SAFARI
YA MALEZI
ya Utawa wa
Ndugu Wadogo wa Afrika
YALIYOMO
0. UTANGULIZI
1. KUSHIKA INJILI
2. KUENEZA INJILI
3. WATENDAJI
4. UTU NA UKRISTO
5. HATUA ZA KUINGIZWA
6. MALEZI YA KUDUMU
7. HATIMA: MAMA MARIA
0.
UTANGULIZI
0.1.
AINA ZA UFUASI
Yesu, Mwana wa
Baba, ndiye ukombozi na ukamilifu wetu.
Kadiri ya matakwa ya Baba na kwa msukumo ya Roho
Mtakatifu, kila wakati wanapatikana waamini ambao wanamfuata Yesu na kushuhudia
fumbo lake kwa namna mbalimbali, hasa: walei kwa kuratibu malimwengu, wenye
daraja kwa kutoa huduma walizokabidhiwa mitume, na wanaoshika mashauri ya
Kiinjili kwa kufanana zaidi na Yesu safi, fukara na mtiifu ili wote watambue
kuwa kweli yu pamoja nasi hata mwisho wa dunia.
0.2.
KARAMA YETU
Mungu Baba ametujalia tuanzishe chama cha
kimisionari chenye jamaa mbalimbali ndani yake, ambamo tufuate nyayo za Mwanae
katika kujishusha mfululizo ili kutumikia kwa upendo hata kufa msalabani.
Sisi sote wanachama tuishi kati ya watu wa nyakati
zetu tukiwa na msimamo huohuo aliokuwanao yeye, ingawa kila mmojawetu kadiri ya
hali maalumu aliyonayo ndani ya Kanisa, kama mlei, kleri au mshikamashauri ya
Kiinjili.
Tarajio la chama ni kujaliwa kwa wingi mashahidi wa
imani ambao wamelishwa sana Injili hata waweze kuishi kama ndugu wadogo wa wote,
tena kwa namna bora zaidi na zaidi, katika mazingira mbalimbali watakayopangiwa.
0.3.
SAFARI HII
Kwa ajili hiyo yanahitajika malezi ambayo yafuate
maelekezo ya Kanisa na kulingana na karama yetu maalumu, tusiisawazishe na miito
mingine tusije tukamzimisha Roho Mtakatifu na kulidhoofisha taifa la Mungu.
Malezi hayana mwisho
kamwe: ingawa kuna hatua za kupigwa, ni mtiririko mmoja tu wa ustawishaji wa maadili n.k.
Ulinganifu wa malezi ya
Kiroho, ya kitume, ya
kielimu na ya kiufundi utusaidie tangu tunuie kukomaa ndani ya Kristo mpaka
tukutane naye moja kwa moja kwa kupokea ndugu kifo.
0.4.
MIONGOZO MAALUMU
Mpango huu unakusudiwa kuonyesha wazi namna ya
kuchochea karama yetu.
Upande mmoja utuonyeshe namna ya kuitekeleza katika
hatua mbalimbali za maisha hadi kufikia utakatifu.
Upande mwingine utuonyeshe namna ya kuishirikisha
kikamilifu kwa vizazi vijavyo viweze kuitimiza katika utamaduni wowote, kwa kuwa
Ufransisko unafaa kuutakasa na kuuboresha kila utamaduni kwa chumvi na chachu ya
Injili, bila ya kukwama katika wowote ule.
Lakini malezi hayawezi kupangwa jumla tu, pasipo
kuzingatia wahusika ni wepi na wanaishi wapi: kwa hiyo mpango huu utimilizwe na
halmashauri kuu kwa kila jamaa, hatua na nyumba.
Miongozo yake hiyo iwe
sahili, mifupi na wazi,
ilingane na mpango huu halafu ipitiwe kwa marekebisho kila baada ya miaka mitatu.
1. KUSHIKA INJILI
1.1.
UTATU NA UTAWA
Karama yoyote ya kitawa inaongoza kwa
Baba, ikitia
hamu ya kutimiza matakwa yake yote: humo utiifu unazaa uhuru wa kweli, useja
mtakatifu unatokeza jinsi moyo usivyoweza kutosheka na upendo wa viumbe, na
ufukara unachochea njaa ya haki aliyoahidi kuishibisha.
Halafu inaongoza kwa
Mwana, ikirahisisha ushirika
wa ndani naye, katika kuwatumikia kwa bidii Mungu na watu, na katika kusali na
kuteseka ili kueneza ufalme.
Hatimaye inaongoza kwa Roho
Mtakatifu, ikiandaa
kujiachia kwake na kutegemezwa naye katika maisha ya Kiroho, ushirika wa kidugu
na utume.
1.2.
KARAMA ZA KITAWA
Namna mbalimbali za kuishi kitawa zinatokana na
karama maalumu ambazo waanzilishi walijaliwa na ambazo wafuasi wao
wakashirikishwa ili wazitekeleze, wazitunze, wazichimbe na kuziendeleza
mfululizo kulingana na ustawi wa Mwili wote wa Kristo.
Kanisa linataka kila utawa ustawi kadiri ya karama
hai na bunifu ya mwanzilishi, kufuatana na mapokeo yake maalumu ya Kiroho, ya
kijumuia na ya kitume.
Hivyo sio tu kwamba tuna historia tukufu ya
kuikumbuka na kuisimulia, bali pia tunayo nyingine ya kuitimiza bado ili katika
milenia mpya ulimwengu uliokabidhiwa mikononi mwetu binadamu uwe na imani na
upendo, haki na amani zaidi, uwe kama utangulizi wa ulimwengu ujao.
Roho anatusukuma tukafanye
makuu, hivyo tuitazame
kesho kwa tumaini.
1.3.
UTAWA NA NYAKATI ZETU
Tumeitwa tutambue na kuhudumia mpango wa Mungu kwa
ajili ya watu, ambao unatangazwa na Maandiko Matakatifu na kujitokeza katika
maisha yao.
Kwa hiyo tuwe tayari kuchochewa na Neno la Mungu na
ishara za nyakati, tukiunganisha daima upya wa Kiroho na ari ya kitume, ambavyo
cha kwanza kinawezesha cha pili.
Tumshiriki Mungu ili kukabili changamoto za nyakati
zetu, tukiamini ya kuwa Roho anaweza kutoa majibu ya kufaa hata kwa zile ngumu
zaidi.
Mbele ya changamoto kuu tatu za ulimwengu tuonyeshe
jinsi mashauri ya Kiinjili yanavyotustawisha kwa kutuelekeza moja kwa moja kwa
Mungu aliye Wema mkuu, badala ya kufuata mielekeo ya kibinadamu iliyoathiriwa na
dhambi.
Hasa siku hizi wanahitajika watakatifu ambao
watumainishe wale waliokata tamaa kuhusu maisha na maana yake: ubora wa utawa
unaweza kuwatuliza wale wanaoona kiu ya tunu halisi.
1.4.
USEJA MTAKATIFU NA UTAMADUNI WA ANASA
Changamoto ya kwanza ni utamaduni wa anasa unaoona
jinsia ni mchezo tu usio na masharti: matokeo ni maovu ya kila aina yanayoathiri
kinafsi na kiuchumi jamii, familia na watu mmojammoja, kuanzia watoto.
Itikio la maisha ya wakfu ni kuishi useja mtakatifu
kwa furaha, na hivyo kushuhudia uwezo wa Mungu unaofanya kazi katika udhaifu wa
binadamu hata akampenda yeye kuliko yote na kumpenda yeyote kwa uhuru wa wanae.
Ushuhuda huo unahitajiwa na wote kadiri
wanavyoshindwa kuuelewa, ili wajifunze kuwa wa kweli katika mafungamano.
Mapendo yao ya kibinadamu yanapewa kielelezo cha
yale safi ya mtawa ambaye anachota katika Mungu-Upendo: kwa kuzama katika fumbo
la Utatu anajisikia apende wote pasipo mipaka na kwa kujitawala.
Hakika, usafi unaukomboa moyo kwa namna ya pekee na
kuzidi kuuwasha upendo kwa Mungu na kwa watu wote.
Mchango mmojawapo mkubwa wa mtawa ni kuonyesha kwa
maisha yake uwezekano wa kujitoa kwa wengine na kushiriki furaha na huzuni zao
kwa uaminifu na udumifu, pasipo vitendo vya jinsia wala misimamo ya utawala na
ubaguzi.
Pia utawa unamaanisha na kuelekea moja kwa moja
uzima wa milele, hasa kwa njia ya useja unaotugeuza tayari kwa ajili ya
ulimwengu ule ambapo watu hawaoi wala hawaolewi.
1.5.
KUZINGATIA TUNU NA GHARAMA YAKE
Kwa kuwa useja huo unadai usafi kamili na kuyahusu
sana maelekeo yetu ya dhati, wanazoezi wasiuahidi wala wasikubalike kabla ya
kujaribu vya kutosha na kufikia ukomavu wa kufaa upande wa nafsi na wa hisi za
moyo.
Watambue kwamba elekeo la umimi tulilonalo linataka
tutie maanani mno mapendo ya kibinadamu, na kumtumia mwenzetu kama njia ya
kujipata heri fulani.
Lakini wasiangalishwe tu kuhusu hatari
zinazowakabili, bali walelewe kukumbatia useja kwa ajili ya ufalme wa Mungu,
kama tunu kwa ustawi wao na wa Kanisa.
1.6.
MALEZI YA USEJA
Malezi ya useja mtakatifu
yajitahidi:
- kuchochea furaha na shukrani kwa upendo ule ambao
kila mmoja ametazamwa na kuteuliwa na Yesu;
- kuangazia matunda ya moyo
usiogawanyika, yaani
uzazi mwingi wa Kiroho hasa katika utume;
- kuhimiza adhimisho la
upatanisho, uongozi wa
Kiroho na upendo halisi katika jumuia;
- kujenga hali ya kuaminiana kati ya walelewa na
mlezi, ambaye awe tayari kusikiliza yoyote kwa upendo ili aangaze na kutegemeza;
- kumsaidia kila mmoja akubali
mang'amuzi yake
mabaya ya zamani kwa kutambua udhaifu, kujinyenyekeza na kukesha;
- kumshukuru Mungu tu na kuzuia kiburi cha
kujipongeza kwa usafi, usije ukazua ugumu wa moyo;
- kufundisha juu ya jinsia mbili upande wa
mwili,
nafsi na roho;
- kueleza maana ya mwili na namna ya kutunza afya
yake;
- kuelekeza kujitawala upande wa ashiki na wa
moyo,
na vilevile upande wa ulafi na ulevi;
- kuwa waangalifu katika kutumia vyombo vya
upashanaji habari na katika mafungamano na watu (busara inawadai watumishi,
walinzi na walezi pia wachukue hatua za kufaa).
1.7.
UFUKARA NA UTAMADUNI WA FEDHA
Changamoto ya pili inatokana na ulimwengu kuabudu
pesa na mali, kwa kutoelewa maana yake kwa maisha, wala kufuata kiasi kinachofaa,
wala kujali mahitaji na mateso ya wanyonge, wala kuhifadhi mazingira kwa ajili
ya wajukuu wetu.
Hivyo leo ufukara unatawala maisha ya watu wengi na
ya nchi nyingi kwa sababu ulimwengu unaendeshwa namna inayozidisha hali ya njaa,
ujinga, maradhi, kukosa kazi, kunyimwa haki za msingi, ukoloni mamboleo, rushwa
n.k.
Itikio la maisha ya wakfu ni ufukara wa Kiinjili
ambao upendo unahimiza kupokea mlio wa wenye mashaka katika matatizo, mateso na
matarajio yao ili kuwasaidia wakabili maisha kwa mshikamano wa wote.
1.8.
YESU NA UFUKARA
Asili ya ufukara huo wa Kiinjili ni kutafakari
alivyoishi Yesu fukara msulubiwa; udhihirisho wake ni kushika maisha ya kawaida
ya watu wadogo kuhusu chakula, mavazi na nyumba, na kukwepa uwezo wowote wa
kutawala wengine kisiasa, kijamii, kiuchumi, kielimu na kidini.
Moyo wa maskini tu ulioamua kumfuata Yesu hivyo
unaweza kushikamana na watu usiambatane na vitu.
Jumuia ndogo za kitawa katika mazingira duni
zinatokeza ule upendeleo wa Kiinjili kwa fukara, unaotufanya sio tu
tuwashughulikie, bali tuishi pamoja nao, tena sawa nao kadiri inavyofaa
kulingana na hali halisi na mahitaji ya kila mmojawetu, hasa akiwa bado katika
hatua za kuingizwa.
Upendeleo huo unatokana na upendo ambao Yesu
aliuishi, hivi kwamba kila mfuasi wake anapaswa kuwa nao, hasa sisi tunaomfuata
kwa karibu zaidi katika maisha ya wakfu, ambayo ni ya kifukara na ya kuwatetea
fukara.
Mshikamano nao ndio msimamo unaotufanya ndugu
wadogo, ni mhuri wa Ukristo halisi, kichocheo cha wongofu, tendo la kitume na
thibitisho la ujio wa ufalme wa Mungu, ambapo fukara wanahubiriwa na kuhubiri
Injili.
Zaidi ya hayo ufukara wenyewe ni tunu iliyotangazwa
na maisha yote ya Yesu kama heri ya kwanza na ushuhuda wa kuwa Mungu ndio
utajiri pekee wa moyo.
1.9.
MALEZI YA UFUKARA
Malezi ya ufukara yakazie maisha ya Yesu
aliyejifanya maskini kwa ajili yetu.
Halafu yahimize:
- kuwa na
unyenyekevu;
- kuishi kwa imani kama wana wa Baba wa mbinguni
anayejua mahitaji yetu na kututunza siku kwa siku;
- kuwajibika katika
kazi;
- kujali vitu vinavyopatikana
jumuiani;
- kutaka vyote viwe kweli vya wote ili kila mmoja
apate anavyohitaji;
- kutumia fedha na vitu kwa usimamizi wa
viongozi;
- kubana matumizi
iwezekanavyo, bila ya kufuata
uwezo uliopo wala ruhusa tu;
- kuwa tayari kukosa vitu
mbalimbali;
- kujiepusha na vitu ambavyo watu wadogo hawawezi
kujipatia, ili kuishi ufukara kwa ukweli zaidi;
- kujinyima kwa hiari hata vitu
halali.
Pia yazingatie:
- historia ya kila ndugu kabla ya kupata wito
(wengine
walijitegemea na kupata vingi, kumbe wengine walikuwa na hali ngumu kuliko ile
ya jumuia);
- hali ya sasa ya familia yake na matarajio
iliyonayo juu ya mwanae;
- mafundisho ya Kanisa kuhusu
jamii, kwa kuwa
ufukara wetu haulengi maendeleo ya roho tu.
1.10.
UTIIFU NA UTAMADUNI WA UHURU USIO NA MASHARTI
Changamoto ya tatu inatokana na mtazamo ambao
unadai hiari ya mtu isibanwe sana na maadili, na hivyo unasababisha kwa wingi
ubinafsi, dhuluma, ukatili n.k.
Itikio la kufaa ni utiifu wa kitawa unaoonyesha
kwamba kutimiza matakwa ya Mungu kunatukamilisha kwa kukuza ukweli wetu kama
viumbe tunaomtegemea kabisa Muumba, na kama watoto wapenzi tunaotafuta na
kutekeleza kwa pamoja yale yote yanayompendeza Baba.
Umoja huo wa jumuia ni ishara kubwa ya jinsi ya
kushinda ugomvi na utengano, na ni hakika ya kufuata njia tuliyopangiwa.
Katika malezi na maisha ya kila
siku, chama
kinatusaidia tupate msimamo wa kudumu, kwa mafundisho ya hakika kuhusu kufikia
ukamilifu, kwa ushirika wa kidugu katika kumfuata Yesu na kwa utiifu
unaoimarisha hiari yetu katika kuitikia wito.
1.11.
KUSHIRIKI UTIIFU WA YESU
Shauri hilo, tunalolipokea kwa upendo ili kumfuata
Yesu aliyetii hata kufa msalabani, linatuelekeza tuweke matakwa yetu chini ya
yale ya wakili wa Mungu, yaani mlinzi, mtumishi, askofu na hasa Baba Mtakatifu.
Utiifu huo hautudhalilishi bali unastawisha uhuru
wetu kama wana wa Mungu wanaoendeleza ule wa Yesu kwa wokovu wa ulimwengu.
Nidhamu utawani isishikwe tu ili kulinda maisha ya
kijumuia na upendo, bali kama sharti la kujijengea tabia ya kujitawala, kukomaa
n.k.
Hivyo itekelezwe namna inayostawisha utayari wa
kutii si kwa hofu, bali kwa kufuata dhamiri na maadili.
Polepole ndugu wazoee kutumia vema hiari yao katika
kujifanyia mipango na kutenda kwa uelewano na watu wa ndani na wa nje ya jumuia,
hasa viongozi.
Mtumishi au mlinzi anayejadiliana na ndugu zake
anawasaidia kutii kwa uwajibikaji, mradi hatimaye awe tayari kutoa uamuzi na
kuagiza la kufanya kwa niaba ya Mungu.
Katika majadiliano hayo tuzuie mawazo ya kibinadamu
mno yasijiingize upande wa kiongozi wala wa ndugu wala kati yao, bali wote
tulenge tu matakwa ya Mungu yafanyike.
1.12.
MALEZI YA UTIIFU
Katika malezi ya utiifu tukumbuke
kwamba:
- ni lazima kwanza tutambue na kutambuliwa hadhi
yetu kama watu na watoto wa Mungu ili tutii kibinadamu, si kwa unyonge;
- tunapaswa kuvuka toka yale yanayotupendeza sisi
hadi yale yanayompendeza Mungu, ambayo yanajitokeza kwa namna ya pekee kwa njia
ya wachungaji wa Kanisa na ya kanuni na katiba walizotuthibitishia;
- ushuhuda wetu kama watawa watiifu una uzito
kuliko nadharia tunayowafundisha walelewa, ingawa hao wanatakiwa kufuata njia
nyofu bila ya kukwazwa na mifano yetu mibaya.
1.13.
USHUHUDA WA JUMUIA
Kwa kuwa tendo la kuweka ahadi linatuingiza katika
chama kwa haki na wajibu vinavyoelezwa na katiba, tunapaswa kuishi kidugu katika
jumuia yake mojawapo kama mahali ambapo upendo, ukichota nguvu katika sala,
uongoze maisha yote na kuzaa heri.
Hivyo uanachama unatuwezesha kumpatia Yesu ushuhuda
wa hadhara na wa pamoja, mradi maisha yetu yawe ishara ya ufalme wa Mungu na
tangazo hai la Injili.
Kwa ushuhuda huo wa jumuia zilizojaa furaha na Roho
Mtakatifu, ambapo ubinafsi unashindwa na uwajibikaji kwa ajili ya wengine,
ambapo madonda yanaponywa na msamaha, na ambapo karama inaongoza uaminifu wa
wote katika wito na utume, ndivyo Kanisa linavyojitambulisha kama sakramenti ya
umoja na Mungu na kati ya watu, na kuonyesha matunda ya amri mpya aliyotuachia
Bwana.
Pamoja na hayo, Kanisa linataka kuonekana wazi
ulimwenguni hata kwa njia ya kanzu zetu.
1.14.
KATIKA USHIRIKA WA KANISA
Maisha ya Wakristo wa kwanza huko Yerusalemu ndiyo
kielelezo ambacho Kanisa lilikizingatia kila lilipojaribu kuchochea ari ya
mwanzoni na kuendelea Kiinjili safari yake.
Kwa mfano wao tuzidi kuchanga na waamini wote neema
na juhudi ili sura ya Kanisa ipendeze, nalo likabili kwa nguvu ya umoja
changamoto za nyakati zetu.
Basi, tusimbane Roho katika chama
chetu, lakini
tusaidie wengine kufaidika na karama yetu.
Sisi watawa tunaitwa kuwa wataalamu wa
ushirika,
mashahidi na wajenzi wa ule umoja ulio lengo la mpango wa Mungu: tuwe hivyo
kutokana na tamko letu la kushika mashauri ya Kiinjili ambayo yanakomboa ari ya
upendo isiwe na kizuio chochote; tena kutokana na mang'amuzi yetu ya kila siku
katika kuishi, kusali na kufanya kazi kama jumuia ya Kikanisa.
Kwa namna ya pekee ushirika wa Kanisa unatudai
utiifu wa akili na moyo kwa maaskofu, ambao utekelezwe mbele ya watu wote, hasa
tukishughulikia katekesi, ufundishaji, uandishi na upashanaji habari.
Msimamo wetu watawa kuhusu jambo hilo ni muhimu kwa
sababu tuna nafasi maalumu katika Kanisa na katika kushiriki utume wa maaskofu.
1.15.
WANDANI WA MUNGU
Ili tujaliwe kuwa kweli
manabii, yaani kusema na
wote kwa niaba ya Mungu, kwanza ni lazima tuwe wandani wake, wasikivu kwa Neno
lake katika nafasi yoyote ya maisha, wenye utambuzi wa Kiroho na kupenda ukweli.
Basi, tuzidi kumuelekea
Mungu, tukitafuta uso wake,
tukiachana na mitazamo isiyolingana na ufunuo wake, halafu kubadili mwenendo
wetu pia.
Tukiwa wanafunzi wa Neno linalotolewa na
Kanisa,
tunakua kumuelekea Kristo katika yote hata tufikie kimo cha utimilifu wake,
tukizidi kujifunza fumbo la wokovu, kumuabudu Baba katika Roho na Ukweli, na
kutekeleza ukweli kwa upendo.
1.16.
TOBA YA KUDUMU
Ili tuwe mashahidi halisi wa Kristo duniani
kote,
kwanza tunapaswa kuhakikisha tumeitwa na Mungu na kumtolea nafsi yetu pamoja na
yote tuliyonayo, hasa yale yanayotuzuia tusimuitikie kikamilifu.
Wito wetu wa toba ya kudumu unataka turekebishe
mfululizo uhusiano wetu na Mungu, na watu na ulimwengu ili Mungu atawale moja
kwa moja maisha yetu.
Kwa ajili hiyo tukiri kwa moyo
udhaifu, ujinga na
uovu wetu, halafu tupambane navyo kwa roho na kwa mwili pia, tukifuata kwa
uaminifu kanuni, katiba, ratiba na mbinu za kufanya juhudi.
1.17.
MAISHA YA KIROHO
Daima maisha ya Kiroho yawe na nafasi ya kwanza
katika malezi yetu ili chama kiwe hasa shule ya Injili.
Ukarimu kwa
fukara, uzazi wa kitume, mvutio kwa
miito na vinginevyo vinategemea ustawi huo wa ndugu mmojammoja na wa jumuia
nzima katika kuishi ndani ya Kristo kadiri ya Roho Mtakatifu kwa utukufu wa Baba.
Tunafanya safari hiyo ya uaminifu mkubwa zaidi na
zaidi kwa Mungu Baba tukiongozwa na Roho anayetulinganisha na Yesu katika
ushirika kamili wa Kanisa.
