kila mmoja wetu afanye kazi za mikono, ambazo ni sehemu ya
maisha yetu kwa kuwa zinatuwezesha kutimiza udogo kwa kushikamana na fukara
wenzetu wanaopata hivyo riziki kwa ajili ya familia zao; pia zinatuwezesha kutoa
mfano mwema, kusaidia wenye shida na kustawisha utu wetu.
5.4.4.
Mapato na malipo ya kazi zetu yasipotutosha, tunaruhusiwa kupokea kwa shukrani
misaada ya lazima, hasa kwa ajili ya malezi, tukijitahidi wote kuitumia vizuri,
kuwashirikisha maskini na kutoa ripoti kadiri ya sheria za Kanisa.
5.5.
MAISHA YA KIJAMII
5.5.1.
Mwana wa Mungu kwa kutwaa mwili ameungana kimaisha na kila mtu, hasa fukara, na
kumfanya binadamu kuwa njia ya kukutana naye.
5.5.2.
Kanisa linapaswa kuwa la Kristo, katika Kristo na kwa ajili ya Kristo, kwa kuwa
la watu, kati ya watu na kwa ajili ya watu.
5.5.3.
Sisi pia tushikamane na mwenzetu yeyote na kushiriki katika maisha ya jamii kama
majirani na raia wema, tukiwajibika kwa ustawi wao, lakini bila ya kushika
mamlaka ya kiserikali wala kujiunga na vyama vya siasa au jeshi.
5.5.4.
Kwa namna ya pekee sisi watawa wa watu wadogo tuwapendelee akina Lazaro
walionyimwa nafasi duniani, ambao leo ni umati mkubwa.
5.5.5.
Kwa kuwa hasa katika sura yao tunamtambua Yesu mteswa, na katika sura yake
tunamtambua Baba wa mbinguni, hatuwezi kukubali sisi tujipatie mahitaji yote na
kuwaacha hao katika hali duni kijamii, kiuchumi, kielimu na kisiasa.
5.5.6.
Zaidi ya kuonja shida zao, tuwasaidie kupata kinga na matibabu, ufundi fulani,
malezi kwa watoto wao na huduma nyingine ndogondogo, tukishirikiana na ndugu
walei kadiri ya uwezo wetu.
5.5.7.
Tudumishe na kustawisha tunu bora za utamaduni wetu ambazo zinawaandaa watu
kupokea ujumbe wa Kristo na kujipatia maendeleo halisi.
5.5.8.
Tutie maanani hasa mila zinazoonyesha furaha kwa mtoto kuzaliwa, heshima kwa
uhai wa mtu, utunzaji wa mwenye shida, ujirani kwa mzee na aliye kufani,
mshikamano na aliyefiwa, halafu tumaini la uzima wa milele kwa marehemu.
5.5.9.
Kwa njia ya hisani yetu, Kanisa lionekane mama wa uzima na kuwasaidia wanadamu
wote waishi kama jamaa ya Mungu, ishara na utangulizi wa ulimwengu ujao.
5.6.
AMANI, HAKI NA UHAI
5.6.1.
Tujitahidi kuwapatanisha watu ili tustahili kuitwa wana wa Mungu, na kujenga
jamii juu ya msingi wa upendo.
5.6.2.
Tukiwa watu wa amani, tuwaelekeze wote njia yake halisi, yaani kuongoka kwa
kupokea huruma ya Baba, halafu kuwatolea wengine kwa kushinda ubaya kwa wema.
5.6.3.
Kwa kuwa amani ni tunda la haki na la mshikamano katika maendeleo, tusipatane
hata kidogo na aina yoyote ya dhuluma, ambayo daima inamlilia Mungu alipe kisasi.
5.6.4.
Tumkimbilie yeye kwa sala na sadaka ili azuie jeshi la uovu, yaani watu wale
ambao kwa visingizio mbalimbali wanapambana na utamaduni wa upendo na wa uzima,
tena wanakanyaga heshima na haki za msingi za binadamu, kuanzia wale wasiozaliwa
bado.
5.6.5.
Tuwasaidie walei watafute utakatifu katika siasa, ambayo ni namna muhimu ya
kutekeleza upendo, na wawajibike pamoja na watu wenye mapenzi mema ili kuleta
maendeleo kwa wote.
5.6.6.
Kwa kuwa bidii nyingi za namna hiyo zinakwamishwa na ushirikina, tusichoke
kumtangaza Kristo ambaye amewashinda pepo wote na kutupatia Roho wa upendo ili
tushikamane bila ya hofu.
5.6.7.
Yeye tu, kwa njia ya Injili yake na ya Kanisa lake, anaweza kutatua matatizo ya
ulimwengu ambayo ni makubwa kiasi cha kukatisha tamaa.
5.6.8.
Tukimtegemea yeye na ahadi zake, tuwatumainishe watu wetu, na hasa vijana,
kuhusu ukombozi kamili wa roho na mwili kwao na kwa wenzao.
5.6.9.
Tuwatie moyo wa kusaidiana, kutetea haki zao na kuipatia nchi maendeleo halisi,
ambayo yanategemea ukomavu wa binadamu na wa dhamiri yake kadiri ya tunu za dini,
maadili na utamaduni, kuliko pesa, misaada, teknolojia na kasumba.
5.6.10.
Wale ambao wananyanyaswa hata kuuawa wasiweze kusema kitu, tuwe sauti yao
tukiamsha dhamiri za wote ili wamjali binadamu na kumpokea kama ndugu anayeleta
baraka, wakimpenda na kushikamana naye hasa akiwa maskini.
5.6.11.
Tupende kidugu viumbe vyote, ambavyo ni zawadi ya Mungu kwetu na bila ya maneno
vinatangaza sifa zake, na tuwahimize wote kuhifadhi mazingira, la sivyo binadamu
wenyewe watashindwa kuishi tena duniani.
5.7.
HESHIMA YA WANAWAKE
5.7.1.
Kwa mpango wa Mungu, maumbile ya wanawake yamewaandaa kuelewa maana ya upendo,
yaani kujitoa kwa mwingine na kumpokea alivyo, kuvumilia mengi ili kumuachia
nafasi akue, bila ya kujali sifa alizonazo.
5.7.2.
Kumbe ubaguzi wa jinsia umezuia vipaji vyao visichangie kikamilifu ustawi wa
jamii na wa familia ya Mungu.
5.7.3.
Kufuatana na mfano wa Yesu, Mkombozi wa wote, tuungane na Kanisa katika azimio
la kuwarudishia akina mama heshima na nafasi wanazostahili.
5.7.4.
Tushughulikie malezi yao, tukijua kumuelimisha mwanamke ni kuwaelimisha watu
wengi kwa njia yake.
5.8. MAMA
WA HURUMA
5.8.1.
Mafungamano yoyote yanahitaji hasa huruma, iliyo sifa bora ya Baba yetu wa
mbinguni.
5.8.2.
Maria anafanana naye zaidi kuliko nafsi zote za kibinadamu, kwa kuwa amefikia
upeo wa upendo akiambatana naye katika maisha ya kila siku kijijini.
5.8.3.
Wimbo wake unatuvutia kila siku kuwa waaminifu kwa Mungu na kushikamana na
matarajio ya watu wadogo.
5.8.4.
Kufuatana na mfano wake mzuri ajabu wa hisani, huruma na ukarimu, tujitahidi
kuonja upendo wa Baba, na kuutangaza ulimwenguni na kuutekeleza vizuri kushinda
akina mama.
5.8.5.
Maria akiwa mwenyewe tangazo hai la huruma ya Mungu, alipokwenda tu kwa haraka
kumtumikia jamaa yake, alifanya kitoto kichanga na mama yake wajazwe furaha ya
Roho Mtakatifu.
5.8.6.
Sisi pia tulete faraja kwa kutumia nafasi yoyote ya kuwasaidia kwa unyenyekevu
wenye shida, kusudi uzuri wa Kimungu wa kuishi kwa upendo useme katika mioyo ya
watu kabla midomo yetu haijamtangaza Kristo kuwa ndiye jibu la maswali yote juu
ya maisha yao.
