MATAKASO KABLA YA KUAHIDI MASHAURI YA KIINJILI   Morogoro: cappella maschile - Morogoro: kikanisa chajumuia ya kiume - Morogoro: the chapel of the brothers

 

 

MATAKASO KABLA YA KUAHIDI MASHAURI YA KIINJILI

 

 

 

TAKASO LA KWANZA YAANI TAKASO LA MATOWASHI

 

219. Siku ya kawaida ya wakati wa matakaso ya watakaoweka ahadi, jamaa inawakusanyikia kwa ibada muhimu ya takaso la kwanza, ambalo linahusiana na shauri la Kiinjili la useja mtakatifu na kulenga kuwaimarisha dhidi ya vishawishi, kunyosha nia zao, kuchochea utashi wao, kuongeza ujuzi mnyofu na mnyenyekevu wa nafsi yao kwa njia ya kujitafiti na kutubu kwa dhati. Hivyo wanaandaliwa kushika vema ahadi hiyo na madai yake. Inafaa kuadhimisha ibada hii katika kikanisa cha jumuia ya zoezi baada ya Zaburi za Sala ya Mchana ikihudhuriwa na wanajumuia tu.

 

220. Kama kawaida, katika ibada ina nafasi ya msingi Liturujia ya Neno, ambayo inapendekezewa masomo mbalimbali ya kuchagua (taz. namba 379) lakini moja tu kutoka Injili, kwa kuwa ni la lazima na ndilo linalolipa takaso jina lake.

 

221. Baada ya hotuba, watakaoweka ahadi wanajipanga mstarini mbele ya padri ambaye, kwanza anawaelekea ndugu waliopo awaalike kuwaombea kimya roho ya toba, hofu ya dhambi na ukombozi kamili wa miili yao. Halafu anawaalika wenyewe kusali kimya wakitokeza msimamo wao wa ndani wa toba na kujiombea neema kwa kupiga magoti.

 

222. Baada ya kimya kidogo, padri anawaalika waote kusali pamoja kwa maneno ya namna hii:

 

Tuwaombee hawa ndugu zetu ambao, baada ya safari ndefu waliyokwishafanya, mwishoni mwa kipindi hiki cha utakaso wanatarajia kuishi na Kristo katika useja ili wampende kwa moyo usiogawanyika.

 

223. Shemasi anatoa nia za namna hii:

 

Ili wakiri kwa unyenyekevu ukosefu wao na kurekebisha maisha yao mbele ya Yesu aliyekuja kuokoa waliopotea, tuombe:

 

Ili waepukane na hali ya kukata tamaa, inayosogeza mbali na njia ya Kristo, tuombe:

 

Ili kwa msimamo wao mnyofu wayakatae siku kwa siku katika mwenendo wao yale yote ambayo hayampendezi Baba bali yanapingana na sheria yake ya upendo, tuombe:

 

Ili Roho Mtakatifu anayechunguza mioyo ya wote autegemeze udhaifu wao kwa uweza wake, tuombe:

 

Ili sisi pia, tukijiandaa kushuhudia ahadi zao, tutakase mioyo yetu isipende kwa namna yoyote dhambi na nyinginezo zinazopingana na utakatifu wa wito wetu, tuombe:

 

Ili katika ulimwengu wote, yaliyo dhaifu yaimarishwe, yaliyoanguka yainuliwe, yaliyooza yaponywe, na hivyo viumbe vyote vishirikishwe ushindi wa Pasaka, tuombe:

 

224. Halafu padri, akiwaelekea watakaoweka ahadi anasali amefumba mikono:

 

Mwenyezi Mungu, uliye mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu,

unapendelea roho zisizo na doa

na kutamani kukaa mwilini mwa walio safi kama hekaluni mwako,

ulivyozoea kufanya katika Mwanao mpenzi Yesu Kristo.

 

Kwa njia yake na kwa ajili yake uliumba ulimwengu

nasi watu kwa sura yake upande wa mwili

na kwa mfano wake upande wa roho.

 

Ulipoamua kurekebisha upya maumbile ya binadamu,

yaliyoharibiwa na hila za Ibilisi tangu wazazi wetu wa kwanza,

hukuridhika kuyarudishia utakatifu asili tu,

bali kwa stahili za Neno wako aliyefanyika mwili,

umewainua watu wafanane na malaika,

ukiwawezesha kutanguliza ndani mwao hali ya ufalme ujao

ambapo hawataoa wala kuolewa, bali upendo utawaenea wote.