Safari hiyo inadai wongofu wetu wa binafsi na wa
kijumuia usikome kamwe, bali uzidi kukamilika kwa kulipokea Neno la Mungu mpaka
ndani ya moyo wetu na ya utendaji wetu, na kwa kuupokea uvuvio wa Roho Mtakatifu
kadiri tulivyojaliwa na Baba, aliye asili na lengo la maisha yoyote.
1.18.
NENO LA MUNGU
Neno la Mungu ndilo chemchemi ya kwanza ya maisha
ya Kikristo: linachochea uhusiano wa dhati na Mungu aliye hai na utekelezaji wa
matakwa yake yenye kuleta wokovu na utakatifu.
Ndiyo sababu toka mwanzo watawa waliheshimu usomaji
wake wa Kiroho, hata hekima ikaangaza maisha yao.
Uzoefu na Neno uliwapa mwanga unaohitajika kwa
utambuzi, wasilingane na mitindo ya ulimwengu.
Kwa mfano wa mwanzilishi
wetu, tuitafakari hasa
Injili ili kuzingatia matendo na maneno ya Yesu, Maria na mitume.
Kutafakari Neno na mafumbo ya Kristo kunaleta ari
katika sala na utume; pia kutumia muda wetu miguuni pake ndio namna wazi ya
kumtangaza Yesu kuwa ni Bwana wetu na kuwa yu hai kati yetu.
1.19.
USHIRIKISHANO JUU YA INJILI
Kwa kuwa maisha yetu ni ya Kiinjili
hasa, tutie
maanani ushirikishano wa mawazo na mang'amuzi kuhusu Injili.
Kuitafakari kijumuia kuna thamani kubwa kwa
kutufanya tuchange kwa furaha utajiri tuliochota humo ili tukue pamoja na
kusaidiana kidugu katika maisha ya Kiroho.
Tena, ushirikishano juu ya Neno unalisha imani na
tumaini, kuheshimiana na kuaminiana, kupatana na kushikamana katika sala.
Halafu zoezi hilo linatusaidia kulieneza kati ya
viungo vingine vya taifa la Mungu.
Tutafute namna za kuwafanya wote wajifunze
kushirikishana kwa unyofu.
Vilevile ugumu wa mtu fulani kushirikisha ulio na
mzizi wa kisaikolojia usiwe kisingizio cha kutomjali, bali wote wapokee toka
kwake pia yale anayotaka kuyatoa kwa maneno na matendo.
1.20.
LITURUJIA
Tuwe na hakika ya kuwa jumuia inajengwa na
liturujia, hasa ekaristi na upatanisho.
Maajabu hayo ya Mungu yanasababisha
sifa, shukrani, furaha, umoja wa mioyo, nguvu za kukabili matatizo ya kila siku na kutegemezana
katika imani.
Yesu anazidi kutuita pamoja kila siku hasa katika
ekaristi ili aseme nasi na kutuunganisha naye na kati yetu: ndio moyo wa maisha
ya Kanisa na ya utawa vilevile.
Ekaristi inafungamana na juhudi za wongofu
zinazokamilika katika kupokea mara nyingi upatanisho, ili tuwe wazi na waaminifu
katika uhusiano na Mungu.
1.21.
EKARISTI
Sisi tuliomfanya Yesu awe maana pekee ya maisha
yetu, tunavutwa kutamani tuzidi kumshiriki kwa njia ya sakramenti inayomfanya
awepo kati yetu, ya sadaka anayojitoa kwa upendo kwetu, na ya meza anayotulisha
safarini.
Kwa njia hiyo tunaitwa kuishi fumbo la Pasaka
tukiungana naye katika kujitoa kwa Baba kwa nguvu ya Roho.
Tumuabudu mara nyingi na kwa muda mrefu katika
ekaristi ili tufurahie na kutamani zaidi zawadi hiyo.
Hata tusipoweza kuhudhuria Misa kila
siku, kiini
cha maisha yetu kiwe ni fumbo hilo la Bwana kuwepo hai ndani ya jumuia.
Katika kulea roho ya kijumuia tuanze daima
hapo,
kwa kuwa ekaristi ikiadhimishwa au kuabudiwa na kuliwa ndipo umoja wa mioyo
unapojengwa.
1.22.
SALA YA JUMUIA
Pamoja na
ekaristi, Sala ya Kanisa inatokeza wito
wetu wa kuinua daima mioyo kwa Mungu ili kumtolea sifa na maombezi.
Adhimisho lake linahuisha mfululizo sala yetu kwa
kutuletea Neno kadiri ya mzunguko wa mwaka wa liturujia na linatufanya tujisikie
washiriki wa taifa la Mungu.
Sala ni zawadi ya Mungu inayotupasa tuipokee na
kuistawisha kwa bidii, mafunzo na uaminifu.
Hasa walelewa waongozwe kuthamini zaidi na zaidi
nafasi za sala ya jumuia zinazoongoza mwendo wa siku zetu, ili wazitumie zote
kwa bidii walau kuanzia zoezi, wakidumu katika uchipukizi na baadaye.
Kila ndugu apate ujuzi wa
kitaaluma, wa Kiroho na
wa kichungaji kuhusu Maandiko na liturujia utakaomwezesha kulishwa navyo na
kuwasaidia waamini wengine wavumbue hazina hizo na kufaidika nazo.
Ili jumuia itimize wajibu wa kulea katika sala,
ndugu wote watoe mchango wao kwa kujenga mazingira yanayofaa, kwa kujiandaa,
kuwahi na kusali vizuri.
1.23.
SALA NA KIMYA
Sala ieleweke kuwa ni muda wa kukaa na Mungu aweze
kufanya kazi ndani mwetu na kuenea katika maisha yetu, akitufariji na kutuongoza
kati ya uchovu na mawazo ya kila aina, kusudi hatimaye tuwe wake tu.
Sala ya pamoja inazaa kadiri inavyoshikamana na ile
ya binafsi: toka mwanzo wa malezi yetu tusisitize umuhimu wa kuhusiana kwa dhati
na Baba, wa kuongea na Bwanaarusi na rafiki moyo kwa moyo, wa kuchimba
yaliyoadhimishwa katika Roho Mtakatifu, na wa kutunza kimya cha ndani na cha nje
kama nafasi ya Roho na Ukweli kutuhuisha kabisa.
Kusikia na kuitikia wito wa utakatifu kunadai kimya
hicho ambacho kimejaa uwepo wa Mungu tu, na kinatuwezesha kuelewa anapotaka na
anavyotaka kusema nasi.
Hivyo tuzoee mapema kimya na
upweke: upweke wa
hiari unaelekeza kwenye kimya cha ndani, nacho kinadai kimya cha nje.
Tufurahi kuwaruhusu ndugu waliokwishaonyesha
ukomavu fulani katika maisha ya kijumuia waweze kujipatia nafasi zaidi za upweke
na sala.
Nyumba zetu ziwe tayari kupokea watu kwa
ukarimu,
hasa kwa sala, lakini bila ya kuvuruga hali ya kimya, nafasi ya faragha na
mengine ya kitawa.
1.24.
SALA NA KUMSHIRIKI YESU
Tukipanda mlima wa sala pamoja na
Yesu, kama
walivyofanya Petro, Yakobo na Yohane, tunafunuliwa fumbo lake katika utukufu wa
Utatu na katika ushirika wa watakatifu, tukatamani kukaa naye moja kwa moja; pia
tunaandaliwa kushuka naye kati ya watu tukabili shughuli za kila siku na
kushiriki msalaba wake bila ya kukwaza nao.
Daima watu wa sala ndio waliofanya
makuu, kwa
kuelewa na kutekeleza vizuri matakwa ya Mungu.
Sala inakusudiwa kutuathiri hata kila
wazo, neno na
tendo letu, katika nafasi muhimu na za kawaida vilevile, lionyeshe tunavyofanana
na Yesu katika kujitoa mhanga.
Ushirika naye utuongoze kujiunga na kila jambo
ambalo mwenyewe aliunganika nalo kwa dhati: na Baba aliyemtuma ulimwenguni, na
Roho aliyemsukuma maishani, na Kanisa alilojitoa kwa ajili yake, na binadamu
wote, hasa wenye hali ngumu zaidi ambazo alipenda kuzishiriki kama kaka yao.
Tusichoke kuhimizana ili wakati wa shughuli
tudumishe ile roho ya sala inayotakiwa iwe lengo la malimwengu yote, hivi kwamba
siku nzima na kazi zake mbalimbali zigeuke kuwa nafasi za kuungana na Bwana.
Maisha hayo ya ndani yanaleta furaha ya Kifransisko
ambayo ni nguvu ya kushinda mabaya na kuzidi kujitoa maisha yote.
1.25.
MALEZI YA SALA
Katika malezi ya sala
tuelekeze:
- kuunda moyo safi unapoweza
kung'aa uzuri wa Mungu;
- kutambua daima uwepo wa Mungu na matakwa
yake;
- kustawisha uwezo wa kuyashangaa maajabu yake
katika uumbaji na ukombozi;
- kuzoea kusikiliza Neno la Mungu na kutumia sala
za Biblia ili kumuonja Mungu na kuingia katika historia ya wokovu;
- kushiriki kikamilifu maadhimisho ya Kanisa kadiri
ya mwaka wa liturujia ili kuishi mafumbo makuu ya ukombozi;
- kufuata vema ratiba ili kudumisha sala hata
isipojibubujikia;
- kuwa na moyo mpana ambao unasali na kuishi
ukishiriki furaha na huzuni za wote;
- kujua jinsi watu mbalimbali wa zamani na wa siku
hizi walivyong'amua fumbo la Mungu;
- kumpenda kitoto Mama wa Mungu aliyekingiwa dhambi
asili.
1.26.
UDUGU
Mang'amuzi ya dhati ya Mungu kuwa ni Baba
yalimuongoza mzee wetu Fransisko kutambua na kuishi upya udugu wake na watu wote,
hasa na wale aliojaliwa na Baba awe nao njia moja.
Tukishiriki karama
yake, tuwapokee na kuwapenda
wenzetu kama zawadi ya Bwana.
Tumetumwa kushuhudia udugu wa Kikristo kwa kuwaona
wote kuwa ni wana wa Mungu tayari, au walau wanaitwa wawe hivyo, na kwa kujitoa
kwa upendo kwa kila mmojawao, hasa wale wa mwisho.
Jina la chama lina uzito mkubwa na linadai
tuwe:
- wadogo wa Yesu, wenye uhusiano wa dhati
naye,
aliye kaka wa wengi;
- ndugu sisi kwa sisi kwa kupendana na kufanya kazi
pamoja;
- ndugu wadogo wa kila mmoja kusudi tustawishe
udugu ndani ya Kanisa na ya jamii, tukishuhudia upendo wa Kristo kwa wote na
kuwakumbusha ukweli huu wa msingi: "Nyinyi nyote ni ndugu".
1.27.
KUIMARISHA UDUGU
Ili tuhifadhi na kuimarisha maisha ya kidugu kadiri
ya Injili:
- tujiite na kuwazoesha wote watuite "ndugu";
- tunapoeleza karama yetu ili kuchochea miito na
kuingiza utawani, tuyakazie mambo makuu ya maisha hayo (kuishi kijumuia, kuwa
wadogo wa wote n.k.) kuliko kazi au hadhi fulani (upadri n.k.);
- kwa kuwa wito wetu kimsingi ni
uleule, malezi ya
utakaji na zoezi yalingane kwa wote; baadaye tu ndugu wapewe nafasi ya
kujiendeleza kadiri ya uwezo wao na ya udogo wetu;
- tutoe huduma za kutufaa zaidi kama wadogo
(kutangaza
Neno, kufundisha sala, kutekeleza matendo ya huruma, kufanya kazi za mikono n.k.);
- tuwe watu wa haki na
amani, tukiwasaidia wote
kuunda dhamiri zao kuhusu tunu hizo;
- tuchangie pia maendeleo halisi ya jamii kuendana
na Injili na katiba yetu ili tuwe watu wa Mungu wasio mbali na mashaka ya maisha
ya watu.
1.28.
UPENDO WA KRISTO
Kristo katika fumbo la Pasaka ndiye kielelezo cha
kudumu cha namna ya kujenga umoja, tena ndiye chemchemi na kipimo cha upendo
unaohitajika.
Ili tufaulu kuishi kidugu ni lazima Roho wake
atuwezeshe kupendana kama Yesu alivyopenda.
Akiwa ni upendo wake uliomiminwa mioyoni
mwetu,
anatusukuma tupende wote kwa kubeba udhaifu wao na matatizo yao hata kujitoa
mhanga kwa ajili yao.
Hasa kuishi na ndugu ambao hawajisikii
vizuri, na
hivyo wanasababisha uchungu kwa wenzao na kuvuruga maisha ya jumuia, ni fursa ya
kukomaa kiutu na Kikristo.
Safari hiyo ya ukombozi wa moyo inadai tujikane ili
tumpokee mwingine alivyo, pamoja na tofauti na mipaka yake, sifa na kasoro
vilevile, kuanzia yule aliyepewa uongozi, tusije tukamdai mno.
Moyo huo tu, ambao unatokana na upendo na kulenga
ustawi wa upendo ndani mwetu na mwa wenzetu, utatuwezesha kutegemezana,
kukosoana, kujishtaki hadharani, kukagua na kupanga maisha kwa pamoja n.k.:
namna hizo zote tuzing'amue kuanzia utakaji.
Ikiwa ndugu atajisikia anapokewa
alivyo, hapo tu
ataondoa kinga zake na hofu zinazomfunga akapokea ukosoaji na shauri na kukua
vema.
1.29.
JUMUIA NA UKOSEFU
Kwa kuwa maisha na malezi yetu yana elekeo la
kidugu, kumuingiza mtu katika utamu na ugumu wa kuishi pamoja kunafanyika katika
jumuia.
Wengi wanavutiwa
nayo, lakini kudumu ndani yake
katika hali halisi ya maisha kunaweza kukawa mzigo mzito: mtu wa kawaida,
akipenda umoja, hataki kuugharimia mwenyewe kwa kuwajibika.
Kwa hiyo toka mwanzo tujulishe kwamba maisha ya
jumuia yanadai sadaka, lakini kujiangamiza kwa ajili ya wenzetu ndiyo njia ya
wokovu: Injili inataka watu ambao, sawa na chembe ya ngano, wanajua kujifia ili
udugu ustawi.
Hivyo jumuia inakuwa shule tunapojifunza kumpenda
kweli Mungu kwa kuwapenda ndugu aliowaweka karibu nasi, na binadamu wote, hasa
wanaohitaji zaidi huruma ya Mungu na mshikamano wa kidugu.
Jumuia kamili haipatikani
duniani, ambapo Kanisa lenyewe, pamoja na miundo na utakatifu wake, linajengwa juu ya udhaifu wa
binadamu.
Hata hivyo kwa msaada wa Mungu tunaweza daima
kuongoka na kujenga kwa pamoja jumuia juu ya msamaha na upendo.
Umoja tunaoulenga unategemea
upatanisho: kwa hiyo
utovu wetu wa ukamilifu usitukatishe tamaa, mradi tushike upya kila siku njia
tuliyoelekezwa na Neno.
1.30.
NJIA ZA UMOJA
Umoja halisi ni zawadi ya Mungu kwa wanaosikiliza
Injili na kuishika.
Ili tupendane kama watoto wa Baba
mmoja:
- tukuze hali ya
kifamilia, ya furaha na ya unyofu
kati yetu;
- tuzidi
kuaminiana, kuelewana, kuthaminiana;
- tuelezane shida
zetu;
- tuimarishane wakati wa taabu na wa kuvunjika
moyo;
- tupendane bila ya
masharti;
- tutumikiane kwa
ukarimu;
- tutiiane kwa
upendo;
- tusihukumiane;
- tuzoee kuvumilia na kusamehe sabini mara
saba;
- tukosoane kidugu tukilenga daima
wongofu;
- tupambane na ugeugeu wetu na misukosuko ya
kujianzia;
- tuachane na chochote kinachoweza kuvuruga maisha
ya kidugu;
- tushirikishane kila
kitu.
Pasipo juhudi
hizo, umoja haupatikani.
1.31.
FUMBO LA JUMUIA
Ushuhuda wa kidugu unadhoofishwa na shughuli nyingi
mno zikituzuia tusishiriki kwa kawaida sala za pamoja, maisha ya jumuia na
huduma za nyumbani.
Basi, ratiba ya kila siku isipangwe kwa kujali
utendaji wa kitume kuliko maisha ya kidugu, bali jumuia ijipatie muda wote
unaohitajika ili kuboresha maisha hayo yasiwe ya kuhangaika hata kujichosha
bure.
Tuelewe mapema kuwa ushirika wa kidugu sio tu njia
ya kufanya vizuri kazi yetu, bali ni mahali pa kung'amua uwepo wa Yesu hai kati
yetu, tena pa kuushuhudia Utatu, yaani Baba anayetaka kuwafanya watu wote kuwa
familia moja, Mwana aliyekusanya waliotawanyika, na Roho anayewaunganisha katika
upendo.
Umoja hautegemei raha ya kulingana kwa
mawazo, kwa
tabia na kwa machaguo, bali wito wa Bwana aliyetuweka wakfu namna moja ili
tuishi pamoja na kufanya utume mmoja.
Hasa mfano wa jumuia za kimataifa unaweza ukasaidia
makabila mbalimbali kushirikiana, kutajirishana na kurekebishana.
Lakini umoja kati ya watu tofauti si
rahisi: unadai
nia imara upande wa wote, na utambuzi upande wa viongozi na walezi.
Juhudi za kuwatii kwa imani, za kupokeana wenyewe
kwa wenyewe na za kutatua matatizo katika jumuia mchanganyiko zinadhihirisha
kwamba tuko pamoja kwa jina la Bwana.
Kumbe tungetaka kuchaguana
tungepunguza: utayari
wetu wa kutumwa kokote, ukweli wa kwamba umoja unamtegemea Roho Mtakatifu, na
hivyo hata ushuhuda wa udugu.
1.32.
JUMUIA NA NDUGU BINAFSI
Jumuia ndiyo mahali tunapovuka kila siku toka
"mimi" hadi "sisi", tukiishi na kutenda kidugu kwa utajiri
wa vipawa mbalimbali.
Kwa ajili hiyo:
- tushukuru pamoja kwa zawadi ya wito na utume
uleule tuliyojaliwa ambayo inazidi tofauti yoyote iliyopo kati yetu;
- tuishangae hekima ya Mungu aliyotufanya tuwe
zawadi kila mmoja kwa wenzake;
- tumsifu kwa kile ambacho kila ndugu
anashirikisha;
- tuvumilie mwendo wa polepole wa walio
dhaifu,
bila ya kuchelewesha ustawi wa wenye neema na bidii nyingi zaidi;
- tuchangie utume wa chama kadiri ya vipawa
tulivyojaliwa kwa faida ya wote;
- tumuone mtawa akitumwa kuwa ni mjumbe
wetu;
- tumsaidie kujiendeleza na kuchangia tathmini ya
maisha na kazi ya jumuia.
1.33.
KUJIKANA NA UKOMAVU
Tulenge uwiano mzuri kati ya kumjali mtu na kujali
ustawi wa pamoja, mahitaji ya binafsi na yale ya jumuja, karama ya mtu na mpango
wa kitume wa chama.
Tusivumilie maelekeo tofauti mno ambayo yanavuruga
chama na kuhatarisha umoja: wingi wa karama za wanachama usisababishe ushindani,
bali ushirikishano kati ya ndugu na ndugu, tena kati ya ndugu na jamaa nzima.
Katika kupima ukweli wa karama ya mlelewa
tuzingatie hasa anavyokubali masharti ya maisha ya kidugu, kwa kujikana na kutii.
Tunamshiriki Yesu hasa tunapojifunza kutii kwa
mateso.
Hiyo ni sehemu ya lazima ya udugu na utekelezaji wa
upendo katika kuwatumikia wenzetu kwa kuwatolea yale yote tuliyonayo hata nafsi
yetu yenyewe.
Tuelewe mapema kwamba kuweka pembeni vipawa na
maelekeo ya binafsi kwa manufaa ya jumuia ni dalili ya ukomavu wa kiutu na wa
Kiroho.
1.34.
FURAHA
Jumuia yenye furaha ni neema toka juu kwa ndugu
wanaoiomba na kupokeana.
Kama vile amani na
umoja, kufurahia maisha hata
yakiwa magumu ni ishara ya ufalme wa Mungu, kwa kuwa ni tunda la kujifia na
kupokea paji la Roho Mtakatifu.
Furaha hiyo ya Pasaka ni ushuhuda mzuri wa kuwa
utawa ni wa Kiinjili kweli, ni hatima ya safari ngumu inayozeweshwa na sala, ni
tegemezo la kudumu kwa wanajumuia na kivutio kikubwa kwa miito mipya.
Kumbe jumuia isiyo na furaha inaelekea
kuzimika,
kwa kuwa wanajumuia watashawishika mapema wakaitafute kwingine.
Kwa hiyo, tujihadhari na ari chungu na tabia ya
kujiulizauliza mfululizo kuhusu wito wetu na hali ya kesho.
Kumbe kumtegemea Roho
Mtakatifu, kujipatia nafasi
za kutulia binafsi na kijumuia, kufurahi na wenzetu, kuangalia shida zao,
kukabili kesho kwa tarajio la kukutana na Bwana daima na kwa vyovyote: hayo yote
yanalisha amani na furaha kwa ndani na kutia nguvu katika utume.
1.35.
KUITIKIA WITO KWA UMOJA
Sisi tunastawi kwa kuitikia wito wa Mungu Baba
ambaye anatuvuta kwa karama maalumu ya Roho Mtakatifu tulingane na Yesu kwa
kutekeleza Injili yake namna fulani pamoja na wenzetu.
Tuone wito wetu kama namna bora ya
kuishi, kama
neema inayoyatia maisha yote ukweli, wema na uzuri, ili tujisikie na hakika
kuhusu sura yetu, tusihitaji kutegemezwategemezwa na watu, wala kujitafutia
faraja mbalimbali.
Hivyo tutaimarisha umoja wetu kwa kuwaona
tunaoitikia nao wito mmoja kuwa ndio wa kwanza kustahili udugu na urafiki wetu.
Kupenda wito ni kupenda Kanisa na chama kama
familia yetu halisi.
1.36.
UDOGO
Mzee wetu Fransisko hakujifanya mtawala wa
ulimwengu, bali ndugu mdogo wa viumbe vyote akiimba sifa za Mungu kwa niaba yao
na kwa ajili yao; pia alivitumia ili kuishi, lakini bila ya kuzidhisha wala
kujilimbikizia.
Udogo huo ndio sifa kuu ya pili ya karama
yetu,
ambayo inatutia na kutudai msimamo wa kujishusha daima mbele ya Mungu na ya watu,
tukimfuata Yesu katika ufukara na unyenyekevu na kushiriki hali ya watu wa
mwisho, tukiishi duniani kama wakimbizi na wapitanjia tu na kwenda ulimwenguni
kwa upole, amani, utaratibu, upendevu, unyofu na utiifu.