6. KUSHIKAMANA NA YESU FUKARA
6.1. HERI
YA KWANZA
6.1.1.
Mwenyezi Mungu aliwakabidhi wanadamu wote dunia na utajiri wake ili wajipatie
kwa haki mahitaji yao na kusaidiana katika shida.
6.1.2.
Toka mwanzo waliodhulumiwa na wenzao walipomlilia, yeye akawasikiliza,
akiwatumia watu kuwakomboa na kuwatetea na hatimaye Mwanae wa pekee ashiriki
moja kwa moja hali yao duni na kuwaelekeza njia ya wokovu.
6.1.3.
Mzee wetu Fransisko naye alijifanya fukara mdogo kati ya wakoma na maskini kwa
sababu ya kuwaonea huruma hao na kutiririka machozi akikumbuka Yesu mwenyewe
alivyozaliwa pangoni na kulazwa horini, halafu alivyoteseka uchi msalabani.
6.1.4.
Tukishikamana naye maskini hata leo, tutasikia njia na kiu ya haki, hata
tushughulikie ukombozi wake na kusimama imara dhidi ya upotovu wa ulimwengu
ambao kwa dai la kujiendeleza unakuja kuabudu mali na kumuangamiza binadamu.
6.1.5.
Bidii hiyo italifanya Kanisa liwe kweli la watu maskini, wanaokusudiwa hasa
kutangaziwa na kutangaza habari njema ya kuwa Mungu yu pamoja nao na pamoja na
wale wanaowapenda.
6.1.6.
Lenyewe linapaswa kufuata nyayo za Bwanaarusi wake hasa katika ufukara, ambao
pamoja na upendo ndio utukufu wake na ushahidi wa kuwa linajiona chombo cha kazi
ya Mungu kinachotegemea uweza wa Roho Mtakatifu tu.
6.1.7.
Kadiri ya Injili ufukara ndio heri ya kwanza na ardhi bora inayostawisha maadili
yote, maana unatushirikisha moyo na maisha ya Yesu vinavyotufunulia kikamilifu
utakatifu wa Baba.
6.2. KUWA
MASKINI WA ROHO
6.2.1
Ufukara wa Yesu unaonekana hasa katika kujitoa kabisa kwa watu na kumrudishia
Baba yote aliyopewa naye, hata roho yake.
6.2.2.
Tukiongozwa na Roho Mtakatifu nyuma yake, tumtamani Mungu tu na utukufu wake, na
kumaliza umimi wetu kusudi tusiishi tena kwa ajili yetu wenyewe, bali Kristo awe
anaishi ndani mwetu.
6.2.3.
Kwa kujiona kuwa si kitu, tujifanye wadogo wa wote na kukaa chini yao hata
wakituonea na kutudharau.
6.2.4.
Tuchanganyikane na watu wa mwisho, tukikubali kujifunza kutoka kwao unyenyekevu
na unyofu, udugu na ukarimu, subira na tunu nyingine.
6.2.5.
Tuwe daima tayari kuwapokea wenzetu na kushirikishana nao mema yale yote ambayo
Mungu ametukabidhi kwa faida ya wote.
6.2.6.
Ndipo unapotokea ule ufukara mkuu kuhusu mali unaodhihirisha maisha yetu ya
Kiinjili.
6.3.
KUBANA MATUMIZI
6.3.1.
Tukitegee masikio kilio cha maskini wanaoshindwa kushiba, tukitambua kuwa ni
sauti ya Mungu anayetuita upya kushiriki kijumuia maisha yao magumu na kuotesha
furaha na tumaini kwenye shida, badala ya kufanya moyo wetu kuwa mgumu na kuzoea
tu kuona watu fukara kuliko sisi wakitamani makombo mlangoni.
6.3.2.
Kadiri majirani wetu walivyo na mashaka tubane matumizi ili kuwashirikiska vitu
vingi zaidi, yaani sio tu vile vya ziada, bali hata nguo ya pili na chakula
chetu, na kila kitu tunachohitaji kwa kuishi, kwa sababu kutoa ni moyo, si
utajiri.
6.3.3.
Watu wakiwa na haja kuu, vitu vyote ni vya kwao pia, yaani vinatakiwa
kuwatimizia: kutokana na haki hiyo ya fukara, kila mmoja wetu ajisikie huru wa
kuwasaidia kulingana na utamaduni wa ukarimu walionao watu wetu, tusije
tukawakwaza bure kwa kuwaacha hivihivi bila ya kuwajibika kwa ajili yao.
6.3.4.
Kinyume chake, kwa matumizi yetu binafsi tunapaswa kuwa daima chini ya watumishi
na walinzi.
6.3.5.
Bila ya ruhusa yao tusiombe wala kutoa chochote kwa ndugu, marafiki na wengineo,
kwa kuwa tumejinyima haki ya kuwa na mali yoyote.
6.3.6.
Tusiwe watu wa kupenda umaskini mradi usitufanye tupungukiwe kitu, bali
tumshukuru Mungu kila anapotujalia kuonja ukali wa ufukara kama anapotujalia
kutimiza masharti mengine ya kitawa na majukumu ya kitume.
6.3.7.
Kusudi ionekane wazi hazina yetu iko mbinguni, na ufukara wetu maana yake nini,
tutumie vitu kwa kufuata kiwango cha chini, yaani kadiri ya lazima tu, si kadiri
ya uwezo tulionao.
6.3.8.
Kila ndugu anaruhusiwa kuwa na kanzu mbili au tatu, kamba, nguo ndogo za ndani,
joho na makubadhi; akina dada wanavaa pia shela; hakuna mavazi mengine
yanayokubalika, ila kwa ugonjwa; tena hayo yote yawe ya gharama ndogo na rangi
hafifu.
6.3.9.
Kabla hatujaomba ruhusa ya kutumia njia za mawasiliano na hasa kusafiri, tupime
mbele ya Mungu sababu za kufanya hivyo, tukizingatia ufukara wetu na masharti
mengine ya utawa.
6.3.10.
Hata kijumuia haturuhusiwi kumiliki au kusimamia mashine za kusafiria, kunasia
sauti au picha, kunakilia, kusafishia na vinginevyo vinavyokwenda kinyume cha
ufukara mkuu tulioitiwa, kwa kuwa si vya lazima, tena pengine ni vya gharama.
6.3.11.
Tujihadhari na kishawishi cha kulegeza ufukara huo, ambacho huenda kikatujia kwa
njia ya watu wanaotupenda, lakini mawazo yao kama yale ya Petro si ya Mungu ila
ya binadamu tu.
6.4 MFUKO
6.4.1 Kama vile Yesu na Mitume
walivyokuwa wakipokea misaada na kuwa na mfuko maalumu uliokabidhiwa kwa mhasibu,
Kanisa linatumia pesa na mali kwa ajili ya ibada, mahitaji ya wahudumu, utume,
na vitendo vya huruma hasa kwa maskini.
6.4.2. Kwa malengo hayohayo
jamaa na jumuia zetu pia zinaweza kutumia vitu na pesa, lakini kadiri
vinavyohitajika tu, hata wote waone kuwa tumekombolewa kutoka tamaa ya mali,
iliyo mzizi wa maovu yote.
6.4.3. Usimamizi wa pesa na
vitu ufuate sheria za Kanisa na za utawa wetu, na kadiri iwezekanavyo ukabidhiwe
kwa walei.
6.4.4. Halmashauri ya jamaa
iwateue katika ngazi zote mhasibu stadi na washauri wake wawili ambao wote
wafanye kazi hiyo chini ya mtumishi au mlinzi mhusika; katika jumuia isiyo na
ndugu wengi, mlinzi mwenyewe anaweza kuwa mhasibu.
6.4.5.