 

Uwaongoze daima wateule hawa,

ambao kwa mwanga wa hekima ya milele

umewajalia kuelewa jinsi useja mtakatifu ulivyo bora

na kuwa chemchemi halisi ya karama hiyo ni wewe tu.

 

Kwa maana roho yenye mwili unaoelekea uharibifu,

inawezaje kushinda silika ya maumbile, upotovu wa hiari,

mitikisiko ya hisi na misukumo ya umri,

isipokuwa kwa sababu wewe, Baba wa rehema,

umewasha na kuchochea ndani mwake moto wa upendo wako,

na kuishirikisha nguvu zako mwenyewe?

 

Basi, uwe ulinzi wao wa kudumu dhidi ya shetani,
anayehatarisha kwa ujanja nia njema kabisa,
asije akachafua katika kitambo cha udhaifu
utakatifu wa mwili na usafi wa roho yao.

 

Tunakuomba hayo kwa njia ya Kristo, Bwana wetu.

 

225. Wote wanaitikia:

 

Amina.

 

226. Padri anamwekea mikono kichwani kila mmoja wa watakaoweka ahadi, halafu, akiwanyoshea wote pamoja, anaendelea na sala:

 

Bwana Yesu, ulilipenda Kanisa ukajitoa kwa ajili yake,

nawe unazidi kulitakasa na kulifanya upya

ulilete mbele yako kama bikira asiye na doa,

kama mchumba aliyepambwa kwa ajili ya arusi,

kama mama anayefurahia wingi wa watoto

wasiozaliwa kwa mwili tu, bali kwa Roho Mtakatifu.

 

Wateule hawa wamevutiwa na uzuri wako na kukukazia macho
wakitamani kushiriki hali uliyokuwa nayo duniani,
wakijitoa roho na mwili kwako
wachangie pamoja nawe utukufu wa Baba
na wokovu wa wadogo wako wote.
 
Kwa kuwa wanakufunulia mioyo yao,
wakikiri kwa tumaini dhambi zao
na kukuonyesha madonda yaliyofichika rohoni mwao,

usikubali wadanganywe na yule mwovu

wala kujiamini kipumbavu,

bali waoanishe adabu na uangalifu, wema na busara,

upole na msimamo, uhuru na usafi,
na hasa wawake upendo kwako,
huku wakikesha hadi urudi mtukufu
kutukaribisha katika arusi yako.
 
Unayeishi na kutawala daima na milele.

 

227. Wote wanaitikia:

 

Amina.

 

228. Kipindi kinamalizika kama kawaida kwa baraka au kwa shangilio:

 

Tumtukuze Bwana.

 

Tumshukuru Mungu.

 

 

TAKASO LA PILI YAANI TAKASO LA WENYE HERI

 

229. Baada ya mwezi mmoja hivi, linafanyika takaso la pili linalohusiana na shauri la Kiinjili la ufukara wa hiari ambao mzee wetu Fransisko ametufundisha kuukumbatia sana kama ufukara mkuu. Kimsingi, taratibu na malengo ya ibada hii ni kama vile vya takaso la kwanza. Inafaa kuifanya siku ya kawaida katika kikanisa cha nyumba ya zoezi baada ya Zaburi za Sala ya Mchana, ikihudhuriwa na wanajumuia tu.

 

230. Kama kawaida, katika ibada ina nafasi ya msingi Liturujia ya Neno, ambayo inapendekezewa masomo mbalimbali ya kuchagua (taz. namba 380) lakini moja tu kutoka Injili, kwa kuwa ni la lazima na ndilo linalolipa takaso jina lake.

 

231. Baada ya hotuba, watakaoweka ahadi wanajipanga mstarini mbele ya padri ambaye, kwanza anawaelekea ndugu waliopo awaalike kuwaombea kimya roho ya kulenga mema ya milele badala ya mali, hamu ya kuwa wadogo na kudharauliwa kwa upendo wa Yesu fukara na wa wale wote wanaobaguliwa badala ya kuwa wakuu. Halafu anawaalika wenyewe kusali kimya wakitokeza msimamo wao wa ndani wa toba na kujiombea neema kwa kupiga magoti.

 

232. Baada ya kimya kidogo, padri anawaalika waote kusali pamoja kwa maneno ya namna hii:

 

Tuwaombee tena ndugu hawa, wanaoelekezwa kufuata nyayo za Kristo katika utawa wetu, ili waambatane na ufukara wake kwa moyo wote, wakikubali yale yote yanayotokana nao.