Neno kuu la utekelezaji wake ni kujikania mali na
sifa, hata zile za Kiroho.
Mtakatifu Fransisko aliongoka kwa kutumikia wakoma
akataka wanaoingia utawa wake waanze na kazi hiyo: basi, kila ndugu azoeshwe
kufanya kazi kati ya watu na kwa ajili yao, kupendelea zile zinazopatana zaidi
na udugu na udogo wetu, na hasa kufungamana na maskini na wenye dhiki.
Udogo unadai tena tujifunze kujitolea katika huduma
za nyumbani, kama vile upishi na matunzo ya mazingira.
Hatuwezi kusisitiza vya kutosha umuhimu wa mchango
wa ndugu wanaotoa huduma hizo, wakitunza hali ya kimya na makini, usahili na
furaha, na hivyo kufanya jumuia zetu ziwe na sura ya Kifransisko kweli.
Kwa misimamo hiyo na kwa vitendo
hivyo, ndivyo
udugu wetu katika udogo unavyojengwa siku hadi siku.
Hata uwajibikaji katika sala na mafunzo ni sehemu
mojawapo ya kazi, kwa kuwa ni sharti la kuhudumia vizuri chama, Kanisa na jamii.
1.37.
KAZI
Kadiri ya sheria asili ya binadamu tunatakiwa
kufanya kazi ya mikono au nyingine yoyote kiasi cha kustahili chakula.
Walelewa wazoee kufanya kazi kweli ili kutekeleza
udugu, kuimarisha umoja, kushirikisha vipawa vyao, kustawisha uwajibikaji,
kukomaa kiutu na kuaminika kiwito.
Kufuatana na mfano wa Yesu na maonyo ya mzee wetu
Fransisko, wazoee kufanya kazi kwa roho ya sala, kwa kuziona ni nafasi muhimu za
kukutana na Mungu katika kuchangia uumbaji na ukombozi.
Si njia za kujipatia riziki tu, bali utekelezaji wa
maisha ya Kiroho na ya kitume, kwa namna ya pekee kwetu tuliowekwa wakfu pamoja
na maisha yetu yote.
Kumbe utamaduni wa teknolojia unapima vyote na wote
kwa kuzingatia wanavyoleta faida: wanaoufuata wanaweza wakaona inafaa tutumie
tofauti maisha yetu kwa kulenga zaidi maendeleo ya kijamii.
Lakini upendo unatuhakikishia kwamba kuungana na
Yesu kwa kushiriki maisha na utume wake, ndiyo shukrani furahivu ambayo
tunaitikia mwaliko wake, ndiyo njia ya kuzaa matunda, hivyo ndiyo faida pekee.
1.38.
USHIRIKIANO WA MIITO MBALIMBALI
Mtaguso umeangaza jinsi miito mbalimbali ndani ya
Kanisa inavyokamilishana na kumshuhudia kwa pamoja Bwana mfufuka katika kila
hali na mahali.
Ushirikiano kati ya waamini ni kielelezo cha
ushirika wa Kanisa na unastawisha nguvu za kitume.
Hasa tunu maalumu za walei
(kuhisi sana maisha ya ulimwengu, utamaduni, elimu, siasa, uchumi n.k.) na zile za watawa
(juhudi za
pekee katika kumfuata Kristo, kuelekea sala na uzima wa milele n.k.) zikikutana
bila ya kuchanganyikana zinaweza zikaleta faida kwa wote.
Mabadilishano hayo yanatakiwa kuwa ya dhati zaidi
kwetu, ambako walei na makleri wanajimbo wanaitwa kushiriki kwa namna yao karama
na umisionari wa chama, kufuata safari ya malezi ya Kifransisko, na kuhusiana
kwa msingi wa usawa.
Ili walei waweze kushiriki utajiri wa utawa na
kuchangia sala na utume wake, kama wanachama wa ulimwenguni au wakiishi kwa muda
jumuiani, wanahitaji malezi maalumu na kutimiza masharti fulani.
Vilevile wanajumuia wanaweza wakatumwa na mtumishi
kushiriki kazi kadhaa za wasekulari, hasa huduma kwa maskini wa kila aina, mradi
wadumishe yaliyo maalumu ya maisha ya kitawa.
Tuwe wazi pia kwa ndugu wa matawi mengine ya
familia ya Kifransisko, tukisali pamoja na kushirikiana katika utume ili kutiana
moyo na kutajirishana.
Wanachama na viongozi wao wawe macho kuhusu ndugu
kujiunga na mifumo mingine ya Kiroho na ya kitume asije akasogea mbali na karama
na masharti ya chama chetu.
1.39.
VISHAWISHI
Tutambue na kushinda vishawishi vinavyoweza
vikaonekana vyema, kumbe sivyo; kwa mfano:
- malezi yetu ya Kiroho ya ndani zaidi yanaweza
yakatufanya tujisikie bora kuliko waamini wenzetu;
- haja ya ujuzi kwa ajili ya ufanisi wa kazi
inaweza ikageuka imani potovu ya kuwa huo unatutegemea sisi binadamu kuliko
Mungu;
- haja halisi ya kujua jamii ya leo na changamoto
zake inaweza ikapunguza ari ya Kiroho na ya kitume au kukatisha tamaa;
- hamu ya kuwakaribia watu wa leo inaweza
ikatufanya tuige mitindo ya ulimwengu;
- kushiriki matarajio ya taifa na kuzingatia
utamaduni wetu kunaweza kukatufanya tushikilie utaifa au desturi zinazohitaji
kutakaswa na Injili.
2. KUENEZA INJILI
2.1.
USHIRIKA WA KIMISIONARI
Kanisa limejaa
Utatu, hivyo nalo ni ushirika;
ushirika huo unadumishwa na mitume na waandamizi wao chini ya mamlaka ya Petro,
iliyo msingi wa kudumu wa umoja wa waamini wote.
Hilo taifa lenye asili katika ushirika wa Utatu
limetia mizizi katika historia ya binadamu hivi kwamba haliwezi kuanzishwa tena
na mtu yeyote.
Ni taifa ambalo linachota Neno la Mungu katika
Maandiko, mapokeo na ualimu wake kwa pamoja na linalenga umoja kamili wa
madhehebu yote.
Ni taifa ambalo linajitambua kuwa ni fumbo lenyewe
la Mungu linaloshirikishwa kwa watu wa jana, leo na daima; hivyo haliwezi
kueleweka kibinadamu (k.mf. kijamii au kisiasa) kwa sababu uhai wake halisi
unafikiwa na imani tu.
Hatimaye ni taifa la kimisionari lisiloridhika
kubaki kundi dogo, bali linatamani kuihubiri Injili kwa viumbe vyote hata
ulimwengu mzima uungane katika kukiri kwamba jina la Yesu tu unaleta wokovu.
2.2.
UMISIONARI WETU
Tukiishi Injili kwa unyofu na
furaha, Roho
anatusukuma tushiriki kazi ya Kanisa, nalo linatutuma ulimwenguni tumwakilishe
Bwana katika kuokoa watu na kueneza amani yake kwa njia ya ushuhuda wa maisha,
utekelezaji wa upendo na tangazo wazi la Neno.
Hauwezekaniki utawa usio na karama na lengo
maalumu,
wala utawa wa kimisionari usiolenga utakatifu kwa njia ya utume wake.
Umisionari unahusu maumbile ya utawa wetu kiasi
kwamba maisha yote ya kitawa yanatakiwa kujaa roho ya kimisionari, kama vile
utendaji wetu wote unavyopaswa kuhuishwa na roho ya kitawa.
Tunawekwa wakfu upya kwa Mungu kwa ajili ya
umisionari wa Kanisa: katika tendo hilo vinaingia kazi ya Mungu, itikio la ndugu
na upokeaji na utoleaji wa Kanisa.
Hivyo maisha yetu ya
Kiinjili, kadiri
yalivyochochewa na Roho Mtakatifu na yalivyokubaliwa na Kanisa, yanalenga utume
pia: lakini tukumbuke daima kuwa huo unadai tumshuhudie Yesu kama watu ambao
tunafyonza uzima wake, sio tu tutoe huduma kadhaa.
Kila ndugu ajisikie zaidi na zaidi mwenezainjili
kwa kuungana na Yesu na kupata ari yake: hapo wito wa kitume, baada ya kuanza
kutekelezwa, utazidi kukomaa.
Pia aungane na Kanisa
lote: katika ujuzi wake hai
wa Injili na katika hamu yake kama bibiarusi ya kutunza safi imani kwa
Bwanaarusi, pia katika hamu yake kama mama na mwalimu ya kueneza imani hiyo
kulingana na utamaduni, umri na hali yoyote ya watu.
Alingane hasa na Kanisa maalumu
anamoishi, akielewa
na kushiriki juhudi za jimbo na za parokia.
2.3.
IMANI
Habari Njema inawaalika wanaume na wanawake wote
kuongoka na kusadiki: wito huo wa Yesu unazidi kusikika kwa njia ya Kanisa,
jumuia ya wafuasi wake inayopokeza imani sahihi.
Imani hiyo:
- ni kukutana mwenyewe na
Yesu, kumuongokea na
kugeuka kuwa mwanafunzi wake, kama ilivyotokea kwa mitume;
- inadai mapinduzi kamili kuanzia
moyo, kwa
kuwajibika moja kwa moja kuwaza kama yeye, kupima mambo kama yeye na kuishi kama
yeye;
- ni kama kuzaliwa
upya: halafu mtoto mchanga
anatarajiwa kukua polepole awe mtu mzima aliyekomaa hadi utimilifu wa Kristo;
- ni zawadi inayotarajiwa kustawi kwa wongofu wa
kudumu katika Kanisa.
2.4.
HATUA ZA IMANI NA WONGOFU
Katika maendeleo hayo ya imani na wongofu kuna
hatua muhimu kadhaa:
- kuvutiwa na
Injili, ingawa mtu hajaamua kuipokea;
- kuitafiti: mvuto wa kwanza unahitaji muda uwe
uamuzi imara;
- kuongoka kwa kuambatana na
Yesu: juu ya msingi
huo yanajengwa maisha yote ya Kikristo;
- kupokea
katekesi: aliyeamua kumfuata Yesu
anatamani kumjua ili alingane naye, kuelewa fumbo lake, ufalme alioutangaza,
masharti na mashauri yake, na njia yote aliyotuelekeza: ujuzi huo wa imani
unahimiza safari ya Kiroho;
- kubadili mitazamo na mienendo kwa changamoto na
sadaka lakini pia kwa furaha nyingi;
- kuungama imani hadharani kwa namna hai inayozaa
matunda;
- kuelekea ukamilifu ili kutimiza hamu ya Kristo ya
kutuona tumefanana na Baba wa mbinguni: mwamini, akizidi kusukumwa na Roho
Mtakatifu na kusaidiwa na malezi ya imani, akilishwa na sakramenti, sala na
utekelezaji wa upendo, anajitahidi kuitikia wito wa utakatifu wa wabatizwa wote.
2.5.
KUHAKIKISHA MSINGI KWANZA
Katika utekelezaji wa utume si rahisi kutofautisha
hatua za kwenda na kukaribisha, kutangaza na kulea, kuita na kuingiza.
Pengine anayejitokeza kutaka katekesi na
sakramenti,
au hata kuingia utawani, anahitaji bado kupashwa habari njema na kuongoka kweli.
Kumbe, bila ya msimamo katika imani, katekesi
haiwezi kutimiza kazi yake ya kulea, wala sakramenti haziwezi kuzaa matunda
maishani.
Halafu uchungaji wowote pasipo katekesi ya awali
unakosa msingi na kubaki wa wasiwasi: tatizo lolote linaweza likaangusha jengo
lote.
Malezi hayo ya
msingi, ambayo kiini chake ni zile
hakika kuu za ungamo la imani na zile tunu kuu za Injili, yanalisha mizizi ya
maisha ya Kiroho pamoja na kuingiza katika jumuia ya Kikanisa ambayo inakiri,
inaadhimisha na kushuhudia imani kimatendo, na ambamo mwamini anaweza kupokea
lishe ngumu zaidi inayotolewa kila siku.
2.6.
KATEKESI
Imani iliyosababishwa na neema na kushughulikiwa na
Kanisa inatakiwa kukomaa.
Ustawi wa dhati wa Kanisa na wa kila mmoja ndani
yake unategemea sana malezi kamili na ya mpango ya imani.
Katekesi bora inayohudumia ustawi huo ni kumuingiza
mtu kwa utaratibu katika ufunuo wote wa Mungu, ambao unatunzwa katika kumbukumbu
ya Kanisa na katika Maandiko na kukabidhiwa kwa namna hai toka kizazi hadi
kizazi ili kuhimiza ungamo la imani wazi na lenye matunda maishani.
Kwa kuwa katekesi inahusiana sana na liturujia na
maisha, tunapoitoa tuzingatie sawasawa mafundisho, adhimisho lake na utekelezaji
wake.
Mtu mzima ajisikie anatajirishwa na Neno la
Mungu,
ageuke mpaka ndani na kuwajibika kadiri ya ubatizo asimkaribie tu Yesu, bali
aishi moja kwa moja katika ushirika naye kama tawi ndani ya mzabibu.
Atambue kwamba upendo wa Mungu unataka kuenea
katika nafsi yake yote, asiwe tena mali yake binafsi, bali Kristo aishi ndani
mwake.
Kwa hiyo anatakiwa kutoa itikio la upendo la
kujitoa moja kwa moja, kwa kujikana na kukubali misalaba ya kila aina ili
aungane na Kristo kwa dhati na kutimiliza yaliyopungua katika mateso yake kwa
ajili ya Kanisa; hatimaye akubali kupoteza maisha yake na hata uhai wake ili
kumpata yeye milele.
2.7.
MIKAZO YETU
Kwamba katekesi ni sehemu ya msingi ya malezi
yoyote ya Kikristo si kizuio kwa malengo ya chama na kwa utekelezaji wa karama
yetu, kwa kuwa tunaweza kuiwekea katekesi mikazo maalumu, mradi tusipotoshe
maumbile yake.
Kulea roho ya Kifransisko ni mwendelezo halali wa
malezi ya msingi yanayotarajiwa kutolewa kwa Wakristo wote.
Basi, mafundisho yetu yamfanye Yesu kuwa kiini
chake, ambacho kinaunda na kuangaza mengine yote, kama alivyo kiini cha mpango
wote wa Baba katika kuumba, kukomboa na kutakasa ulimwengu kwa upendo mkuu.
Tumtambulishe katika maisha yake halisi hadi
Pasaka,
kwa kuwa ndiye ukweli, yaani utimilifu wa ufunuo wa Mungu.
Kwa ajili hiyo tuzitegemee daima
Injili, zilizo
moyo wa Maandiko yote, kwa sababu ndizo shuhuda kuu juu ya maisha na mafundisho
ya Neno aliyefanyika mwili.
Tuingize katika kusoma Maandiko kulingana na Roho
anayehuisha Kanisa ambalo daima linalitazama Neno hilo hai kwa imani,
linalisikiliza kwa ibada, linalitunza kwa uangalifu na kulifafanua kwa uaminifu.
Tusichoke kuteka katika Mapokeo na Maandiko
Matakatifu ambayo kwa pamoja ndiyo amana takatifu iliyokabidhiwa kwa familia ya
Mungu ili ichote humo mfululizo mapya na ya kale.
2.8.
YESU, NENO
Walioanza kumfuata Yesu wanahitaji mfululizo
kulishwa Neno la Mungu ili wakue katika maisha yao ya Kikristo.
Neno ndiye Yesu
ambaye, bila ya kuacha kuwa Neno wa
milele wa Baba, anajitokeza katika sura nyenyekevu ya maneno ya kibinadamu.
Huduma ya Neno inapokeza ufunuo wa Mungu kwa
kutumia maneno ya binadamu; lakini inahusu daima matendo, yaani yale ambayo
Mungu aliyatenda zamani na bado anayatenda hasa katika liturujia na katika
maisha ya watakatifu.
Tujulishe kwa mpango ujumbe wa Kikristo kwa
kuzingatia yote kupitia nyakati tatu za historia ya wokovu (Agano la Kale,
maisha ya Yesu na historia ya Kanisa) na sehemu kuu nne za ujumbe wenyewe (Kanuni
ya Imani, liturujia, maadili na sala), ambazo zote zinatokana na chemchemi moja,
yaani fumbo la Kristo.
Kwa njia ya huduma hiyo Roho Mtakatifu anaendeleza
majadiliano ya wokovu kati ya Mungu na binadamu: yeye tu anafanya Injili iwe hai
ndani ya Kanisa na kwa kulipitia hilo isikike kweli ulimwenguni.
2.9.
BIBLIA NA KATEKISIMU YA KANISA KATOLIKI
Maandiko yanatakiwa kushika nafasi ya kwanza katika
huduma ya Neno: mafundisho yetu yahusiane nayo daima na kupenywa kabisa na
mawazo, maelekeo na misimamo ya Biblia, hasa Injili.
Matunda ya huduma hiyo yanategemea kuyasoma
Maandiko kwa akili na moyo wa Kanisa, yaani kwa mwanga wa Mapokeo, ambapo
Katekisimu ya Kanisa Katoliki inashika nafasi muhimu.
Ingawa kitendeakazi hicho peke yake
hakitoshi, wala
hakipo juu ya Neno la Mungu, kinalihudumia ili lipokezwe kwa ukweli na usafi.
Basi, Maandiko Matakatifu na Katekisimu ya Kanisa
Katoliki vinatakiwa kuongoza malezi yote ya imani ya nyakati zetu, vikichangia
katekesi ya Biblia na mafundisho mengine vilevile, kila kimoja kwa namna yake na
kwa mamlaka yake maalumu: Maandiko yakiwa ni Neno la Mungu lililoandikwa kwa
uvuvio wa Roho Mtakatifu, na Katekisimu hiyo ikiwa ni tokeo muhimu la kisasa la
Mapokeo hai ya Kanisa na kanuni ya hakika kwa ufundishaji wa imani kwa watu wa
leo.
Maandiko yawe mada kuu na roho yenyewe ya malezi
yote, na Katekisimu ya Kanisa Katoliki rejeo kuu la mafundisho.
Tuviamini vyote viwili ili kupokea na kupokeza Neno
kwa namna hai na yenye maana.
2.10.
KATEKISIMU YA MAJIMBO NA UTAMADUNISHO
Katekisimu ya Kanisa Katoliki imetolewa kwa waamini
wote na kwa wanaopenda kujua imani na maadili yake.
Halafu imekusudiwa kuhamasisha na kusaidia utungaji
wa katekisimu mpya za majimbo ambazo zizingatie zaidi lugha na hali mbalimbali
za walengwa, bila ya kuvuruga umoja wa mafundisho ya Kikatoliki.
Tutumie pia katekisimu hizo zilizothibitishwa na
askofu wa jimbo au na baraza la maaskofu kusudi Injili imuelee kila mmoja hata
aione kweli ni habari njema kwake na nguvu yake ifanye kazi mpaka moyoni mwa
utamaduni wowote.
Tukumbuke kuwa utamadunisho hautoki
juu, bali
unachipuka na kukua kutoka shina, yaani unaanzia kwa watu na ni kazi ya Kanisa
mahalia; kwa hiyo tujali mapokeo yake na kutamadunisha kwa busara na hekima,
tukielimisha kwanza na kutekeleza hatua kwa hatua.
Lengo liwe kuleta mwamko wa kiroho kama ule
aliouleta mzee wetu Fransisko.
2.11.
TANGAZO NA MANG'AMUZI
Kushirikisha imani ni tukio la neema linalofanyika
Neno la Mungu likikutana na mang'amuzi ya mtu na kumuonyesha maana ya matukio (ya
Biblia, ya liturujia, ya maisha ya Kanisa na ya maisha ya kawaida) kadiri ya
ufunuo.
Tunaweza kuanza na tangazo la habari njema halafu
kuona namna ya kulipokea maishani, au kuanza na maisha yalivyo, yaani hali na
maswala ya watu, halafu kuyaangaza kwa Neno.
Njia zote mbili zinafaa zikitumika vizuri kwa
kujali imani na akili, yaani fumbo la neema na mang'amuzi ya binadamu.
Mang'amuzi hayo yatathminiwe mfululizo kwa
makini,
kwa kuwa:
- yanasababisha ndani ya mtu
mivuto, maswali, matumaini, mafadhaiko, mawazo na maamuzi ambayo yote yanaungana katika hamu ya
kubadili maisha;
- yanasaidia kuelewa ujumbe wa
Kristo, tunavyoona
alipoyatumia ili kudokeza mambo ya juu, na alipoelekeza msimamo wa kufaa mbele
ya hayo;
- yakitumiwa na imani, ni mahali ambapo Mungu
anamfikia binadamu na kumuokoa.
Malezi yamsaidie ndugu kuchambua
mang'amuzi yake ya
msingi na kuyapima kwa Injili ili aishi upya.
Kwa ajili hiyo, kabla hajaweka ahadi asipelekwe
mbali mno na mazingira ya utamaduni wake, ili ajitahidi na kusaidiwa kuuelewa
zaidi (pamoja na namna za kufikiri, kusema, kutenda na kukabili maisha, hekima,
desturi, ishara, lugha, fasihi, sanaa n.k.).
Akipambanua kwa mwanga wa Injili tunu alizozirithi
ataweza kutathmini utamaduni wowote wa watu atakaotakiwa kuwasiliana nao baadaye.
Walezi wa utakaji na zoezi wasipotokea katika
mazingira hayohayo, waelewe utamaduni wa mlelewa na kuwapenda watu wake.
2.12.
IMANI NA MAISHA
Uhusiano wa Injili na
mang'amuzi ya msikilizaji si
swala la mbinu tu, bali unatokana na kiini cha imani: Neno alipojifanya mtu
alitwaa ubinadamu wetu wote isipokuwa dhambi.
Akiwa mfano kamili wa Mungu
asiyeonekana, ni pia
mtu kamili kuliko wote, ndiye kielelezo cha utu, hivi kwamba mwenyewe tu
anatuangazia fumbo la ubinadamu wetu tuweze kujielewa kweli pamoja na wito wetu
wa ajabu.
Malezi yetu yanapokea kwake sheria ya uaminifu kwa
Mungu na kwa binadamu kwa pamoja.
Kwa vile imani haitenganiki na
maisha, bali
inayaangazia yote, tulee kwa kulinganisha vizuri ya kibinadamu na ya Kimungu,
tukisisitiza ukweli na uhuru kadiri ya Injili, uundaji wa dhamiri, ukomavu kwa
ajili ya upendo, utambuzi wa wito na uwajibikaji.
Yesu aliishi kibinadamu kwa ukamilifu
wote,
akifanya kazi kwa mikono ya kibinadamu, akiwaza kwa akili ya kibinadamu,
akitenda kwa utashi wa kibinadamu na kupenda kwa moyo wa kibinadamu; hivyo
anatuwezesha tuishi hayo yote ndani yake, naye ayaishi ndani mwetu.