Kila baada ya miezi mitatu hao watoe ripoti kwa halmashauri ya ngazi ileile na
kwa mtumishi; kila mwaka baraza litoe ripoti kwa askofu wa Morogoro; mtumishi wa
jamaa atoe ripoti kwa mutano mkuu kila unapofanyika.
6.4.6.
Baraza lipange kiwango ambacho watumishi na walinzi wanaruhusiwa kuingia deni,
kutoa na kuuza vitu na kutumia pesa kwa mahitaji yasiyoingia katika kawaida ya
huduma zao kwa ndugu waliokabidhiwa; juu ya kiwango hicho wanapaswa kuomba
kibali cha halmashauri yao.
6.4.7.
Malipo, zawadi na vitu vyovyote vinavyomfikia ndugu kwa namna yoyote, avitoe kwa
mlinzi kwa manufaa ya jumuia nzima, ili tupate chakula, mavazi na mahitaji
mengine kwa usawa kadiri ya ufukara wetu, bila ya kusahau maskini.
6.4.8.
Matumizi yoyote ya pesa yanadai ndugu apate kwanza ruhusa ya mlinzi, halafu atoe
ripoti kwake.
6.5.
MAKAZI NA MAENEO
6.5.1.
Makazi tunayoishi yawe madogo na kulingana kwa ufukara na yale ya maskini
wanaotuzunguka, lakini yapendeze kwa usafi na utaratibu.
6.5.2.
Mlinzi asijenge chochote kabla hajaruhusiwa na mtumishi pamoja na halmashauri
yake, tusije tukapatwa na matatizo yale mazito yanayoelezwa na historia ya utawa.
6.5.3.
Kadiri iwezekanavyo nyumba na maeneo tunavyovitumia viwe mali ja jimbo au ya
wengine, tukikwepa ujanja wa kisheria na unafiki wowote katika utekelezaji wa
neno hilo la msingi.
6.5.4.
Tukilazimishwa kuhama, twende kwa furaha kumtumikia Mungu mahali pengine, badala
ya kutetea haki ya kumiliki tuliyoamua kujinyima moja kwa moja.
6.6.
KUWAJIBIKA KWA PAMOJA
6.6.1.
Ufukara mtakatifu ni kama hazina tuliyokabidhiwa ili tuitunze kwa uangalifu na
kuonyesha wazi kuwa si kujinyima tu, bali hasa ni sharti na tunda la kuwapenda
wenye shida alivyotufundisha Yesu.
6.6.2.
Katika mikutano ya ngazi zote tuhakikishe utekelezaji bora wa neno hilo kadiri
ya mazingira, kwa kuwa kulegea katika ufukara mwisho wake ni uvuguvugu wa roho
katika yote.
6.6.3.
Watumishi na walinzi wawatangulie ndugu zao katika njia hiyo ili wawe na haki ya
kuwahamasisha wote wawafuate.
6.6.4.
Ndugu wakikiri udhaifu wao wafurahi kumkaribisha mtumishi akitembelea mara kwa
mara kila chumba ili awasaidie kupunguza chochote cha ziada.
6.6.5.
Kisha kusikia mkutano wa jumuia, mlinzi akague mara kwa mara vitu vyote
ilivyonavyo, halafu akatoe vile vya ziada, tusije tukafanya dhambi kwa kujiwekea
akiba vitu vinavyohitajiwa haraka na wengine.
6.7.
MARIA FURAKA MNYENYEKEVU
6.7.1.
Kati ya mambo yanayotupendeza zaidi katika maisha ya Yesu, mojawapo ni jinsi
alivyoshika ufukara, akiwa ni Mwana wa Baba mwenye kuwakomboa maskini.
6.7.2.
Hata katika hilo alitanguliwa na Mama yake, kielelezo cha ufukara wa Kiinjili na
cha maadili yote yanayotokana nao, hasa unyenyekevu mpole na mnyofu, na uimara
mtulivu na mkarimu kwenye mashaka ya maishani.
6.7.3.
Wimbo wake wa furaha umekuwa shangilio la kudumu la wanyonge wote ambao
wametambua wanavyopendelewa na Mungu na wanatarajia mapinduzi yake.
6.7.4.
Tukilenga utakatifu kwa kufuata mifano ya Bikira Maria, tujitahidi kuwakaribia
kwa huruma ya kimama wasulubiwa wa siku hizi, badala ya kupita haraka kwenda
zetu tukiwaachia Wasamaria kujifanya majirani wa watu ambao wamevamiwa na kubaki
hoi kabisa.
6.7.5.
Tung’amue na kukiri wazi tunavyoshindwa kutimiza hata wajibu mkuu wa kuwapenda
kama tunavyojipenda
6.7.6.
Tuwahimize wote kurekebisha sana mitazamo na maisha yao ili wasisababishe Mwana
na Maria azidi kuteswa katika wadogo wake, hasa wale wa bara la Afrika ambao
ndio wa kwanza kushirikishwa naye msalaba wake kwa njia ya Simoni na Kirene.
7. KUISHI KIDUGU KATIKA JUMUIA
7.1.
UMOJA
7.1.1.
Yesu, mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi, alisali na kuonyesha njia ya
upendo, akatoa uhai wake, akampeleka Roho wake ili wana wote wa Mungu
waliotawanyika wawe kitu kimoja na Baba aliyemtuma.
7.1.2.
Habari njema tunayoiamini na kuitangaza ni kwamba yeye ametufanya kuwa familia
ya Mungu, yaani watoto wa Baba na ndugu kati yetu.
7.1.3.
Katika mishipa yetu inazunguka damu ileile moja, yaani damu ya Yesu Kristo; nasi
tuna uzima kwa roho ileile moja, yaani Roho wa upendo wa Mungu.
7.1.4.
Kanisa linahamasisha watu waunde vyama vya kila aina, na mataifa yashirikiane,
ili kustawisha utu wa kila mmoja na udugu kati ya wote, kadiri ya mpango wa
Muumba.
7.1.5.
Kwa namna ya pekee linapokea kwa shukrani karama ya maisha ya kijumuia ambayo
inajitokeza ndani mwake na kulidhihirisha fumbo lake, yaani kuwa Kanisa hasa ni
ushirika wa watu na Mungu na kati yao.
7.1.6.
Mambo yote yaliyo maalumu ya utawa yanahusika nayo: usafi katika useja
unatuwezesha kuwa wa kweli katika upendo wa kidugu, ufukara unatuongoza
kushirikishana yote, utiifu unajenga umoja, tena sala inatukusanya mbele ya
Mungu na utume unapata nguvu kwa ushuhuda wa pamoja.
7.1.7.
Tukimpokea Kristo mshindi kati yetu, tufufue na kueneza ule udugu halisi tena
mfurahivu ulioonekana wazi kati ya mtakatifu Fransisko na wenzake, na pia kati
yao na viumbe vyote, kama matokeo ya kuungana na Utatu mtakatifu.
7.1.8.
Kama wanafunzi wa Yesu wanaotambulikana mara, tuulenge daima umoja huo kwa
upendo ule ambao mwenyewe ametushirikisha kutoka kwa Mungu na kwa hiyo una nguvu
kuliko mauti.
7.1.9.
Hivyo wote wavutiwe na uzuri wa mpango wake huo na kuona namna za kuutekeleza
kwa kufungua tena njia za mawasiliano kati ya wale wasioelewana, mpaka upendo
ujaze ulimwengu.
7.2.
NEEMA YA UDUGU
7.2.1.
Jumuia za Kikristo asili yake si mapenzi au mipango ya binadamu, bali ni upendo
wa Mungu aliyewaita pamoja watu kadhaa, ili tofauti zozote kati yao zilete faida
kwa kila mmojawao, na umoja wao ushinde matokeo ya dhambi asili, hata uonyeshe
kwa namna fulani ule wa nafsi tatu za Kimungu.
7.2.2.
Yesu aliwaita Mitume kwa jina washiriki maisha yake kama kundi moja ambalo liwe
mbegu ya ushirika wake utakaokamilika mbinguni.
7.2.3.