 

233. Shemasi anatoa nia za namna hii:

 

Ili wateule hawa watafakari sana hekima ya msalaba, ambayo Mungu anaaibisha ile ya ulimwengu, tuombe:

 

Ili wadumu kuwa waaminifu kwa roho ya Kiinjili ya udugu na mshikamano, unyofu na furaha, hata ulimwengu utakapojaribu kuwameza, tuombe:

 

Ili katika maisha ya wateule hawa, watu maskini na wenye njaa, wanaobaguliwa na kudhulumiwa, waone thibitisho la heri yao, tuombe:

 

Ili sisi sote tunuie tena kufuata ufukara wa Kiinjili hata tushuhudie unavyoleta uhuru wa moyo, tuombe:

 

Ili Kanisa, likisafiri hapa duniani kati ya udhia za ulimwengu na faraja za Mungu, limfuate kabisa Bwanarusi wake na kuifanya roho ya ufukara na ya upendo iwe ndiyo fahari yake, tuombe:

 

Ili ulimwengu mzima uache kudanganywa na miungu yote ya uongo na upate ukombozi kamili katika Kristo na katika Kanisa lake, tuombe:

 

234. Halafu padri, akiwaelekea watakaoweka ahadi anasali amefumba mikono:

 

Baba, mfalme wa mbingu na nchi,
wewe unapenda kuwafunulia watoto wadogo
mafumbo ya ufalme wako,
hazina iliyositirika kwa wenye elimu na akili
ambayo inastahili tuuze vyote kusudi tuipate,
na kwa kujifanya wa mwisho tujaliwe kuwa wa kwanza.

 

Lo, ufukara wa Kimungu!

Bwana wetu Yesu Kristo,

ambaye akisema vyote vinafanyika,

aliukumbatia kuliko yote,

akikosa hata mahali pa kulaza kichwa chake,

mpaka akakiinamisha atutolee Roho wake!

 

Ufukara wenye heri unaowashirikisha mema ya milele

wale wanaoupenda!

 

Ufukara mtakatifu ambao walionao na wanaoutamani

uliwaahidia ufalme wa mbinguni

na kuwatolea utukufu na uzima usio na mwisho!

Kwa upendo wa pekee ulionao kwao
uwatazame wateule hawa wanaokiri kuwa walitawaliwa
na tamaa ya malimwengu na kiburi cha maisha.
 
Ung’oe ndani mwao mzizi wa maovu yote,
yaani uroho wa pesa,
wasije wakakosa ufalme wa mbinguni kwa kitu kidogo hivi.
 
Wasifadhaikie ya kesho,
kama kwamba wewe usingetosha kushughulikia mahitaji yao,
bali waone furaha yao katika kushikamana na watu duni
na kwenda ulimwenguni kama wageni na wapitanjia tu,
bila ya kumiliki chochote,
wakiridhika daima na chakula na mavazi
unavyowapatia siku kwa siku,
vile unavyowafanyia ndege wa angani na maua ya kondeni.
 
Ndani mwako, Bwana, wajipatie vyote,
kwa kuwa wamekuchagua wewe peke yako,
na kwa rehema yako tu wanatumaini kuwa nawe milele.
 
Kwa njia ya Kristo, Bwana wetu.

 

235. Wote wanaitikia:

 

Amina.

 

236. Padri anamwekea mikono kichwani kila mmoja wa watakaoweka ahadi, halafu, akiwanyoshea wote pamoja, anaendelea na sala:

 

Bwana Yesu, ulimchagua Bikira fukara

ili utwae mwili na kukaa kwetu

kwa nguvu ya Roho Mtakatifu,

ukawatangazia maskini habari njema ya ukombozi kamili;

ukawaweka wawe mitume wako Wagalilaya duni,

waliofahamu ukosefu wao,

na waliokuwa tayari kuacha vyote kwa ajili yako.

 

Ummimine tena Roho Mtakatifu juu ya wateule hawa

wasadiki kweli na kuonja heri uliyoitangaza kwanza,

kwa kushika ufukara mkuu wa Injili yako.

 

Wawe wanyenyekevu na wanyofu,

wamtii mtu yeyote kwa ajili yako,

wajichukie na kuwapenda wanaowapiga shavu,

wapokee siku kwa siku riziki zao,

na kushirikisha kwa ukarimu kilichopatikana.