Kwa njia ya umoja huo imani inamfundisha mwanafunzi
afikiri, atende na kupenda kama Mwalimu wake, na akimshiriki hivyo ang'amue uhai
mpya unaomwezesha kuishi upya.
Kwa sababu hiyo tumkazie Yesu na kuangaza kwa
Injili mang'amuzi ya walelewa binafsi na ya jamii ili tuchochee hamu ya
kujirekebisha kimaisha.
2.13.
KUZINGATIA WASIKILIZAJI
Kulingana na nafasi tunayopokeza Neno la
Mungu,
tulitoe kwa namna maalumu, kwa kuzingatia tofauti za wasikilizaji upande wa
utamaduni, umri, ukomavu wa Kiroho, hali katika jamii na Kanisa, maswala,
matazamio na mahitaji ya ndani, lakini bila ya kusahau umoja wao wa msingi na
ukweli wao kama binadamu kadiri ulivyofunuliwa na Mungu.
Tusiridhike kuitumia Injili kwa kupamba tu
utamaduni, yaani kama nyongeza isiyo ya lazima, bali tuipendekeze kwa namna hai
na ya dhati hata ipenye mizizi yenyewe ya utamaduni.
Kwa ajili hiyo:
- tutambue katika utamaduni wa watu tunu halisi
ambazo zinalingana na Injili au walau ziko tayari kuipokea;
- tutakase yaliyoathiriwa na
uovu, ujinga na
udhaifu wa binadamu;
- tuchochee watu kukomaa kwa ndani na kumuongokea
Mungu kabisa;
- tuhakikishe imani isipokewe kinadharia tu, bali
iguse mioyo na kubadili mienendo hata isababishe maisha motomoto ambayo
yanahuishwa na upendo na kuzaa matunda ya utakatifu.
2.14.
DINI SHULENI
Vipindi vya dini vinavyotolewa shuleni vieleweke
kuwa vinatofautiana na kukamilishana na katekesi.
Kilicho maalumu cha vipindi hivyo ni kuchimba elimu
ya dini kuhusiana na masomo mengine ili kuchangia ujuzi mzima wa mtu kuhusu
asili ya ulimwengu, maana ya historia, msingi wa maadili, nafasi ya dini katika
elimu na utamaduni, lengo la binadamu na uhusiano wake na viumbe vingine.
Somo la dini shuleni linaingiza Injili kama chachu
katika juhudi za mpango kwa ajili ya elimu, ili itegemeze, ichochee, istawishe
na kukamilisha fani zote na kupenya mawazo yote ya wanafunzi.
Kwa msingi huo linatakiwa kulingana na masomo
mengine kwa hadhi, madai na usahihi, na kujadiliana nayo ili kumjenga mtu pande
zote kwa umoja wa ndani.
2.15.
KUKARIRI
Katekesi inashirikisha kumbukumbu ya
Kanisa, hivyo
toka mwanzo kutumia kumbukumbu ya mtu ni sehemu ya lazima ya malezi ya imani,
kwa kuwa imani na ibada hazichipuki katika jangwa la malezi yasiyotumia
kumbukumbu.
Ili kukwepa hatari ya kukariri kimashine tu, kazi
ya kushika kwa moyo inatakiwa kuhusiana na njia nyingine za kujifunza, kama vile
maitikio ya kujianzia, majadiliano, kimya, tafakuri na maandishi.
Maneno muhimu zaidi ya
Biblia, dogma, liturujia na
sala ya Kikristo na ya Kifransisko yakaririwe pamoja na kueleweka kwa ndani na
kushikwa kwa dhati: kwa hiyo yatolewe kama muhtasari baada ya ufafanuzi ili
kudumisha umoja wa Kanisa katika mafundisho na lugha yake.
2.16.
MWANGA WA HABARI NJEMA
Tuwatangazie wasikilizaji Habari Njema kwa namna
inayowafanya waone jinsi inavyotimiliza maumbile na matazamio yao na
inavyoshibisha kiu ya moyo wao.
Katekesi ya Biblia iwasaidie kuelewa maisha ya leo
kwa mwanga wa mang'amuzi ya taifa la Israeli, ya Yesu Kristo na ya Kanisa.
Katekesi ya Kanuni ya Imani iwaonyeshe jinsi
mafundisho makuu ya ufunuo (uumbaji, dhambi asili, umwilisho, Pasaka, Pentekoste
na vikomo vyetu) yanavyoangaza utu wetu.
Katekesi ya maadili ikiwaelekeza upendo kamili
iwaonyeshe pia msingi wake katika maadili ya kibinadamu.
Katekesi ya liturujia iwakumbushe mang'amuzi
yanayodokezwa na ishara na ibada zenye asili katika utamaduni wa Kiyahudi na wa
wazee wetu katika Ukristo.
2.17.
TULEE KUJADILIANA
Mbele ya wingi wa dini na madhehebu tutoe malezi ya
Kiinjili kwa namna inayofaa wahusika wajisikie furaha ya kuwa watoto wa Mungu na
wa Kanisa, wawe na msimamo katika imani na waweze kujadiliana na yeyote kuhusu
dini, wakitambua yasiyo ya kweli lakini pia wakifurahia chembe za ukweli ambazo
katika dini hizo ni kama maandalizi ya Injili.
Tulee kwa uangalifu wa pekee kujali ukweli, haki na
heshima kuhusu dini ya Kiyahudi, kwa kuwa Kanisa linahusiana sana na taifa la
Israeli, lililokuwa la kwanza kusikiliza Neno la Mungu: pande hizo mbili
zinafungamana zisiweze kujifanya hazifahamiani.
Tuimarishe misingi ya imani na kuchochea wongofu wa
kudumu; tuchimbe ukweli na tunu za Kikristo dhidi ya vipingamizi mbalimbali vya
kinadharia na vya kimaisha; tutambulishe kiini cha Injili na utekelezaji wake wa
kila siku; hatimaye tuhamasishe umisionari kwa ushuhuda wa maisha, kwa
ushirikiano na majadiliano, na kwa tangazo wazi la jina la Yesu.
2.18.
EKUMENI
Kila jumuia ya Kikristo inasukumwa na Roho
Mtakatifu kujenga umoja; basi, malezi yoyote ya imani, hasa utawani, yanatakiwa
kuwa na mtazamo wa kiekumeni:
- yalishe hamu halisi ya umoja, hasa kwa kupenda
Maandiko;
- yafafanue kweli za imani, zinazotunzwa na Kanisa
Katoliki, kwa kujali mpangilio wa umuhimu wake;
- yaonyeshe umoja uliopo tayari kati ya Wakristo
wowote, pamoja na hatua za kuchukua ili kuyamaliza mafarakano, hasa kukazania
wongofu na sala kusudi Roho abomoe kuta zote;
- hatimaye yaandae kuishi na ndugu wa madhehebu
mengine kwa kuheshimu dhamiri yao bila ya kupotewa na sura halisi ya Kikatoliki.
2.19.
IBADA ZA WATU WADOGO
Katika Kanisa Katoliki zinapatikana namna maalumu
za kuishi kidini ambazo zimejaa ari, nia safi na kiu ya Mungu kiasi ambacho watu
sahili na maskini tu wanaweza kuwa nazo.
Hizo zinaweza kuwafanya:
- wahisi sana sifa za Mungu (k.mf. maongozi yake na
uwepo wake wenye upendo);
- watimize kwa urahisi maadili kadhaa (k.mf.
uvumilivu, kutoambatana na malimwengu, utayari wa kutumikia);
- wajitoe mhanga hadi ushujaa katika kuungama
imani.
Hata hivyo imani hiyo inaweza ikahitaji kutakaswa
na kuimarishwa isije ikapatwa na udanganyifu, ukali wa msimamo,na ushirikina
wala kuchanganyikana na dini nyingine.
Kumbe ikiongozwa kwa hekima na utajiri wa katekesi
inaweza kuleta umati wa watu wadogo wakutane kikamilifu na Mungu kwa njia ya
Yesu Kristo: basi tufanye kazi hiyo hata kwa wenye wito wanaoonyesha kuwa na
mwelekeo huo.
2.20.
MALENGO NA MBINU
Moyo wetu uzidi kupanuka na kutusukuma tufanye juu
chini kwa wokovu wa watu.
Kila ndugu, pamoja na kutoa ushuhuda kwa matendo
yake yote, anapaswa kuwa mwalimu wa imani.
Tangazo wazi la jina la Yesu ndilo kipaumbele cha
kudumu cha umisionari ili watu waongoke kwa kuambatana naye na Injili yake.
Humohumo mna nafasi kwa utamadunisho na majadiliano
na dini nyingine: changamoto hizo zikabiliwe kama wito wa kushirikiana na Roho
Mtakatifu aliyetangulia kufanya kazi ndani ya watu wowote wa mazingira yoyote.
Kwa ajili hiyo turekebishe malengo na mbinu za
utume kadiri ya mabadiliko ya mazingira; tujiandae kwa makini, tufanye utambuzi
wa busara, tusipotoshe karama ya chama na tushikilie imani sahihi, uadilifu na
ushirika na Kanisa lote.
Tukabili utamaduni wa wenzetu kwa msimamo wa
kujikana na kutumikia kama Yesu, tukifuata nyayo alizoziacha Mungu katika
historia ya watu binafsi na ya mataifa yao.
Utafiti huo unaweza kutuletea faida sisi wenyewe,
kwa kuwa tunu tunazozivumbua zinatufanya tuelewe upya mapokeo ya Kikristo na ya
Kifransisko.
2.21.
MALEZI YA KITUME
Utume wowote unapungukiwa nguvu ikiwa wanaoufanya
wanakosa utakatifu, halafu vipawa, ujuzi na mang'amuzi.
Mipango, mbinu na vitendeakazi visipotumiwa na watu
wenye sifa hizo havitoshi.
Kwa hiyo baraza lihakikishe malezi ya kitume kwa
wote, katika hatua za kuingizwa na katika malezi ya kudumu.
Malezi hayo yana pande nyingi, lakini wa msingi
zaidi unamhusu ndugu mwenyewe kama mtu, mwamini na mtume kulingana na karama
alizojaliwa kama kleri, mtawa au mlei wa Kifransisko.
Utume wa kisasa unahitaji ndugu wanaoweza
kuunganisha usahihi wa imani na ubora wa matendo, maswala ya Kikanisa na ya
kijamii.
Lengo liwe kukomaza wamisionari kwa mazingira
halisi ya leo, wenye sura ya ndani ya Kikristo, ya Kikanisa na ya Kifransisko
ambao wanaweza:
- kutangaza jina la Yesu na Pasaka yake;
- kujulisha maisha yake katika mtiririko wa
historia ya wokovu:
- kufafanua fumbo lake kama Mwana wa Mungu
aliyejifanya mtu, tena mtumishi mtiifu hata kufa, naam, hata kufa msalabani;
- kushirikisha ujumbe wa Injili yake kwa urahisi,
usahihi na nguvu;
- kuelekeza watu hatua kwa hatua katika kumfuata
kwa imani;
- kusaidia kuungana naye zaidi na zaidi kwa njia ya
sakramenti.
Mtazamo huo unaomkazia macho Yesu uathiri moja kwa
moja nafsi na utume wa ndugu.
2.22.
UTUME NA WATU
Aandaliwe kurahisisha ustawi wa imani ya watu, bila
ya kusahau kuwa imani si tunda la kazi yake, kwa kuwa Mungu tu anaipanda
mioyoni.
Ajue vema: ujumbe anaokusudiwa kuueneza, wale
anaotumwa kwao pamoja na mazingira yao, na namna ya kupasha ujumbe kwa unyofu
katika mafungamano na majadiliano, kwa utulivu wa mitazamo kuhusu maisha, kwa
uwezo wa kufariji na kutumainisha, na kwa nia safi ya kuongoza kwa niaba ya
Yesu.
Amvutie yeye mioyo ya watu kwa kuzingatia heshima
na uelewano; kwa kuwakaribia wenye shida; kwa kuwahurumia wakosefu na dhaifu;
kwa kuamini uwezekano wa neema kuongoa watu; kwa kujitoa sadaka kwa ajili yao.
Utume unatarajiwa kustawisha upendo alionao kwa
watu anaowashughulikia; upendo huo sio tu ule wa mwalimu kwa mwanafunzi wake,
bali wa mzazi kwa mtoto wake: Bwana anataka kila mhubiri wa Injili na mjenzi wa
Kanisa awe na upendo wa namna hiyo.
Vilevile imani aliyonayo inakusudiwa kukuzwa na
utume wake: tunafundisha imani kwa kujifunza kwanza wenyewe, na
tunapoishirikisha inaongezeka ndani mwetu.
2.23.
UTUME WAKATI WA KUINGIZWA UTAWANI
Kulingana na elekeo letu maalumu tulee hatua kwa
hatua, kuanzia utakaji, kuwahudumia na kuwahubiria maskini.
Ni juu ya mlezi kuhakikisha kwamba kila ndugu,
kadiri ya mahitaji na ya uwezo wake, apate mang'amuzi mbalimbali na ya kutosha
kuhusu utume wetu, aufanye pamoja na wengine chini ya ndugu aliyekomaa zaidi na
kwa namna ambayo idumishe jumuia, akikabili shida za mazingira bila ya kumezwa
nayo.
Kwa msaada na mwongozo wa mlezi aelewe mapema
masharti ya utume bora na kutambua jinsi karama yake inavyoweza kuchangia utume
wa chama bila ya kuuvuruga, kwa kuoanisha kila siku maisha ya kijumuia na utume,
yaani hali ya mfuasi anayeishi pamoja na Yesu na kundi lake dogo, na hali ya
mtume anayepelekwa naye ashiriki kazi yake ya ukombozi.
Pia mbinu zinazotumika katika malezi ni za msingi
kwa utume, kwa sababu ni vigumu kwa ndugu kubuni mitindo ambayo hajazoeshwa.
Halafu mwenyewe ajipatie namna yake ya kufanya
utume akilinganisha misingi ya kazi hiyo na nafsi yake.
2.24.
MALEZI NA UTAMADUNISHO
Injili na karama ya Kifransisko vitaumua utamaduni
wa watu (taifa, kabila na vikundi maalumu, k.mf. wasomi, wanafunzi, wafanyakazi,
vijana, walalahoi) vikifaulu kuwasisimua na kuyakidhi mahitaji ya utu wao.
Hivyo inatubidi tuwajue vizuri ili kutamadunisha
ujumbe wa wokovu uwaelee.
Lakini hatuwezi kuwa tangazo hai la Habari Njema
kwa watu tukirudi nyuma upande wa imani na kujilinganisha na ulimwengu badala ya
kuuangaza Kiinjili.
Basi, tuonyeshe kimaisha muungano safi wa imani na
tunu za utamaduni, na kupinga mapotovu yanayoenea pasipo kuchujwa.
Tunapaswa kuwa waangalifu na kuchambua, kwa kuwa
mema na mabaya, ambayo yanaathiri kila wakati na mahali na kujitokeza katika
miundo ya jamii, yanapiga hodi katika maisha ya wote, hata ndani ya Kanisa na ya
utawa.
2.25.
VYOMBO VYA UPASHANAJI HABARI
Tuwe makini kuhusu ujanja wa kikoloni wa wale
wanaotumia vyombo vya mawasiliano ili kupotosha watu na kuwatawala kwa
kujifaidisha.
Katika hatua za kuingizwa tueleze vyombo vya habari
vinavyoweza kutuathiri sana, tuelekeze juu ya ukweli na uadilifu wa ujumbe wake,
na kuzoesha msimamo safi katika matumizi ya kiasi tusije tukadhuriwa navyo.
Zaidi ya hayo, tusisambaratike katika kufuatafuata
mfululizo habari za kila aina, kama kwamba kujua hali halisi ya Kanisa na ya
ulimwengu kunategemea wingi wa habari.
Kinyume chake, tuwajibike kutambua yaliyo muhimu
katika mwanga wa Mungu na tuyalete mbele yake katika sala.
Vilevile tuwaongoze watu wote wasizame katika
malimwengu kwa mvuto wa vyombo hivyo, bali watambue ubatili mtupu wa mambo
yapitayo na umuhimu wa jambo lile ambalo peke yake ni la lazima.
Tufuate katiba kuhusu vyombo vya habari: sharti
hilo litatusaidia kutunza usafi wa moyo na roho ya sala, yaani kumuona Mungu
katika vyote na yote.
Mawasiliano ya mlelewa na watu wa nje (kwa barua
n.k.) yaratibiwe na mlezi, ili kuepa urafiki usiofaa au unaotawanya mawazo tu.
2.26.
MALEZI YA KIDARAJA
Kuhusu kusomea upadri au ushemasi, karama yetu ya
kidugu inadai malezi yawe sawa kwao na kwa wenzao wote hadi kuweka ahadi.
Baada ya hapo malezi ya wale wanaojiandaa kupata
daraja au huduma fulani yafuate sheria za Kanisa na za chama, bila ya kuweka
pembeni masharti ya maisha ya kitawa tuliyoahidi, wala pengine madai ya
uchipukizi.
Kozi maalumu za kusomea daraja zifuatwe kama sehemu
ya mpango mpana zaidi unaohusisha malengo ya utawa wetu.
Kipaumbele katika masomo ya kidaraja ni kuchimba na
kutafakari Maandiko Matakatifu na mafundisho halisi ya Kikatoliki hadi yawapenye
kabisa, pamoja na kujifunza kupima vizuri dhana za teolojia ambazo
hazijatathminiwa na Ualimu wa Kanisa.
Kwa ajili hiyo uzingatiwe hasa mfano na urithi wa
mtakatifu Thoma wa Akwino na wa walimu wa Kanisa wa Kifransisko.
2.27.
MALEZI YA KICHUNGAJI
Ingawa malezi hayo yote yanalenga kazi ya
kumuingiza mtu wa leo katika maisha ya Kanisa, yanahitajika malezi maalumu ya
kichungaji ambayo yalingane na karama ya chama, na kuendana na utekelezaji wa
huduma na daraja ambazo wanateolojia wanakabidhiwa moja baada ya nyingine.
Wanaolenga kuwa mapadri waandaliwe kwa kozi maalumu
kutoa sakramenti ya upatanisho na uongozi wa Kiroho.
Kwa msaada wa padri mlezi na kadiri ya mtindo wa
maisha yetu, wajitahidi hasa kulingana na Mchungaji Mwema katika kutamani wokovu
wa watu na kujitoa kabisa kwa ajili hiyo.
Wachochee upendo huo kwa kuishi Kiroho kwa dhati,
kusoma kwa bidii na kushiriki katika maisha ya Kanisa.
Mwishoni mwa masomo yote, wakati wanapotekeleza
ushemasi katika uchungaji, wasaidiwe kusanisi yale yote waliyojifunza ili waone
kwa umoja fumbo la Kristo.
Mtumishi kabla hajamuomba askofu wa jimbo ampe
ndugu daraja takatifu ya ushemasi au ya upadri, awe na thibitisho la maandishi
la mlezi kuhusu sifa zinazohitajika kisheria, pamoja na kibali cha halmashauri
yake.
2.28.
MTAWA MWENYE DARAJA
Miaka mitatu inayofuata upadirisho ndugu wapangwe
wanapoweza kujiendeleza kiteolojia na kichungaji.
Halmashauri kuu iwapangie walau vipindi kadhaa,
hasa vya kichungaji, na semina moja kwa mwaka.
Mang'amuzi yanaonyesha kuwa katika mapadri watawa
daraja takatifu inazaa zaidi kwa sababu mashauri ya Kiinjili waliyoyashika
yanadai na kusaidia muungano wa ndani na Bwana.
Katika maisha yao upadri na utawa vinaunganika kwa
dhati na kukamilishana katika kutimiza fumbo lote la Kristo.
Kanisa maalumu ndilo nafasi ambamo wito wowote
unatekelezwa Kiroho na kitume: kila mmojawetu ajitahidi kustawi katika jimbo
lolote kama mahali pake, bila ya kupoteza mwelekeo wa kimataifa wa chama chetu
na wa taifa lote la Mungu.
Zaidi tena padri au shemasi ni msaidizi wa kundi la
maaskofu kwa kushiriki utume wao chini ya mmojawao: basi ajisikie nyumbani
katika jimbo lolote.
Malezi ya ndugu wanaotarajia kupewa daraja
yazingatie watakavyopaswa kuingia katika kundi la makleri mara wa jimbo hili,
mara wa jimbo hili.
Ndugu padri au shemasi akishiriki uchungaji pamoja
na wenzake wanajimbo, anapaswa kuonekana wazi kimatendo kuwa ni mmisionari
mtawa, tena wa Kifransisko.
Kwa ajili hiyo, anayejiandaa kupewa daraja na
aliyekwishaipata vilevile azingatie masharti yafuatayo ili kulinganisha pande
zote (utawa, umisionari na daraja) za wito wake ulio mmoja tu (kuwa padri au
shemasi mmisionari wa Kifransisko):
- awe anaelewa kuwa daraja inahusu muundo na
uongozi wa Kanisa, na kuwa utawa, hata ukidai utume, unahusu uhai na utakatifu
wa Kanisa;
- kwa maisha ya Kiroho achote hasa katika chemchemi
za Kifransisko na kuchochea ndani mwake karama ya chama ambayo ni zawadi ya
Mungu kwa Kanisa;
- maisha yake yalingane na ushuhuda na mafundisho
ya mwanzilishi;
- atekeleze kanuni na katiba alizoahidi;
- aishi katika jumuia hivi kwamba ushirika wa
kidugu uwe ndio mwanzo na mwisho wa utume wake;
- awe tayari sikuzote kupelekwa na mtumishi
akahudumie jimbo lolote.
2.29.
UMOJA WA NDANI MWETU
Katika utume wowote tukumbuke tunavyopaswa kuwa
hasa viongozi wa Kiroho, jambo linalodai tustawishe paji lililo bora yaani Roho
Mtakatifu.
Kwa njia yake tunamiminiwa upendo, ambao unaongoza
na kuhuisha utekelezaji wa mashauri ya Kiinjili na utume vilevile.
Kwa kuwa yeye ni Roho wa umoja hata ndani mwetu,
hatutakiwi kugawanyika kati ya maisha ya kitawa na utendaji wake.
Kwa ajili hiyo katika nafasi yoyote tudumu katika
maisha yaliyofichika pamoja na Kristo ndani ya Mungu, tukimtafuta na kumpenda
kuliko yote yeye aliyetangulia kutupenda: ndimo unamobubujika upendo kwa jirani,
unaojitosa kwa ujenzi wa Kanisa, wokovu wa ulimwengu na ustawi wa jamii.
Basi, kumpenda na kumhudumia jirani
kusitutenganishe na Mungu, bali huduma hizo zitokane kweli na upendo wa Kikristo
ziwe ibada kwa Mungu.
