Ndugu Wadogo Wa Afrika

Karama ya pekee kwa ajili ya mpango wa Baba

 

Jina lenyewe la chama linaonyesha kuwa karama maalumu ni ile ya Kifransisko ya udugu na udogo ikiwa na uhusiano wa pekee na bara la Afrika.

 

Kwanza kabisa Roho Mtakatifu anawajalia wanachama, kidogo kama alivyomjalia mtakatifu Fransisko wa Asizi, kumtazama kwa namna ya pekee Yesu, Mwana wa Baba, katika kujishusha moja kwa moja kwa ajili yetu.

 

Kwa kuwa yeye kwa upendo na unyenyekevu amejifanya ndugu na mtumishi wetu, wao pia kwa upendo na unyenyekevu wanajisikia mvuto wa kuishi kama ndugu wadogo wa wote, hasa wa watu wa mwisho, ambao wanafanana zaidi na Mwana wa Mtu aliyeteswa.

 

Tangu karne nyingi Afrika ni kielelezo cha mtu kudhulumiwa na mwenzake, jambo la aibu lililochapwa kwa dhati katika saikolojia ya umati.

 

Mlio wa maskini wake, ambao hausikilizwi na wakuu wa ulimwengu huu, unazingatiwa na Mungu hata kwa kuwatuma ndugu wadogo wa kiume na wa kike ambao wawainamie majeraha ya roho na ya miili yao ili kuwaelekeza kwenye uhuru wa wanae.

 

Sharti la kuwaokoa Waafrika kwa njia ya Waafrika ni kutamadunisha kwa dhati ujumbe wa Injili na maisha yaliyowekwa wakfu kwa njia ya useja mtakatifu, ufukara na utiifu, hata viwe na maana na manufaa katika hali halisi ya maisha yao yalivyo leo.

 

Mshikamano, jina jipya la amani.

 

Ukweli usiopingika wa kwamba binadamu wote ni ndugu unadai tuishi kidugu, tusikubali tofauti kubwa mno kati ya hali za maisha.

 

Katika ulimwengu uliojaa maonevu, ni lazima tushikamane na wanyonge, kwa mfano wa Yesu, Mwana wa Mungu aliyejifanya fukara kwetu sisi sote, lakini hasa kwa ajili yao.

 

Kwa ndugu wadogo wa Afrika mshikamano huo maana yake sio tu kutaka kuwasaidia fukara, kama toka juu, bali kushiriki iwezekanavyo mateso na matumaini yao.

 

Wito huo wa kuwa jirani kabisa na watu wa mwisho ndio unaoathiri zaidi ufukara wao halisi katika chakula, mavazi, makao, matumizi ya vyombo vya mawasiliano na mengineyo yote.  

Nguzo za utawa  

 

  • USEJA MTAKATIFU. Nguvu ya kupenda iliyo maalumu ya moyo safi, ulio tayari daima kujitoa na kumtumikia yeyote, usiotawaliwa kamwe na umimi wa tamaa, ulio lengo la kulikazania kwa makusudi, ili kuzaa matunda mengi zaidi.  

  • UFUKARA. Uhuru wa kimaisha unaotokana na kuchagua moja kwa moja mema ya milele, na kujiaminisha kwa tumaini mikononi mwa Mungu, na kushikamana kabisa na watu wa mwisho, wale ambao hawana hata vitu vya lazima.  

  • UTIIFU. Msimamo wa msingi wa Mwana wa Mungu, wa kuweka pembeni matamanio yake ili kutambua na kutekeleza mpaka mwisho mpango wa upendo wa Baba kwa faida ya ndugu wote.

LINKS:

 

WIMBO WA TAIFA

Mungu Ibariki Afrika

Wabariki viongozi wake

Hekima, umoja na amani

Hizi ni ngao zetu

Afrika na watu wake. 

CHORUS:    

Ibariki, Afrika

Ibariki, Afrika

Tubariki, watoto wa Afrika

Morogoro: Un momento di formazione - Morogoro: Kipindi cha malezi - Morogoro: A moment of formation