Alfagems Co. ltd

Secondary School

Morogoro Tanzania

Sheria za shule

ALFAGEMS SECONDARY SCHOOL

P.O.Box 6083 – MOROGORO

Tel. 0765-899959 / 0713-784600

www.alfagems.com

 

SHERIA ZA SHULE

 

1. Sheria za kiutu

 

1.1.       Uwahi shuleni muda uliopangwa, uwepo muda wote wa masomo na wa kazi ukifuata ratiba ya shule ndani na nje ya darasa.

1.2.       Uheshimu bendera, picha za viongozi na wimbo wa taifa unaotumiwa na shule kama sala ya pamoja kila siku; uuimbe umesimama pamoja na kundi linalokuhusu.

1.3.       Popote ulipo uwe na tabia njema, heshima na utiifu kwa walimu, wafanyakazi na majirani wa shule, wanafunzi wenzako na binadamu yeyote.

1.4.       Ukifikiwa au kukutana na mwalimu au mtu yeyote anayekuzidi umri usimame kumsalimia.

1.5.       Ukiitwa na mwalimu yeyote umuitikie mara.

1.6.       Uwe daima safi (mwili, nguo na vitu vyote unavyotumia).

1.7.       Uwe na nywele fupi; usifuge ndevu.

1.8.       Usijirembe kwa kutia nywele dawa, kujichora, kutia wanja n.k.

1.9.       Usiache kucha ndefu wala kupaka rangi au hina.

1.10.     Usivae kofia, jaketi, viatu vya ghorofa wala mapambo yoyote (herini, bangili, mikufu n.k.).

1.11.     Uvae daima sare ukiwa shuleni (hata wakati wa likizo), ukitoka kwa shughuli za kishule, ukienda hospitalini, ukisafiri kufika shuleni au kurudi nyumbani, n.k.

1.12.     Usionekane katika mazingira ya wasiwasi (klabu, kumbi za starehe, nyumba za wageni n.k.) wala kujihusisha na ulevi na uvutaji wa aina yoyote.

1.13.     Usiwe na urafiki wa kimapenzi; hata hivyo ukipata mimba utakubaliwa likizo ya uzazi, usije ukaua mimba.

1.14.     Darasani ukae mahali pako, pasipo kuhamahama wala kuchanganyikana na jinsia nyingine.

1.15.     Uthamini kazi za aina zote na kuzifanya kwa bidii, ukishirikiana na wenzako katika usafi na utunzaji wa mazingira.

1.16.     Ulinde mali yako binafsi na ya shule (majengo, madawati, vitabu na vifaa vingine utakavyopewa).

1.17.     Usitoe dawati nje ya jengo lake pasipo agizo au ruhusa.

1.18      Utambue ni marufuku kuiba, kugombana, kupigana, kutumia lugha chafu, kuchonganisha, kuchochea vurugu na kufanya mgomo.

1.19.     Usitembelee nyumba za walimu na wafanyakazi wengine wala bweni la jinsia tofauti.

1.20.     Usitoroke shule, bali utoe taarifa kama utashindwa kuhudhuria masomo.

1.21.     Usilete shuleni simu, redio n.k. la sivyo utafukuzwa mara moja.

1.22.     Ukubali mamlaka ya wanafunzi viongozi katika kushauri, kuonya na hata kuadhibu kabla tatizo lako halijaufikia utawala wa shule.

1.23.     Usikatae adhabu.

 

2. Sheria za kitaaluma

 

2.1.       Uwe msikivu na mtekelezaji wa maagizo na mashauri ya walimu.

2.2.       Ukamilishe kazi zote zinazotolewa na walimu kwa wakati unaotakiwa.

2.3.       Uwe mtulivu muda wote darasani, mwalimu awepo au asiwepo vilevile.

2.4.       Ushirikiane vema na walimu pamoja na wanafunzi wenzako ili kupata msaada wa kitaaluma.

2.5.       Ujitahidi kufanya vizuri mitihani ya mara kwa mara, usije ukaondolewa shuleni kwa kutoifanya mara tatu mfululizo (hata kama umeruhusiwa kwa shida maalumu) au kwa kutofikia mara tatu mfululizo wastani wa alama 40.5 kwa masomo yote.

2.6.       Utambue ni kosa kubwa kuibia, kusaidiwa au kusaidia katika mtihani wowote.

 

3. Sheria za nyongeza kwa wanaokaa bweni

 

3.1.       Uvae sare muda wote uwapo shuleni au bwenini, bila ya kuichanganya na vazi lingine wala urembo wowote.

3.2.       Kisha kwenda darasani uombe ruhusa ukihitaji kurudi bwenini wakati wa vipindi.

3.3.       Uzingatie muda wa chakula kwa sababu huruhusiwi kukipeleka bwenini.

3.4.       Usiende nje bila ya ruhusa maalumu; ukienda kwenye ibada uvae sare na kurudi shuleni mara, bila ya kupitia sehemu nyingine.

3.5.       Usimpokee mgeni yeyote tofauti na walioandikwa na mzazi, wala nje ya siku za kutembelewa, tena upate kwanza ruhusa ya mkuu wa bweni na usimuingize bwenini.

3.6.       Usiwasiliane na mtu yeyote bila ya mkuu wa bweni kujua.

 

4. Adhabu

 

4.1.       Kwa kosa la kukwepa mtihani wowote, na vilevile la kuibia, kusaidiwa au kusaidia wakati wa kuufanya, utaandikiwa alama sifuri (0%) katika matokeo yako.

4.2.       Kwa baadhi ya makosa utapewa kwanza maonyo mawili, ambayo yataandamana na adhabu shuleni na kudai uandike barua ya kukiri kosa na kuahidi hutalirudia.

4.3.       Kwa makosa makubwa zaidi hutapewa maonyo, bali utasimamishwa kwa siku au wiki kadhaa, kama si kufukuzwa shule.

4.4.       Ukipoteza au kuharibu kitabu au kitu chochote cha shule utatakiwa kununua kipya na kurejesha, la sivyo hutarudishiwa fedha za tahadhari.

4.5.       Hutarudishiwa vitu visivyotakiwa shuleni vikinyang’anywa na uongozi.