Tufanye juu chini ili kuunganisha hivyo maisha ya
Kiroho na utendaji, kusudi kazi tunazomfanyia Bwana zitufikishe kwake, aliye
chemchemi na lengo la utendaji wowote.
Tujifunze mapema jinsi sala ilivyo moyo wa utume,
na jinsi utume unavyotakiwa kuchochea sala, halafu kila mmojawetu atathmini
mfululizo kama utendaji wake unatokana na muungano wake na Mungu, unaudumisha na
kuuimarisha au la.
2.30.
UTUME NA JUMUIA
Utendaji wetu utokane vilevile na maisha ya pamoja
na moyo wa kijumuia, na ueneze udugu kwa maneno na matendo.
Ushirika wetu wenyewe ni utume tayari, kwa kuwa
ndio ishara kuu ya wafuasi wa Bwana inayofanya ulimwengu usadiki.
Utawa utazaa matunda kadiri yalivyo bora maisha
yake ya kidugu; kadiri hiyohiyo watawa watadumu katika wito na hivyo watakuwa
ishara ya uaminifu wa Mungu kwetu itakayotegemeza uaminifu mgumu wa Wakristo wa
ulimwenguni kwake.
Maisha ya kijumuia yana thamani hasa mishenini kwa
kuwa yanawaonyesha wasio Wakristo upya wa dini yetu, yaani upendo: kumbe ndiko
utekelezaji wake unapopambana na matatizo mengi zaidi na unakodai juhudi za
pekee ili kuyatatua.
Utiifu kwa matakwa ya Mungu yaliyodhihirishwa na
watumishi na walinzi ndio njia ya kujipatia umoja maishani.
3. WATENDAJI
3.1.
BABA
Wokovu wetu binadamu, ulio lengo la milele la
mpango wa Mungu, ni tunda la malezi yake ya ajabu katika historia yetu yote.
Katika Maandiko anajifananisha na baba, mwalimu na
mzee mwenye hekima ambaye anampokea mtu alivyo, anamkomboa katika vifungo vya
uovu na kumvuta kwake kwa vifungo vya upendo, akimfanya akue hatua kwa hatua
kuelekea ukomavu wa mwana huru na mtiifu.
Ili kufikia lengo hilo anatumia majaribu, tuzo na
adhabu.
Akijilinganisha na nyakati na hali mbalimbali za
watu anaowalea, anawageuzia matukio ya maisha yawe mafundisho ya hekima ambayo
yakabidhiwe toka kizazi hata kizazi.
3.2.
MWANA
Wakati ulipotimia Baba alimtuma Mwanae aendeleze
malezi hayo ya Kimungu kwa kutumia mbinu zote za mawasiliano kati ya watu, kama
vile semi, mifano, kimya, ishara na matendo.
Yesu aligusa wote kwa jinsi:
- alivyotangaza ufalme wa Mungu kama habari njema
ya ukweli;
- alivyowapokea watu, hasa maskini, wadogo na
wakosefu kama wapenzi wa Baba;
- alivyowapenda wote kwa hisani na nguvu ili
kuwakomboa;
- alivyowahimiza kuishi kwa imani, tumaini na
upendo usio na mipaka.
Hivyo alifunua Mungu na binadamu walivyo, akiokoa
na kuongoza, akisema na kusukuma, akikosoa na kusamehe.
Aliwalea kwa makini hasa wanafunzi aliotaka wawe
wajumbe wake:
- alijitambulisha kwao kama mwalimu pekee, mwenye
utambuzi na ubunifu, akiwafundisha kwa maisha yake yote; na papo hapo kama
rafiki mvumilivu na mwaminifu akiwajulisha yote aliyoyasikia kwa Baba;
- aliwachochea kwa maswali ya kufaa;
- aliwafafanulia kwa ndani zaidi yale alioutangazia
umati;
- aliwaingiza katika sala yake;
- aliwapeleka kufanya mazoezi ya kitume;
- aliwapitisha kwenye majaribu;
- aliwatabiria yatakayowapata;
- hatimaye aliwaahidia Roho wa Baba ambaye
atawaongoza kwenye ukweli wote na kuwategemeza katika nafasi ngumu.
Yesu Emanueli yupo bado pamoja nasi, akija kwetu
kila siku tuongozane safarini mpaka aje kwa utukufu.
3.3.
ROHO WA BWANA
Mzee wetu Fransisko tangu aongoke, pamoja na
kuzingatia ishara yoyote ya matakwa ya Baba ili ayatimize, imara katika nia ya
kufuata upeo Injili ya Mwanae, alizidi kutambua na kushangaa kazi ya Roho
Mtakatifu ndani mwake mwenyewe na katika utawa wake, akishirikiana naye kwa
unyenyekevu na usikivu.
Akiwa mtu wa Roho, aliita "Roho wa Bwana"
uwepo huo wa Mungu katika maisha yetu, ambao unakuwa hakika na upendo katika
maisha ya imani tupu, na unatuchochea tushuhudie na kutangaza Injili.
Malezi na maisha yote ya Kifransisko yanategemea
kuwa wazi daima kwa Roho Mtakatifu, anayefanya kazi ndani ya moyo hadi matunda
yaonekane kwa nje, katika ulinganifu wa mwamini na Yesu kwa utukufu wa Baba.
3.4.
UPAMBANUZI WA ROHO
Yeye ni Roho wa ukweli ambaye anafundisha,
anakumbusha na kuongoza hadi ukweli wote; ni mpako unaowezesha kupima, kuchagua
na kuonja; ni mtetezi na mfariji ambaye anasaidia udhaifu wetu, akitutegemeza na
kutufanya wana wa Mungu; ni mtendaji asiyeonekana wa malezi na wa utakatifu
ambaye anadai tuwe macho kutambua na kufuata sauti yake kwa kuweka pembeni
mivuto ya ubinadamu na ya shetani.
Utambuzi huo ni tunda la kujizoesha mfululizo:
- kupokea matakwa ya Baba ili kuambatana naye
kabisa;
- kujichunguza ili kuanza upya kila siku kadiri ya
Injili;
- kusoma ishara za nyakati, mahitaji ya Kanisa na
tunu za watu;
- kusali, kutafakari na kujadiliana;
- kuwa na busara, unyofu na uhuru wa ndani;
- kutojiamini mno, bali kuwajali wengine, kuelewa
mitazamo yao, kusikiliza lawama zao na kujirekebisha mapema panapotakiwa.
- kutambua Roho anavyotenda na kusema kwa njia ya
watu aliowakabidhi huduma na karama nyingine, tukiwa tayari kushauriwa na
kuelekezwa hasa katika uongozi wa Kiroho, kwa kuwa si rahisi mtu kukomaa peke
yake.
3.5.
KANISA
Tangu mwanzo Kanisa, kama sakramenti ya Kristo,
limeshiriki katika malezi hayo likipata kwake neema za juu, mvuto wa kudumu na
mfano wa hakika kwa kazi hiyo yote.
Karne hadi karne limejipatia hazina kubwa ya
mang'amuzi: ushuhuda wa watakatifu, aina mbalimbali za maisha ya Kiroho, hatua
za malezi, utajiri wa mafundisho n.k.: hayo yamekuwa urithi wetu hasa kupitia
mapokeo ya Kifransisko.
Kanisa ni mama na mlezi wetu halisi, linaloendeleza
utume wa Bwana Yesu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Kwa mfano wa Bikira Maria linatunza moyoni hazina
ya imani, halafu linaitangaza na kuiadhimisha na kuitekeleza.
Hivyo linashirikisha imani linayoishi, tumaini
lililojawa nalo na upendo lililonao ili viumue maisha ya wapokeaji, nao
wavitajirishe kwa tunu za utu na utamaduni wao.
Tustawishe mapema tabia ya kuambatana daima na
Kanisa na viongozi wake.
Ndani yake, kwenye meza ya Neno la Mungu na ya
Mwili wa Kristo, tunapata mkate wa uzima ambao ulishe maisha yetu yaliyowekwa
wakfu kuanzia ubatizo; kwa sakramenti ya kitubio tunayopata mara kwa mara
tunajaliwa huruma ya Mungu na kupatanishwa na jumuia ya waamini tuliyoijeruhi
kwa dhambi: hivyo liturujia ni kilele kinacholengwa na jumuia yoyote ya
Kikristo, na chemchemi ya nguvu yake ya Kiinjili.
3.6.
KULEA KIKANISA
Kwa kuwa malezi ya Kikristo ni tendo la Kikanisa
hasa, wanaoyashughulikia wawe daima waaminifu kwa Kristo na kwa Kanisa vilevile,
wakishikilia ufunuo ulivyotufikia: tunaipokea Injili kwa Kanisa na kuielewa kwa
msaada wa mapokeo yake na wa ufafanuzi rasmi wa ualimu wake.
Hasa malezi ya kitawa yanatakiwa kufanywa katika
ushirika wa Kanisa, kwa kuwa watawa ni watoto wake kwa namna ya pekee.
Tuliojitoa kabisa kwa Mungu tunahusiana sana na
fumbo la Kanisa, maisha yake na utakatifu wake, na tunasukumwa na mashauri ya
Kiinjili tutende kwa moyo usiogawanyika kwa ustawi wa Mwili wote wa Kristo.
Ndiyo sababu katika sadaka ya Misa siku ya ahadi ya
daima tunawekwa wakfu upya kwa Mungu kwa ajili ya umisionari wa Kanisa: katika
tendo hilo vinaingia kazi ya Mungu, itikio la ndugu na upokeaji na utoleaji wa
Kanisa.
3.7.
ASKOFU
Daima kutangaza, kuadhimisha na kutekeleza Injili
kunafanyika katika Kanisa maalumu (jimbo), yaani jumuia ya wanafunzi wa Kristo
inayoishi katika mazingira fulani ikitimiza sifa zote za Kanisa lililo moja,
takatifu, katoliki na la mitume.
Mtaguso wa Pili wa Vatikano umesisitiza nafasi ya
askofu katika maisha yote ya Kanisa, kuanzia malezi ya imani anayoyatoa kwa
karama ya ukweli.
Kama mwalimu halisi wa ukweli wa Kimungu na wa
Kikatoliki, ufundishaji wa imani jimboni ni juu yake.
Vilevile kama mlezi wa ukamilifu kwa wanajimbo ana
jukumu la kuwaelekeza wote wamfuate Yesu, na kwa namna ya pekee waliojaliwa
karama ya kumfuata kwa karibu zaidi.
Hivyo anapaswa kukesha juu ya safari yetu watawa
kuelekea utakatifu ili alinde uaminifu wetu kwa wito huo maalumu.
Huduma hiyo ya askofu haitakiwi kugongana na ile ya
viongozi wa utawa, kwa kuwa yeye anapaswa kutumia mamlaka yake kwa kuheshimu ya
kwao, nao wamewekwa kuongoza katika maisha ya Kiinjili jamaa nzima au jumuia
yake mojawapo, kwa kulingana daima na maaskofu.
Chama chetu pia kina taratibu zake na mamlaka yake
kwa ustawi wa maisha ya kitawa, lakini hizo zinapaswa kutekelezwa katika
ushirika wa Kanisa, zikilindwa na kudumishwa na askofu.
Chama chetu kama shule ya ukamilifu na njia ya
utakatifu ni mali ya Kanisa; kwa hiyo ustawi wa taifa lote la Mungu unamdai
askofu awajibike sio tu kuhusu utendaji wetu, bali kimsingi zaidi kuhusu
utakatifu wetu na usahihi wa imani yetu.
Basi, askofu wa jimbo tunamoishi ajulishwe na
mtumishi safari yetu ya malezi aweze kujihusisha ipasavyo.
3.8.
JUMUIA ZA KIKRISTO
Ushirika, ambao ni tunda la Roho Mtakatifu na kiini
kinachounda Kanisa la kimataifa na kila Kanisa maalumu katika umoja,
unatekelezwa katika jumuia za namna nyingi, ambamo Wakristo wanazaliwa katika
imani, wanalelewa na kuishi: familia, parokia, mashirika, vyama, jumuia
ndogondogo, shule za Kikatoliki.
Jumuia yoyote ya Kikristo ni asili, mahali na lengo
la malezi ya imani: tangazo la Injili linaanza daima katika jumuia likimuita
kila ndugu kuongoka na kumfuata Kristo; ndiyo inayowapokea wanaotaka kumjua
zaidi na kuishi upya; ndiyo inayowasindikiza kimama ikiwashirikisha mang'amuzi
yake.
Kimsingi, malezi ya imani ni yaleyale daima, ila
aina ya jumuia yanapofanyika inayatofautisha.
Jumuia ya Kikristo inaundwa na kujitokeza hasa
katika parokia kwa kuwa ndiyo mahali penyewe pa huduma ya Neno na maadhimisho
mbalimbali na ndipo tofauti zote za kibinadamu na za karama zinapoyeyushwa na
upendo ili kuunda umoja.
Kwa hiyo:
- toka mwanzo wa malezi ya kitawa tusisitize
kujisikia wanaparokia;
- tusilee bila ya uhusiano na parokia;
- tuwe wepesi kushiriki maisha yake chini ya paroko;
- tuchangie kuifanya iwe familia inayovutia, ambapo
Wakristo wote wajitambue kama ndugu.
3.9.
CHAMA NA VIONGOZI WAKE
Ndani ya Kanisa, malezi yetu ni jukumu la chama
kizima, nacho kinayachangia hasa kadiri kinavyoishi kulingana na karama, bila ya
kupatwa na uvuguvugu katika mienendo na mitazamo ya jumla na ya wanachama
binafsi.
Ni kwamba ustawi wa mtu katika hatua zote
unategemea sana mazingira yake.
Ni hivyo hasa upande wa imani kwa kuwa tunakutana
na Yesu hai katika jumuia.
Kila mmojawetu anamuitikia akifungamana na wengine
walioitwa namna ileile kusudi tuishi kwa umoja.
Basi, maisha bora ya pamoja yatazamwe kuwa
mazingira ya lazima ya malezi yetu, hasa ya awali.
Jumuia ambayo kweli inatokana na imani, inajitahidi
kutekeleza Injili na kuwa ishara ya upendo kati ya watu, inasali na kufanya
kazi, inashirikisha na kutumikia kwa ari ya kitume: ndiyo shule ya kufaa kwa
vizazi vipya.
Wanaolelewa wanahitaji kukuta humo ari ya Kiroho na
ya kitume ambayo iwavute kumfuata Kristo kwa nguvu zao zote.
Jumuia zote za malezi zishike sana kanuni, katiba
na ratiba: ndilo jambo ambalo linalea zaidi na kustawisha wito.
3.10.
JUMUIA YA KITAWA
Jumuia inaundwa siku kwa siku chini ya Roho
Mtakatifu, ikikubali kupimwa na kuongozwa na Neno la Mungu, kutakaswa na
kitubio, kujengwa na ekaristi, kuhuishwa na maadhimisho ya mwaka wa liturujia.
Halafu umoja wake unastawi tukisaidiana kwa ukarimu
na kushirikishana mema ya Kiroho na ya kimwili.
Mafungamano kati yetu yawe na unyofu na tumaini,
yakitegemea hasa imani na upendo.
Kila ndugu ajisikie anapokewa kama zawadi ya Bwana
na anasaidiwa na hali ya kifamilia kutambua vipawa vyake na kustawi kwa kuitikia
wito kwa bidii kubwa zaidi na zaidi.
Jumuia bora inajitambulisha kwa jinsi
inavyoshughulikia malezi, ikiyaweka mbele kuliko kazi za nje, na inavyomwezesha
kila mmojawetu kukua katika uaminifu kwa karama ya chama.
Basi, tuwe tumekubaliana kweli kuhusu malengo yetu,
mipango ya malezi na mbinu zake; halafu mara kwa mara tutathmini malezi na
maisha yetu kwa jumla.
3.11.
WALELEWA
Jumuia haitoi tu kwa walelewa, bali inapokea pia
toka kwao: wanaojiunga wanailetea utajiri wao wa kibinadamu na wa kidini, hivi
kwamba jumuia inakua na kustawi.
Malezi yenyewe hayakomazi tu walelewa, bali jumuia
pia.
Kila mmoja ajitambue mlelewa na mlezi sawia na
kuwajibika kukua si kwa ajili yake mwenyewe tu, bali kwa manufaa ya jamaa yote,
akitekeleza karama yetu na kushirikiana na watumishi, walinzi na walezi.
Jumuia zetu ni jinsi tunavyoziunda: ili ziweze
kutulea, zinadai kwanza tuzipende, tuzistawishe na kuzitumikia.
Jumuia ya Yesu na mitume wake iwe lengo letu na
onyo kwetu ili tujenge jumuia kwa bidii na unyenyekevu, bila ya kukata tamaa
wala kusahau ubinadamu wetu ulivyo.
3.12.
WALEZI
Malezi ni ushirikiano wa upendo hasa kati ya
wawili: Mungu akiwa daima wa kwanza, mwamini aliyeitwa naye ana jukumu la
kumuitikia, akitegemea kuwa Mungu atakamilisha alichokusudia.
Hisi ya wajibu huo na ya uwezekano huo inamsukuma
mtu atafute kwa unyenyekevu mwanga na njia, iwe ni moja kwa moja toka kwa
Mwenyezi Mungu, au kupitia maelekezo na misaada ya kidugu ya waliokomaa zaidi
ambao Bwana anawaweka karibu naye ili wamsaidie kutambua na kufuata uongozi wa
Mungu katika safari yake ya maisha.
Wenyewe ni washiriki tu wa kazi anayoifanya Mungu
ndani ya kila mmoja, kwa sababu hakuna kiumbe kinachoweza kushika nafasi ya
uhusiano hai wa moyo wa Baba na moyo wa mwanae wa kambo.
Mungu tu anaweza kumuita, naye tu anamwezesha
kuishi Kikristo, akimuunda kwa njia ya Roho awe na msimamo uleule wa Mwanae
mpenzi.
Kuitikia kwa hiari ni kukubali yale yote
yatakayotokana na jibu la ndiyo, ambalo si la kinadharia bali la kimaisha.
Basi, kwa vile hali za maisha hazirudii kamwe, na
upendo, wito na utendaji wa Mungu ni mpya daima, mtu anaalikwa mfululizo
kumuitikia upya.
Safari yake inafanana na ile ya taifa la Israeli
toka Misri, jangwani hadi nchi ya ahadi; pia inakumbusha mabadiliko ya polepole
ya wanafunzi wa Yesu wenye mioyo mizito ya kuamini.
3.13.
USHIRIKIANO KATIKA MALEZI
Malezi ni kazi kubwa na ya msingi kwa ustawi wa
Kanisa na chama ambayo haiwezi kufanywa na mlezi binafsi, bali inadai
ushirikiano wa wote ili tuyakamilishe iwezekanavyo.
Mtumishi na mlinzi wana majukumu maalumu kama
wastawishaji wa ndugu mmojammoja na kijumuia ili wakomae pande zote (teolojia,
roho, utume, utu, elimu na ufundi) juu ya msingi wa Kristo kadiri ya karama
yetu.
Ingawa mlelewa ndiye wa kwanza kuwa na jukumu
kuhusu wito wake, hawezi kulitimiza nje ya mapokeo ya chama, ambayo mlezi ndiye
shahidi na mwelekezaji wake rasmi.
Yeye ametumwa na chama ili kwa niaba yake, kwa
uaminifu kwa karama yetu maalumu, na kwa ushirikiano na wahusika wengine,
awasaidie walelewa kushika maisha yetu kwa msimamo wa dhati utokanao na imani.
Kwa kazi hiyo nyeti sana tuandae ndugu ambao,
pamoja na kujua vizuri na kukubali imani na maadili katoliki, wawe na sifa za
kufaa kama vile:
- hekima itokanayo na usikilizaji wa dhati wa Neno
la Mungu;
- upendo kwa liturujia na ujuzi wa nafasi yake
katika malezi;
- mang'amuzi ya sala;
- uwezo wa kushirikisha karama yetu kama tunu kwa
siku hizi;
- tumaini imara kwa Mungu kuhusu kesho ya
ulimwengu, ya Kanisa na ya chama;
- utulivu wa ndani na mapendo halisi kwa wale
aliokabidhiwa;
- kipawa cha kupokea na kuelewa watu;
- nia ya kujitoa ahudumie kila mmoja, sio kikundi
tu;
- uhusiano mzuri na jumuia;
- elimu inayohitajika na hamu ya kujiendeleza.
3.14.
UMUHIMU WA KAZI YA MLEZI
Katika hatua yoyote, karama aliyojaliwa mlezi,
uimara wake katika imani na ushuhuda safi wa maisha yake, ndivyo roho ya mbinu
zozote kwa kuwa ndivyo vinavyoweza kuhakikisha matumizi ya kufaa ya maandishi na
vitendeakazi vingine.
Mlezi ni mshenga kati ya walelewa na fumbo la
Mungu, kati yao wenyewe kwa wenyewe, na kati yao na jumuia.
Maneno na maisha yake yawasaidie kutamani, kupokea
na kuchimba ujumbe wa Kristo.
Ajue sana njia ya Mungu hata aweze kuielekeza kwa
wengine, akiwaonyesha vizuio lakini hasa uzuri na thamani ya karama inayowezesha
kumfuata Yesu kwa karibu zaidi.
Ustahimilivu na tumaini yawe maadili yake maalumu,
akikumbuka kwamba ustawi wa roho ni tunda la neema ya Mungu na la hiari ya
mhusika, hivyo ategemee hasa kazi ya Roho Mtakatifu na sala, toka mwanzo hadi
mavuno yatakapopatikana.
Atambue vema lengo la kazi yake, kwa kuwa katika
malezi malengo ni muhimu; mojawapo, tena kuu, ni kuwafikisha ndugu kwenye uwiano
wa maadili yote.
Awahimize watekeleze mambo yote ya kanuni na katiba
zetu bila ya kukwazwa na ruhusa ambazo wengine wanaweza wakapewa kwa udhaifu
wao; kinyume chake wajitahidi kufidia kwa niaba yao.
3.15.
MALEZI NA MOYO WA MTU
Malezi yamguse mtu mpaka ndani, kwa kuchochea
dhamiri yake awajibike kujipatia tunu za Kiinjili na za Kifransisko pamoja na
kushika taratibu anazoelekezwa, akiamini anachofanya kwa msukumo wa Roho
Mtakatifu, badala ya kuiga tu au kulazimishwa.
Kwa ajili hiyo walezi waoanishe malezi ya kundi
zima na ya kila mmoja, kwa kujali muda uliopangwa jumla kwa kila hatua na hasa
muda anaohitaji mtu maalumu kadiri ya mwendo wake.
Kwa kuwa kiwango cha elimu na cha ukomavu cha
walelewa ni tofauti, wazingatie kwa makini mahitaji ya kila mmoja ili
wawahudumie kwa hisani na uaminifu.
Wawe karibu nao sana, daima tayari kwao, kwa moyo
unaojali maswala yao na ni mwepesi kuhisi mambo wanavyoyaona wao.