Mwenyewe anazidi kutukusanya kila siku ili aseme nasi na kutuunganisha naye na
kati yetu katika ekaristi, ili tumfuate kwa umoja tunavyoelekezwa na karama
aliyotujalia.
7.2.4.
Tuko pamoja kwa jina lake, si kwa kuchaguana: basi tupokeane kwa shukrani kama
zawadi za Bwana, tukijisikia familia moja na kuitana sote ndugu, tukijifanya
kila mmoja mdogo wa mwenzie na kuungana katika malengo ya jumuia.
7.2.5.
Kumega mkate wetu wa kila siku, kusali pamoja, kufuata mafundisho na maagizo ya
wachungaji wa Kanisa na kushirikiana katika mambo yote kuonyeshe na kustawisha
upendo tulionao sisi kwa sisi na ambao utatutegemeza katika magumu yote ya
maisha yetu.
7.2.6.
Kama Kristo alivyotuletea umoja kwa mateso yake, mapingamizi yanayotupata katika
kuujenga tuyapokee kama nafasi za kuimarisha na kusafisha nia yetu ya kujitoa
mhanga kwa wenzetu.
7.2.7.
Kwa kujifanya chemchemi, kielelezo na kipimo cha upendo wetu, Yesu
ametuhakikishia kuwa tumependwa upeo na kuwa tunaweza kupenda upeo: upendo huo
unajenga jumuia siku kwa siku ukishinda udhaifu wetu.
7.3.
MAISHA YA KIJUMUIA
7.3.1.
Sisi kama jumuia ya kitawa si kundi la watu wanaojitafutia utakatifu wa binafsi,
bali utakatifu na ukomavu wetu unategemea kabisa utekelezaji wa upendo katika
maisha ya kijumuia.
7.3.2.
Hiyo si kazi rahisi au ya muda mfupi, wala haikamiliki hapa duniani: lakini
inawezekana daima kusonga mbele kwenye njia ya upatanisho na upendo.
7.3.3.
Hivyo maisha ya kijumuia ni safari ya ukombozi wa kiroho, ni tendo kuu la toba
yetu, ni shule tunapojifunza kuishi kidugu na watu wa nje pia.
7.3.4.
Kwa ajili hiyo tustawishe adabu njema, ukarimu, unyofu, upole, ukunjufu na
unyenyekevu.
7.3.5.
Tujitahidi kuheshimiana na kuelewana, kusikilizana na kuaminiana, kushirikishana
vipaji na madaraka, furaha na uchungu, mipango na matumaini.
7.3.6.
Katika kila ngazi tufanikishe mikutano ya kidugu na kujadiliana ili kufahamiana
zaidi, kuwaza na kupanga kwa pamoja, kukagua maisha yetu katika mazingira
tunamoishi, yaani Kanisa na ulimwengu.
7.3.7. Tuarifiane juu ya maendeleo na matukio ya jumuia zetu mbalimbali,
tukijua kuwasiliana ni njia ya kushirikiana.
7.3.8. Tusaidiane kila mmoja na mwenzie tukihisi na kushughulikia mahitaji
ya ndugu yeyote upande wa roho na wa mwili, hasa akiwa mgonjwa, mkongwe au
mwenye matatizo ya ndani.
7.3.9. Tusiwaonee kijicho ndugu waliojaliwa wingi wa neema na mafanikio,
bali tumshukuru Mungu kwa kuwa utajiri anaomjalia mmoja ni hazina ya jumuia
nzima.
7.3.10. Kadiri tunavyofaulu kudumu kwa umoja na furaha katika wito wetu,
tukilinganisha tofauti za umri, kabila, elimu, tabia na mengineyo, tunashuhudia
tayari kuwa utawala wa Mungu umefika.
7.4. NDUGU WA UKOO, MAREHEMU NA WATAKATIFU
7.4.1. Hata katika kuambatana na mpenzi wetu, anayeweza kutudai kuliko wote,
tuwaheshimu waliotushirikisha uhai, na tutimize kama wana wema wajibu wetu kwao.
7.4.2. Ruhusa za kuwatembelea zitolewe na mtumishi kufuatana na sheria zetu
ndogondogo na kwa kuzingatia hali yao, ahadi ya mwanao kuwa ya muda au ya daima,
kipindi kilichopita baada ya safari ya mwisho na mengineyo.
7.4.3. Katika haja za pekee, kisha kusikiliza halmashauri yake, mtumishi
awatolee misaada kwa niaba ya jamaa nzima, kwa kuwa tunawapenda wazazi wa kila
ndugu kama wazazi wetu sote.
7.4.4. Ushirika wa kidugu unadumu hata baada ya kutembelewa na ndugu kifo:
basi tumuombe Baba mwema awahurumie ndugu wa utawa na wa ukoo waliofariki dunia.
7.4.5. Tuwaheshimu kwa moyo wa ibada wazee wetu wa Kifransisko ambao
wametangazwa na Kanisa kwamba wako kwa Mungu na wanatuombea.
7.5. MAMA WA KANISA
7.5.1. Jumuia ya Yerusalemu ilipoanza, Bikira Maria alichangia umoja kamili
wa viungo vya Mwanae, akisali pamoja nao wajazwe paji la Roho Mtakatifu.
7.5.2. Kwa kusali na Maria, kumpenda kama watoto na kutamani kumuiga
tutaunganika sisi kwa sisi kama ndugu wa tumbo moja, na kumtukuza pamoja Bwana
kwa moyo wa shukrani, mshangao, unyenyekevu, tumaini na unabili, kama wa kwake.
7.5.3. Hapo jumuia zetu zote, zikiwa zimejaa furaha na Roho Mtakatifu
zitakuwa tayari kutumiwa na Mwenyezi Mungu kwa kutenda maajabu yake.
8. KUTII KWA UPENDO
8.1 MATAKWA YA BABA
8.1.1. Yesu chakula chake kilikuwa ni kutimiza sikuzote matakwa ya Baba yake;
upendo aliokuwanao kwake ulimzuia asitamani chochote zaidi kuliko hicho.
8.1.2. Ingawa ni Bwana aliishi miongoni mwa watu kama mtumishi wa wote,
akiwatii wazee wake na kufundisha heshima kwa wenye mamlaka kwa kuwa inatoka kwa
Mungu.
8.1.3. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu akanywea kikombe cha mateso na kutii
mpaka kufa, naam hata kufa msalabani, ili atimize kabisa kazi aliyoagizwa.
8.1.4. Kwa kufanya hivyo Mwana wa Mungu ametufumbulia kuwa hiari
tuliyojaliwa ni safari ya kumtii Baba, na kwa njia hiyo kuchangia wokovu wa watu
na kujipatia amani na uhuru wa kweli, ule wa watoto wa Mungu waliojaa upendo.
8.1.5. Mfuasi wake mdogo Fransisko akatuelekeza njia hiyohiyo ya kujikana
ili kumwekea wakfu Mungu utashi wetu tusije tukaachana naye, sisi viumbe na
watoto wake.
8.1.6. Dhidi ya umimi, ukaidi na utengano yanayomtawala binadamu, wanaojidai
kuwa huru wa kufanya lolote linalowapendeza, tushuhudie heri ya umoja unaotokana
na nia ya kutambua na kuitikia kwa pamoja wito wa Mungu kwetu kuhusu maisha ya
kidugu na ya kitume.
8.1.7. Kama tulivyoahidi tunapaswa kumtii Baba na neno lake kwa kupitia
wawakilishi wake katika Kanisa na katika utawa, walioshirikishwa mamlaka ya
kufundisha, kutakasa na kuongoza kwa jina la Bwana.
8.1.8. Hivyo tuna hakika ya imani ya kumpendeza Mungu na kutumwa naye,
badala ya kufuata mipango au matazamio yetu wenyewe, ambayo hata yakiwa mazuri
namna gani, hayawezi kulingana na ya kwake, hasa kama ametuandalia msalaba ili
utimilize upendo wetu.