 

Wavihesabu vyote kuwa ni takataka ili wakupate wewe

ambaye kwa upendo wao ulijinyima hata pa kupumzikia,

ukaufanya msalaba tupu uwe ndio kiti chako cha enzi.

 

Wakukazie macho wewe,

uliyeanzisha na kutimiliza imani yetu,

wakijihadhari na mashauri ya kibinadamu tu,

wasije wakaacha kwa namna yoyote nyayo zako,

wala wasiangalie nyuma baada ya kushika jembe,

wala wasiache katikati ujenzi waliouanza,

kama mpumbavu asiyejua sharti la kuacha vyote

ili kukufuata hadi kikomo cha safari ya upendo,

kufa uchi msalabani ulivyofanya wewe,

unayeishi na kutawala daima na milele.

 

237. Wote wanaitikia:
 
Amina.

 

238. Kipindi kinamalizika kama kawaida kwa baraka au kwa shangilio:

 

Tumtukuze Bwana.

 

Tumshukuru Mungu.

 

 

TAKASO LA TATU YAANI TAKASO LA NDUGU

 

239. Baada ya mwezi mmoja hivi, linafanyika takaso la tatu linalohusiana na shauri la Kiinjili la utiifu wa kitawa ambao pia mzee wetu Fransisko ametusisitizia sana akiuweka kama mpaka dhambi tu. Kimsingi, taratibu na malengo ya ibada hii ni kama vile vya matakaso yaliyotangulia. Inafaa kuifanya siku ya kawaida katika kikanisa cha nyumba ya zoezi baada ya Zaburi za Sala ya Mchana, ikihudhuriwa na wanajumuia tu.

 

240. Kama kawaida, katika ibada ina nafasi ya msingi Liturujia ya Neno, ambayo inapendekezewa masomo mbalimbali ya kuchagua (taz. namba 381) lakini moja tu kutoka Injili, kwa kuwa ni la lazima na ndilo linalolipa takaso jina lake.

 

241. Baada ya hotuba, watakaoweka ahadi wanajipanga mstarini mbele ya padri ambaye, kwanza anawaelekea ndugu waliopo awaalike kuwaombea kimya roho ya kujikana kabisa, hadi kujikatalia maoni na matakwa kadiri yanavyopingana na yale ya Mungu. Halafu anawaalika wenyewe kusali kimya wakitokeza msimamo wao wa ndani wa toba na kujiombea neema kwa kupiga magoti.

 

242. Baada ya kimya kidogo, padri anawaalika waote kusali pamoja kwa maneno ya namna hii:

 

Tuwaombee tena ndugu zetu wanaokusudia kumkaribia Mungu wamtolee si sadaka za kujichagulia, ila utu wao wote kwa kutekeleza daima matakwa yake matakatifu tu.
 

243. Shemasi anatoa nia za namna hii:

 

Ili  wateule hawa wazidi kuungana na Baba kwa njia ya utiifu mtakatifu, tuombe:

 

Ili wamfuate Yesu, aliyejifunza kwa njia ya mateso kutii, na hivyo wakamilishwe pamoja naye, tuombe:

 

Ili Roho Mtakatifu awasaidie kutambua zaidi na zaidi matakwa ya Mungu, yaliyo mema, ya kumpendeza na makamilifu, tuombe:

 

Ili wajue namna ya kuwajibika, wakishirikiana na watumishi na walinzi katika utambuzi huo, tuombe:

 

Ili sisi sote tuchunguze upya msimamo wetu wa ndani kuhusu uongozi wa Mungu katika maisha yetu, na hasa imani yetu, iliyo msingi wa utiifu, tuombe:

 
Ili katika Kanisa na utawa ustawi moyo wa kunyenyekeana na wa kuwatii viongozi tuliopewa na Mungu, tuombe:
 
Ili ulimwengu, unaogawanywa na ubinafsi wa kila aina, uone kuwa utatuzi wa matatizo yake ni katika upendo unaokubali kutii, tuombe:

 

244. Halafu padri, akiwaelekea watakaoweka ahadi anasali amefumba mikono:

 

Baba Mtakatifu sana,

umependa Mwanao mbarikiwa na mtukufu

ajitoe mhanga juu ya altare ya msalaba

kama sadaka hai ya kufidia uasi wetu.