Halafu:
- walete mwanga;
- watoe maelekezo;
- wasahihishe mitazamo;
- wakosoe kwa busara, imara na upendo;
- wasaidie kuchagua yanayofaa na kujibandua
inavyotakiwa;
- wachochee maswali, juhudi na mabadiliko wakati wa
wasiwasi, udhaifu na ulegevu;
- waratibu mipango;
- watambue pamoja na walelewa vipawa vyao na
kuwahimiza wavitumie vizuri hivyo na muda waliojaliwa;
- wawalishe kadiri ya hatua waliyofikia;
- wapime pamoja nao maendeleo yao na jinsi
wanavyotimiza masharti ya hatua hiyo.
3.16.
USINDIKIZAJI WA BINAFSI
Watumie hekima ya Roho na ujuzi wa kibinadamu
katika kufanya utambuzi wa wito na kumlea mtu awe huru.
Njia kuu ni uhusiano mzuri na mlelewa na maongezi
ya mara kwa mara naye: usindikizaji wa binafsi unaonekana kidogo na kudai sana,
lakini ni muhimu kuliko kazi nyingine na miundo ya malezi.
Ni kumsikiliza kwa moyo wazi na kumpokea alivyo,
anapojitahidi kujitambua na kujifunua, aweze kujithamini zaidi jinsi alivyo
pamoja na anavyoitwa kuwa.
Kwa mfano wa Yesu na wanafunzi wake, fungamano la
mlezi na mlelewa ni la lazima daima kwa kuwa linagusa kuliko mafundisho ya
hadhara.
Walezi waunde mazingira yanayosaidia kuwa wazi,
kuaminiana na kuwasiliana kwa unyofu na uhuru, la sivyo hawataweza kutimiza kazi
hiyo kwa urahisi.
Hata hivyo wasisikilize maungamo ya wale wanaowalea
wasipowaomba wenyewe.
3.17.
MUUNGAMISHI NA KIONGOZI WA KIROHO
Pamoja na hayo waheshimu nafasi ya padri
muungamishi (yule wa kawaida ateuliwe na askofu wa jimbo husika) na ya kiongozi
wa Kiroho (halmashauri imteue mmoja kwa kila nyumba ya malezi).
Pia wahakikishe kwamba wanazoezi na watawa
chipukizi wanafuata kweli uongozi wa Kiroho.
Ni lazima katika chama tuwe na watawa wenye uwezo
wa kuwasaidia wenzetu upande huo: kwa kuwa ndio wanaopenda zaidi maisha yetu na
wameng'amua shida zake maalumu pamoja na namna za kuzikabili.
Kazi yao inategemea maendeleo ya yule anayeongozwa,
lakini kwa jumla jukumu lao hasa ni kutambua kazi ya Mungu ndani yake, kumlisha
maneno ya imani, kumuelekeza katika utekelezaji wa maadili na sala, kumsindikiza
katika njia ya Bwana na kutathmini safari aliyokwishafanya, bila ya kuishia
katika saikolojia, kwa kuwa mbinu za kibinadamu haziwezi kushika nafasi ya zile
za Kiroho.
Ndugu akijifunua kwa unyenyekevu na unyofu anaweza
kupata mwanga wa hakika katika kuelekea ukamilifu wa Injili, anavyohitaji hasa
katika hatua za kuingizwa na nyinginezo za pekee.
3.18.
USHIRIKIANO
Chini ya mtumishi uongozi wa walelewa ni juu ya
mlezi wao tu: asitingwe na shughuli yoyote inayoweza ikamzuia asifanye
kikamilifu ile ya malezi; akiwa na wasaidizi, wawajibike chini yake na kumsaidia
kufanya utambuzi wa miito halisi.
Katika kundi la walezi kazi ni tofauti lakini zina
lengo moja; hivyo kila mmojawao atambue nafasi yake na mipaka yake pamoja na
kuheshimu kazi za wenzake.
Wote watende kwa umoja hata wakishughulikia hatua
mbalimbali.
Kwa ajili hiyo mara moja kwa mwaka mchochezi wa
malezi ya kudumu, mlezi wa machipukizi, wa wanazoezi na wa watakaji watathmini
kwa pamoja malengo na utekelezaji wake ili kulinganisha kazi zao kufuatana na
mpango huu.
Wakiitwa kutoa huduma ya mafundisho, sakramenti au
uongozi wa Kiroho mapadri, watawa au walei wa nje ya chama, wasaidiwe kuelewa
karama yetu maalumu na kuistawisha kwa kushirikiana na kuheshimiana na mlezi
katika kazi zao tofauti.
Walelewa wakitumwa kupata mafunzo katika vituo
yisivyo vya chama, watumishi na walezi wawe macho ili mafunzo hayo yachangie
malezi yetu bila ya kuyavuruga.
3.19.
WAZEE WETU NA WATU WA NJE
Biblia na utamaduni wetu vinamuona mzee kama mlezi
asili kwa kujawa na hekima, uchaji wa Mungu na mang'amuzi.
Jumuia na walezi wamsaidie ndugu mzee kuutumia
utajiri wake huo kwa ustawi wa chama: mabadilishano kati ya ndugu wa marika
mbalimbali yatawafaa wote, hasa vijana.
Mafungamano na watu wa nje pia, hasa maskini,
yanaweza yakachochea karama ya kitawa na kuwa njia ya malezi.
Watu wadogo wanatufundisha tuwe kweli ndugu wasio
na makuu, washiriki wa hali yao na washirikishaji wa yale yote tuliyojaliwa,
wasikilizaji wa dhati wa watu, hali na matukio.
Inapowezekana familia ya mlelewa ipewe nafasi ya
kujua chama chetu, maana ya utawa na namna inavyoweza kushiriki katika malezi na
utambuzi wa wito wa mtoto wao.
Upande wetu, kama Wafransisko, tunapaswa
kudhihirisha tunavyojisikia ndugu hasa kwao, ingawa jamaa ya kitawa ndiyo
familia yetu mpya.
3.20.
MAKLERI, WATAWA NA WALEI KUCHANGIA MALEZI
Makleri, watawa na walei wachangie kwa pamoja
malezi yetu ili yatolewe kikamilifu iwezekanavyo: ikikosekana aina mojawapo ya
waamini kati ya hizo, malezi yanapungukiwa kiasi cha utajiri wake.
Mchango maalumu wa padri unatokana na sakramenti ya
kudumu ya daraja inayomlinganisha na Kristo Kichwa ili aunde jumuia kwa kuratibu
na kuimarisha huduma na karama nyingine za waamini wote.
Mang'amuzi ni kwamba ubora wa malezi unategemea
sana uwepo na utendaji wa padri, hasa katika kitubio na uongozi wa Kiroho.
Pia ahamasishe wote wawajibike kwa pamoja na
kuheshimu waliopewa rasmi kazi ya kulea; aelekeze mafundisho na malezi kwa jumla
yatolewe vizuri kulingana na mipango ya Kanisa; ahusianishe malezi na liturujia,
hasa anapoadhimisha ekaristi.
Mchango maalumu wa mtawa unatokana na mashauri ya
Kiinjili anayoyashika ambayo amewekwa wakfu upya na kufanywa ishara hai ya uzima
wa milele.
Kwa kuwa hiyo ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa lote,
yeye anaitwa kutoa katekesi kwa namna ya pekee, na kila shirika linatakiwa
kujitahidi iwezekanavyo katika kazi hiyo.
Karama ya mwanzilishi ina uzito mkubwa kidini,
kijamii na kimalezi, hivyo isiwekwe pembeni katika utume wa wafuasi wake, bali
watoe ujumbe uleule wa Kanisa kwa mikazo maalumu; historia inaonyesha uhai
ulioletwa na karama hiyo.
Basi hayo yaliyo kweli kuhusu utume kwa watu wa
nje, ni kweli zaidi kuhusu malezi ya wanaojiunga na utawa: ni lazima hayo
yatolewe kadiri ya karama yetu maalumu, hasa na sisi tuliyonayo.
Hatimaye, mchango wa mlei una sifa maalumu
inayotokana na hali yake ya kuishi ulimwenguni kabisa akipokeza Injili kwa
kuzingatia sana utekelezaji wake katika maisha ya kila siku ya watu wa kawaida.
4. UTU NA UKRISTO
4.1.
MALEZI YA KIBINADAMU
Milenia mpya inapoanza tutazame kwa huzuni ya
kimama umati mkubwa wa wanaume na wanawake, watoto na wazee wanaokosewa haki na
heshima wanazostahili.
Dhuluma za kila siku zinamfanya kila mmojawao awe
maskini sio tu upande wa uchumi, bali pia upande wa elimu, maadili na dini.
Kumbe watu wote, wa kabila, hali, umri na jinsia
yoyote, kutokana na hadhi yao kama binadamu, wana haki ya kupata malezi
yanayolingana na matarajio, vipawa na utamaduni wa kila mmoja.
Malezi hayo yanatakiwa kuwaelekeza wafungamane
kidugu na watu wowote ili kuchangia maendeleo ya jamii katika umoja na amani, na
hasa wawe tayari kuipokea Habari Njema ili walifikie lengo kuu la kuishi na
Mungu milele.
4.2.
MALEZI YA KIKRISTO
Vilevile wabatizwa wote, kutokana na hadhi yao kama
wana wa Mungu, wana haja na haki ya kupewa na mama Kanisa malezi ya Kikristo ili
wakomae Kiroho.
Imani waliyojaliwa kwa mfumo wake inatakiwa
kujulikana, kuadhimishwa, kutekelezwa na kugeuka sala, tena si kibinafsi tu,
bali katika jumuia ya Kikristo na kwa kuelekea utume ulimwenguni.
Tunapofanya kazi hizo tuzingatie hali ya ardhi,
yaani mambo yanayoweza kuchangia au kuzuia mavuno moyoni mwa mtu, ili apokee
mbegu vizuri iwezekanavyo na hatimaye azae sana kwa utukufu wa Baba.
Tukumbuke daima kwamba kila mmoja ni mtu wa pekee,
anaishi katika hali maalumu na kuathiriwa na malezi, jamii, utamaduni na dini,
ajue asijue.
Kwa mfano, tofauti kati ya maisha ya vijijini na ya
mijini inasababisha athari mbalimbali.
Mara nyingi vijijini kuna ufukara, hofu na
ushirikina, lakini pia usahili, tumaini, mshikamano, imani kwa Mungu na uaminifu
kwa mapokeo.
Kumbe hali za wanaozidi kumiminika mijini ni za
kila aina, kuanzia utajiri mkubwa hadi unyonge mkubwa zaidi: huko kuna upweke,
uchovu, kishawishi cha kutowajibika na urahisi wa mabadiliko.
4.3.
DALILI ZA NYAKATI
Tukifundishwa na Neno la Mungu kutambua katika
malimwengu dalili za uwepo wa Mungu na za mpango wake, tukiri kwamba tumejaliwa
kuishi katika hatua mpya ya historia: mabadiliko ya haraka zaidi na zaidi
yanaathiri mtu binafsi na jamii, namna ya kuwaza na kutenda.
Hivyo tunahitaji kuliko zamani kukabili na
kuchambua maelekeo mapya na matokeo yake, tukizingatia hakika tatu: utendaji wa
Mungu anayeshirikisha wema wake, uwezo wa dhambi wa kumfunga na kumpoteza
binadamu, nguvu za uzima mpya uliotokana na ufufuko wa Kristo.
Sayansi na teknolojia zinazidi kuathiri watu wote
hata upande wa dini na maadili, pia kwa sababu wengi hawatambui mipaka yake na
hatari zake, hivyo wanameza bila ya wasiwasi matunda yake pamoja na sumu yake.
Papohapo katika utandawazi utamaduni wa kigeni
unatuvamia kwa nguvu na kuvuruga urithi wa tunu zetu pamoja na uwiano wa aina za
watu; wengi wanafuata kasumba wakidhani zitawasaidia kukabili maisha.
Tuwaonyeshe namna ya kujipatia tunu halisi kutoka
pande zote, pamoja na kuchuja yale yanayozuia ustawi wa mtu mzima (roho na
mwili) na wa watu wote; tukifanya hivyo waweze kutambua kwamba hatuwaondolei
yanayowafaa, bali tunawafaidisha.
4.4.
VIJANA
Hasa vijana ni changamoto kubwa kwa kuwa wanawahi
zaidi kuathiriwa; mageuzi ya harakaharaka katika jamii, mivuto ya ulimwengu,
maendeleo duni ya nchi zetu, utovu wa ajira unaowachelewesha wasichukue majukumu
ya utu uzima: hayo yote yanachangia kuwafanya wawe na matazamio makubwa, na
papohapo wakate tamaa na kujisikia wametupwa.
Utamaduni wa anasa unawadanganya watamani vitu
wasivyoweza kujipatia kwa njia halali; hivyo wanashawishika kufuata njia mbovu
wasijali matokeo yake.
Kutokana na vikwazo vingi, upande wa maadili giza
ni nene zaidi: dhambi na neema hazieleweki, wala uzito wake.
Kwa jumla, misingi ya ukweli si imara kwao, hivyo
wanashindwa kujielewa, kujieleza na kujiwekea malengo.
Kwa wengine maendeleo yao katika elimudunia
hayalingani na yale ya ukomavu wao katika utu; wengi hawakupitia familia imara;
wanajifunza kupitia picha lakini wanasoma kidogo mno mambo ya maana; hawana
mtazamo wa kihistoria, ni kana kwamba ulimwengu unaanza leo tu.
Uenezi wa vikundi vya kidini unachochea maswali
mengi kuhusu imani, na kuwafanya watamani kujua zaidi dini, lakini bila ya
hakika tulivu ya imani inayohitajika.
Kwa kutotegemezwa kiroho na kiadili na familia na
parokia, wengi wanasogea mbali na Kanisa, wakilitazama kibinadamu tu kama
muundo, si kama fumbo la imani.
Basi, tujenge mapema msimamo wa dhati wa ushirika
na Kanisa lote, hasa na askofu wa Roma, na wa usikilizaji na utekelezaji wa
mafundisho yake, bila ya kuishia katika Biblia tu.
4.5.
VIJANA NA MIITO
Kutokana na hayo yote ni vigumu kuhudumia miito
yao, kuwachambua na kuwalea.
Wajitambue au la, wengine wanakimbilia utawa ili
kujiepusha na mabaya ya ulimwengu (ukimwi n.k.); wengine wanatafuta tu maisha,
yaani maendeleo na hakika kwa kesho.
Hivyo inatubidi tunyoshe motisha zao na kuwaelekeza
njia pekee ya ukomavu: kuaminika, kujikana, kujitoa kwa ukarimu na udumifu,
kufurahi katika Bwana na hasa kupenda kama yeye.
Juhudi yoyote ya kuboresha jamii inawatumainia
vijana, nao ndio tumaini la Kanisa pia: lenyewe lina mengi ya kuwaambia, nao
wana mengi ya kuliambia.
Ingawa wanapatikana watu wazima wanaojisikia wito
wa kitawa, walio wengi wana umri kati ya miaka 18 na 25.
Moyo wao unatamani udugu, urafiki, mshikamano,
amani na haki; wanatarajia kuona ulimwengu bora zaidi, usio na ubaguzi, vita,
njaa, ujinga, dhuluma.
Baadhi wanaishi Kikristo tayari na kuwajibika
katika utume; wengi wao wanatafuta maana ya maisha: wanahisi sana mambo ya dini,
lakini wanahitaji bado kutangaziwa Habari Njema.
Basi, tunapaswa kuwatolea ushuhuda wetu kwa ari na
ubunifu, hata wakutane na Kristo kwa namna hai ambayo iwabadili kwa ndani
wakaanze maisha mapya ya kujitoa, wakiwajibika kustawisha jamii na kuhubiri
Injili.
Tutatue kwa busara tatizo la lugha (mitazamo,
miguso, mitindo na misamiati) kati ya vijana na Kanisa, ili kuwatafsiria ujumbe
wa Yesu na wa Kanisa uweze kujitokeza kwa namna mpya katika utamaduni wao bila
ya upotovu.
Katika kufanya kazi hiyo tusiogope kutumia pia
misamiati maalumu ya mapokeo ya imani, mradi tuifafanue na kuonyesha umuhimu
wake kimaisha, kwamba ni habari iliyo njema kwao na kwa jamii nzima.
4.6.
HABARI NJEMA KWA VIJANA
Kiini cha Injili kwa vijana kiwe wito wa Yesu kwa
kijana tajiri, ambao upendekezwe kwa wanaotaka kujiunga nasi na kwa vijana wote,
kama alivyofanya Yohane Paulo II katika barua aliyowaandikia tarehe 31-3-1985.
Katika ukurasa huo kijana anamuelekea Yesu, naye
anamfunulia utajiri wake wa pekee na kumualika awajibike kuutumia kwa faida ya
wote, hasa walio maskini, akiwa na hakika ya kuwa ndiyo njia ya kutajirika kweli
kwa kuishi kama yeye.
Kila mmoja atambue mapema kwamba namna za kumfuata
Yesu ni nyingi, kwa kuwa Roho wake anavuma anakotaka: maisha ya Kikristo na ya
Kifransisko yana matawi ya kila aina ambayo katika majira yoyote ya historia ya
Kanisa yanafyonza rutuba ya Injili na kuzaa sana.
Katika ushirika wa Kanisa na wa chama chetu, hali
za maisha ni mbalimbali lakini zinafungamana na kukamilishana, kwa kuwa wito wa
msingi ni sawa kwa wote, yaani kwamba tuishi kitakatifu kadiri ya hadhi yetu
kama wana wa Mungu.
Utume wa miito lengo lake si kudumisha chama, bali
kuhudumia karama hizo mbalimbali ili mpango wa Mungu juu ya kila mmoja
utekelezwe.
Ndani ya Kanisa sisi pia tuwajibike kuchochea,
kupokea, kusindikiza na kulea wanaojisikia wito, tukitegemea hasa sala na
ushuhuda wa maisha bora ya mtu binafsi na ya jumuia.
4.7.
NYUMBA YA MAPOKEZI
Ingawa chama chote kinapaswa kufanya kazi hiyo,
tuwe na nyumba maalumu ambapo, kwa msaada wa ndugu kadhaa na kwa njia za kufaa,
wenye wito waimarike katika imani, wajifunze kusali, kuishi kijumuia na
kulihudumia Kanisa, waweze kutambua namna wanavyoitwa kumfuata Kristo.
Waishi hapo hadi mwaka mmoja wakiwajibika katika
sala na kazi na kufundishwa yafuatayo: Wito, Agano la Kale, Agano Jipya,
Katekisimu Ndogo, Maisha ya Mtakatifu Fransisko.
Ili mgeni alifikie lengo hilo tumsaidie:
- ajifahamu na kujipokea alivyo, pamoja na vipawa
na kasoro zake;
- achanganyikiwe na Yesu ili ajiunge naye katika
kutimiza matakwa ya Baba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu;
- atambue wajibu wake kama mbatizwa, yaani mtoto wa
Mungu na wa Kanisa;
- atamani kuitikia mlio wa fukara;
- apange Kikristo tunu ambazo ziongoze maisha yake;
- apambanue kilichomleta kwetu;
- aelewe maisha yetu ili kutambua kama ndiyo
yanayomfaa.
4.8.
WATU WAZIMA
Malezi ya watu wazima yanawalenga binadamu ambao
maishani wana majukumu mbalimbali na kupatwa na majaribu makubwa.
Hivyo imani yao inahitaji mfululizo kuangazwa,
kukomazwa na kulindwa ili hekima ya Kikristo iunganishe na kukamilisha
mang'amuzi yao yote.
Kwa ajili hiyo, katika kulea wasekulari walei:
- tuyazingatie hayo pamoja na msingi walionao
kiroho na kielimu, hali yao ulimwenguni na wito wao wa kulenga ufalme wa Mungu
katika kuratibu malimwengu;
- tuimarishe misingi ya imani yao kwa mchango wa
akili pia;
- tuwaingize katika kusoma Maandiko katika sala;
- tustawishe maisha yao katika Kristo mfufuka kwa
njia ya liturujia, mafungo na uongozi wa kiroho;
- tuwaonyeshe uhusiano kati ya wajibu katika jamii
na wajibu katika Kanisa;
- tuangaze maswala ya kisasa kuhusu dini na
maadili;
- tuwasaidie kupima mageuzi ya jamii.
4.9.
INJILI, UTAWA NA UTAMADUNI
Yesu Kristo na Injili yake wanapita utamaduni
wowote na kuweza kuuboresha mpaka ndani kwa nguvu ya Roho Mtakatifu; upande wake
kila utamaduni unahitaji kupenywa na Habari Njema ili uponywe madonda
yaliyotokana na dhambi, na ili tunu zake zikamilishwe na hekima ya msalaba.
Utawa pia unahusiana na utamaduni, kwa maana
utamaduni unalenga kumwezesha mtu apokee na kutawala hali na maisha yake awe
bora zaidi; upande wake tamko la kushika mashauri ya Kiinjili, ingawa linamdai
mwamini ajinyime tunu za maana, linachangia sana maendeleo halisi: historia
inathibitisha kuwa wengi walikuta utawani nafasi bora ya kujielewa na kukomaa
kwa dhati.
Kwa hiyo:
- tuzingatie utamaduni na ujuzi wa mlelewa, ambao
hauishii katika elimu inayotolewa shuleni;
- tumsaidie kutamadunisha imani yake ili ipenye
maisha yake yote;
- tuandae wanaokwenda kuishi nje ya mazingira ya
utamaduni wao wajue na kuheshimu ule wa kigeni;
- tustawishe maisha ya kitawa yaliyotamadunishwa;
- tutathmini maisha yetu kwa kuzingatia
tunavyotunza na kuoanisha uaminifu kwa Yesu na Injili yake, kwa Kanisa na
umisionari wake, kwa utawa na karama yetu maalumu, kwa binadamu na mahitaji ya
nyakati hizi, bila ya kuzidisha upande mmoja na kupungukiwa upande mwingine.
4.10.
MBINU
Malezi ya kisasa yanataka mlelewa awe mtendaji
sana, pamoja na kuwa wazi na kushirikiana vizuri na wenzake: mtindo wa kujifunza
kwa njia ya kutenda unalingana na mawasiliano halisi kati ya watu.
Hata Mungu katika mpango wake wa kujifunua na
kutuokoa anatuita wote tuitikie zawadi yake kwa upokeaji wa sakramenti,
liturujia na sala, uwajibikaji katika Kanisa na jamii, matendo ya upendo na
ustawishaji wa tunu za kibinadamu (k.mf. uhuru, haki, amani na hifadhi ya
mazingira).
Basi, malezi yetu katika kulenga itikio la hiari la
mtu na kudai mchango wa utendaji wake, yafungamanishe ujumbe na mbinu za kuutoa:
mbinu zinahitajika ili ujumbe upokewe, nazo zinapaswa kulingana na ujumbe
wenyewe, na mazingira halisi na hali ya mhusika.