8.2. UONGOZI WA ROHO MTAKATIFU
8.2.1 Roho yuleyule aliyemuongoza Yesu katika kumpendeza Baba, anajenga
Mwili wake akiwagawia waamini kazi za huduma na karama nyingine na kuwaunganisha
katika upendo.
8.2.2. Ndiye uhai na mhudumu mkuu wa utawa wetu pia, akifanya kazi kwa njia
ya miundo na viongozi na moja kwa moja ndani ya kila ndugu.
8.2.3. Miundo yetu iwe midogo iwezekanavyo, yenye sura ya kifamilia, na hasa
ifuate mvumo wa Roho, kwa faida ya kila mmoja na ya wote kwa jumla, kwa kuwa
pasipo mwanga na nguvu zake katika kutimiza wajibu wa kidugu tunajichosha bure
tu.
8.2.4. Vilevile kila mmoja wetu anapaswa daima kusikiliza na kufuata sauti
yake, inayotufikia hasa kwa njia ya mikutano, watumishi na walinzi, ingawa mara
nyingi anamfunulia aliye mdogo zaidi mambo yaliyo bora.
8.3. MIKUTANO
8.3.1. Kila mkutano wetu, katika ngazi mbalimbali, unahudhuriwa na Bwana
kama alivyoahidi, tena unaonyesha udugu unaotuunganisha.
8.3.2. Katika hali ya imani na furaha washiriki wachange mang’amuzi
mbalimbali na ufafanuzi wa haja maalumu zilizojitokeza, ili kutafuta njia
zinazofaa kulingana na karama yetu sote.
8.3.3. Katika kupima kila jambo wakumbuke majukumu waliyonayo pia kwa ajili
ya ndugu ambao pengine hawahudhurii, lakini wanahusika na kuwajibika hasa kwa
sala.
8.3.4.
Tusaidiane kuchunguza jinsi tunavyoshika Injili, kuchimba mada muhimu kwetu sote,
kukabili maswala makuu ya maishani mwetu, halafu kukata mashauri kadiri ya
sheria zetu, ikiwezekana kwa kauli moja, la sivyo kwa thuluthi mbili za kura,
halafu kwa kutoa maelezo ili kurahisisha utekeIezaji wa wote.
8.3.5.
Mamlaka ya juu katika kila jamaa inao mkutano mkuu, lakini ndani ya mipaka ya
katiba hii.
8.3.6.
Wenyewe uitishwe na mtumishi mapema kila baada ya miaka mitatu na kuhudhuriwa na
ndugu ambao wasizidi ishirini lakini wawakilishe kweli jamaa nzima kadiri ya
sheria zetu ndogondogo.
8.3.7.
Mkutano mkuu upange ajenda zake, kisha kupata mapendekezo ya halmashauri kuu
yaliyotokana na mchango wa ndugu wote.
8.3.8.
Mkutano mkuu unaweza kuunda kanda zenye jumuia kadhaa, kuziunganisha,
kuzirekebisha na kuzifuta ili ziwe daima hai katika Kanisa.
8.3.9.
Mkutano wa jumuia uitishwe na mlinzi walau mara moja kwa mwezi, na kuhudhuriwa
na ndugu wote wenye ahadi, isipokuwa kuhusu maswala ya malezi na mengineyo
anaweza akawaalika wenye ahadi ya daima tu.
8.3.10. Ajenda za mkutano huo zipangwe na mlinzi kisha
kupata mapendekezo ya wanajumuia.
8.4.
HUDUMA KATIKA JAMAA
8.4.1.
Mbali ya mikutano, utawa wetu una ndugu wenye madaraka katika jamaa na ngazi
mbalimbali wanazoziwakilisha rasmi.
8.4.2.
Ndugu hao, hasa watumishi, wakiishi katika nyumba iliyopangwa iwe makao yao,
wanatakiwa kuímarisha ushirika wetu na Kanisa tena kati yetu, kumthibitisha
kila mmoja katika wito wa Kiinjili wa Kifransisko, kutoa neno la mwisho katika
kutambua matakwa ya Mungu na kustawisha ushuhuda wetu sote katíka jamii.
8.4.3.
Kila mmojawao awe na washauri wawili ambao waishi naye na kushiriki katika
madaraka yake kadiri ya sheria za utawa wetu.
8.4.4.
Awe nao walau vikao vinne kwa mwaka, na kujali sana mchango wao.
8.4.5.
Mmojawao awe kaimu wakati mtumishi au mlinzi asipokuwepo, ila asijihusishe na
mambo yale ambayo huenda akajiwekea.
8.4.6.
Mtumishi asishughulikie mambo ambayo yanampasa mlinzi, ila kwa salabu nzito.
8.4.7.
Awaongoze watoto wa Mungu kwa upendo ule ambao Baba anao kwao, na kwa mifano
mitakatifu ya maisha yake mwenyewe na ya jumuia anamoishí, ambamo ajitahidi ili
Mungu atamaniwe na kupendwa kweli kuliko yote.
8.4.8.
Asitende kama chifu, bali awasaidie kutii akiimarisha imani na kuheshimu utu wao,
akiwasikiliza kwa moyo wa kimama.
8.4.9.
Awasaidie ipasavyo wanayoyahitaji, hasa katika ugonjwa, akikumbuka atatakiwa
kujieleza mbele ya Mungu kama ndugu fulani atapotea kwa sababu amemtendea kwa
ulegevu au kumpa mfano wa kukatisha tamaa, au kumkosoa na kumuadhibu haraka na
vikali mno.
8.4.10.
Mbali ya kuwasiliana na jumuia zote alizokabidhiwa kwa njia ya barua,
azitembelee rasmi walau mara moja kwa mwaka ili kuzistawisha kiroho na kiutume;
halafu ampangie mlinzi muda wa kutoa ripoti juu ya utekelezaji wa maagizo
aliyotoa.
8.4.11.
Mtumishi kwa kibali cha halmashauri yake na kisha kuwasikia wanaohusika zaidi,
anaweza kuweka jumuia mbili au zaidi chini ya ndugu mtunzaji ambaye azisimamie
kwa karibu kwa niaba yake.
8.4.12.
Kwa sababu maalumu, watumishi, watunzaji na walinzi wanaweza kumkabidhi ndugu
fulani sehemu ya mamlaka yao ili ashughulike kwa niaba yao.
8.4.13.
Hao wote, zaidi ya kuzitumikia jumuia zao, wawajibike kuhusu maisha na maendeleo
ya jamaa nzima, wakikuza ushirikiano wa kiroho, kiutume na kiuchumi.
8.5.
UCHAGUZI NA UTEUZI
8.5.1.
Mkutano mkuu wa kila jamaa uchague mtumishi na washauri wake, ukiwakabidhi
utekelezaji wa maagizo mbalimbali.
8.5.2.
Kisha kuthibitishwa na askofu wa Morogoro, hao wachague katibu, walinzi na
makamu wao, walezi na wengineo, afadhali kati ya wenye ahadi ya daima.
8.5.3.
Wachaguliwe ndugu ambao wanathamini wito wetu, wanazingatia hali ya Kanisa na
jamii, wako tayari kujadiliana na kushirikiana na wote.
8.5.4.
Hao wote wanadumu miaka mitatu, halafu wanaweza kuchaguliwa tena mara mbili
mfululizo katika kazi ileile; baada ya hapo wapumzike walau mwaka mmoja.
8.5.5.
Katika uchaguzi wowote tuwe na nia njema na kufuata taratibu za Kanisa na za
kwetu, pengine kisha kupata mapendekezo ya ndugu wengine; ziandikwe kumbukumbu
zake ambazo zitunzwe katika masajili ya jamaa, pamoja na hati nyingine.
8.5.6.
Tukiwa wadogo kweli, tusitamani kazi hizo wala tusizikatae kwa ukaidi,
tukikubali kwa upendo matakwa ya Mungu kwetu na wajibu wa kutumikia wenzetu hata
kwa kushika madaraka.
8.5.7.