 

Hivyo alituachia mfano tufuate nyayo zake

kwa kuweka mapenzi yako matakatifu juu ya yote,

yawe chakula cha kwanza kwa ustawi wa uhai wetu.

 

Uwatazame sasa wanao hawa wanaojiandaa

kupokewa kwenye utiifu ndani ya utawa wetu:

uwafumbue macho ya imani ili,

wakikutolea sadaka kile kilicho muhimu zaidi kwao, yaani hiari,

watambue kutii si swala la nidhamu tu,

bali ni njia ya hakika ya ukamilifu

ambayo wewe, mchungaji wao,

unawaelekeza nukta baada ya nukta.

 

Watambue pia kizuio kikuu cha utakatifu na wokovu,

yaani kujitwalia utashi wao kama alivyofanya Adamu,

na kujitukuza kwa mema yale

ambayo mwenyewe unaonyesha na kutenda ndani mwao.

 

Kwa hiyo wajikane kabisa

na kujitia mikononi mwa viongozi wa Kanisa na wa utawa,

wasimtazame mtu tu, uliyemshirikisha mamlaka yako,

ila ndani mwake wakuheshimu wewe

ambaye wamejiweka chini yake kwa upendo wako.

 

Uwajalie wasijisingizie kwamba wanataka kufuata mambo mema

kuliko yale waliyoagizwa,

wala wasirudie matapishi ya matakwa yao

hata kukwaza na kuua roho nyingi.

 

Uwatie nguvu za kutekeleza unayoyaagiza,

halafu uwaagize yoyote yale unayoyataka.

 

Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

 

245. Wote wanaitikia:

 

Amina.

 

246. Padri anamwekea mikono kichwani kila mmoja wa watakaoweka ahadi, halafu, akiwanyoshea wote pamoja, anaendelea na sala:

 

Bwana Yesu Kristo,

uliwapenda watoza ushuru na makahaba

kuliko wanaokataa kufuata njia ya Mungu

wajiundie sura ya kuwapendeza.

 

Ulitia matakwa yako katika matakwa ya Baba

hata kufa, naam, hata kufa msalabani,

ukatualika tubebe siku kwa siku

mzigo unaoufanya kuwa mwepesi,

tukitekeleza mfululizo wajibu wetu

na kumtii kabisa Baba

kama watoto wanyenyekevu wenye upendo

ili tuwe kweli wadogo wako.

 

Uwajalie wateule hawa watambue na kuonja

jinsi ilivyo tukufu, takatifu na kuu

kuwa na Baba mbinguni ambaye wafanye kazi zake;

jinsi ilivyo takatifu, nzuri na tamu kuwa na Bwanaarusi mbinguni

ambaye waungane naye katika nia moja.

 

Wasiwe wapumbavu kiasi cha kujifanyia mipango,

bali wawe daima macho kutambua na kutekeleza ule wa Baba,

ambao ni bora hata ukileta uchungu mwingi.

 

Wasisogee mbali na maagizo yake, yawe ni wazi au la,

wala wasizurure nje ya utiifu,

bali wapendelee kuagizwa kuliko kuruhusiwa

na zaidi tena kuitikia wito wa kimisionari utokao kwake.

 

Kwa njia ya utiifu mtakatifu washinde

matakwa yote ya kibinadamu tu,

wakiweka mwili chini ya roho,

na utu mzima chini ya watu na viumbe

kadiri Baba atakavyopenda.

 

Wasitamani kukaa juu ya wenzao,

bali waamini kuwa aliyekubali nira ya wengine

hakuna nukta inayopotea bure kwake,

tena kuwa unyenyekevu wa yule anayetii kikamilifu kwa furaha

ni mkubwa kadiri alivyo duni yule aliyetoa agizo.

 

Kwa njia hiyo wajipatie uhuru wa wana wa Mungu,

wasiwe watumwa wa machaguo ya ubinafsi na ya ukaidi,

wa shaka, wasiwasi na fadhaiko,

wala wasifuate fikra za kidunia, mitindo ya ulimwengu na mabishano;

hatimaye wawe tayari kupenda na kutumikia tu

bila ya kujitafutia faida yoyote, isipokuwa wewe

unayeishi na kutawala daima na milele.

 

247. Wote wanaitikia:

 

Amina.

 

248. Kipindi kinamalizika kama kawaida kwa baraka au kwa shangilio:

 

Tumtukuze Bwana.

 

Tumshukuru Mungu.