Tangu mwanzo wa malezi tufute udanganyifu wa mtu
kuwadai kila kitu wenzake; tumsaidie kuvumbua kwa shukrani yale yote ambayo
amekwishasaidiwa na anaendelea kusaidiwa; tumuandae kuwa mjenzi wa jumuia, si
mtumiaji tu, yaani awajibike kwa ustawi wa wenzake, awe tayari kupokea na kutoa
msaada, mwepesi kushika nafasi ya mwingine na kumuachia nafasi yake mwenyewe.
Vipimo vya ustawi wa utu ni ukomavu katika
mawasiliano na mafungamano, uwezo wa kujitolea, msimamo wa tabia, busara katika
uamuzi, uwezo wa kujitawala, utaratibu na upendo katika kusema, utulivu wa
nafsi, huruma kwa wenye shida, ulinganifu wa maneno na matendo.
Tustawishe yale maadili ambayo yanadaiwa na
mafungamano yoyote na kuheshimiwa na watu wowote: adabu njema, uungwana, haki,
uaminifu, nidhamu, mshikamano, usemakweli, unyofu, upole na ukunjufu, pamoja na
kupima vema watu na matukio, kubuni na kuanzisha mambo ya kufaa.
Tuzoee kuwa na upana wa akili na wa moyo, kujali
fumbo la kila mtu na kumheshimu hasa akiwa mzee au mgonjwa, kwa kuona kila mmoja
ni wa pekee kwa Mungu na kwetu.
Kujadiliana ni jambo gumu lakini la lazima kati
yetu wenyewe, tena kati yetu na wowote; hivyo katika hatua za kuingizwa kila
mmoja ajifunze kufanikisha majadiliano, kwa kutambua anavyopaswa kuwa macho
kuhusu namna yake ya kukabili maswala, kwa sababu anaathiriwa na mambo
mbalimbali ya leo na hasa ya zamani, ya nje na hasa ya ndani mwake.
4.11. AFYA
YA NAFSI
Safari ya kuelekea ukomavu haina mwisho kwa kuwa
inadai kutajirika mfululizo sio tu kinafsi, kielimu na kijamii, bali hasa
Kiroho; hivyo inaendana na ile ya kuishi Kikristo kweli.
Roho ndiye kipaumbele cha kudumu katika malezi, kwa
kuwa lengo hasa ni kuzidi kumzamisha mtu ndani ya Utatu, ulio dira ya maisha
yetu.
Mtakatifu Fransisko, kielelezo cha afya ya nafsi,
alikuwa tajiri wa miguso na vionjo, tena mwenye uwezo wa kuvitokeza; mwenye
adabu na ustaarabu sana; mwenye kuvutiwa na yaliyo mema na mazuri.
Kuwa na upendo wa Kimungu na wa kibinadamu kwa
pamoja ni sifa maalumu ya moyo uliofanywa mpya; upendo huo ulio tayari kusaidia
kwa heshima na kujitoa bure unakusudiwa kuonjesha ule wa Bwana uliodhihirika
hivi msalabani hata tusiweze kutia shakani kwamba tunapendwa na yule aliye
upendo.
Ingawa siku hizi ni vigumu kuliko zamani
kulinganisha yote ili kumpata mtu aliyekomaa pande zote katika umoja wa dhati,
tulenge hali hiyo kwa kushirikisha tunu za Injili kuliko wingi wa habari
mchanganyiko.
4.12.
UKOMAVU
Mtazamo wa imani unatakiwa kuhuisha na kukamilisha
malezi yote, lakini malezi ya Kiroho yanapotea bure yasipoendana na ustawi wa
nafsi ambao ndugu waweze kujipatia tunu za kitawa (hasa usafi kamili) mpaka
ndani, wakivuka toka tabia ya kujipendea na kujinufaisha kwa ubinafsi hadi ile
ya kupenda na kujitoa kwa wengine.
Matatizo yakija kujitokeza upande huo, mara nyingi
yametokana na athari za mambo yaliyotokea kwingine, ambazo hazijarekebishwa.
Kwa kuwa utawa unategemea na kutimiliza ubatizo,
wanaoshindwa kutekeleza kwa kiasi kikubwa masharti ya ubatizo kulingana na umri
wao, hawawezi kujitwisha mzigo mkubwa zaidi usije ukawalemea kabisa.
Kwa msingi huo wazuiwe wasianze zoezi wale ambao
wanashindwa kutawala tamaa ili kutekeleza jinsia yao kwa namna isiyotegemea
mwili, au wanataka kushika njia isiyoelekea ndoa wala usafi kamili.
Kama vile ukomavu fulani unavyohitajika ili kuishi
kijumuia, upendo wa kidugu unahitajika ili ndugu akomae hata akapenda wito wake
na viumbe kadiri ya wito wake, bila ya kuvamia wala kutawala wengine: ndio uhuru
wa dhati unaomwezesha kutekeleza vema haja ya kupendana ndani na nje ya jumuia.
Hiyo iwe mahali pa kukomaa kimiguso, ambapo
mazingira ya utulivu, uwazi, utayari wa kupokeana yanamwezesha ndugu kustawisha
vionjo vyake, kushirikisha shida zake, kuwa na urafiki halisi, kufanya kazi kwa
mshikamano na kujilinganisha na watu na hali tofauti.
Pamoja na hayo, tusikose kumpatia kila ndugu ujuzi
wa nafsi na mazingira yake ili aishi kwa ukomavu mkubwa zaidi.
Walau ajue motisha za ndani za binadamu; muundo wa
nafsi yake; haja kuu na matarajio ya moyoni; maendeleo ya nafsi na hatua za
maisha; mang'amuzi yanayoweka wazi kulipokea fumbo la Mungu; hali ya kidini, ya
kijamii, ya kiutamaduni na ya kiuchumi zinazomuathiri kimaisha.
4.13.
JINSIA
Mwenyezi Mungu hakuumba watu wa aina moja tu:
alipomuumba mtu kama kiumbe mwenye akili na utashi anayeweza kumjua na kumpenda,
hakutaka awe peke yake, bali aambatane na mwingine wa jinsia tofauti.
Mafungamano mengi ya wanaume na wanawake na
maelekeo ya ulimwengu leo yanadai malezi imara upande wa jinsia, kwa namna ya
pekee katika chama chetu chenye watu mchanganyiko.
Kwa kawaida wavulana na wasichana wa siku hizi
wanalelewa kwa pamoja bila ya kusaidiwa watambue tunu zao na mipaka yao
kijinsia.
Kuchanganyikana mapema si hakika ya kukomaa katika
mafungamano ya jinsia mbalimbali, bali ni lazima tulenge ukomavu huo na kuchukua
hatua ili usafi wa moyo na pengine useja mtakatifu viweze kutekelezwa kweli.
Wanaume na wanawake wanahitaji kuelewa hali yao
tofauti katika mpango wa Muumba na mchango maalumu wanaokusudiwa kuutoa katika
kazi ya uumbaji na ya wokovu kadiri ya jinsia yao.
Kwa hiyo tuwaonyeshe ukweli wa kutofautiana na
kukamilishana kwao, sio tu upande wa mwili katika ndoa na wa jamii katika kazi
za kufanya, bali kimsingi zaidi upande wa nafsi.
4.14.
WANAWAKE
Kwa namna ya pekee Bikira Maria anaangazia ukweli
wa mwanamke yeyote aweze kutekeleza ipasavyo jinsia yake na kujikomboa kweli.
Kwa njia yake Kanisa linavumbua katika sura ya
wanawake uzuri wa miguso bora ya binadamu: uwezo wa kuhisi shida ya mtu na
kumfariji, ukamilifu wa kujitoa kwa upendo, uaminifu mkubwa katika wajibu,
utendaji usiokubali kuchoka na nguvu ya kuvumilia lolote.
Kwa mfano wa Maria wanawake wanaitwa kuwa ishara ya
hisani ya Mungu kwa kila mtu, na ya sura ya kimama ya Kanisa, ambalo
linawategemea sana katika utamaduni na maisha ya kiroho, katekesi, teolojia na
maadili, maisha ya kifamilia na ya kijamii, na hasa hadhi yao na utetezi wa
uhai.
Wasishindwe na kishawishi cha kuwaiga wanaume, bali
katika sekta zote watokeze uwezo asilia waliojaliwa na namna yao maalumu ya
kuwaza na kutenda.
Kwa kujijali na kushika nafasi zao bila ya woga
wala unyonge, watawasaidia wanaume kuangalia upya namna wanavyojielewa,
wanavyotazama mambo na wanavyopanga maisha ya kijamii, ya kisiasa, ya kiuchumi
na ya kidini.
Hivyo malezi bora, pamoja na kuwasaidia wanawake
kuelewa vipawa vyao, yatachochea ushirikiano unaohitajiwa na jinsia zote mbili.
5. HATUA ZA KUINGIZWA
5.1.
KUINGIZWA UTAWANI HATUA KWA HATUA
Neno "kuingizwa" lina maana ya kusaidiwa
kuachana hatua kwa hatua na mtindo fulani wa maisha ili kuingia mtindo mwingine
ulio maalumu wa kundi fulani.
Hatua za kuingizwa katika maisha yetu ya
Kifransisko zinategemea zile za kuingizwa katika Ukristo, na zinafanana nazo.
Baada ya muda wa mapokezi, ambao ni wa kujisikia
kuvutiwa na maisha yetu, ziko hatua tatu, yaani:
- utakaji, ulio hatua ya kuyatafiti na kuyachagua;
- zoezi, lililo hatua ya kukoleza karama ya
Kiinjili ya Kifransisko;
- uchipukizi, ulio hatua ya kuimarika kimaisha.
Tuhakikishe hatua hizo zilete maendeleo
yaliyotazamiwa kadiri ya lengo maalumu la kila moja na kwa kusonga mbele daima
kuelekea ukomavu.
Malengo ya hatua hizo ni vituo vya kufikia na
kuondokea kwa wakati mmoja; kwa kifupi ni kuvumbua, halafu kujaribu, hatimaye
kuchimba maisha matakatifu ya udugu na udogo.
Ndugu asipige hatua ya mbele kabla hajafikia lengo
la awali.
Kwa hiyo, kwa kiasi fulani, urefu wa hatua hizo
ulinganishwe na mwendo wa kila ndugu, ambao ni wa pekee kutokana na tofauti za
neema za Mungu, itikio la hiari yake, mchango wa jumuia, umri n.k.
Katika safari hiyo ndugu wasaidiwe na ibada maalumu
ambazo ziwatakase na kuwategemeza, ziwapatie baraka za Mungu katika kupiga hatua
fulani n.k.
Kulingana na mafundisho wanayopata wakabidhiwe
Injili, Kanuni ya Imani, Sala ya Bwana na kanuni ya utawa wetu.
5.2.
HAJA YA UJUZI
Katika hatua zote za maisha tunahitaji kujiongezea
ujuzi, kila mmoja kadiri ya uwezo na mahitaji yake, ili tuzidi kutambua na
kuitikia wito tuliojaliwa na Mungu ndani ya Kanisa.
Ustawi wa Kiroho na wa kitume unatudai daima
tukabili masomo yanayotuhusu ili yatusaidie kumjua Yesu, kushika misimamo ya
Kanisa, kutekeleza tunu za karama yetu, kukomaa kwa ndani, kushirikisha ujumbe
wa wokovu, kuumua utamaduni kwa chachu ya Injili na kuchangia maendeleo kamili
ya jamii.
Hasa katika hatua za kuingizwa chama kiwajibike
kushirikisha kwa mpango ujuzi unaohitajika, ingawa malezi hayaishii hapo bali ni
kumkuza mtu mzima.
Uzingatiwe umoja wa ndani wa mafundisho yote ili
ndugu watambue ni elimu ileile ya Injili.
Wahusika wawajibike kuhudhuria kwa kawaida na kwa
bidii vipindi walivyopangiwa: wakikosa kuhudhuria thuluthi moja ya vipindi vya
kozi fulani, itawabidi kuirudia.
Kwa muda uliopangwa waonyeshe maendeleo yao kwa
njia ya majadiliano, maandishi na mitihani.
Watakaoonekana hawajajua vya kutosha (60%)
itawabidi warudie mtihani, na wakifeli tena wairudie kozi husika.
5.3.
UTAKAJI
Baada ya mapokezi, wanaoomba kuanza rasmi malezi ya
kitawa wanaweza kupokewa katika utakaji.
Ikiwezekana nyumba yao isiwe ile ya zoezi, bali
nyingine ambayo ijitegemee hata upande wa mafundisho yanayokazaniwa wakati huo.
Katika utakaji zitolewe kozi zifuatazo, isipokuwa
kama mmojawapo hahitaji baadhi yake kwa kuwa ana ujuzi huo tayari au ametangulia
kupata kozi nyingine za hatua za mbele: Marko, Tunasadiki, Mungu Baba,
Liturujia-msingi, Sakramenti za Kwanza, Misa, Sakramenti za Uponyaji,
Maadili-msingi, Amri za Mungu, Sala-msingi, Elimunafsia-Jinsia, Maisha ya
Kijumuia.
Mtakaji na chama wanatakiwa kuhusiana sana ili yeye
aweze kutambua na kuchagua maisha, nasi tuweze kumfahamu vizuri na kumfikiria
kuhusu wito.
Lengo hilo linahitaji mbinu na muda: hivyo
tusiogope kuurefusha hadi miaka mitatu, ingawa bila ya kuuzidisha bure, wala
kuchelewa kuwaelekeza kwingine wale wasiofaa kwa maisha yetu.
Kazi za mtakaji ni hasa:
- kupunguza uhusiano na ulimwengu;
- kuishi kijumuia kweli;
- kukomaa upande wa hisi na vionjo;
- kujitambua kiutu na Kiroho;
- kuelewa maana na aina za miito;
- kuzoea Biblia, liturujia na sala;
- kujiongezea ujuzi wa imani na maadili.
5.4.
KABLA YA ZOEZI
Matatizo mengi katika malezi mashirikani yanatokana
na vijana kuingia unovisi pasipo ukomavu wa kutosha.
Si kwamba wadaiwe kuwa wakamilifu toka mwanzo, bali
kwamba waweze kutimiza masharti ya utawa wakimaliza unovisi.
Ili wito wao ueleweke na uwezo huo upimwe, kabla
hawajaanza wasaidiwe kuziba mapengo yaliyoachwa na malezi yao ya awali.
Mtumishi anapoingiza zoezini afuate kwa makini
katiba yetu akizingatia:
- ukomavu wa kiutu na wa Kikristo unaohitajika ili
zoezi lisilazimishwe kurudia misingi tu;
- msimamo wa miguso, hasa upande wa jinsia;
- uwezo wa kuishi kijumuia chini ya viongozi;
- ujuzi wa lugha inayotumika katika zoezi;
- elimu inayodaiwa na serikali kwa wananchi wote.
5.5.
UNGAMO LA IMANI
Tokeo muhimu la urithi hai wa Mitume ni Kanuni ya
Imani: hasa katika nafasi ngumu za historia yake, Kanisa likiongozwa na Roho
Mtakatifu lilijumlisha vema imani yake likaikabidhi rasmi kwa waamini wapya
kabla ya Sala ya Bwana.
Siku hizi ibada hizo zimerudishwa kwa wakatekumeni
na kuhimizwa kwa nafasi nyingine ili mwanafunzi wa Yesu apokee kwa ujuzi na ari
mafumbo anayopaswa kuyazingatia.
Watakaji wetu, muda mrefu baada ya kukabidhiwa
imani hiyo waiungame mbele ya mtumishi na jumuia kabla hawajaanza zoezi.
5.6.
ZOEZI
Lengo la zoezi ni kuingizwa katika mtindo wa maisha
wa Mwana wa Mungu, kwa kuzingatia hasa ufukara na unyenyekevu wa Injili yake
takatifu.
Wanazoezi wakijaribu kuishi hivyo, jamaa inapima
nia na uwezo wao wa kudumu siku za mbele.
Masomo na kazi visivyolenga moja kwa moja malezi
hayo haviruhusiwi.
Wanazoezi waongozwe kupata mang'amuzi ya Kiroho ya
dhati zaidi kwa:
- kuwajua kwa namna hai Yesu na Baba;
- kustawisha maadili ya kibinadamu na ya Kimungu;
- kuongeza kasi katika kuelekea ukamilifu;
- kutunza kimya, kukazania sala na kujikana;
- kuzama katika mafumbo ya imani;
- kusoma na kutafakari Neno la Mungu na kuona namna
ya kuliitikia kwa nguvu zote;
- kumuabudu vema katika liturujia kwa mtindo wa
Kifransisko na wa Kiafrika;
- kupenda Kanisa na wachungaji wake;
- kujifunza kutimiza masharti ya maisha yetu, hasa
mashauri ya Kiinjili;
- kujua sifa na karama, lengo na sheria, historia
na maisha ya familia ya Kifransisko na ya chama chetu.
Katika zoezi zitolewe kozi zifuatazo: Mathayo,
Luka, Yesu Kristo, Roho Mtakatifu, Sakramenti za Ushirika, Baba Yetu, Maisha ya
Sala, Maisha ya Kiroho - I, Historia ya Wafransisko, Kanuni, Katiba, Mashauri ya
Kiinjili, Kujifahamu.
Baadhi yake zinaweza kutangulizwa au kuairishwa
katika hatua nyingine za malezi ya awali, isipokuwa kozi za mwisho.
5.7.
MAZINGIRA YA ZOEZI
Ili wanazoezi watie mizizi katika maisha
yaliyofichika pamoja na Kristo ndani ya Mungu na waunde akili na moyo kadiri ya
karama yetu haifai nyumba iliyozama kati ya watu, bali mazingira na hali
vinavyosaidia kuvutiwa na sala.
Isipowezekana kwa mwaka wa kwanza na kwa ule wa
mwisho, walau wa pili utumike katika mazingira ya namna hiyo na kwa kuzingatia
utulivu wa kukaa na Mungu kuliko utendaji na uhusiano na watu.
Kinyume chake, miaka ya kwanza na mwisho ikitumika
jangwani zaidi, mwaka wa pili unaweza ukatumika kumpa mwanazoezi nafasi ya:
- kustawisha uwajibikaji wake katika maisha ya
kidugu;
- kung'amua utume wetu maalumu;
- kujifunza kudumisha muungano wake na Mungu katika
kazi yoyote, kama tunu mojawapo ya msingi.
Zoezi lote lifanyike katika nchi asili ya
mwanazoezi au nyingine inayofanana nayo, tusije tukazidisha ugumu wa hatua hiyo
ambapo:
- anapaswa kujipatia msimamo wa ndani;
- mafungamano kati yake na mlezi yanatakiwa kuwa
rahisi;
- tunahitaji kuchambua miito midanganyifu
inayosukumwa na motisha isiyo ya Kiroho, kama vile kusafiri na kuona mazingira
mapya.
5.8.
UBORA WA KUJITOA MOJA KWA MOJA
Mtu yeyote anaweza kupimwa kwa kuzingatia
anafungamana na nani na nini.
Hiari yake inaweza kufikia ukomavu mkuu kwa
kujifunga kiarusi kupendana na Kristo.
Upendo wake unaweza ukatushika hata tujisikie haja
ya kumtolea moyo na maisha yetu yote.
Mwenyewe akitualika tufanye hivyo, haifai kujitoa
kwake kwa muda au kwa jaribio.
Kwa kutegemea uaminifu wake na karama ya Roho
Mtakatifu tunaweza kujitoa kabisa kwake, halafu kuzidi kujitoa siku kwa siku kwa
uhuru na furaha: wakati wa zoezi uonyeshwe uwezekano na ubora wa kujitoa moja
kwa moja.
Maana ya kiarusi ya maisha ya wakfu ina umuhimu wa
pekee kwa kulikumbusha Kanisa wajibu wa kuwa aminifu kabisa kwa Bwanaarusi wake,
ambaye toka kwake linapokea mema yote.
Hasa wanawake wanakuta humo ukweli wa jinsia yao na
namna yao maalumu ya kuhusiana na Bwana.
Kielelezo kikuu ni Mama Maria aliyejaliwa kwamba
upendo wake wa kibikira umzae Mungu duniani na kuchangia hata leo uzima wa
Kimungu upatikane na kustawi ndani ya watu.
Katika hatua zote za kuingizwa tustawishe upendo na
ibada kwake, ambaye kila ndugu na jumuia ya malezi wajiaminishe kwake.
5.9.
KUWEKA AHADI
Ahadi ya daima inadai mang'amuzi na maandalizi
marefu yanayohakikisha iwezekanavyo udumifu.
Ndiyo sababu Kanisa linaweza likadai utangulie muda
wa kuthibitisha uaminifu wa mtawa hata katika nafasi ngumu.
Maadhimisho ya ahadi yawe tofauti sana: ahadi ya
muda isiwe na fahari yoyote; kumbe ahadi ya daima ifanyike kwa kuwaalika askofu
wa jimbo na waamini wengine, kwa kuwa ni tendo la kuwekwa wakfu na ni ishara ya
muungano wa moja kwa moja kati ya Kristo na Kanisa.
Kwa njia ya wenye mamlaka ndani ya chama, lenyewe
linazipokea ahadi zetu za daima na za muda vilevile na kuziunganisha na sadaka
ya Bwana.
Tufuate kwa makini taratibu zote za katiba kuhusu
kuweka ahadi.
5.10.
KIPINDI CHA MATAKASO
Miezi mitatu kabla ya ahadi ya kwanza, anayetaka
kuiweka aandike ombi kwa halmashauri ya jamaa.
Nia yake hiyo na kibali cha chama vitangazwe rasmi
katika ibada ya kuandikisha jina la kitawa.
Ndiyo mwanzo wa kipindi cha matakaso, ambacho ni
kilele cha zoezi na ambacho kiini chake ni ibada tatu zinazohusiana na mashauri
matatu ya Kiinjili, yaliyo nguzo za utawa na ambayo yanakazaniwa wakati huo.
Urafiki wa ndani na Yesu ndio neema ambayo
inatuwezesha, na kwa namna fulani inatutaka tuwe kitu kimoja naye kimawazo na
kimaisha na kuona mengine ni hasara tupu, hata tukaahidi kushika mashauri
aliyotuachia kwa mifano na mafundisho yake.
Mashauri hayo ya Kiinjili si kujinyima tu, bali ni
kuliishi fumbo la Kristo ndani ya Kanisa kwa ukamilifu ule unaowezekana duniani
na kulingana na karama fulani.
Mapokeo ya Mitume yameungama daima ubora wa maisha
ya useja, ufukara na utiifu, kwa kuwa ndiyo maisha ya Mwana wa Mungu kama
binadamu, yanayotokeza upendo wa Mwana kwa Baba katika umoja wa Roho Mtakatifu,
kwa hiyo ni namna ya Kimungu ya kuishi duniani.
Ndiyo changamoto na wajibu mkuu wa maisha ya
kitawa: kadiri yanavyolingana na yale ya Yesu, mwenyewe anakuwepo na kuokoa
ulimwengu.
Utume wa watawa unatokana na wito huo wa kuungana
naye: ni hasa kumfanya awepo ulimwenguni kwa ushuhuda wa maisha yaleyale ya
kwake.