Katika kuzitekeleza tukumbuke daima wajibu wa kutunza siri.
8.5.8.
Akiwa na sababu za haki, askofu wa Morogoro anaweza kumuondoa madarakani
mtumishi, baada ya kuwasikiliza yeye na washauri wake.
8.5.9. Kwa manufaa ya jamaa, halmashauri kuu inaweza
kumuondoa madarakani yeyote aliyechaguliwa nayo au kumhamisha kwingine.
8.5.10. Wadhifa wowote ukibaki wazi, pengo lizibwe na
ndugu aliyechaguliwa na halmashauri kuu, ila wadhifa wa mtumishi ushikwe na
mshauri mkuu wa kwanza, na wadhifa wa mshauri mkuu ushikwe na yule wa kwanza
kati ya washauri wawíli wa akiba waliochaguliwa mapema na mkutano mkuu.
8.5.11. Hao wote walioziba pengo wadumu mpaka mkutano mkuu ujao, ambao
ufanyike kama kawaida miaka mitatu baada ya ule uliotangulia.
8.5.12. Tunapotakiwa kujipanga
kisheria, watangulie wenye ahadí ya daima kufuatana na tarehe ya kuiweka
na ile ya kubatizwa, halafu ndugu wengine kufuatana na tarehe ya kuweka ahadi ya
muda kwa mara ya kwanza na ile ya kubatizwa; nje ya liturujia wanaweza wakapewa
nafasi ya pekee wenye madaraka utawani kadiri ya ngazi zao, lakini si kwa msingi
wa daraja takatifu.
8.6. UMOJA WA UTAWA
8.6.1. Utawa wetu ni mmoja tu, ingawa tumegawanyika katika jamaa
mbalimbali ambazo ushirikiano wake ufuate katiba hii na kuratibiwa na baraza
linalokutanika mara moja kwa mwaka.
8.6.2. Katika baraza hilo kila
jamaa, zikiwa ni pamoja na ile ya ulimwenguni, inawakilishwa na mtumishi
pamoja na washauri wake; ila kwa kurekebisha katiba hii, na katika nafasi
nyingine za pekee, waongezwe kwa kila jamaa ndugu watatu kati ya waliotangulia
kuweka ahadi ya daima.
8.6.3. Baraza hilo halina mamlaka juu ya jamaa zenyewe, ila linasimamia
hasa: malezi, ili kustawisha karama yetu; uundaji wa misheni mpya, ili kueneza
Injili kwa mpango wa Kikanisa; halafu mgawanyo wa misaada ipatikanayo, ili
kufanikisha shughuli hizo.
8.6.4. Ni juu ya baraza
kukubali ombi la baadhi ya ndugu la kuanzisha jamaa mpya, na kuikataza jamaa
fuIani isiendelee kupokea watakaji kuanza zoezi ikiwa imepatwa na uvuguvugu.
8.6.5. Ikíwa ndugu fulani
ameshauriana na mtumishi wake na kuona ni vema ahamie jamaa nyingine ya utawa
wetu aiombe halmashauri ya jamaa hiyo, ambayo ikimkubalia, kisha kupewa na
mtumishi huyo taarifa zinazohitajika, impangie muda na masharti ya jaribio,
ambalo likishindikana arudi katika jamaa ya awali.
8.6.6. Kwa sababu nzito askofu
wa Morogoro anaweza kumteua mkurugenzi ambaye kwa niaba yake asimamie kwa muda
utawa wote badala ya baraza, au jamaa mojawapo badala ya mtumishi.
8.7. JUMUIA ZA MAHALI
8.7.1. Jumuia zetu za mahaIi
zina sura tofauti kwa kuwa ndipo mipango ya utawa wetu inapoitikia mahitaji ya
Kanisa maalumu na watu wa utamaduni fulani, ndugu wakiwajibika siku kwa siku
kutekeleza karama zao tofauti na kukomaa kwa umoja.
8.7.2. Kuunda jumuia ni juu ya
halmashauri kuu, kisha kushauriana kwa wanabaraza, kuhakikisha mazingira yanafaa
kwa maisha yetu na kupata kwa maandishi kibali cha askofu wa jimbo husika.
8.7.3. Kwa kawaida jumuia
ziishi pembeni mwa vijiji, nazo ziwe na ndugu sita hadi kumi na wawili, ila
monasteri na nyumba za malezi zinaweza kuwa na ndugu wengi zaidi wakihesabiwa
wanaolelewa; kinyume chake makazi ya upwekeni yanaweza kuwa na ndugu watatu au
wanne tu.
8.7.4. Mtumishi pamoja na halmashauri yake wajitahidi kuwapanga vizuri
ndugu ili waishi Kiinjili kweli katika mazingira husika.
8.7.5. Wachague walinzi ambao
wadumishe umoja na uaminifu wa wote, wakilinganisha hasa madai ya sala na ya
utendaji.
8.7.6. Kwa faida ya maisha ya
kidugu na ushuhuda wa Kikanisa, ikiwezekana kila jumuia inapoundwa ndugu zetu
kadhaa wa ulimwenguni wahamie karibu nayo; makleri wanajimbo wafanye hivyo kwa
ruhusa ya askofu wao.
8.7.7. Kínyume chake, jumuia
mbalimbali za waliojiweka wakfu zisiishi kijiji kimoja, isipokuwa kwa lengo la
kuboresha malezi au lingine muhimu.
8.7.8. Kisha kushauriana na askofu wa jimbo husika, jamaa moja inaweza
kuhama nyumba au kuiachia jamaa nyingine, kadiri ya mipango ya baraza; hapo vitu
vilivyopo nyumbani vigawiwe kidugu kati ya jamaa inayohama na jimbo, au kati ya
jamaa hiyo na ile inayohamia.
8.7.9. Tufanye pia mipango ya
kwenda kukaa kwa muda tu katika vijiji kimojakimoja, tukishika maisha yetu ya
kijumuia, pamoja na kuwatembelea watu nyumbani kwao, na kuwakutanisha
ili wasikilize Neno la Mungu na kushirikishana katika hali ya sala.
8.7.10. Baada ya kumaliza
uchipukizi, ndugu wa kiume watakaopenda waruhusiwe kushika Kanuni ya Ndugu
Wadogo iliyothibitishwa na papa Honori III, ili kufuata maisha yenyewe ya
mtakatifu Fransisko yaliyoiga yale ya Mitume walipotumwa na Yesu safari ya
kwanza.
8.7.11. Ili ndugu wa jamaa
moja aweze kuishi kwa muda mrefu katika jumuia ya jamaa nyingine ya jinsia yake,
anahitaji ruhusa ya watumishi wa pande zote mbili; ila ndugu yetu wa ulimwenguni
inamtosha ruhusa ya mtumishi wa jamaa inayompokea.
8.7.12. Ndugu akitakiwa kuishi nje ya jumuia zetu kwa muda mrefu kwa
sababu za afya au masomo, apangiwe na halmashauri ya jamaa ndugu wa kwenda naye
na nyumba fulani ya kitawa; halafu aendelee kuwasiliana mara nyingi na mtumishi
na ndugu wa jamaa yake kwa kuwa maisha ya kijumuia ni kiini cha wito na utume
wetu.
8.8.
BIKIRA MTIIFU
8.8.1.
Aliposikia tu maneno ya malaika Gabrieli, Maria mnyenyekevu alipokea kwa moyo
mkuu matakwa ya Mungu akijitoa mhanga kumtumikia katika nafsi na kazi za Yesu
aliye mtumishi mtiifu.
8.8.2.
Ili Mungu aweze kutimiza kazi aliyoianza ndani mwetu na kwa njia yetu, tujiachie
kwa furaha mikononi mwa Baba, tukipokea yale yote anayotupa, tukimpa yale yote
ambayo anatuondolea au kutuomba, tukikubali kwa imani tu atutumie anavyotaka,
tukisikiliza na kutekeleza yale anayotuambia kwa njia ya viumbe vyake, hasa
viongozi, tukimtolea akili na utashi, neema za kiroho na za kimaumbile katika
kutimiza sawasawa yale tuliyoagizwa.
8.8.3.
Kwa kurahisisha hayo, kila mmoja wetu aitikie upendo wa Mama Maria,
akijiaminisha kwake kwa namna ya pekee ili asaidiwe naye kuwa sadaka ya upendo
kwa Mungu na chombo cha amani yake kwa watu.
8.8.4.
Hivyo kwa njia yake, Yesu ndiye atakayefikiri katika akili zetu, na kufanya kazi
kwa mikono yetu, na kupenda kwa mioyo yetu.
8.8.5.
Kutoka kwa Mama wa Kanisa tujifunze kufungamana na wenzetu kwa unyofu na upendo
hata uhusiano kati yetu unapotakiwa kufuata sheria, kwa sababu upendo ndio
utimilifu wa sheria.
9. KUWA MASHAHIDI WA KRISTO
9.1. UMISIONARI
9.1.1.
Yesu aliwekwa wakfu kwa Roho Mtakatifu na nguvu akatangaze upendo wa Baba
aliyemtuma; mwenyewe akajionyesha kuwa ni Habari Njema kwa watu wote kwa kuja
kuwatafuta toka mbinguni na kutoa uhai wake kuwa fidia ya dhambi zao.
9.1.2. Kwa wokovu wa watu,
ambao Mwana wa Mungu aliujali kiasi hicho, mzee wetu Fransisko alijisikia
msukumo wa kuijaza Injili dunia nzima, akitamani kumwaga damu yake kama ushahidi
bora wa ukweli na upendo.
9.1.3. Hivyo akaliamsha Kanisa
litekeleze agizo la Kristo la kumshuhudia kwa wasiomjua ili ulimwengu wote
ukisikiliza tangazo la wokovu uamini, ukiamini utumaini, ukitumaini upende.
9.1.4. Tunapofanya kazi hiyo,
ambayo bado sana, papohapo inabidiisha na kukomaza imani yetu tunayotaka
kuwashirikisha wengine, na inaimarisha umoja kati yetu.
9.1.5. Tuizingatie upeo ili
makabila yale ambayo bado yampokee Mwokozi pekee, na kufurahia ukweli wote wa
Mungu aliye Baba yetu mwema, na kuingizwa kwa maji na Roho Mtakatifu katika
umoja wa familia yake yakiiletea utajiri wa tunu zao.
9.1.6. Hatuwezi kuwaongoa watu
tusipotubu wenyewe kila siku, wala hatuwezi kuwa wamisionari tusipokubali kwa
moyo maisha yetu yabadilike kwa kushikamana na watu tunaowatafuta, tukiingia kwa
unyenyekevu katika utamaduni wao ili kuchochewa nao na kuumua kwa chachu ya
Injili iliyokwishafanya kazi ndani mwetu.
9.1.7. Tukifungamana hivyo na
watu wowote tutawasaidia pia kukaribiana, kuchanga mema yale mbalimbali
waliyojaliwa, na kuunda utamaduni wa upendo.
9.1.8. Tutumie sana nyimbo na
muziki, michezo na maigizo, michoro na mithali, hadithi na njia nyingine rahisi
za kupashana habari ili tuwashirikishe wote hekima ya utamaduni uliostawishwa na
imani ya Kikristo, ili ikoleze mioyo ya watu na miundo ya jamii.
9.1.9. Tukiitegemea hazi ya
Roho Mtakatifu ndani ya wote, na kuziheshimu dhamiri zao, tujadiliane kwa wema
na busara na wanaofuata dini za jadi, wanaojitahidi kumtii Mungu katika Uislamu,
wanaomtafuta kwa moyo mnyofu, waliomsahau maishani na wengineo wowote, ili
tuelewane nao mpaka ndani kama marafiki na kuongozana nao katika kumrudia
aliyetuumba wote sawa.
9.1.10. Upendo wetu mpole
mnyenyekevu katika kuwatolea ujumbe wa wokovu utawasaidia kuupokea kwa mikono
miwili wakitambua kuwa ndio unaoshibisha kweli njaa ya roho zao.
9.1.11. Tuwaombee wamisionari
wengine, tukifuata habari zao na kuwapokea kwa furaha wakifika kwetu.
9.1.12. Ingawa si wengi sana
wanaojaliwa neema tukufu ya kumfia Yesu mwishoni mwa safari yao, ni lazima wote
tuwe tayari kujitoa mhanga kwa ajili ya wenzetu na kumuungama Kristo mbele yao,
tukifurahi kumfuata kwenye njia ya msalaba ambao wanafunzi wake halisi
hawapungukiwi kamwe.
9.2. SALA NA UTUME
9.2.1 Sala ilimtegemeza Yesu
daima, katika utume na katika mateso; ndiye kielelezo cha umoja unaohitajika
maishani kati ya kuungana na Baba na kutenda mengi.
9.2.2. Kwa kuwa upendo ni
mmoja tu, kumkazia macho Bwana kusipunguze juhudi zetu kwa ajili ya binadamu
walio mfano wake, bali kumjua Mungu mpaka ndani na kupokea upendo wake
kutusukume kuwashirikisha wengine mang’amuzi hayo, yaliyo utajiri wetu pekee,
na chemchemi ya furaha tusiyoweza kunyang’anywa.
9.2.3. Tujitahidi kuwa
wanasala hodari katika umisionari na wamisionari hodari katika sala, tukitunza
muda wa kuongea na Mungu kwa niaba ya watu, na tukitumia vizuri muda wa
kuwashughulikia watu kwa ajili ya Mungu.
9.2.4. Mchanganuo huo mzuri
utaziwezesha juhudi zetu katika sala na toba kutakasa na kustawisha utume hata
ukiwa mgumu namna gani; hapo utume utailetea sala bidii mpya; isipotokea hivyo
maana yake tumekwama kiroho na kiutume.
9.2.5. Mara kwa mara tumrudie
katika sala yule aliyetutuma ili tupime pamoja naye kazi yetu, tukijikumbusha
tulivyo vyombo vyake vya udongo tu, na tukimshukuru kwa yale anayoyatenda kwa
njia yetu.
9.3. NENO LA UZIMA
9.3.1. Kama vile Yesu
alivyokuwa hachoki kuwatolea watu Injili, wakiwa mmoja mmoja au katika umati,
sisi sote tutumie sawasawa kila nafasi ya kuieneza, tukijua wokovu unatokana na
imani, nayo imani inatokana na kusikiliza ujumbe.
9.3.2. Hakuna jina lingine la
kulishuhudia au neno lingine la kulitangaza, ila Yesu aliye Neno la uzima, kwa
kuwa aliupokea uzima wa Baba akaja kutushirikisha uzima huo kwa njia ya Roho
Mtakatifu na sakramenti za Kanisa.
9.3.3. Upendo wake unatusukuma
kumtangaza hasa kwa wasio Wakristo, kwa sababu wote wana haja na haki ya kumjua
yeye aliye kiini na lengo la viumbe vyote: hakuna huduma nyingine muhimu zaidi.
9.3.4. Tuwasaidie wote
kukutana naye kweli na kumkimbilia katika shida, ili watambue kuwa ndiye
anayewaokoa na kuwapenda, anayewajalia mvua na uhai, watoto, afya na maendeleo,
na ndiye anayewakomboa kutoka dhuluma na utumwa wowote.
9.3.5. Tuna deni hilo kwao:
ole wetu tusipowapasha habari njema katika mazingira yao ili waambatane kweli na
Yesu na Injili yake kwa imani, kwa sakramenti na kwa matendo!
9.3.6.Katika ibada za Jumapili,
mafundisho ya kuandalia sakramenti mbalimbali, na vipindi vya dini shuleni,
tuwazoeshe waamini kuelewa Maandiko Matakatifu na imani ya Kanisa tangu utotoni
kabisa, na tuwahimize kujitolea mapema katika utume.