Tuwaingize kwa makini wanazoezi katika maana na
masharti ya mashauri hayo, upande wa nadharia na wa utekelezaji.
Imani, tumaini na upendo vinatusukuma tuweke ahadi
ya kuyashika ili kukwepa vinavyoweza vikazuia ari ya ukamilifu katika kumtumikia
Mungu ndani ya Kanisa.
Kila shauri linarekebisha nafsi yetu katika jambo
mojawapo la msingi, yaani mapenzi, mali na hiari, hivyo linaweza kutatua tatizo
kuu mojawapo linaloutawala na kuuharibu ulimwengu, yaani tamaa za mwili, tamaa
za macho na kiburi cha maisha.
Kutimiza vema mashauri hayo kunamkomaza mtu,
kunampa uhuru wa Kiroho, kunamtakasa moyo, kunamwasha upendo na kumsaidia
kujenga dunia bora.
5.11.
UCHIPUKIZI
Baada ya kuweka ahadi, malezi yanaendelea
kuhitajika ili watawa chipukizi, wanapozidi kuingizwa katika maisha yetu yote,
wazoee kuoanisha kimaisha juhudi za Kiroho (ambazo zidumu kushika nafasi ya
kwanza), za kitume na za kielimu katika jumuia.
Ni hatua mpya inayokusudiwa kufaidika na msukumo na
msimamo wa tamko la ahadi; yaani mtawa chipukizi anatakiwa kuchuma matunda ya
hatua zilizotangulia na kuendelea kukua kiutu na Kikristo akitekeleza kiaminifu
ahadi yake, na kuelekea pengine ile ya daima.
Katika hatua hiyo anahitaji kudumisha juhudi za
Kiroho za zoezi hasa kwa sababu ongezeko la kazi na la mafungamano na watu wa
nje linasababisha kwa urahisi hali ya ukavu na ya kuyumbayumba.
Hivyo lengo kuu ni kumwezesha afuate wito kwa umoja
wa ndani na kukabili vema mvutano kati ya sala na shughuli zinazozidi kumpasa,
au kati ya maisha ya kijumuia na utume unaodaiwa na maendeleo yake wakati huo.
Pia aelewe karama yetu zaidi, atimize masharti ya
ustawi wake, akubali maisha yetu jinsi yalivyo, aheshimu wengine katika tofauti
zao na kuwajibika katika jumuia.
Asikabidhiwe kazi zinazoweza zikayazuia malengo
hayo, ila apate mang'amuzi ya Kikanisa na ya kijamii kulingana na karama ya
chama na kwa kujitambua daima kuwa si mtendakazi tu, bali ni hasa shahidi hai wa
maisha ya Yesu, hivyo utendaji wake unahitaji kufanyiwa utambuzi na kuwekewa
masharti.
5.12.
MALEZI YA UCHIPUKIZI
Ni wajibu mzito wa chama kumpatia hali
inayomwezesha kukua katika kujitoa kwa Bwana.
Kwanza kimpatie mlezi wa kufaa na jumuia ya nguvu,
yaani yenye uongozi imara na ndugu wengiwengi, hata wa mataifa mbalimbali,
wanaochanga utajiri wa tunu zao mbalimbali.
Kwa kuwa hatua hiyo, tofauti na zoezi, inahitaji
jumuia kubwakubwa, yenye vitabu bora vingivingi pamoja na uwezekano wa
kuhudhuria kozi za dini na za elimudunia, ingawa hata kozi kwa njia ya posta
zinaweza zikafikiriwa.
Lakini mafunzo mazito ya nadharia na ya ufundi ni
vigumu kuyapatanisha na madai ya uchipukizi: kwa hiyo mwaka wa kwanza baada ya
ahadi ndugu asifuate mafunzo yasiyo ya dini, isipokuwa pengine ya lugha ya
Kiingereza.
Halafu yapangwe si kwa kumridhisha kibinadamu
kadiri ya malengo yake binafsi, bali kwa ajili ya utume wa chama kulingana na
karama yetu na mahitaji ya Kanisa na ya jamii.
Tena yalinganishwe na malezi yote ya hatua hiyo,
ambayo yawe na malengo yaleyale kwa wote, hata wasipokaa nyumba moja miaka yote
mitatu.
Ni jukumu la mtumishi pamoja na mlezi kulinganisha
mpango wa jumla na mahitaji ya watawa, nyakati na mahali.
Kwa vyovyote, ndugu akiishi nje ya jumuia ya
uchipukizi, arudi humo walau miezi miwili kwa mwaka kwa kuhudhuria kozi
zifuatazo (zisipotarajiwa baadaye katika malezi ya daraja takatifu): Zaburi,
Yohane, Historia ya Kanisa, Mababu, Matapo ya Kiroho, Mtaguso, Sheria za Kanisa,
Kanisa Barani Afrika, Maisha ya Kiroho - II, Fransisko-maadili, Sheria
Ndogondogo, Ushauri, Elimu ya Malezi, Utamaduni, Elimujamii, Mawasiliano,
Katekesi, Uchungaji, Ekumeni, Umisionari, Uislamu, Tunu za Afrika, Sayansi,
Falsafa, Teolojia-msingi, Teolojia ya Historia.
Watawa chipukizi (na vilevile wanaosomea daraja au
fani maalumu) wapaswe kumtii mlinzi, lakini wawe chini ya mlezi wao, hivi kwamba
mlinzi asiamue lolote juu yao asipokubaliana na mlezi.
6. MALEZI YA KUDUMU
6.1.
HAJA YAKE
Ufafanuzi ufuatao unahitajika ili kila mmojawetu
awe na mpango tayari kwa maisha yake yote, kusudi azidi kukua kama mtu na kama
mfuasi, bila ya kujitenga na wenzake wala kujiamini mno: hakuna wakati wa
kujisikia tumekamilika.
Hasa aliyemaliza muda wa uchipukizi hawezi kujidai
yuko imara kwa maisha yake yote, yawe yaweje; ila anakusudiwa kuwa amejipatia
ari na mbinu za kujirekebisha na kujiendeleza sikuzote katika namna ya kuishi,
kufikiri na kutenda ili akabili vema zaidi na zaidi hali zozote, za zamani na
mpya, za ndani na za nje.
Awe amejifunza jinsi ya kujifunza, kwa kumuendea
Mungu upwekeni, kujisomea hasa Neno lake na hati za Kanisa, kuchunguza ishara za
nyakati na kutambua itikio la kufaa, kuchimba karama yetu, kufaidika na maneno
na mang'amuzi ya wengine asidhuriwe nayo, kuhudhuria semina, mikutano n.k.
Ndugu mwenyewe ndiye wa kwanza kupaswa na malezi
yake ya kudumu, kulingana na maongozi ya Mungu, mahitaji ya Kanisa na ya
ulimwengu.
Pamoja na kuwa mtendaji wa malezi katika hatua zote
za maisha yake, ndiye mlengwa pia katika utu wake wote unaoitwa kuwapenda kabisa
Mungu na jirani.
Upendo huo ndio unaoweza kuchochea daima uaminifu
na ustawi.
6.2.
MPANGO WAKE KATIKA MTIRIRIKO WA MAISHA
Malezi ya kudumu yanaanza miaka mitatu baada ya
kumaliza zoezi na yanachukua miaka ya ukomavu wa mtu, halafu ile inayolazimisha
kupunguza kazi na kujiandaa kukutana na Bwana moja kwa moja.
Miaka ya kwanza ya kufanya utume muda mwingi kila
siku pasipo usimamizi ni hatua ngumu inayotutaka tuwajibike kikamilifu kwa
msaada wa ndugu zetu kutekeleza ari ya upendo.
Hatua inayofuata inaweza ikaleta hatari ya kuzoea
hata kukinai maisha na kazi, pamoja na kishawishi cha kukata tamaa kwa kuona
matunda machache ya Kiroho na ya kitume: hapo tunahitaji tena msaada tujitoe tu,
bila ya kujali matokeo yanayoonekana bali kwa kuzingatia upya yale ambayo peke
yake ni ya lazima.
Umri wa makamo unaweza ukaleta hatari mbalimbali:
kupatwa na ubinafsi au hofu ya kupitwa na wakati, kushikilia namna fulani tu,
kujifanya lengo la yote na kupotewa na juhudi; hapo tunahitaji kuinua maisha ya
Kiroho na ya kitume ili kuzaa sana kwa kujitoa kwa Mungu kwa ukweli na ukarimu
mkubwa zaidi, na kujitoa kwa watu kwa utulivu, usahili na hekima kubwa zaidi.
Uzee unaweza ukaleta matatizo mapya ambayo
tuyakabili Kiroho mapema, tukijiandaa kupokea changamoto za umri huo: kupunguza
polepole utendaji wetu ni namna mpya ya kuishi inayoweza kutufanya tung'amue
kuwa ubora wa utawa hautegemei uwezo wa kuendesha shughuli; hata maumivu ni
fursa ya kujiunga na Kristo mteswa na kujiaminisha mikononi mwa Baba.
Wasiojiweza tena wasijione mzigo, bali wasadiki
kuwa wamealikwa mbele zaidi katika fumbo la Pasaka, wachangie ustawi wa chama na
wa utume wake kwa sala na sadaka: matunda yataonekana Bwana atakaporudi.
Wawe pia tayari kutoa huduma ya uongozi wa Kiroho;
wasipofikiria matatizo yao tu, bali wakidumisha upendo, furaha, amani na
tumaini, wanaweza kumtegemeza sana kijana: shuhuda, busara na sala zao zinamtia
moyo mfululizo katika safari yake.
Kusudi wasijione pembeni katika maisha ya jamaa,
tuthamini uwepo wao na kupokea utendaji wao, pamoja na kuwapatia kidugu misaada
wanayohitaji kwa roho na mwili, tukithibitisha ukweli wetu kama familia
iliyokusanyika kwa jina la Bwana.
Saa ya kufa katika Bwana iandaliwe na kungojewa
kama tendo kuu la kujitoa kwake kwa upendo, kwa kuwa ndipo Baba anapoikamilisha
kazi ambayo aliianza ndani mwetu akaifanya kwa miaka kadhaa.
6.3.
NAFASI ZA PEKEE
Bila ya kutegemea hatua hizo, tunaweza tukapatwa na
magumu kwa sababu za nje (k.mf. uhamisho, kazi mpya, matatizo ya kazi, uhaba wa
matunda katika utume, misiba, hisi ya kutoeleweka au kutengwa) au za ndani
(k.mf.ugonjwa, ukavu rohoni, vishawishi vikali, wasiwasi juu ya imani au wito,
hisi ya kutokuwa na maana).
Tuyakabili hayo yote kwa hakika ya kuwa kilicho
muhimu ni kudumu kiaminifu katika wito: udumifu huo unashuhudia vema fumbo la
Pasaka, yaani imani katika Bwana mshindi anayeshika mikononi mwake watu binafsi
na mataifa, miundo yao na historia yote.
Tuyatazame majaribu yenyewe kama njia za kulelewa
na Baba na za kuokolewa na nguvu ya msalaba.
Uaminifu unapokuwa wa shida, mtawa asaidiwe na
ndugu binafsi na jumuia nzima kwa upendo na tumaini: hasa ujirani wa mtumishi na
wa mlinzi ni wa lazima.
Hao na ndugu wahusika wafanye juhudi za pekee
katika malezi kwenye nafasi zifuatazo: wakati wa uhamisho kati ya watu wa
utamaduni tofauti, miaka ya kwanza baada ya upadirisho, vipindi vigumu vya
binafsi, jubilei n.k.
Miaka kumi baada ya ahadi ya kwanza ndugu anaweza
kutumia mwaka mzima asisitize kipaumbele cha uhusiano na Mungu, kwa kuwa maisha
yetu ni hasa itikio la upendo kwa upendo wake mkuu.
Asiyejisikia hamu ya mwaka huo wa Sabato, aombe
walau mwezi mmoja wa mazoezi ya Kiroho ili kutambua kinachomfanya asiwe na hamu
ya kukaa zaidi na Bwana.
6.4.
MSINGI WAKE: MAISHA YA KIROHO
Bila ya shaka maisha ya Kiroho ndiyo msingi, kwa
kuwa ndiyo njia ya kujitambua mbele ya Mungu, kupokea kila siku changamoto za
Neno na za maisha, kufuata karama tuliyojaliwa na kuonja amani ya dhati.
Chini ya Roho Mtakatifu ndugu ajihakikishie nafasi
za kimya na kujiombea mfululizo ushindi katika mapigano.
Wito wa Mungu na itikio la mtu vinaendelea maisha
yote kwa namna ambazo pengine hazieleweki wala kutarajiwa, ila zinamdai daima
mtu awe tayari kumfuata Mwanakondoo kokote.
Uhai wa Kiroho unadumu pale ambapo katika hatua
yoyote mtu anatafuta na kuona namna maalumu za kuishi, kutumikia na kupenda
upya.
Ustawi wa mtawa binafsi ni baraka kwa chama kizima
na chemchemi ya nguvu katika utume kwa manufaa ya watu tunaowalenga.
Vilevile mwamko wa jumuia unaimarisha maisha ya
pamoja na ushirikiano kati ya ndugu tofauti kwa asili, umri, elimu n.k. na hivyo
unakuza ushuhuda wetu wa Kiinjili.
6.5.
KUJENGA JUMUIA
Malezi ya kudumu hayamlengi tu ndugu binafsi, bali
jumuia pia ikomae katika upendo kwa Mungu na kwa ndugu wote, wa ndani na wa nje
yake.
Ombi la umoja la Bwana Yesu linatuita mfululizo
tuukaribie zaidi na zaidi kwa njia ya usikivu kwa Neno na kwa lishe ya Mwili na
Damu: ndio chakula cha sikuzote kwa safari ya kumrudia Baba.
Mezani hapo hotuba inatakiwa kututia moyo tuanze
upya kila leo.
Huduma ya Neno ina namna nyingine pia, kama vile:
- kusoma na kutafakari pamoja Maandiko, hasa kwa
njia ya lectio divina ili kuyaitikia Kikanisa na kijumuia;
- kuchambua matukio kwa msaada wa mafundisho ya
Kanisa kuhusu jamii ili kupima kama yanalingana au kupishana na Injili;
- kufafanua liturujia ili kuzidi kung'amua maana ya
sala, ishara na vitendo, namna ya kushiriki, kunyamaza na kuzama katika mafumbo
yanayoadimishwa;
- kutoa mawaidha ya dharura yanayojaribu kufasiri
nafasi maalumu za maisha ya mtu, jumuia, Kanisa na jamii ili kuziishi kwa imani;
- kuhimiza mikakati ya Kiroho ili kuimarisha
misimamo, kupanua mitazamo na kudumisha sala na uwajibikaji;
- kuchimba kwa mpango imani ya Kikristo ili kukuza
ujuzi wake na kumwezesha kila ndugu ashuhudie ulimwenguni sababu za kutumaini.
6.6.
NDANI YA CHAMA
Sawa na hatua za kuingizwa, malezi ya kudumu
yanafanyika ndani ya jamaa na kwa kushirikiana na watumishi na walinzi
waliokabidhiwa na Kanisa mamlaka na majukumu ya kufundisha, kutakasa na kuongoza
wanachama wenzao, wakichochea karama yao wasichoke.
Maisha yenyewe, yakifuatwa kwa dhati, kulingana na
Injili na mazingira tuliyopangiwa na Mungu ndiyo jambo la kwanza, la thamani na
la kudumu linalochangia ustawi wetu.
Pamoja na hayo, halmashauri kuu ielekeze njia za
kukomaa hasa Kiroho na nafasi za kuchimba ujuzi unaotuhusu, kadiri tunavyoweza
na tunavyohitaji, bila ya kutegemea mno taasisi za nje.
Kwa ajili hiyo imteue ndugu mwenye jukumu la
kushughulikia malezi ya kudumu katika jamaa nzima kama jambo la lazima kwa wote.
Mawasiliano ni moja kati ya mambo ya kibinadamu
yenye uzito mkubwa kwa jumuia za kitawa: ili tuwe ndugu ni lazima tufahamiane,
na ili tufahamiane ni muhimu kufungamana kwa upana na kwa undani.
Kwa kawaida mikutano, ziara, barua, majarida,
vikilingana na mtindo wetu hasa upande wa ufukara, vinaimarisha roho ya
kifamilia, hamu ya kujihusisha na maisha ya chama, na umoja katika utume.
6.7.
MIKUTANO NA USHIRIKISHANO
Mikutano juu ya hati za Kanisa na juu ya maswala
yetu inafaa pia kwa kusikiliza wenzetu, kushirikisha mawazo, kukosoana kidugu,
kukagua maisha, kutathmini yaliyopita na kupanga pamoja.
Udugu unaimarika kadiri yalivyo muhimu yale
tunayoshirikishana, kama vile Neno, imani na mang'amuzi ya Kiroho.
Kosa la kutoshirikishana vya kutosha mambo hayo
linaweza likachangia ubinafsi na kishawishi cha kujali mafungamano na watu wa
nje kuliko yale na ndugu wa ndani.
Fursa hizo zinahitajika hasa katika jumuia kubwa au
wakiishi pamoja watawa mbalimbali kwa asili, umri, elimu na mang'amuzi, waweze
kuungana kwa kutumia utajiri huo wote.
Katika utekelezaji mlinzi ana nafasi muhimu, hivyo
asaidiwe kuzifanikisha.
6.8.
UAMINIFU KWA KARAMA
Malezi ya kudumu si kujiendeleza upande wa elimu na
kazi tu, bali ni kujifanya upya mfululizo kwa kuchochea karama yetu na
kustawisha uaminifu kwa ahadi yetu katika kila nafasi ya maisha.
Kwa ahadi kila mmojawetu amejitoa kwa Baba ndani ya
chama, hivyo anaitwa daima azidi kuungana na ndugu wengine katika kumfuata Yesu
kadiri ya karama ya Kifransisko.
Hiyo ni sharti la msingi la umoja wetu katika
jumuia na katika utume, kwa hiyo tuielewe sawasawa, tuzidi kujisomea na
kuhudhuria kozi kuhusu mwanzilishi, roho, historia na umisionari wa familia
yake, kanuni na katiba zetu, ili tuwe pamoja hata tunapokabili hali mpya za
maisha.
Tukumbuke pia kuwa karama yoyote inazaliwa ndani ya
Kanisa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu; hivyo itakuwa hai kadiri inavyozingatia
asili yake hiyo na lengo lake hilo.
6.9.
MASOMO
Masomo yanatakiwa kutokeza hamu isiyozimika ya
kumjua zaidi Mungu, asili ya mwanga na ukweli wote: kwa hiyo elimu yote iendelee
kujengeka juu ya ujuzi imara wa mafundisho ya imani.
Badala ya kusomasoma magazeti kwa udadisi,
tunahitaji juhudi za kudumu upande wa akili kama njia ya kujilea na
kujikamilisha iliyo muhimu hasa leo, tunapokabiliana na mabadiliko
yanayoyumbisha.
Lengo lisiwe kuabudu elimu wala kujidai, bali
kukuza sala na ushirikiano, uwezo wa kupima na kuchuja mambo, pamoja na kuelewa
watu na maisha yao, tusije tukaishia katika sura za nje na mitazamo ya juujuu,
wala kujihisi tumebaki nyuma na kuanzisha mambo kwa pupa tu.
Wajibu wa kusoma hauishii katika malezi ya msingi
wala katika kujipatia vyeti na digrii.
Hivyo wakati wowote wa maisha yetu tunaweza
tukaitwa kufuata masomo maalumu: hicho ni kipindi nyeti hasa tusipoweza
kuyaendesha wenyewe.
Ikiwabidi ndugu waishi nje ya jumuia zetu,
halmashauri kuu iwachagulie kituo ambacho kinahakikisha malezi bora ya Kiroho na
ya kitume, ya kinadharia na ya kiutendaji, na kuwezesha kushika masharti yetu ya
udugu na udogo, ufukara, sala na uaminifu kwa Ualimu wa Kanisa.
Wenyewe wajitahidi binafsi na kwa pamoja
kulinganisha masomo wanayofuata na tunu za Kifransisko, wakisaidiwa na mlezi wao
na wataalamu.
Tujiendeleze vilevile kuhusu ufundi ili kutumia
misaada ya maendeleo, mradi tusiachane na ufukara wetu.
Tujihadhari na vipingamizi vya malezi ya kudumu:
kuzama katika kazi, kupuuzia haja ya kujiendeleza mfululizo na kuogopa utambuzi
wa hali halisi ya roho.
7. HATIMA: MAMA MARIA
7.1.
MARIA NA UTATU
Maria, mfano bora wa upokeaji wa neema,
anatukumbusha kwamba Mungu Baba ndiye anayeanza na kuwezesha daima mema yote.
Kwa jinsi alivyoishi na Yesu Nazareti na kuhudhuria
nafasi muhimu za utume wake, anatufundisha kumfuata pasipo masharti na
kumtumikia kwa ukarimu.
Akiwa hekalu la Roho Mtakatifu, ndani mwake
unang'aa uumbaji mpya.
Maria anafungamana sana na Kanisa pia kama kiungo
bora na mama.
Tukimtazama hivyo kama kielelezo cha kuwekwa wakfu
kwa Baba, kuungana na Mwana hadi msalabani na kuwa wazi kwa Roho, tuelewe na
kuonyesha ya kuwa kufuata maisha manyenyekevu na safi ya Yesu ni kuiga maisha ya
Maria pia.
7.2.
MARIA NA WITO
Daima yeye anashiriki kazi ya Roho Mtakatifu, kama
katika umwilisho na siku ya Pentekoste.
Aliyoyafanya karibu na Yesu anayaendeleza kwa
manufaa ya Mwili wake mzima na ya kila Mkristo, hasa yule anayewajibika kumfuata
Mwanae kwa karibu zaidi.
Mama Maria yupo pale wito unapoanza, unapoundwa na
unapostawi: uwepo huo ni muhimu kwa kila mmoja na kwa uimara na umoja wa jumuia
nzima.
Kwa hiyo fungamano na Bikira Maria lizingatiwe
katika hatua zote.
Tuwaombee watumishi, walinzi, walezi na ndugu wote
wadumu kwa uaminifu chini ya ulinzi wake.
7.3.
KUMUIGA MARIA
Katika maneno yake ya "Fiat" na
"Magnificat" tunakuta ukamilifu wa imani, tumaini na upendo katika
kukubali mpango wa Baba na wa furaha inayotokana na hali hiyo.
Malezi yote yaelekeze njia hiyo ya hakika katika
kusikiliza na kutekeleza Neno na hivyo kufanikisha lengo la utawa.
Bikira wa Maamkio na wa Kana atusaidie kuitikia
shida za watu kwa kuleta msaada, lakini hasa kwa kumleta na kumdhihirisha Yesu
ili wafanye yote atakayowaambia, halafu watangaze pamoja naye maajabu ambayo
Mwenyezi Mungu anawatendea wanyonge wanaokiri jina lake takatifu.
|