9.3.7. Imani ionyeshwe daima
kuwa ni zawadi ya Mungu inayotakiwa kuenezwa, kuadhimishwa na hasa kutekelezwa
kwa pamoja katika familia, parokia, jumuia na vyama mbalimbali, kwa kuwa uzima
wa milele tulioahidiwa unayatia maanani maisha ya hapa duniani, na kutudai
tuitikie sasa wito wa kuwa wana wa Mungu kwa kuongozwa na upendo kwa Baba na kwa
ndugu wote.
9.3.8. Shukrani na furaha
tulizonazo kwa kuumbwa zinatutuma kumshirikiska kila mtu hata aheshimu, alinde,
apende na kutumikia uhai wa mwenzake yeyote, na ashike amri nyingine za Mungu
ambazo kwa pamoja zinatuhakikishia uzima.
9.3.9. Tuwajulishe wote vilema
na maadili, adhabu na utukufu wa milele, kusudi mbele ya Yesu msulubiwa watambue
kwa unyofu uovu wa dhambi na njia ya wokovu.
9.3.10. Tuwe tayari
kushirikiana na wenye mitambo ya vyombo vya upashanaji habari, vinavyotengeneza
kwa kiasi kikubwa utamaduni wa umati, na tuwaelekeze watu kuvitumia kwa faida,
si kwa kujiangamiza.
9.4. USHUHUDA WA UTAKATIFU
9.4.1. Tunaishi kwa nguvu ya
Neno, tunafurahia uwepo wake ndani mwetu, tunasafiri pamoja naye na kushiriki
utume wake alioufanya kwa kujishusha moja kwa moja badala ya kutegemea uwezo
wake tu.
9.4.2. Juhudi zetu za
kumzingatia daima Yesu na mifano aliyotuachia ili tufuate nyayo zake,
zinatuelekeza kufanya shughuli ambazo hazihitaji vifaa vingi na uwezo wa
kibinadamu, bali pamoja na bidii zinadai hasa imani kuwa anayeeneza kweli Injili
ni Roho Mtakatifu.
9.4.3. Tufuate kwa makini
uongozi wake ili atulinganishe na yule tunayetaka kumshuhudia, kusudi ndani
mwetu, katika jumuia na katika Kanisa, watu wamuone na kumpenda Yesu na
kushangaa maajabu anayoyatenda katika udhaifu wetu, sisi watumishi wa bure.
9.4.4. Tuwaonyeshe hasa upendo
mkubwa wa kidugu, tukijua binadamu wanawaamini mashahidi kuliko walimu, na
kuzingatia matendo kuliko maneno, na kuguswa wakiona namna bora ya kuwapokea na
juhudi kwa ajili ya maskini, wadogo na wenye shida.
9.4.5. Tusisahau kuwa wito wa
umisionari unatokana na ule wa utakatifu, kwa sababu msingi na sharti la kazi ya
wokovu, na kipimo cha utekelezaji wake si utendaji mwingi, bali ni upendo.
9.4.6. Kadiri tunavyoupokea
upendo wa Baba na kumrudishia kwa uaminifu alivyofanya Mwana hadi msalabani,
tuwe na hakika ya kuwashirikisha watu uzima wa Utatu mtakatifu kwa uweza wa Roho,
hata tusipoona mafanikio yoyote.
9.5.
HUDUMA MBALIMBALI
9.5.1.
Tufanye juu chini ili jumuia ndogondogo za Kikristo ziwe hai, kwa kuwa ndipo
watu wanapojifunza kutekeleza upendo kwa wote, na kuishi kama familia ya Mungu,
wakimtii Baba, wakimfuata Mwana na kuungana katika Roho.
9.5.2.
Upande mwingine, Kanisa litastawi hivyo ikiwa tu familia za Kikristo zitakuwa
kweli vikanisa vya nyumbani, shule za Injili, patakatifu pa uzima na misingi
imara ya jamii.
9.5.3.
Kwa mfano wa familia takatifu iliyokimbilia bara letu, tuwasaidie baba, mama na
watoto kukuza upendo kati yao na tunu nyingine zinazofanya maisha kuwa zawadi
ambayo tunaipokea na kuwashirikisha wengine.
9.5.4.
Tuadhimishe vizuri sakramenti ili zituwezeshe sisi na wenzetu kuzikabili hatua
na hali mbalimbali za maisha pamoja na Bwana msulubiwa na mfufuka.
9.5.5.
Ndugu makleri waheshimu sana daraja yao ambayo imewafanya kitu kimoja na makleri
wote, na kuweka wokovu wa watu hasa mikononi mwao; watimize kazi yao kitakatifu,
kwa ukarimu na kulingana na karama yetu ya Kifransisko.
9.5.6.
Ndugu wanaowajibika katika vitendo vya huruma ya kiroho na ya kimwili, washiriki
zaidi katika uchungaji wa Kanisa kwa kuwaelekeza watu kwenye imani na sakramenti
zake.
9.5.7.
Ndugu wale ambao hawawezi kutenda kazi za kitume au wamejifunga kusali tu,
kadiri wanavyoishi kwa ajili ya Baba, walivyonaswa na upendo wa Yesu na
wanavyoongozwa na Roho Mtakatifu, wanachanga umisionari wetu kwa njia bora
isiyoelezeka.
9.5.8.
Hivyo kwa njia mbalimbali kila jumuia yetu itaeneza katika mazingira yake uzima
wa Kristo mfufuka.
9.6. MPANGO WA KIKANISA
9.6.1. Kwa moyo uleule wa Yesu
na wa Mama Kanisa wa kutaka wokovu umfikie kila mtu, tuangalie tusilemewe na
miundo yetu, wala tusimezwe na ile ya majimbo, bali tuwe wepesi wa kwenda kokote
duniani ili umati wa watu hoi kama kondoo wasio na mchungaji utambue tena huruma
ya Yesu.
9.6.2. Tuwaombe wale
wanaoratibu umisionari wa Kanisa watutume hasa kushika nafasi ngumu, kati ya
watu fukara wa bara letu au wenye asili ya Kiafrika, waliosahaulika zaidi au
waliolazimika kuhama nchi yao, ili tuwasaidie tunavyoweza mpaka watakapopata
uchungaji wa kawaida.
9.6.3. Tuchochee moyo wa
kimisionari hata katika Makanisa machanga, na kushiriki kikamilifu katika
kuandaa na kutekeleza mipango ya askofu na ya paroko, jinsi inavyotufaa sisi
ndugu wadogo, bila ya kudai malipo, kwa ushirikiano mzuri na waamini wenzetu,
tukishika nafasi yetu maalumu na kuwasaidia washike vema nafasi zao mbalimbali.
9.6.4. Katika mkataba ambao
inatubidi tuufanye na mkuu wa kila jimbo tunamokwenda kuishi, izingatiwe kuwa
huduma yoyote ambayo tuitoe inatakiwa kulingana na karama maalumu tuliyokubaliwa,
kwa sababu ustawi wa Kanisa unategemea hasa vipaji vile mbalimbali ambavyo Roho
anawagawia waamini, hao wakivipokea na kushirikishana kwa mikono miwili.
9.7.
NYOTA YA KUONGOZA KWA KRISTO
9.7.1.
Bikira Maria ni mfano bora wa ule upendo wa kimama ambao wawe nao wanaoshiriki
katika Kanisa kazi ya kuzaa upya watu na kutunza uzima wao wa Kimungu.
9.7.2. Tukiwa mitume pamoja na
Maria, tuwe pia mitume wake, tukimtoa kama zawadi kwa watu wapate kumjua na
kumpenda na kuongozwa naye kwa Mwanae.
9.7.3. Maana roho ya ibada kwa
Bikira mwenye heri, chini ya ile kwa Mkombozi, inafaa sana kuunda imani na
mwenendo wa Kikristo, kwa kuwa Maria ni muhtasari wa mafundisho ya Yesu na picha
yake inayotuvutia kutamani ukamilifu wa maadili yake yote, hasa upendo.
|